Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema sh. bilioni 1.3 zimetolewa ili kuanza kazi ya upembuzi yakinifu wa barabara ya Kilwa-Nangurukuru-Liwale.
Ametoa kauli hiyo (Jumapili, Oktoba 25, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa kata za Likongowele, wilayani Liwale, mkoani Lindi kwenye mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa Ujenzi wilayani humo. Pia alizungumza na wakazi wa kata za Kibutuka, Ngunichile, Lionja, Ruponda na Chiola kwa nyakati tofauti alipokuwa akirejea Ruangwa kutoka Liwale kupitia Nachingwea.
Alisema barabara ya Kilwa-Nangurukuru-Liwale yenye urefu wa km. 258 upembuzi wake unatarajiwa kuanza wakati barabara ya Liwale - Nachingwea - Ruangwa yenye urefu wa km.185 usanifu wake wa kina unaendelea na ukikamilika zitatafutwe fedha za kuzijenga kiwango cha lami. “Barabara hizi zinapatikana uk. 75 wa Ilani ya CCM ya 2020-2025.”
Akifafanua zaidi kuhusu barabara za mji wa Liwale, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. bilioni 1.7 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa barabara za Liwale huku sh. milioni 891 zikitolewa kwa ajili ya matengenezo ya muda maalum na kwa kiwango cha lami kwa barabara za Sanabu – Mangota - Mponda, Mchanda - Ngosha Bucha, Wamao- Soko la Zain na Reiner Club- Nyanga.
Akielezea maboresho yaliyofanyika kwenye sekta ya afya, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. milioni 500 zimetolewa kwa ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Liwale ambapo ujenzi wa jengo la OPD lipo hatua ya linta na ujenzi wa jengo la maabara lipo hatua ya kuezeka.
Alisema kwa mwaka 2020/2021 Halmashauri imepangiwa sh. bilioni moja kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa hospitali hiyo. Kwa upande wa vituo vya afya, alisema sh. bilioni moja zimetolewa kwa ajili ya ujenzi Kituo cha Afya cha Mpengere ambacho kimekamilika na huduma zinatolewa kwa wananchi. “Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kibutuka nao umekamilika na wananchi wanahudumiwa,” alisema.
Alisema sh. milioni 69.4 zimetumika kwa ukamilishaji wa zahanati za Mkundi, Chigugu na Barikiwa pamoja na kuchangia ujenzi wa jengo la mama na mtoto. “Pia shilingi bilioni 1.43 zilitolewa kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi. Fedha za ununuzi wa dawa ni wastani wa shilingi milioni 22.6 kwa mwezi,” alisema.
Mheshimiwa Majaliwa alikuwa wilayani Liwale ambako alienda kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Liwale, Bw. Zuberi Kuchauka na mgombea ubunge wa jimbo la Nachingwea, Dkt. Amandus Chinguile na madiwani wa kata alizopitia.
Akiwafafanulia mambo yaliyofanywa na Serikali ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ndani ya miaka mitano wilayani humo, Mheshimiwa Majaliwa alisema kwenye sekta ya maji, sh. bilioni 2.9 zimetolewa kwa ajili ya miradi mikubwa ya maji ikiwemo mradi wa Kipule – sh. milioni 559.2, ambao alisema umekamilika na unatoa huduma maeneo ya Kipule na Mkonganaje.
Aliitaja miradi mingine kuwa ni mradi wa maji Likombola ambao umegharimu sh. milioni 355.1 na kwa sasa umekamilika na unatoa huduma maeneo ya Likombola na Kitamamuhi. Mwingine ni mradi wa Maji Mangirikiti uliotumia sh. milioni 135.5 na sasa umekamilika na unatoa huduma vijiji vya Mangirikiti na Kimbamba.
Aliitaja miradi mingine ambayo bado inaendelea kujengwa na fedha zake kwenye mabano kuwa ni mradi wa maji Kibutuka (sh. milioni 213.1) ambao unakamilishwa kwa ajili ya Kijiji cha Kibutuka na mradi wa maji Kitogoro (sh. milioni 214) ambao unakamilishwa kwa ajili ya kijiji cha Kitogoro.
“Mradi wa Maji Mikunya uliogharimu sh. milioni 359 unakamilishwa kwa ajili ya vijiji vya Mikunya na Legezamwendo wakati mradi wa maji Mpigamiti uliojengwa kwa sh. milioni 11 unakamilishwa kwa ajili ya vijiji vya Mpigamiti, Namakororo na Mitawa.
Akielezea mpango wa elimu bila ada, Mheshimiwa Majaliwa alisema kwa shule za msingi 55 zilipatiwa sh. bilioni 1.5 kwa ajili ya ukarabati, utawala, michezo, mitihani na posho kwa maofisa elimu kata na walimu wakuu.
“Kwa shule za sekondari, shule 16 zilipatiwa kiasi cha shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya fidia ya ada, chakula kwa shule za bweni na posho ya madaraka kwa wakuu wa shule.
No comments:
Post a Comment