Matokeo chanyA+ online




Friday, February 26, 2021

TANESCO FANYENI VIKAO VYA MARA KWA MARA NA WAFANYAKAZI WENU

 


Naibu Waziri Wa Nishati, Wakili Stephen Byabato ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kufanya vikao vya mara kwa mara na wafanyakazi wa shirika hilo kwa kila Kitengo na Idara husika ili kusikiliza changamoto zinazowakabili watumishi hao.

Wakili Byabato alisema hayo, wakati akizungumza na wafanyakazi wa shirika hilo mkoani Simiyu Februari 25, 2021, wakati wa ziara yake mkoani humo.

Alisema vikao hivyo vihusishe wafanyakazi wote bila kujali viwango vya elimu na ngazi za madaraja walizonazo, ili kila mtumishi aweze kueleza yanayomsibu sehemu za kazi pamoja na kueleza namna bora ya kuboresha utendaji kazi wao.


Aliwaeleza kwamba vikao hivyo ndivyo vinavyowafanya wafanyakazi kujiona wao ni sehemu ya familia ya shirika kwa kuwa wanapata muda wa kukaa pamoja na kuzungumza na viongozi wao.

Aidha alitaka watumishi hao kupewa nafasi ya kutoa maoni au mapendekezo yao ya nini kifanyike ili kuboresha utendaji kazi wao pamoja na shirika kwa jumla na maoni hayo yasikilizwe na kufanyiwa kazi.

“Mfanyakazi hutumia muda mwingi wa maisha yake sehemu ya kazi, eneo hili ni muhimu sana kwa kuwa wote hujiona ni familia moja licha ya kila mmoja kutekeleza majukumu yake, hivyo ni muhimu viongozi wa eneo husika kuweka utaratibu kuwa na vikao vya pamoja ili waweze kueleza changamoto zao, na zifanyiwe kazi kwa wakati sahihi, hii inaongeza morali ya kufanya kazi muda wote kwa kasi, ubunifu na usahihi, na katika vikao hivyo mara nyingi hupatikana mawazo chanya ya kujenga na kuimarisha zaidi ubora wa shirika”, alisema Wakili Byabato.


Katika hatua nyingine aliwaonya watumishi hao kufika kazini wakiwa wamelewa ama kunya pombe muda wa kazi, na atakayebainika kuwa na tabia hiyo achukuliwe hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria za kazi.

Hata hivyo alipongeza wafanyakazi wa shirika hilo mkoani humo kuwa wamekuwa wakifanya kazi zao kwa umakini na kutoa huduma nzuri kwa wateja licha ya changamoto mbalimbali zinazowakabili za kukatika umeme mara kwa mara mkoani humo.

Aidha aliwaeleza kuwa waendelee kuwa wavumilivu  kwakuwa muda si mrefu changamoto hiyo itatuliwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Imalilo.

Kituo hicho kitakuwa na uwezo kuzalisha umeme wa Megawati 90 itakayokuwa ikitumika katika mkoa huo na mikoa jirani, mahitaji ya umeme kwa Simiyu kwa sasa ni Megawati 10 tu.

Mkoa wa Simiyu unapokea umeme kutoka mkoani shinyanga na hivyo kuufanya umeme huo kuwa na nguvu ndogo kuhimili matumizi halisi.

SEKTA YA HIFADHI YA JAMII KUCHOCHEA KASI YA MAENDELEO YA KIUCHUMI NCHINI



Imeelezwa kuwa Sekta ya Hifadhi ya Jamii ikitumika vizuri itawezesha kukuza kasi maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi na taifa kwa ujumla endapo itawekeza kwenye maeneo au miradi ya kimkakati.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama wakati akitoa majumuisho ya ziara yake alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa Kiwanda cha Machinjio ya Kisasa cha Nguru Hills kilichopo Mvomero, Mkoani Morogoro.

Akikagua Mradi huo Waziri Mhagama alieleza kuwa Serikali inaitazama sekta ya hifadhi ya jamii kuwa ni chachu ya kukuza kasi ya maendeleo ya uchumi ya Taifa kutokana na uwekezaji mzuri unaofanywa na sekta hiyo katika kuwekeza kwenye maeneo ya kimkakati na miradi mikubwa ya kimkakati inayoanzishwa hapa nchini.


“Tumeshuhudia tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani chini ya Kiongozi wetu mahiri Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alitoa maelekezo kuwa sekta ya hifadhi ya jamii iwe sehemu ya kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kuwekeza kwenye maeneo ya kimakati ambayo yanatija ama miradi ya kimakati inayoweza kukuza uchumi wetu kwa kasi zaidi,” alieleza Waziri Mhagama

“Ujenzi wa kiwanda hiki cha Machinjio ya Kisasa cha Nguru Hills inaashiria kuwa sasa sekta ya hifadhi ya jamii imeamua kuitikia wito wa ukuzaji wa uchumi wa Taifa kwa kuwekeza kwenye mradi huo ambao utakuwa na tija kubwa,” alisema


Aliongeza kuwa, kukamilika kwa kiwanda hiko kutawezesha uzalishaji wa nyama yenye ubora na ngozi itakayotoka kiwandani hapo kuwa na ubora wa kuuzwa kwenye masoko ya ndani au nje ya nchi na hivyo kuingiza fedha za kigeni ambazo zitawezesha uchumi wa Taifa kukua kwa kasi.

“Kiwanda hiki cha Nguru Hills ni eneo moja wapo muhimu ambalo litatumika kama eneo la kimkakati la kuongeza thamani ya bidhaa zinazotokana na mifugo,” alisema Mhagama

Alifafanua kuwa, Serikali imedhamiria katika kipindi hiki cha pili 2020 – 2025 kuongeza viwanda vikubwa vya machinjio ya kisasa ambayo yatakuwa na uwezo wa kuongeza idadi ya ngombe na mbuzi ambao watakuwa wanachinjwa kwa wingi hapa nchini.

Meneja Mkuu wa Ranchi ya Nguru Hills Bw. Paul Phillips (kulia) akifafanua jambo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama. Katikati ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo.
Muonekano wa mabwawa yanayojegwa katika Ranchi ya Nguru Hills kwa ajili ya kupokea maji yatakayokuwa yanatoka kwenye machinjio na kutibiwa kabla ya kutumika kwenye kilimo cha Umwagiliaji.


Sehemu ya Mafundi ujenzi wakiendelea na Shughuli za Ujenzi katika Kiwanda hicho cha Machinjio ya Kisasa Nguru Hills kilichopo Mvomero, Mkoani Morogoro.


“Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alizindua kiwanda cha Ngozi cha Taifa cha Ace Leather Industries kilichopo Mahonda na pia Kiwanda cha Kilimanjaro International Leather Industries Co. Ltd ambacho ni kiwanda fungamanishi cha bidhaa za ngozi, uwepo wa viwanda hivyo unaanza kufungua fursa kwa wafugaji hapa nchini,” alisema Mhagama

Sambamba na hayo, Waziri Mhagama alisema kuwa Kiwanda kitatoa fursa ya ajira za zisizopungua 350 na pia kuwezesha wakazi waliokatika maeneo ya karibu na kiwanda hicho kupata mbolea ambayo itatoa fursa kwa vijana kuanzisha shughuli za kilimo ikiwemo cha mbogamboga ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Waziri Mhagama aliwataka waratibu wanaosimamia mradi huo kuhakikisha ifikapo Aprili, 2021 mradi huo unakamilika na kukabidhiwa kulingana na makubalianao ya ujenzi huo.

Kwa Upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Albinus Mgonya alieleza kuwa wilaya ya Mvomero ina mifungo mingi hivyo uwepo wa kiwanda hicho kitatoa fursa kwa wafungaji waliopo kwenye maeneo hayo pamoja na kutoa fursa za ajira kwa wakazi wa mvomero na Mkoa wa Morogoro kwa ujumla.

“Wafugaji hapo awali walikuwa wakiuza mifugo yao kwenye minada ya kawaida lakini sasa wataweza kuuza mifugo yao kwenye kiwanda hiki kwa kuwa na soko la uhakika, pia wakazi wa maeneo haya wataweza kupata ujuzi wa masuala mbalimbali katika kiwanda hicho,” alieleza Mgonya

Naye, Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Ndg. Fortunatus Magambo alihahidi kuhakikisha wanasimamia ujenzi wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati pamoja na ufungaji wa mashine kwa ajili ya kuanza shughuli za uzalishaji.

Pia alieleza kuwa Kiwanda kina lenga kuwa na uzalishaji mkubwa utakao changia katika uchumi wa nchi na kupata faida ili fedha zilizowekezwa na wanachama kuongezeka thamani.

 

HALMASHAURI NAMTUMBO YAMCHEFUA NAIBU WAZIRI MABULA KWA KUANDAA HATI NNE KWA MIEZI NANE


Na Munir Shemweta, WANMM SONGEA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amekerwa na halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma kuandaa Hati za Ardhi nne katika kipindi cha miezi nane tangu kuanzishwa kwa ofisi ya Ardhi mkoa wa Ruvuma.

Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi ameonesha kutoridhishwa na kasi ya utoaji hati katika halmashauri zote za mkoa wa Ruvuma ambapo katika kipindi cha miezi nane halmashauri za mkoa huo zimeandaa jumla ya hati 623.

Akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Ruvuma tarehe 24 Februari 2021 katika kikao kazi cha kuzungumzia masuala ya ardhi na kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi, Dkt Mabula alisema haiingii akilini halmashauri kuandaa hati nne kwa miezi nane huku halmashauri hiyo ikiwa na watendaji wanaolipwa mishahara.

Alisema, katika kuhakikisha halmashauri za mkoa wa Ruvuma zinaongeza kasi ya utoaji hati ni lazima wakurugenzi wa halmashauri hizo kuwawekea malengo watendaji wa sekta ya ardhi ya kuandaa hati zisizopingua tatu kwa wiki kwa kila mtumishi.

‘’Uandaaji hati ufanywe na watendaji wote wa sekta ya ardhi kwa kupeana malengo ya kila mtumishi aandae hati ngapi, kwenye halmashauri  mtumishi anaweza kuanza na kuandaa hati 5 au 3  kwa wiki na mkifanya hivyo mnaweza kuandaa hati nyingi’’ alisema Dkt Mabula.

Taarifa ya Sekta ya ardhi katika mkoa wa Ruvuma iliyowasilishwa na Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa Ildefonce Ndemela ilieleza kuwa, jumla ya hati 623 ziliandaliwa na halmashauri za mkoa wa Ruvuma tangu kuanzishwa ofisi ya ardhi mkoa Machi 2020. Alitaja idadi ya hati zilizoandaliwa kwa kila halmashauri kuwa, ni halmashauri ya wilaya ya Mbinga hati 52, Mbinga Mji 153, Manispaa ya Songea 249, halmashauri ya wilaya ya Namtumbo hati 4, Madaba 16, Songea 34, Nyasa 82 na Tunduru  33.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,  baadhi ya halmashauri katika mikoa mingine zimekuwa zikifanya vizuri katika kuandaa hati ambapo halmashauri mmoja huandaa hati 300 kwa mwezi na kutolea mfano wa halmashauri ya Manispaa ya Ilemela katika mkoa wa Mwanza kuwa imekuwa ikiandaa hati 300 hadi 350 kwa mwezi.

Dkt Mabula aliziagiza idara za ardhi katika halmashauri za mkoa wa Ruvuma kuhakikisha zinampatia taarifa ya utekelezaji maagizo aliyoyatoa yakiwemo makusanyo ya kodi ya pango la ardhi, ufuatiliaji wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi pamoja na utoaji wa hati za ardhi.

Naibu Waziri wa Ardhi  Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameonesha pia kutoridhishwa na hali ya makusanyao ya kodi ya pango la ardhi kwa mkoa wa Ruvuma  ambapo hadi sasa mkoa huo umeweza kukusanya shilingi 740,775,023.00 sawa na asilimia 16 kati ya malengo ya kukusanya bilioni 4.6.

GEKUL AMSIMAMISHA KAZI MKUU WA KITUO CHA UKAGUZI WA MIFUGO RUVU DARAJANI


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul akijadiliana jambo na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo (kushoto) na Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (kulia) alipofanya ziara kukagua Kituo cha Ukaguzi wa Mifugo cha Ruvu Darajani kilichopo Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani jana.

Msimamizi  wa Ujenzi wa Bwawa la Kunyweshea Mifugo la Chamakweza, Robert Baltazar akimuonesha michoro ya bwawa hilo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (wa kwanza kulia) alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa bwawa hilo lililopo Chalinze, Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani jana. Wa pili kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi, Evarist Ndikilo.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Rogers Shengoto akijibu moja ya hoja ziliyoibuliwa katika ziara ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul aliyoifanya Mkoani Pwani. 

 


Na Mbaraka Kambona, Pwani

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul amemsimamisha kazi Mkuu wa Kituo cha Ukaguzi wa Mifugo cha Ruvu Darajani, Gabriel Lyakurwa kwa tuhuma za kutorosha mifugo na kusababisha upotevu wa mapato ya Serikali, huku akimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi, Evarist Ndikilo kuwachukulia hatua Watumishi waliochini ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo ambao walikuwa wanashirikiana na Mkuu huyo wa kituo.   

Gekul alitoa maamuzi hayo baada ya Mkuu huyo wa Mkoa wa Pwani kuibua tuhuma hizo katika ziara yake aliyoifanya kwenye kituo hicho kilichopo Ruvu Darajani, Wilayani Bagamoyo jana. 

Mhandisi Ndikilo alisema uchunguzi alioufanya umebaini kuwa Mkuu wa kituo hicho amekuwa akishirikiana na wenzake wasiowaaminifu kutorosha mifugo inayopelekwa katika kituo hicho kwa ajili ya kukaguliwa kabla ya kuruhusiwa kupelekwa katika maeneo mengine ya minada. 

“Mhe. Naibu Waziri nimefanya uchunguzi wa kina na kugundua kuwa utoroshaji huu unahusisha mtandao wa watu wengi wakiwemo baadhi ya Wananchi, Wafanyabiashara na Watumishi wa Serikali…, kwa mfano tarehe 17 mwezi huu wa pili kuna Magari matano yalileta ng’ombe katika kituo hiki kwa ajili ya kukaguliwa lakini ni gari moja tu lililokwenda Dar es Salaam kama kawaida ilivyo, huku mengine yaliyobaki yakichepushwa na mifugo ilipelekwa Kisarawe, Kibaha na Kijiji cha Kidogozero kinyemela,” alisema Mhandisi Ndikilo. 

Kufuatia tuhuma hizo, Naibu Waziri Gekul alitoa maagizo hayo ya kusimamishwa kazi mkuu huyo wa kituo huku akisema kuwa Wizara itaunda tume maalum kwa ajili ya kwenda kuchunguza tuhuma hizo ikiwemo kupitia mahesabu yote ili kubaini ni kwa kiasi gani mapato ya Serikali yamepotea na wale wote watakaoonekana kuhusika katika upotevu huo watachukuliwa hatua kali. 

"Hatuwezi kucheza na maduhuli ya Serikali, haiwezekani tuwe na ng’ombe zaidi ya milioni 33 lakini mchango wa sekta ya mifugo katika pato la taifa hauzidi asilimia 7, ni kwa sababu ya michezo kama hii, hatutakubali, na tutakwenda kukagua katika maeneo yote ya minada," alisema Gekul. 

Naye, Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete alisema kuwa katika jambo ambalo wamekuwa wakilisemea sana ni kituo hicho kukithiri kwa vitendo vya ubadhilifu ambavyo vimekuwa vikichangia Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kupoteza mapato. 

Ridhiwani alimuomba Naibu Waziri huyo kuhakikisha anachukua hatua madhubuti za kudhibiti vitendo hivyo vya ubadhirifu ikiwemo kuondoa mtandao wote wa waharifu ili halmashauri iweze kupata mapato yanayostahili.

Monday, February 22, 2021

DC IKUNGI AIAGIZA HALMASHAURI KUWAACHIA WANANCHI MASHAMBA YA KUPANDA KOROSHO


Mkuu wa Wilaya ya Ikungi,  Edward Mpogolo (kushoto) akizungumza na wananchi wa Vijiji vya Ulyampiti na Mwau katika eneo lenye mgogoro.
Wananchi wa Vijiji vya Ulyampiti na Mwau wakiwa katika eneo lenye mgogoro.

Na Dotto Mwaibale, Singida

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida, Edward Mpogolo ameagiza Halmashauri  kuwaachia mashamba yao wananchi zaidi ya 36 ambayo walimpa mkulima mmoja mgeni bila ya kufuata utaratibu ili apande korosho.

Katika hatua nyingine Mpogolo ameiagiza halmashauri ya kijiji  na Idara ya Kilimo ya Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kumpatia eneo lingine mkulima huyo ili aweze kuliandaa na kuanzisha kilimo hicho badala ya kuyachukua mashamba ya wananchi hao waliyo yaendeleza na kupanda mazao ya chakula.

Mpogolo amechukua hatua hiyo baada ya kutokea mgogoro wa kugombea mashamba baada ya mkulima mgeni kupewa mashamba ya wananchi waliyoyafyeka na kuyatumia kwa kilimo.

Mpogolo alisema kama halmashauri imetenga eneo hilo kwa kilimo cha korosho ni vyema na wananchi hao wakawezeshwa na wao kunufaika na zao hilo la korosho badala ya kuwafukuza.

Vijiji vilivyokuwa na mgogoro huo ni Ulyampiti na Mwau huku kila upande ukiomba kuangaliwa upya wa mipaka ya maeneo yao ya ardhi.

Mpogolo ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo alitoa agizo hilo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo lililotengwa na Halmashauri ya wilaya hiyo kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo cha zao la korosho.

Aidha mkuu huyo wa wilaya  alisisitiza  kwamba kutokana na mgogoro wa mipaka uliopo katika eneo hilo ni marufuku kwa viongozi wa serikali za vijiji hivyo kuendelea kukata na kugawa maeneo kwa wananchi au wawekezaji wenye ni ya kulima zao hilo la kibiashara bila kufuata taratibu.

“Sasa ndugu zangu pambaneni mlime, wewe ambaye hujapalilia nenda ukapalilie usije ukauwa watoto lakini kwenda kujikatia maeneo  mengine wenyewe ni marufuku kwa sababu kuna mgogoro kwenye maeneo  ya mipaka." alisema Mpogolo. 

Mpogolo alitaja mkulima huyo mgeni aliyepewa ekari 300 kwenye maeneo ya wananchi kutoziendeleza kutokana na  mgogoro uliyopo.

Hata hivyo Mpogolo alitumia fursa hiyo pia kuuagiza uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi kwa kushirikiana na kamati za watu Tisa za ugawaji ardhi na usuluhishi migogoro kutoka katika vijiji vya Mwau na Ulyampiti na kuunda kamati ya kushughulikia mgogoro wa mpaka wa vijiji hivyo. Alisema wakati zoezi hilo likiendelea wananchi kwa upande wao wataendelea na shughuli za kilimo kwenye maeneo yao waliyokuwa wakiyatumia awali.

“Sasa katika kipindi hiki natoa maagizo kwanza kwa mtaalamu  ardhi wa Wilaya kwa kwa kushirikiana na Halmashauri za vijiji vyote viwili mtatengeneza kamati jumuishi na wajumbe tisa kutoka katika kila kijiji kushughulikia mipaka.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye eneo lenye mgogoro wa mipaka baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mwau, walisema kwamba mgogoro huo wa mpaka umetokana na uongozi wa Kijiji cha Ulyampiti kugawa eneo kwa wageni bila kuushirikisha uongozi wa Kijiji cha Mwau.

“Kwa sababu migongano ya mipaka siyo la hapa tu bali wengi  tunagongana kwa sababu ya kutoshirikishana, sasa mimi nakuomba mheshimiwa DC kwa kuwa leo umekanyaga ardhi hii tupe uamuzi kama si watu wa Ulyampiti utuambie kama ni wa Mwau we angalia mwenyewe Ulyampiti mpaka uko wapi na Mwau vile vile? alihoji kwa Shabani  Kijanga.

Thursday, February 18, 2021

MAKAMU WA RAIS SAMIA AJUMUIKA NA WANANCHI WA ZANZIBAR KUMUAGA MAALIM SEIF

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akijumuika pamoja na Wananchi wa Zanzibar katika Sala Maalum ya Kusalia Mwili wa  aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad iliyosaliwa kwenye Viwanja vya Mnazi mmoja Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja  Febuari 18,2021.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiagana na Wananchi mbalimbali wa Zanzibar katika Viwanja vya Mnazi mmoja baada ya kumalizika kwa Sala Maalum ya Kusalia Mwili wa  aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad iliyosaliwa kwenye Viwanja vya Mnazi mmoja Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja  Febuari 18,2021.(Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

 

WAZIRI MKUU AONGOZA MAPOKEZI YA MWILI WA ALIYEKUWA KATIBU MKUU KIONGOZI BALOZI JOHN KIJAZI

 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ameongoza mapokezi ya mwili wa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Mhandisi John William Kijazi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA). Mwili wa marehemu Balozi Kijazi utaagwa Ijumaa Februari 19, 2021 katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam na kisha kusafirishwa kwenda Wilayani Korogwe, Tanga kwa ajili ya mazishi







 

RAIS DKT. MWINYI AJUMUIKA NA WANANCHI KATIKA MAZIKO YA ALIYEKUWA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR MAALIM SEIF SHARIF HAMAD NYALI MTAMBWE PEMBA

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi akitowa mkono wa pole kwa familia ya aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, nyumbani kwao kuifariji familia kabla ya kufanyika kwa mazishi katika Kijiji cha Nyali Mtambwe Wilaya ya Wete Pemba .

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua ikisomwa na Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume (kushoto kwa Rais) wakati alipofika nyumbani kwa marehemu kutowa mkono wa pole kwa familia, kabla ya kuaza kwa mazishi ya aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad yaliofanyika Kijijini kwao Nyali Mtambwe Wilaya ya Wete Pemba na (kulia kwa Rais) Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Pemba) CDR.Mohammed Mussa Seif na Katibu wa Rais Dkt. Abdalla Hasnu Makame

Wananchi wa Pemba wakihudhuria maziko ya aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad yaliofanyika Kijijini kwao Nyali Mtambwe Wilaya ya Wete Pemba

Maofisa wa JWTZ wakiwa wamebeba jeneza likiwa na mwili wa aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad wakiwa katika viwanja vya eneo la kaburi kwa ajili ya mazishi hayo yaliofanyika Kijijini kwao Nyali Mtambwe Wilaya ya Wete Pemba.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi akiweka udongo katika kaburi la aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, wakati wa maziko yake yalifanyika Kijijini kwao Nyali Mtambwe Wilaya ya Wete Pemba

Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi akiweka udongo katika kaburi la aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.Maalim Seif Sharif Hamad, mazishi yaliofanyika Kijijini kwao Nyali Mtambwe Wilaya ya Wete Pemba.

Rais wa Zanzibar Mstaaf Awamu wa Sita Alhajj Dk. Amani Karume akiweka udongo katika kaburi la aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, wakati wa maziko hayo yaliofanyika Kijijini kwao Nyali Mtambwe Wilaya ya Wete Pemba.(Picha na Ikulu)

Tuesday, February 16, 2021

AIRTEL NA DSE WASHIRIKIANA KUPANUA WIGO WA UNUNUZI NA UUZAJI WA HISA NCHNI.


Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania kwa kushirikiana na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), leo imetangaza kuzindua huduma ambayo inawapa nafasi Wateja wa Airtel Money kufungua akaunti zao za biashara, kununua na kuuza hisa, IPO na kupokea malipo kupitia akaunti zao za Airtel Money
 Applikesheni hiyo (MTP) inayojulikana kama ‘Hisa Kiganjani’ imeanzishwa kwa lengo la kurahisisha shughuli za uwekezaji kwa wawekezaji kupatikana moja kwa moja na kuwekeza katika soko la Hisa la DSE. 

Ubunifu huu unatarajiwa kuongeza ufanisi wa kibiashara kwa wawekezaji waliopo sasa na kuongeza wawekezaji wapya ambao kwa sasa hawahudumiwi kwa sababu ya kutopatikana kwa jukwaa la biashara ya dhamana ya DSE.


Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Airtel Money Isack Nchunda amesema kuwa “jukwaa la DSE Mobile Trading ni alama mpya ya kuboresha uzoefu kwa wawekezaji. 

"Soko la Hisa la Dar Es Salaam (DSE) kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ya huduma za kifedha (FSDT) na Serikali imeweza kutengeneza mfumo wakiditali wa Mobile Trading Platform yaani (MTP). Sasa ushirikiano wa DSE na Airtel Money kama mtoa huduma anayeongoza kwa kutoa huduma za fedha kwa njia simu za mkononi, inatoa fursa kwa Watanzania kuwekeza kupata huduma hizi kwa Airtel Money ambapo mteja anaweza akafungua akaunti ya biashara ya Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), akanunua au kuuza hisa pamoja na kupokea malipo.

 “Airtel Money siku zote tumekuwa tukizindua huduma ambazo ni za kiubunifu zaidi ili kutimiza mahitaji ya kila siku ya wateja wetu, kwa mfano sasa wateja wanaweza kufanya malipo na bili tofauti kwa urahisi zaidi na sasa Airtel Money inazindua huduma ya kununua kwa kupitia Airtel Money ambayo ni rahisi salama itawawezesha wateja wa Airtel Money kununua hisa na IPO kupitia Airtel Money kwa urahisi muda wowote ule bila mipaka,  alisema Nchunda huku akiongeza kuwa vijana na wazee sasa wamepata suluhisho wakitaka kuwekeza na wakati huo huo kuokoa muda kadri iwezekanavyo,

 Nchunda alisema ili wateja wa Airtel kufurahia huduma hii, wanatakiwa wafuate njia zifuatazo,
• Piga *152*00#
• Changua malipo ya serikali
• Changua DSE
• Changua nunua hisa
• Changua herufi ya kampuni
• Changua kampuni ya kununua
• Ingiza idadi ya hisa za kununua
• Ingiza bei ya kununua
• Changua dalali wa kununua
• Ruhusu dalali atume tena oda yako
• Changua ndio
• Changua akaunti inayonunua
• Ingiza CSD PIN
• Endelea na malipo
• Changua ndio

 “Airtel tunafuraha kubwa sana kuingia kwenye ushirikiano kama huo ambao unaongeza thamani kwa wateja wake. Tunafurahi kuingia katika ushirikiano na Soko la Hisa la Dar es Salaam. Hii itaongeza thamani kwa huduma zetu zilizopo kwa faida ya wateja wetu, ambapo wateja wetu wataweza kufanya biashara kwa kutumia simu zao za mkononi. 

Kwa kuongezea, katika kuunga mkono ajenda ya serikali kuleta suluhisho la kifedha kupitia kuwezesha malipo ya kidijitali kama hii ya ununuzi wa hisa na IPOs. Natoa wito kwa wateja wetu kutumia huduma  ili kuokoa muda na kuwekeza wakiwa mahali popote wakati wowote.” alisema Nchunda.

Kwa upande wake,  Mkurugenzi wa Baishara  wa DSE Ibrahim Mshindo   ilisema kuwa Hisa Kiganjani inalenga kurahishisha kazi ya uwekezaji pamoja na wawekezaji kupitia kukuza upatikanaji wa moja kwa moja wa jukwaa la soko la hisa la DSE. 

Ubunifu huu wa Hisa Kiganjani ni imani yetu kuwa utaongeza ufanisi zaidi kwenye biashara kwa wawekezaji waliopo na kuleta wawekezaji wapya, ambao kwa sasa hawakupata nafasi ya kununua hisa zaidi au kuhudumiwi kwa sababu ya kutopatikana kwa jukwaa kama hili la DSE.

 Aliongeza kuwa la "DSE Hisa Kiganjani App na USSD" lina huduma za usalama ambazo zinaruhusu wateja kufanya shughuli salama. 

'Hisa Kiganjani ina faida kadhaa ambazo ni pamoja na, upatikanaji rahisi wa bidhaa na huduma, kupunguza gharama za usafiri na upatikanaji wake kwa urahisi, itaongeza uwazi na usalama wa wawekezaji.

 Alisema kuwa ili mtu apate sifa ya kununua hisa ni lazima awe Mtanzania, anapaswa kuwa na Kitambulisho cha Taifa cha NIDA, anapaswa kujiandikisha kwa DSE kupitia simu kwa ussd au Applikesheni  ya DSE na mwisho awe na Airtel Money akaunti yenye fedha.

Monday, February 15, 2021

WAZIRI BASHUNGWA KUKUTANA NA WANAMUZIKI ZAIDI YA 500 HOTELI YA MOUNT MERU JIJINI ARUSHA


Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa.

Katibu Mkuu wa wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO), , Stella Joel.
Wasanii wa Kikundi cha Sanaa cha Dofa kutoka Karatu ambao wataimba wimbo maalumu kwenye kongamano hilo.
 


Na Dotto Mwaibale


Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa anatarajiwa kukutana na wanamuziki zaidi 500 katika kongamano la fursa litakalofanyika Jumamosi Hoteli ya  Mount Meru jijini Arusha.

Katika kongamano hilo baadhi ya wanamuziki watakabidhiwa kadi za bima ya afya ya Taifa (NHIF) na Bashungwa ambaye anatarajiwa  kuwa mgeni rasmi.

  "Wanamuziki watakao pata kadi hizo ni wale ambao wametimiza vigezo kama walivyoeleza Rais wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO), Eric Kisanga na Katibu Mkuu wa umoja huo, Stella Joel ambao ndiyo waandaaji wa kongamano hilo.

Baadhi ya wanamuziki watakao kabidhiwa kadi hizo wametajwa kuwa ni mwanamuziki mkongwe hapa nchini, Kida Waziri,  Emmanuel Mbasha, Madamu Flora, Goodluck Gozibeth, Stara Thomas, Hafsa Kazinja Renatha Sedekia na Rehema Tajiri.

Akiwazungumzia Wanamuziki hao Katibu Mkuu wa TAMiUFO Stella Joel alisema wanaishukuru Serikali kwa kuwakumbuka kuwapatia kadi hizo ambazo zitawasaidia kupata vipimo na matibabu katika hospitali za Serikali na binafsi.

Joel alisema kabla ya hapo wanamuziki wengi wamekuwa wakipoteza maisha kwa kushindwa kumudu gharama za vipimo na matibabu.

" Kwa hatua hii iliyochukuliwa na Serikali ya awamu ya tano hakika wanamuziki wote tunakila sababu ya kuipongeza  kwa kutekeleza ahadi yake kwa vitendo ya kutusaidia wasanii" alisema Joel.

Rais wa TAMUFO,  Eric Kisanga alisema kongamano hilo ni la kipekee kwani litawahusisha wanamuziki wa kada zote  na kuwa maandalizi yote yamekwisha kamilika.

" Maandalizi yote ya kongamano letu ili la fursa kwa wanamuziki yamekwisha kamilika kwa asilimia kubwa na sasa tupo kumalizia mambo madogo yaliyosalia" alisema Kisanga.

Kisanga alitumia fursa hiyo kuwakaribisha kwenye kongamano hilo wananchi, wasanii  na wadau wengine wa muziki  na kuwa halitakuwa na kiingilio ni bure. 

Sunday, February 14, 2021

UHABA WA WATAALAMU WENYE UJUZI KILIO KWA WAWEKEZAJI


Mkuu wa Kiwanda cha Kutengeneza Chanjo cha Hester, Dkt. Umapati Dasgupta (kulia) akimueleza jambo Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) alipotembelea kukagua kiwanda hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani jana.

  • Mtaalam wa Kuendesha Mitambo katika Kiwanda cha Kutengeneza Chanjo cha Hester, Geofrey Mahende (kulia) akitoa maelezo ya namna anavyofanyakazi yake kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto)alipotembelea kukagua kiwanda hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani jana.
  • Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wataalam wa Kitanzania wanaofanyakazi katika Kiwanda cha kutengeneza Chanjo cha Hester alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Mkoani Pwani jana. Wa kwanza kushoto ni Mratibu na Mkurugenzi wa Operesheni, Tina Towo Sokoine.

  • Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akibadilishana mawazo na Mkuu wa Kiwanda cha Kutengeneza Chanjo cha Hester, Dkt. Umapati Dasgupta (kushoto) muda mfupi baada ya kumaliza kutembelea kiwanda hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani jana.

     


    Na Mbaraka Kambona, Pwani

    Mratibu na Mkurugenzi wa Operesheni, Kiwanda cha Kutengeneza Chanjo cha Hester, Tina Towo Sokoine amesema kuwa lengo la kiwanda hicho ni kutumia Wataalamu wa ndani lakini uhaba wa Wataalam wa masuala ya sayansi wenye ujuzi hasa wa vitendo unaelekea   kukwamisha dhamira yao hiyo. 

    Towo aliyasema hayo alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa kiwanda hicho kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani jana. 

    Alisema kuwa kwa sasa wana wataalamu watatu tu kutoka nje nchi ambao wamewaajiri katika Kiwanda hicho lakini   kwa hali ilivyo wanaona watashindwa na labda wanaweza kuomba vibali vingine vya kuajiri wataalamu kutoka nje. 

    “Nia yetu ni kufanyakazi na Watanzania tu lakini bado vijana wengi tunaowafanyia usahili wanakosa ujuzi hasa wa vitendo, tunaiomba Serikali na Vyuo vinavyoandaa hawa Wataalam kuhakikisha wanajikita katika elimu ya vitendo na sio nadharia peke yake ili kukidhi mahitaji ya sasa na kulinda ajira za Watanzania,” alisema Towo 

    Kuhusu uzalishaji, Towo alisema kuwa wanatarajia kuzalisha chanjo ya kwanza mwezi wa nne mwaka huu, huku akiiomba Serikali kuona uwezekano wa taasisi zinazohusika na kusimamia uwekezaji kuunganishwa ziwe na lugha ya pamoja ili kumfanya muwekezaji aweze kupata huduma zote sehemu moja bila kuhangaika kama ilivyosasa. 

    Naye Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel aliutaka Uongozi wa Kiwanda hicho  kuhakikisha wanazalisha chanjo zenye ubora ili nchi iweze kuondokana na utegemezi wa chanjo na bidhaa nyingine za mifugo kutoka nchi za nje. 

    “Lengo la Wizara ni kuhakikisha kuwa nchi inaondokana na uagizaji wa chanjo kutoka nje, tunatamani kuwa na chanjo tunazoweza kudhibiti ubora wake na tuwe na uhakika nayo, hivyo uwepo wa kiwanda hiki kutatusaidia kuzalisha chanjo hapa hapa nchini ili kukidhi mahitaji ya Wafugaji wetu na Watanzania kwa ujumla,” alisema Prof. Ole Gabriel. 

    Aliongeza kwa kusema kuwa Serikali inaweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili mahitaji ya wafugaji na wananchi yawe yanashughulikiwa ndani ya  nchi. 

    Aidha, Prof. Ole Gabriel aliwaomba Wafugaji na Watanzania kuanza kujenga utamaduni wa kuthamini bidhaa za ndani na waondokane na ile dhana ya kwamba bidhaa bora ni ile inayotoka nje, wakithamini vya ndani wataongeza pato la Taifa na kukuza uchumi wa nchi.

    Thursday, February 11, 2021

    NAIBU WAZIRI KATAMBI AZINDUA BARAZA LA WAFANYAKAZI WCF


    Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana), Mhe. Patrobas Katambi amezindua Baraza la Wafanyakazi Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na kutoa wito kwa wafanyakazi kuchapa kazi kwa bidii kwani ndio nguzo kuu katika mafanikio ya Mfuko.

    Mhe. Katambi ameyasema hayo mjini Morogoro  Februari 10, 2021 wakati akizindua baraza la Wafanyakazi WCF kwenye ukumbi wa Magadu.

    “Lazima tujue uwajibikaji ni nguzo kuu ya mafanikio katika sehemu yoyote ya kazi, hivyo wajumbe mnaowawakilisha wafanyakazi wa Mfuko mnapaswa kuwahimiza wenzenu kuhusu  swala hilo.” Alifafanua  Mhe. Katambi.

    Alisema Serikali inatambua mchango wa wafanyakazi wote nchini lakini vile vile inatambua sana  na kuheshimu mchango wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi katika kukuza uchumi wa nchi yetu kwa kuhakikisha kuwa nguvu kazi ya wafanyakazi wanaougua au kuumia kutokana na kazi haipotei kwa wakati wote kupitia huduma ya matibabu inayotolewa kwa waathirika.

    “Napenda niwahakikishie kuwa Serikali ya awamu ya tano inaendelea kushirikiana na Mfuko katika kuhakikisha unanufaisha watu walio wengi na kufanikisha malengo ya kuanzishwa kwake.”

    Naibu Waziri Katambi pia aliupongeza Mfuko huo kwakuwa na wafanyakazi wachache lakini waliouwezesha Mfuko kupiga hatua kubwa katika utekelzaji wa majukumu yake.

    “Mnatupa heshima kubwa sana Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Waziri mama Jenista Mhagama, tangu mmeanza kutekeleza majukumu haya mmeanzia ziro baada ya mwaka mmoja mkalipa shilingi bilioni 1.5 na bado mnaendelea kufanya vizuri kwakweli habari hizi zilifurahisha na hata kamati ya bunge ilishukuru na kuwapongeza hongereni sana sana.” Alisema Mhe. Naibu Waziri Katambi.

    Alisema hata baadhi ya wajumbe wa kamati ya Bunge wametoa ushuhuda jinsi Mfuko huo umekuwa ukihudumia vema katika suala la fidia na HUDUMA za utengamao (rehabilitation aervices).

    Awali Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi Bw. Masha Mshomba alisema katika kipindi cha miaka sita ya uhai wa Mfuko kumekuwepo na mafanikio kadhaa chini ya nguvu kazi ya wafanyakazi 129 ambao wameweza kutekelza vema majukumu yao

    “Sambamba na hilo tumekuwa tukiwapatia mafunzo ya mara kwa mara ili kuongeza weledi katika utendaji wa kazi.” Alifafanua Bw. Mshomba.

    Bw. Mashomba pia alisema miongoni mwa maeneo ambayo Mfuko umeboresha sana HUDUMA zake  ni kuweka mfumo wa utoaji taarifa kwa njia ya mtandao.

    “Huduma zetu hivi sasa zinatolewa kwa kiasi kikubwa sana kwa njia ya mtandao karibu asilimia 85 ya shughuli zetu, kujisajili, kuwasilisha michango, uchatakati wa malipo lakini pia muhimu zaidi ni kutoa taarifa pale mfanyakazi anapougua au kupata ajali ya kikazi na hata inapotokea bahati mbaya akafariki kutokana na kazi tumeweka mfumo mzuri unaowezesha taarifa hizo kutufikia kwa haraka kupitia mtandao.” Alifafanua Bw. Mshomba.

    Alisema Mfuko unatambua kuwa nchi ni kubwa na sio sehemu zote mtandao unapatikana kwa urahisi hivyo Mfuko umefungua ofisi za kikanda, kuna ofisi Makao makuu ya Serikali Dodoma, Mbeya, Arusha, Morogoro, Mtwara na mwisho wa mwaka huu wa fedha Mfuko utafungua ofisi kwenye mikoa ya Tabora, Geita na Shinyanga hususan maeneo ya migodi kama Kahama.

    “Ukiacha hayo Mfuko wetu kifedha tumejenga uwezo wa kutosha kwa mujibu wa hesabu zilizokaguliwa na CAG tarehe 30/06/2020 tulikuwa na ukubwa wa thamani (Assets) wa Bilioni 333, lakini pia hesabu ambazo hazijakaguliwa na CAG hadi Desemba 2020 tumefikia bilioni 389.” Alifafanua Mkurugenzi Mkuu Mshomba.

    Lakini pia Mfuko umeboresha sana huduma za tathmini kwa kutoa mafunzo kwa madaktari wapatao 1,085 ambao ndio wanaofanya kazi ya kutathmini pale mfanyakazi anapougua au kuumia kutokana na kazi.

    Naye Katibu Mkuu wa  chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Bw. Heri Mkunda alisema Mafanikio yaliyopatikana WCF ni kutokana na wafanyakazi kufanya kazi kwa kujituma kushauri vizuri uongozi na kushirikishwa katika masuala mbalimbali yanayohusu taaisi.

    “Niipongeze Menejimenti na kuwaomba waajiri wengine kujifunza kutoka WCF, hawa wafanyakazi ndio walio jikoni wanaweza kushauri vizuri kuhusu masuala mbalimbali inayohusu taasisi ili kufikia malengo.”

    Awali kabla ya uzinduzi wa baraza hilo, wajumbe walifanya uchaguzi wa kuchagua Katibu wa Baraza na Katibu Msaidizi, ambapo Bw.Mbarikiwa Masinga alichaguliwa kuwa Katibu wa Baraza na Bi.Irine Mngure alichaguliwa kama Katibu Msaidizi.

    Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana, Mhe. Patrobas Katambi (kulia) akipeana mikono na MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa WAFANYAKAZI (WCF) Bw. Masha Mshomba Mara baada ya kuzindua Baraza la Wafanyakazi wa Mfuko huo mjini Morogoro Februari 10, 2021. Anayeshuhudia ni Karibu Mkuu wa TUGHE Bw. Heri Mkunda
    Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana), Mhe. Patrobas Katambi, akitoa hotuba ya uzinduzi. Kulia ni MKURUGENZI Mkuu wa WCF, Bw. Masha Mshomba.
    Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana), Mhe. Patrobas Katambi, akitoa hotuba ya uzinduzi.

    Baadhi ya wajumbe wa baraza la Wafanyakazi WCF wakishangilia kwa kupiga makofi.
    Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Masha Mshomba (wapili kulia) akimkabidhi Katibu wa Baraza Hilo Bw.Mbarikiwa Masinga Mkataba Kati ya Baraza na Menejimenti huku Katibu Msaidizi Bi. Irine Mngure akishuhudia.
    Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana), Mhe. Patrobas Katambi, (katikati) na Karibu wa Baraza la Wafanyakazi WCF, Bw. Mbarikiwa Masinga wakimsikiliza MKURUGENZI Mkuu wa WCF Bw. Masha Mshomba wakati akitoa hotuba take.
    Baadhi ya wajumbe wa baraza Hilo wakifuatilia kikao
    Baadhi ya wajumbe wa baraza Hilo wakifuatilia kikao
    Baadhi ya wajumbe wa baraza Hilo wakifuatilia kikao
    Baadhi ya wajumbe wa baraza Hilo wakifuatilia kikao
    Baadhi ya wajumbe wa baraza Hilo wakifuatilia kikao
    Baadhi ya wajumbe wa baraza Hilo wakifuatilia kikao
    Baadhi ya wajumbe wa baraza Hilo wakifuatilia kikao
    Baadhi ya wajumbe wa baraza Hilo wakifuatilia kikao
    Baadhi ya wajumbe wa baraza Hilo wakifuatilia kikao
    Bw. Julius Lwenje akizungumza wakati wa uzinduzi huo
    Mhe. Katambi (kulia) na Bw. Mshomba wakiimba wimba was solidarity forever
    Mgeni rasmi akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya WCF.

    Picha ya pamoja ya wajumbe na mgeni rasmi