Thursday, December 31, 2020
WAZIRI WA UJENZI CHAMURIHO AKAGUA MAENDELEO YA UJENZI WA MRADI WA KITUO CHA PAMOJA CHA UKAGUZI (OSBP)
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho, akimsikiliza Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Pwani Mhandisi Wilicis Mwageni, wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi wa Kituo cha pamoja cha Ukaguzi (OSBP), alipokagua mradi huo mkoani Pwani.
Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya sehemu ya mzani katika mradi wa Kituo cha pamoja cha Ukaguzi (OSBP), Vigwaza Mkoani Pwani
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Pwani, Mhandisi Wilicis Mwageni, alipokuwa akikagua maendeleo ya mradi wa Kituo cha pamoja cha Ukaguzi (OSBP), Mkoani Pwani .
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt.Leonard Chamuriho, akifafanua jambo kwa Wahandisi alipotembelea na kukagua mradi wa Kituo cha pamoja cha Ukaguzi (OSBP), mkoani Pwani, ambao kwa sasa umefikia asilimia 90.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI, KHAMIS HAMZA CHILO AKAGUA UJENZI WA NYUMBA ZA POLISI MKOA WA KUSINI PEMBA
RAIS WA ZANZIBAR DKT. MWINYI AMTUNUKU SHAHADA YA HESHIMA YA UDAKTARI WA FALSAFA KATIKA SAYANSI ZA TIBA RAIS MSTAAF DK. ALI MOHAMED SHEIN
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambae pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akihutubia wakati wa hafla ya Mahafali ya 16 ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) katika ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein Tunguu Wilaya ya Kati Unguja 30-12-2020.(Picha na Ikulu)
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi ametawazwa kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Ndg. Mwita Mgeni Mwita na (kulia kwa Rais) Makamu Mkuu wa Chuo Dkt.Zakia Mohamed Abubakar, hafla hiyo imefanyika wakati wa Mahafali ya 16 ya SUZA yaliofanyika katika ukumbi wa Dk.Ali Mohamed Shein Tunguu Wilaya ya Kati Unguja 30/12/2020.(Picha na Ikulu)
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambae pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi, akimtunuku Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa Katika Sayansi za Tiba Rais Mstaaf wa Zanzibar Awamu ya Saba Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, katika Mahafali ya 16 ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) yaliofanyika katika ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein Tunguu 30-12-2020.(Picha na Ikulu)
RAIS WA ZANZIBAR DK HUSSEIN ALI MWINYI AWATUNUKIA SHAHADA WAHITIMU WA SUZA
MAAFISA USTAWI WA JAMII NA MAAFISA MAENDELEO YA JAMII WAHIMIZWA KUENDELEA KUTOA HUDUMA BORA KWA WATU WENYE ULEMAVU
Maafisa Ustawi wa Jamii pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii wamehimizwa kutoa huduma bora kwa watu wenye ulemavu ili kuimarisha ustawi na kuchochea maendeleo ya kundi hilo maalum.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga alipokutana na Maafisa hao katika kikao kazi kilichofanyika Jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Mkutano wa Anatouglou uliopo kwenye ofisi ya halmashauri ya Ilala lengo ikiwa ni kujadiliana pamoja na kushauriana namna bora ya kuhudumia watu wenye ulemavu pamoja na kutatua changamoto zinazo wakabili.
Ummy alieleza kuwa Serikali kwa kutambua na kuthamini haki za wenye ulemavu imekuwa ikishirikiana na asasi za Watu wenye ulemavu kwa nia njema na dhamira ya dhati ili kuhudumia kundi hilo kwa kuwapatia huduma bora kulingana na jamii inayowazunguka.
“Katika kipindi kifupi serikali imetimiza wajibu wake huo kwa kutoa Elimu, huduma za Afya, mafunzo ya stadi za kazi, ajira, nyenzo za kujimudu, huduma za kijamii, kuwezeshwa kiuchumi na vilevile kuboresha miondombinu ili iwe Rafiki kwa matumizi ya watu wenye ulemavu katika kupata huduma stahiki,” alieleza Mheshimiwa Ummy
Aliongeza kuwa kundi hilo hapo nyuma liliachwa lakini tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani kundi hilo linapigiwa chapuo na limekuwa likijumuishwa katika kila nyanja muhimu, lakini serikali iliyopo imeendelea kujenga mazingira kwa wenye ulemavu ili waweze kujiletea maendeleo kwa kutumia rasilimali zilizopo katika kuboresha huduma zao.
“Malengo ya serikali ni kuhakikisha inaendeleza watu wenye ulemavu pasipo kuachwa nyuma na hivyo katika kutambua hilo imeendelea kuwahamasisha wenye ulemavu kushiriki katika kila nyanja,” alisema
Sambamba na hayo, amewata Maafisa hao kuongeza juhudi na kasi katika kuhamasisha Watu wenye Ulemavu, Vijana na Wanawake kuanzisha vikundi ambavyo vitachangamkia fursa ya mikopo inayotolewa na halmashauri kwa kuanzisha miradi au kuendeleza miradi waliyonayo ili waweze kujikwamua kiuchumi.
“Upo umuhimu wa kutambua uwezo na vipaji maalum vya watu wenye ulemavu, vijana na wanawake na kuweka mikakati madhubuti ya kuviendeleza vikundi wanavyoanzisha ili waweze kujikomboa kiuchumi na waweze kuajiri watu wengine,” alisema Ummy
Alifafanua kuwa katika suala la uwezeshaji wa watu wenye ulemavu inaonyesha kuwa wametambua umuhimu wa mikopo hiyo inayotolewa na halmshauri na ndio maana wamekuwa wakijitokeza kuchukua mikopo inayotolewa na halmashauri.
“Jambo hili limenifurahisha kuona sasa mikopo inatolewa kwa wingi kwa watu wenye ulemavu ambao wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi, tunashuhudia kupitia uwezeshaji huo kumekuwa na ongezeko la miradi mbalimbali inayoendeshwa na wenye ulemavu,” alisema Ummy
“mafanikio haya yanayoonekana yanatokana na juhudi zenu kama maafisa wa serikali katika kupanga utekelezaji wa shughuli zenu vizuri, muongeze juhudi katika kutoa huduma bora ili kwa pamoja kutimiza malengo ya kukuza uchumi wa taifa letu,” alieleza
Aidha, Naibu Waziri Ummy alitoa rai kwa vikundi ambavyo vimekuwa na tabia ya kukopa katika halmashauri moja na baadae kuhamia kwenye halmashauri nyingine kutaka kukopa tena kwenye halmashauri nyingine kuacha mara moja tabia hiyo huku akiwataka warejeshe mikopo yao kwanza ndio wakope tena.
Pia, Mheshimiwa Ummy alitumia fursa hiyo kuvitanga vikundi vya watu wenye ulemavu kuachana na kasumba kuwa mikopo wanayopatiwa na halmashauri ya 2% kuwa ni misaada au inatolewa bure badala yake wakope na kurejesha kwa wakati ili waweze kukopeshwa tena zaidi.
Akizungumza kabla, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Bi. Charangwa Makwiro alieleza kuwa bado yanafanyika maboresho makubwa katika kuwezesha watu wenye ulemavu, vijana na wanawake ili kuboresha miradi yao iweze kunufaika kiuchumi zaidi.
Kwa upande wake, Afisa Mipango na Uratibu ambaye pia ni Mwakilishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Gerald Sando alieleza kuwa Halmashauri zote sita za mkoa zimekuwa zikitoa mikopo hiyo katika kila mwaka wa fedha sambamba na kujiwekea mikakati ya kuwezesha vikundi vingi zaidi.
Naye, Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri ya Kigamboni Bi. Christina alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa halmashauri hiyo wamefanikiwa kuwezesha vikundi vingi ikiwemo watu wenye ulemavu kwa kuwapatia mikopo ya bajaji, usindikaji na mikopo mingine inayoendana na ulemavu alionao mtu husika.
Katika kikao kazi hicho walishiriki Maafisa Ustawi wa Jamii, Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na Maafisa Vijana ambao walipata fursa ya kutoa taarifa ya uwezeshaji wa mikopo ya 10% inayotolewa na halmashauri zao kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu.
IDADI YA WAPIGA KURA IRAMBA HAIKUTOSHA KWA RAIS MAGUFULI KUTOKANA NA MAENDELEO ALIYOYAFANYA
Na Mathias Canal, Iramba-Singida
Idadi ya wapiga kura ya asilimia 30.34% ya wananchi waliojitokeza kupiga kura katika uchaguzi Mkuu wa Disemba 29, 2020 Jimbo la Iramba Magharibi Mkoani Singida imetajwa kuwa ilikuwa ni ndogo ikilinganishwa na wapiga kura waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
Idadi ya wananchi waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura wilayani Iramba ni 141,521 lakini waliopiga kura hawafiki hata nusu ya idadi ya wananchi hao waliojiandikisha.
Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ameyasema hayo tarehe 20 Disemba 2020 wakati akizungumza kwenye Kikao cha Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Iramba kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Kiomboi.
Mhe Mwigulu amesema kuwa hilo ni jambo la kufanyiwa kazi kwa haraka kwani katika tathmini za kiushindani linapaswa kupatiwa majibu ikiwemo kubaini chanzo cha tatizo hilo.
“Tumeshinda kwa kiwango kikubwa kwenye nafasi ya Mgombea Urais, Mbunge na Madiwani lakini kuna kiporo cha kukifanyia kazi kwani idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura ni wachache kuliko idadi ya wanachama waliojiandikisha” Mhe Mwigulu
Katika kikao hicho Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba ametunukiwa vyeti viwili vya pongezi ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wake wa kuimarisha chama namna ya ushiriki wake kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Katika hatua nyingine Dkt Mwigulu amewasihi watanzania kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli.
Amesema kuwa watanzania wamelipa fadhila kwa uchache dhidi ya Rais Magufuli kwani idadi ya waliojitokeza kumpigia kura sio sawa kabisa na idadi ya wananchi waliojiandikisha.
Ameongeza kuwa rekodi ya utendaji kazi iliyofanywa na Rais Magufuli kwa wananchi wa Tanzania katika huduma mbalimbali za kijamii ni ya kifani na itatumika kama somo Duniani kote.
“Ingekuwa imepitishwa kuwa na Rais mmoja wa Afrika ni wazi kuwa Tanzania tungekuwa tumetoa Rais huyo ambaye ni Dkt John Pombe Magufuli kutokana na mambo makubwa aliyoyafanya” Amekaririwa Mhe Mwigulu
DC LUHAHULA AIPONGEZA TRA IRAMBA, ATAKA IONGEZE KASI UTOAJI ELIMU YA MLIPA KODI- WAZIRI MWIGULU KULIPA KODI NI MCHANGO WA LAZIMA AMBAO UMEWEKWA KISHERIA
Mwenyekiti wa kamati ya Ushauri wa kodi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida Mhe Emmanuel Luhahula akizungumza wakati wa kikao cha ushauri wa kodi kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa Halmashauri ya Mji -Mjini Kiomboi tarehe 29 Disemba 2020. Kushoto ni Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba na mwingine ni Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Iramba Ndg Novline Munuo. (Picha Zote Na Mathias Canal)
Na Mathias Canal, Iramba-Singida
Mwenyekiti wa kamati ya Ushauri wa kodi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida Mhe Emmanuel Luhahula amempongeza Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Iramba Ndg Novline Munuo kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha ukusanyaji wa kodi unaimarika.
Dc Luhahula ametoa pongezi hizo tarehe 29 Disemba 2020 wakati akizungumza kwenye kikao kazi cha ushauri wa kodi kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Mjini Kiomboi.
Kikao hicho kimehudhuriwa na wajumbe ambao ni Meneja TRA Wilaya ya Iramba Ndg Novline Munuo, Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt Mwigulu Nchemba, Katibu Tawala Wilaya ya Iramba Ndg Sango Songoma, Mkuu wa Usalama wa Taifa Wilaya ya Iramba Ndg Nick Chilale, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Iramba Ndg Peter Lusesa, Mwenyekiti wa wafanyabiashara ambaye ni Diwani wa kata ya Kiteka Mhe Wilfred Kizanga, Muwakilishi wa Mkurugenzi wa Mji wa Kiomboi ambaye ni Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Ndg Romwald Mwendi pamoja na wajumbe wengine kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya.
Mhe Luhahula amesema kuwa wakati Meneja huyo anaanza kazi katika wilaya hiyo kulikuwa na mashine 4 za EFD lakini kwa muda mfupi kumekuwa na ongezeko la matumizi ya mashine hizo kwani zimefikia 86 ikiwa ni ongezeko la asilimia zaidi ya 96%.
Pamoja na pongezi hizo lakini Mkuu huyo wa Wilaya ya Iramba ameitaka Ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Iramba kuongeza juhudi za ukusanyaji kodi kwani miradi mingi inayofanywa na serikali kwa ajili ya huduma mbalimbali inatokana na kodi za wananchi.
Amesema kuwa ongezeko la ulipaji kodi ndio chachu ya ongezeko la shughuli mbalimbali za huduma za maendeleo katika jamii huku akisisitiza kuwa kulipa kodi ni alama ya uzalendo na sio adhabu kwani ni sehemu ya mpango wa kuongeza mapato ya kukuza uchumi na kuleta maendeleo nchini.
“Kulipa kodi ni alama ya uzalendo na sio adhabu ni mpango wa Serikali kuipeleka mbele nchi kimapato na kukua uchumi wake”, Amekaririwa Mhe Luhahula.
Akizungumza wakati wa kikao kazi hicho Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa kulipa kodi ni mchango wa lazima ambao umewekwa kisheria kwa raia na wageni kwa lengo la kukusanya mapato kwa ajili ya matumizi ya Taifa.
Akizungumzia masuala ya makadirio, Waziri Nchemba aliitaka mamlaka hiyo kuhakikisha wanatenda haki kwa kuangalia uhalisia wa biashara au huduma inayotolewa kwa sababu unaweza kumpa mtu makadirio ya bei ya juu badala ya kumsaidia ukidhani kwamba ndio utapata kodi kumbe umechochea kufungwa biashara.
“Mkiwapa kodi ambayo ni halali watajua ni wajibu wao na wataweza lakini niwaambie kwamba Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli inawapenda walipa kodi na wafanyabiashara hivyo wahimizwe kuhakikisha wanalipa kodi” Alisema
Amesema kuwa ulipaji wa kodi ndio uti wa mgongo wa Taifa lolote hivyo hawana budi kujipanga vizuri kuhakikisha watumishi wa TRA na wafanyabiashara hawajengeani mazingira ya chuki na walipa kodi ambao ni wananchi.
Wajumbe wa kikao cha ushauri wa kodi Wilaya ya Iramba kwa kauli moja wameridhia umuhimu wa kutolewa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa kulipa kodi.
Tuesday, December 29, 2020
MBUNGE SANGA ATIMIZA AHADI YAKE YA KUWEKA UMEME JUA ZAHANATI YA ILINDWE
Mbunge wa Makete Festo Sanga amekabidhi na kufunga umeme jua (Solar Panel) tatu katika zahanati ya Kijiji Cha Ilindiwe iliyopo Kata ya Mang'oto ikiwa ni ahadi yake aliyoitoa wakati akiomba kura kwenye kampeni za uchaguzi mkuu 2020.
Akikabidhi vifaa hivyo Sanga amewaomba wananchi kuvitunza Ili viwasaidie kwa muda mrefu wakati mchakato unaendelea wa kuunganishwa na umeme wa REA.
"Nilipokuja kuomba kura mliniambia hitaji lenu la kwanza ni Umeme wa Solar kwenye zahanati yenu hii, mlihitaji umeme kwa sababu huduma nyingi zinakwama nyakati za usiku na hasa zile zinazohitaji umeme,nami niliwaahidi kuwasaidia na leo nimetimiza ahadi yangu,"alisema.
Amesema ametimiza ahadi hiyo kwa haraka Ili kuendana na ahadi iliyotolewa katika ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2020-2025 ya kuimarisha huduma za afya Ili kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
"Natambua umuhimu wa Zahanati hii katika kuwahudumia wananchi,kama
mbunge niliyepita kunadi Ilani hiyo nimeona ni vyema nikaitekeleza
mapema ili mama zetu wanapohitaji huduma ya uzazi waipate masaa yote
pakiwa na umeme, lakini wahudumu wetu wapumzike kutumia tochi kuhudumia
wananchi nyakati za usiku na kwa kufanya hivyo tutafikia lengo na
dhamira ya chama chetu,"alisisitiza.
Wakizungumza katika makabidhiano hayo baadhi ya wananchi wamemshukuru mbunge kwa kutimiza ahadi yake kwa haraka kwa kweli
"Changamoto
ilikuwa kubwa hasa tulipohitaji huduma nyakati za usiku,tunamshukuru
kwa kutimiza ahadi hii kwa kuwa wapo waliotangulia kuahidi lakini bado
hawajatimiza, huyu Sanga ametupa matumaini makubwa sana sisi wananchi wa
Ilindiwe tunamuombea kwa Mungu ambariki kwa pale alipotoa kwa ajili
yetu,"alisema Sarah Singwa mkazi wa eneo hilo.
WAZIRI MKUU AMUWAKILISHA RAIS DKT. MAGUFULI MAZISHI YA ASKOFU BANZI
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kumuenzi Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Tanga, Baba Askofu Anthony Mathias Banzi kwa kuuishi utumishi wake uliogubikwa na upole na unyenyekevu aliowaonesha wakati wa kipindi cha uchungaji wake.
Ametoa wito huo (Jumanne, Desemba 29, 2020) kwenye mazishi ya Askofu Banzi yaliyofanyika ndani ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Anthony wa Padua, Jimbo Katoliki la Tanga. Waziri Mkuu ameshiriki mazishi hayo kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Ibada ya mazishi imeongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Mtwara, Askofu Titus Mdoe.
Waziri Mkuu amesema katika maisha na utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, Askofu Banzi alitoa kipaumbele katika masuala mbalimbali ya kijamii zikiwemo za elimu, afya na maji. Askofu Banzi alifariki dunia Jumapili, Desemba 20, 2020 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.
“Leo hii tunapomsindikiza Baba Askofu Anthony Banzi tunajivunia mchango wake mkubwa katika kupigania amani, maelewano na mtangamano wa jamii kwa lengo la kujenga umoja, upendo na mshikamano wa Kitanzania. Sisi upande wa Serikali tutamkumbuka sana.”
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa pole kwa familia, ndugu na jamaa, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na waamini wote wa kikatoliki nchini. “Tumuombee kwa Mwenyezi Mungu azipokee kazi zake za kiuchungaji alizozifanya katika kipindi cha uhai wake na ampumzishe kwa amani.”
Naye, Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu
amesema kuwa wanawake wa Mkoa wa Tanga wamempoteza baba mwema na mlezi
ambaye alipenda kuwashauri na kuwaunganisha kama watoto wake kwa kutumia
kaulimbiu yake ya hekima, umoja na amani
“Mimi
ni mmoja wa wanufaika wa upendo, wema na hekima za baba Askofu, licha
ya kuwa mimi sio Mkatoliki lakini baba Askofu Banzi amekuwa
akinikaribisha nyumbani kwake na kunipa baraka zake na kuniombea kwa
sababu yeye anaamini watu wote ni wamoja”
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela amesema Baba askofu Banzi alikuwa ni kiongozi mnyenyekevu, muadilifu na mpenda maendeleo aliyependa kuuona mkoa wa Tanga unapiga hatua.
Akisoma wasifu wa marehemu Askofu Banzi, Padri Richard Kimbwi alisema alizaliwa Oktoba 28, 1946 katika Parokia ya Tawa, Jimbo Katoliki la Morogoro, ambapo baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, Julai 29, 1973 alipewa daraja takatifu la upadre, Jimbo Katoliki la Morogoro.
Alisema kuwa Mwaka 1976 aliteulia kuwa Msarifu wa Seminari kuu ya Ntungano, Jimbo Katoliki la Bukoba na mwaka 1976 hadi mwaka 1981 alipelekwa nchini Austria kwa masomo ya juu na kufanikiwa kutunukiwa Shahada ya Uzamivu katika Falsafa. Mwaka 1981 hadi mwaka 1982 aliteuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Mandera na mhudumu wa maisha kiroho kwenye Hospitali ya Turiani, Jimbo Katoliki la Morogoro.
Aidha, mwaka 1981 hadi mwaka 1985 aliteuliwa kuwa Mhasibu wa Jimbo Katoliki la Morogoro na kati ya Mwaka 1985 hadi mwaka 1987 alikuwa ni Padre wa kiroho, Sekondari ya Masista Bigwa, Morogoro. Kati ya Mwaka 1988 hadi mwaka 1991 alikuwa mwalimu na mlezi, Seminari kuu ya Ntungano, Jimbo Katoliki la Bukoba na baadaye akateuliwa kuwa Gambera.
Mwaka 1992 hadi mwaka 1994 aliteuliwa kuwa Gambera wa Seminari kuu ya Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi na ilipofika tarehe 10 Juni 1994, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Tanga na kuwekwa wakfu tarehe 15 Septemba 1994 na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam.
Alisema Askofu Banzi amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 74 ya kuzaliwa, miaka 47 ya Daraja Takatifu la Upadre na miaka 26 ya Uaskofu, Utume ambao aliufanya kwa uaminifu mkubwa katika kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Tanga.