MAELEZO, DAR
ES SALAAM
Wananchi wa Kijiji cha Igawa, Halmashauri ya Wilaya ya
Mbarali Mkoani Mbeya wamepongeza Serikali kwa kuboresha
miundombinu ya barabara hatua inayolenga kufungua fursa za kiuchumi na ukuaji
wa miji katika maeneo mbalimbali nchini.
Wakizungumza katika mahojiano maalum na Idara ya Habari
(MAELEZO) hivi karibuni Kijijini hapo, wananchi hao walisema udhubutu
uliofanywa na Serikali katika kutekeleza miradi mikubwa ya
maendeleo ikiwamo ujenzi wa barabara utaacha alama ya kihistoria kwa vizazi
vijavyo kuhusu wajibu wa Serikali katika kuwatumikia wananchi.
Bw. Christom Variyamba Mkazi wa Kijiji cha Igawa alimpongeza
Rais Dkt. John Magufuli kwa udhubutu uliofanywa na Serikali
kwa kutengeneza barabara nyingi zenye viwango vya kimataifa katika kipindi
kifupi ikiwemo barabara ya Igawa-Mafinga, na kutoa fursa kwa wananchi kuweza
kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo usafirishaji wa mazao
ya kilimo.
‘’Kwa sasa Dar es Salaam tunafika kwa wakati na salama
kabisa, barabara hii ya Igawa-Mafinga imejengwa kwa miundombinu ya kisasa
kabisa ikiwemo mataa ya barabarani na hii itasaidia kupunguza ajali wakati wa
usiku kwani iwapo kutatokea gari likapata tatizo wakati huo utaweza kuliona’’
alisema Variyamba.
Naye Bw. Hamadi Nuru anasema awali Kijiji cha Igawa hakikuwa
na maendeleo, lakini hali ni tofauti kwa sasa kwani ujenzi wa barabara katika
Kijiji hicho kumeweza kutoa hamasa ya wananchi kushiriki katika shughuli za
biashara wakati wa biashara na hivyo kuwaongezea kipato kutokana na uwepo ya
taa za kisasa zilizofungwa katika barabara hiyo.
Kwa upande wake Bi. Rehema Ally anasema Igawa ya sasa si ile
ya zamani, kwani Kijiji hicho cha sasa kinakua kwa kasi na kukimbizana na Miji
mikubwa nchini ikiwemo Jiji la Dar es Salaam, hatua inayowalazimu wakazi
mbalimbali kutoka Mikoa mbalimbali nchini kurejea katika Kijiji hicho kuweza
kutumia fursa ya miundombinu ya barabara hiyo kushiriki katika shughuli za
kiuchumi.
‘’Mimi binafsi niliondoka Igawa kwa muda mrefu lakini
niliporejea mwaka 2019 niliona hali ni tofauti kabisa, mji umekuwa, biashara
zimeshamiri na hiyo inatokana na maboresho makubwa ya barabara ya
Igawa-Mafinga, tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kutokana na jitihada
kubwa inazofanya katika kusogeza huduma muhimu kwa wananchi wake’’ alisema
Rehema.
Mwananchi mwingine Mkazi wa Igawa, Rehema Kwila alisema
tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano Kijiji cha Igawa na
wananchi wake wameshuhudia mageuzi makubwa ya huduma za kijamii ikiwemo
barabara ambazo zimesaidia kuondoa changamoto za muda mrefu ambazo zilishindwa
kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
‘’Tangu kuingia kwake madarakani Rais Dkt. John
Magufuli mambo mengi yamebadilika, kwani uhalifu umepungua kwa kiasi kikubwa
sana katika Kijiji chetu cha Igawa, barabara zimeboreshwa kwani awali kulikuwa
na mashimo mengi barabarani hali iliyotulazimu kutumia masaa matatu-manne
kufika Makambako’ alisema Kwila.
Naye Bw. Aloyce Peter, Dereva wa magari makubwa yaendayo Nje
ya Tanzania, anasema kwa sasa wanatumia siku 2 kutoka Dar es Salaam hadi mpaka
Tunduma, Mkoani Songwe ikilinganishwa na hapo awali ambapo katika kipande cha
barabara ya Igawa-Mafinga hali haikuwa nzuri kwani walikuwa wakitumia masaa
takribani 8 na siku nne kufika eneo la mpaka wa Tunduma.
Anasema miundombinu ya barabara za Tanzania ni nzuri
ikilinganishwa na nchi anazosafiri za Zambia Congo ambazo nyingi zina mashimo
na kusababisha kusafiri kwa umbali mrefu kutoka katika eneo la Mpaka wa Tunduma
huku magari hayo yenye uzito wa tani 30 yakilazimika kusafiri kwa takribani
masaa 12 kufika katika miji mikuu ya nchi hizo.
‘’Miundombinu ya barabara za Tanzania imeboreshwa sana, kwa
nchi nyingine tunazokwenda barabara zao siyo nzuri, kwa mfano kutoka Dar es
Salaam hadi Tunduma tunatumia muda mfupi sana wa siku 2, lakini hali ni tofauti
sana tunapokwenda katika barabara za mataifa jirani, miundombinu yao siyo imara
kama ilivyo hapa nyumbani Tanzania’’ anasema Peter.
No comments:
Post a Comment