Matokeo chanyA+ online




Monday, October 26, 2020

HATUA ZA KUCHUKUA KWA KAMATI ZA USIMAMIZI WA MAAFA NA SEKTA MBALIMBALI KUTOKANA NA UTABIRI WA MVUA ZA MSIMU

Ofisi ya Waziri Mkuu ina jukumu la kuratibu shughuli za maafa kwa kuhakikisha Wizara, Idara, Taasisi, Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na asasi zote zisizo za kiserikali zinashiriki kikamilifu katika kuzuia, kupunguza madhara na kujiandaa kukabiliana na kurejesha hali kwa mujibu wa Sheria ya Menejimenti ya Maafa namba 7 ya mwaka 2015. 


Hivyo, kufuatia utabiri wa mwelekeo wa mvua za Msimu katika kipindi cha miezi ya Novemba, 2020 hadi Aprili, 2021 uliotolewa leo na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imeonekana kuna haja ya Serikali na wadau wengine kuchukua hatua kama ilivyoelezwa taarifa ya utabiri huu ni kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua. 

 

Imeelezwa kwamba mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi.Hali inaweza kusababisha madhara mbalimbali kama uharibifu wa miundombinu, mazao na mifugo kusombwa na maji na milipuko ya magonjwa katika maeneo husika. Taasisi zote na wananchi wanaelekezwa kuchukua hatua kuzuia madhara ya maafa. Kabla mvua kubwa kuanza kunyesha kwa kipindi kilichoelezwa cha miezi ya Januari na Aprili 2021. 

Mikoa husika ni Dodoma, Singida, Mbeya, Songwe, Ruvuma, Njombe, Iringa, Lindi, Mtwara, kusini mwa mkoa wa Morogoro na mashariki mwa mikoa ya Tabora na Katavi. 

Vilevile, mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatabiriwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Kanda ya Magharibi. Wadau wote na wananchi wanaelekezwa kuchukua hatua za kuzuia madhara yanayoweza kusababishwa na mvua kuwa ndogo ikiwemo kupanda mazao yanayokomaa mapema, kuvuna maji na kutunza malisho ya mifugo. Maeneo yanayo husika ni Mikoa ya Kigoma, Rukwa pamoja na magharibi mwa mikoa ya Tabora na Katavi. 


Kufuatia utabiri huo Ofisi ya Waziri Mkuu inatoa maelekezo kwa Kamati za Usimamizi wa Maafa za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji katika mikoa husika nchini, ambazo ndizo zenye jukumu kubwa la kusimamia menejimenti ya maafa, kuchukua hatua mara moja za Kuzuia au Kupunguza, Kujiandaa, Kukabili na Kurejesha hali endapo maafa yatatokea. 

Kamati zote za usimamizi wa maafa katika ngazi zote, zieleze mipango na hatua za kuchukua kwa taasisi na wananchi juu ya menejimenti ya maafa ya mvua za msimu katika ngazi husika.
Ili kutekeleza agizo hili kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa namba 7 ya Mwaka 2015, ninaziagiza Kamati za Usimamizi wa maafa ziwajibike kutekeleza mambo yafuatayo katika sekta za kilimo, maji, afya, mifugo, miundombinu na nishati; 

1.    Wananchi washauriwe kutumia mvua hizi katika shughuli za maendeleo ikiwemo; kilimo, kuandaa mabwawa na malambo kwa ajili ya kuvuna maji, kupanda mazao yanayo hitaji maji mengi kama vile mpunga, uzalishaji wa samaki, kuandaa malisho na nyasi za akiba za mifugo katika mikoa inayotarajiwa kupata mvua nyingi.
2.    Kamati zote za Usimamizi wa maafa katika ngazi zote, ziweke mipango ya kuzuia milipuko ya magonjwa kama homa ya matumbo na kipindupindu na magonjwa ya milipiko ya mifugo.
3.    Kamati hizo zishirikiane na idara na taasisi zinazohusika na mazingira na miundombinu, ili kuhakikisha barabara zinapitika wakati wa msimu huo na mitaro, makalvati yanasafishwa kwa ajili ya kuruhusu maji kutiririka.
4.    Kamati zishirikiane na sekta za maji na umeme kuweka mipango yao na tahadhari kuhakikisha kuwa usumbufu unaotokana na ukosefu wa maji na umeme unapewa ufumbuzi mapema.
5.    Ili kukabili maafa na kurejesha hali kwa wakati endapo maafa yatatokea kamati katika ngazi zote ziainishe na kuandaa rasilimali za usimamizi wa maafa kwa kila sekta kushiriki kikamilifu katika eneo lake.
6.    Kamati zishirikishe wadau wa maafa (Wananchi, Taasisi na Sekta binafsi) katika mipango yao yote ya menejimenti ya maafa hayo.
7.    Kamati zishirikishe wadau wa maafa kuhakikisha upatikanaji wa mbegu zinazokomaa kwa muda mfupi pamoja na utunzaji wa chakula cha binadamu na mifugo katika maeneo ya mikoa inayotabiriwa kuwa na mvua chini ya wastani.

Ofisi ya Waziri Mkuu inatoa wito kwa kila mwananchi, kaya, kijiji, ngazi ya wilaya na mkoa kuhakikisha kuwa tunatimiza wajibu wetu katika suala zima la kushughulikia maafa kwa mujibu wa sheria ili mvua hizi ziwe na manufaa kwa taifa.  
Aidha, Serikali itaendelea kuutaarifu umma hatua za kuchukua kupitia taasisi husika
na vyombo vya habari kwa kadri Mamlaka ya Hali ya Hewa itakavyokuwa ikitoa utabiri wake. Hivyo basi, wananchi wote mnaombwa kufuatilia kwa makini tahadhari na kutumia taarifa hizo za wataalam kutoka sekta mbalimbali kwa usahihi na kuchukua hatua stahiki kwa ustawi wa uchumi wa nchi yetu. 

No comments:

Post a Comment