Matokeo chanyA+ online




Wednesday, February 10, 2021

CHIKOTA ASHAURI MAMBO MATATU KATIKA KILIMO CHA KOROSHO

Mbunge wa Nanyamba Abdallah Chikota ameishauri serikali kuzingatia mambo matatu katika kuendeleza kilimo cha Korosho ikiwemo kuondoa tozo na kodi zilizopo wakati wa uingizaji wa mashine za kubangua korosho ili mashine nyingi ziweze kuingizwa nchini.

Aidha ameshauri kuwekwa kwa vivutio maalum kwa wawekezaji wapya na kuondolewa kwa kodi na tozo katika vifungashio.

Akichangia mpango wa kitaifa wa maendeleo wa mwaka 2021/2022 na mpango wa tatu wa maendeleo wa miaka mitano 2021/2022 hadi 2025/2026 februari 10 jijini Dodoma,Chikota amesema ushauri huo ukizingatiwa itapunguza gharama na hivyo kupata wawekezaji wengi wan je na ndani.

“Suala la ubanguaji ndio njia pekee ya kuhakikisha korosho inapata bei nzuri kwenye soko la dunia na korosho yetu ni mkakati ambao tulianza nao huko nyuma,lengo ni kuweka Oxport levy ili wasafirishe korosho ghafi,”amesema.

Amesema uwezo wa kubangua korosho katika viwanda vyetu ni kama tani 70,000 na sasa hivi wanazalisha kama tani 120,000 na korosho nyingi inauzwa ikiwa ghafi.

“Mheshimiwa Mwenyekiti mimi nashauri tukose fedha kidogo leo ili tupate fedha nyingi baadae hii itawezekana kama tutaondoa tozo na kodi zilizopo wakati wa uingizaji wa mashine za kubangua korosho ili mashine nyingi ziweze kuingizwa,”aliongeza.

Amesema kiwanda kidogo cha ubanguaji mtaji wake ni kama milioni 60 na kwa sababu Korosho inalimwa katika mikoa zaidi ya 12 hivyo badala ya kutoa zile fedha za mfuko wa vijana kwa kijana mmoja mmoja wanaweza kuanzisha viwanda vidogo vya kubangua korosho na vikaongeza ajira pia kwa wanawake na thamani ya fedha itaonekana.

Ameongeza kuwa “Wenzetu  wa Vietnam na India wanatumia sana Korosho zetu  kuongeza ajira kwao na mipango hii wakiisikia watakuwa na hofu na korosho ghafi haitaenda kwao,sasa tuwekeze katika ubanguaji ili tuongoze ajira,

Akizungumzia kuhusu mradi wa Mchuchuma na Liganga amesema wakati umefika wa kuweka fedha za kutosha sambamba na ujenzi wa reli kutoka Mtwara Mbababay ili kuweza kupata fedha za kutosha kuwekeza kwenye reli ya kusini na hivyo kuwezesha bandari ya Mtwara kutumika ipasavyo kusafirisha tumbaku na kuwezesha nchi nyingine ya Malawi Zambia na DRC Congo kutumia reli hiyo.

No comments:

Post a Comment