Matokeo chanyA+ online




Friday, April 30, 2021

MKUTANO MKUU MAALUMU WA CCM WAMCHAGUA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN KUWA MWENYEKITI WA CCM LEO JIJINI DODOMA

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiagana na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete mara baada ya Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika leo tarehe 30 Aprili, 2021 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre Jijini Dodoma.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha na Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi pamoja na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete mara baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM baada ya kupigiwa kura zote za Ndiyo na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika leo tarehe 30 Aprili, 2021 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre Jijini Dodoma.




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwa katika Mkutano Mkuu wa CCM ambao Wajumbe wake Walimchagua kwa Kura zote za Ndiyo kuwa Mwenyekiti Mpya wa CCM leo tarehe 30 Aprili, 2021 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre Jijini Dodoma.



Mkutano Mkuu Maalum wa Chama cha Mapinduzi (CCM) umempitisha Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mwenyekiti wa Sita wa CCM kwa  kura za ndiyo 1862 sawa na asilimia 100.

Rais Samia amechaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya kufuatia kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho na Rais wa Tanzania, Hayati Dk John Magufuli kilichotokea Machi 17 2021, jijini Dar Es Salaam mwaka huu.

Akitangaza matokeo hayo, Mwenyekiti wa uchaguzi huo ambaye pia ni Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema kura zilizopigwa ni 1,862 ambapo kura za ndiyo zilikua  zote 1,862 ikiwa ni asilimia 100 ya kura zote.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwa katika Mkutano Mkuu wa CCM ambao Wajumbe wake Walimchagua kwa Kura zote za Ndiyo kuwa Mwenyekiti Mpya wa CCM leo tarehe 30 Aprili, 2021 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre Jijini Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwa ameshikilia Tuzo yake ya Heshima na Pongezi aliyopewa na Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi Tanzania (UWT) mara baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti Mpya wa CCM leo tarehe 30 Aprili, 2021 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre Jijini Dodoma.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya Heshima kutoka kwa Mwenyekiti wa UWT Gaudensia Kabaka mara baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM leo tarehe 30 Aprili, 2021 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre Jijini Dodoma.



 
 

Viongozi mbalimbali pamoja na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi wakifurahia ndani ya Ukumbi wa Mkutano wa Jakaya Kikwete Convention Centre mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM leo tarehe 30 Aprili, 2021 Jijini Dodoma. PICHA NA IKULU

 


 

WAZIRI MKUU MAJALIWA: SERIKALI ITAYAFANYIA KAZI MALALAMIKO YA UKAGUZI MIRERANI


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imepokea na itayafanyia kazi  malalamiko ya wabunge juu ya utaratibu  wa ukaguzi unaofanywa kwenye mgodi wa  Mererani,

 

“Nimesikia concern ya namna ukaguzi unavyoendelea pale katika mgodi wa Mirerani, nilipanga kutembelea Mirerani ili kuona hali hiyo na kutafuta ufumbuzi, nikuahidi Mhe. Spika na waheshimiwa wabunge kwamba tumepokea na Serikali tutalifanyia kazi,” amesema.

 

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Aprili 29, 2021) wakati akijibu hoja ya Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka ambaye ambaye alitaka maelezo juu ya utaratibu wa ukaguzi katika mgodi huo. Mbunge huyo alikuwa akichangia mjadala wa hotuba makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini.

 

Amesema Serikali inapata fedha nyingi kupitia madini ya Tanzanite yanayochimbwa katika mgodi huo hivyo haiwezi kushindwa kununua mtambo unaoweza kufanya ukaguzi wenyewe bila kusumbua mtu.

Thursday, April 29, 2021

WANAFUNZI TGC WAFURAHIA UJUZI WANAOUPATA


 

Wanafunzi wa sayansi ya madini ya vito kutoka kituo cha Jemolojia Tanzania kilichopo mkoani Arusha wamesema elimu ya uongezaji thamani madini wanayoipata kupitia kituo hicho inawapa uhakika wa maisha yao ya badaye kutokana na kuwa na wigo mpana wa kujiajiri na hata kuajiriwa.

 

Akizungumza wakati wa mahojiano na maafisa habari kutoka Idara ya Habari Maelezo waliofika kituoni hapo ili kujionea mwenendo mzima wa mafunzo hayo, mwanafunzi Lightness Makundi alisema elimu anayoipata inamsaidia katika kutambua na kuthaminisha aina za madini ya vito, itamsaidia kutambua madini halisi na madini fake na hivyo kutopata hasara endapo ataamua kujiingiza katika kufanya biashara ya madini mara baada ya kuhitimu mafunzo hayo.

 

Amesema elimu ya sayansi ya madini ya vito ina uwanja mpana wa kujiajiri ikiwa ni kujiajiri katika masuala ya ukataji, ung’arishaji, usonara pamoja na biashara ya madini hivyo anaiona fursa kwa upana pindi atakapoamua kujiajiri. Amesema, Manufaa ya elimu hii ni kubwa sana kwenye biashara ya madini.

 

Aidha, amewaasa watanzania hususani vijana kutokujihusisha na biashara ya madini ya vito pasipokuwa na uelewa wa kutambua na kuthaminisha madini hayo kwani kufanya hivyo kutapelekea kupata hasara na kupoteza mtaji anaotaka kuwekeza kwani anaweza kuuziwa madini yasiyo halisi kutokana na uwepo wa kundi kubwa la wafanyabiashara wa madini wasiokuwa waaminifu.

 

“Serikali imewekeza pesa nyingi kwenye kituo hiki ili kutusaidia kupata uwelewa wa madini ya vito, ni vema tuichukue hii kama fursa kwa kujitokeza kwa wingi kusoma kuliko kufanyabiashara pasipokuwa na elimu hii muhimu” alisisitiza.

 

Akizungumzia manufaa anayoyapata kutokana na elimu ya sayansi ya madini ya vito Eva Mowo alisema kutokana na kuwa yeye ni mwajiriwa ndani Sekta ya Madini, elimu anayoipata itakwenda kuongezea nguvu miongoni mwa watumishi wengine wanaojikita katika suala zima la uthaminishaji na utambuzi wa madini ya vito.

 

Amewataka watanzania wengine wenye maono ya kujihusisha na biashara ya madini pamoja na uongezaji thamani wa madini ya vito na miamba kujiandikisha katika kituo hicho ili kupata ujuzi kutokana na chuo kuwa na mazingira rafiki ya kujifunzia pamoja na vifaa vya kutosha vilivyowekezwa na serikali kwa lengo la kuifanya sekta ya madini kuongeza tija kwa wazawa tofauti na ilivyokuwa awali kuwa madini yalikuwa yakinufaisha mataifa mengine ya nje kupitia ajira za uthaminishaji, utambuzi na ukataji wa madini ya vito.

 

Akizungumzia hatua zinazopitiwa katika suala zima la utambuzi wa madini halisia na yasiyo halisi Mjemolojia Eusebi Bernard amesema utambuzi wa madini unapitia hatua kadhaa zikiwemo upimaji wa uzito (specific gravit), upitishaji wa mwanga(polarization), hadubini (Microscope) pamoja na upimaji wa refractive index.

 

Kwa Upande wake, Mkuu wa Idara ya Mafunzo Ester O. Njiwa, amesema chuo hicho kinadahili watu wa rika zote ikiwa ni pamoja na wenye elimu ya msingi pamoja na wasomi kwa ngazi ya shahada pia kinadahiri wafanyakazi katika kada mbalimbali wenye nia ya kupanua uelewa katika tasnia ya Elimu ya Sayansi ya Madini ya Vito na Miamba.



WATOTO, WAZEE WASIOJIWEZA KUPATA HUDUMA BORA - DKT JINGU


 



Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, anayeshughulikia Maendeleo ya Jamaii Dkt. John Jingu amesema Wizara hiyo itahakikisha inatekeleza kikamilifu agizo la Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan la huduma kwa makundi maalum ya watoto na Wazee  wasioniweza.

Dkt. Jingu ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam alipotembelea makazi ya Watoto na Wazee wasiojiweza ya Mama theresa yaliyoko Mburahati.

Amesema Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambayo ina dhamana na Wazee na watoto itahakikisha inatekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati akihutubia  taifa kupitia Bunge jijini Dodoma.

“Mimi ndio mtumishi Mkuu kwenye eneo hili na kazi yangu kubwa ni kuhakikisha kwamba maelekezo ya Rais aliyoyatoa wakati akihutubia taifa Bungeni hivi karibuni, yanatekelezwa kwa kasi kubwa” alisisitiza Dkt. Jingu

Ameyahakikishia makundi hayo maalum ya Watoto na Wazee wasiojiweza kuwa wao ni moja ya vipaumbele vya Serikali ya awamu ya sita katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake Flora Emmanuel ameeleza kufarijika kutokana na hatua zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya sita kwa kuhakikisha walengwa hao wanaishi katika mazingira bora.

“umetuletea ujumbe mzuri,sio kwetu sisi tu humu ndani bali hata nje. Mwenyezi Mungu akupe baraka na nguvu ya kufanya kazi,” alisema Flora

Akihutubia Taifa kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 22 Aprili, mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan aliweka bayana vipaumbele vya Serikali katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma kwa makundi maalum zikiwemo huduma kwa watoto na Wazee wasiojiweza.



MIFUGO YA TANZANIA YAHITAJIKA VIETNAM - WAZIRI NDAKI



Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiagana na Balozi wa Vietnam nchini Tanzania Mhe. Nguyen Nam Tien, wakati balozi huyo alipofika katika ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ili kuimarisha mahusiano baina ya Tanzania na Vietnam ambapo katika Sekta ya Uvuvi, Waziri Ndaki amemuomba Balozi Tien kuwakaribisha wawekezaji kutoka Vietnam ili waje hapa nchini kuwekeza katika ufugaji wa samaki wa kutumia vizimba na mabwawa kutokana na nchi ya Vietnam kufanya vizuri katika sekta hiyo. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiwa kwenye picha ya pamoja na Balozi wa Vietnam nchini Tanzania Mhe. Nguyen Nam Tien, wakati balozi huyo alipofika katika ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ili kuimarisha mahusiano baina ya Tanzania na Vietnam. Katika mazungumzo yao Balozi Tien amewakaribisha wafanyabiashara wa Tanzania kusafirisha mifugo na nyama nchini Vietnam kutokana na nchi hiyo kuwa na uhitaji mkubwa wa nyama. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akifafanuliwa jambo na Balozi wa Vietnam nchini Tanzania Mhe. Nguyen Nam Tien, wakati balozi huyo alipofika katika ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ili kuimarisha mahusiano baina ya Tanzania na Vietnam. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
 

Na. Edward Kondela

Balozi wa Vietnam nchini Tanzania Mhe. Nguyen Nam Tien amesema atawasilisha serikalini vigezo vinavyopaswa kufuatwa na wafanyabishara wa hapa nchini ili waweze kusafirisha mifugo na nyama kwenda nchini Vietnam, kutokana na nchi hiyo kuwa na uhitaji mkubwa wa nyama.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amebainisha hayo leo (28.04.2021) ofisini kwake katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, mara baada ya kuwa na mazungumzo mafupi na balozi huyo aliyefika ofisini kwa Waziri Ndaki ili kuimarisha mahusiano baina ya Tanzania na Vietnam na kupeana uzoefu katika sekta za mifugo na uvuvi.

 Ndaki amesema Balozi Tien amesema nchi ya Vietnam ina uhitaji mkubwa wa nyama kwa kuwa wana ng’ombe wasiozidi Milioni Sita hivyo kutoa fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kuchangamkia fursa hiyo endapo watakidhi vigezo vya kusafirisha mifugo na nyama nchini humo.

“Tunaweza kutumia fursa hii kusafirsha ng’ombe au nyama na kwamba wataleta orodha ya vitu vinavyohitajika ili kama nchi tuweze kupeleka ng’ombe au nyama.” Amesema Mhe. Ndaki

Aidha, Waziri Ndaki amewaomba wawekezaji kutoka Vietnam kuwekeza hapa nchini katika viwanda vya maziwa kwa kuwa maziwa yaliyopo bado ni mengi kulinganisha na viwanda vilivyopo, pamoja na kuwekeza katika viwanda vya kuchakata ngozi za mifugo kwa kuwa kiasi kikubwa cha ngozi kimekuwa kikiharibika.

Kuhusu Sekta ya Uvuvi, Waziri Ndaki amesema amemuomba Balozi wa Vietnam hapa nchini Mhe. Nguyen Nam Tien kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini humo ili kuja kuwekeza katika ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba na mabwawa kwa kuwa nchi hiyo inafanya vizuri katika sekta hiyo.

Amefafanua kuwa lengo la serikali ya Tanzania ni kuwekeza zaidi katika ufugaji wa samaki ili idadi ya samaki wanaopatikana kwa njia ya maji ya asili kwa maana ya kwenye Bahari ya Hindi, maziwa na mabwawa iweze pia kupatikana kwa njia ya ufugaji wa kutumia vizimba na mabwawa.

“Tumewaomba kupata utaalamu wao wa ufugaji samaki, lakini pia kama tunaweza kupata wawekezaji kutoka kwao, tuna fursa kubwa na kama wizara tunataka tupate samaki nusu wanaotoka kwenye maji ya asili na nusu wengine wapatikane kwa njia ya kufuga.” Amesema Mhe. Ndaki.

BAKITA TANGAZENI KISWAHILI NJE YA NCHI - GEKUL

Na Grace Semfuko,MAELEZO.

 Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo  Pauline Gekul amelitaka Baraza la Kiswahili Tanzania-BAKITA kufanya jitihada za kiuza nje ya nchi lugha ya Kiswahili ili iweze kujulikana kwa haraka na kuleta tija ya kiuchumi kutokana na kuzalisha ajira pamoja na ada na tozo mablimbali za ufundishaji wa lugha hiyo.

Amesema ipo haja kwa BAKITA kuwasiliana na Balozi mbalimbali zinazoiwakilisha Tanzania zinazoiwakilisha Tanzania nje ya nchi ili ziweze kutenga vyumba vya madarasa ya kufundishia lugha hiyo adhimu Barani Afrika.

 Wito huo ameutoa wakati wa ziara yake katika ofisi za baraza hilo huku akisisitiza kuwa, zoezi hilo lianze mara moja kwani wanaonufaika sasa na lugha hiyo, ni watu wa kutoka nchi jirani ambazo hajimudu kuzungumza na kufundisha Kiswahili fasaha kama ilivyo kwa waasisi wa lugha hiyo ambao ni Watanzania.

 “Kama kuna kitu mnatakiwa kukifanya sasa ni kukiuza kiswahili nje ya nchi badala ya kuachia majirani zetu wakiuze, wakati sisi ndio hasa tuna kiswahili fasaha kuliko wao ambao wanakiuza na kunufaika sana, hapo kwa kweli BAKITA tunakwama, tena mpendwa wetu Hayati Dkt. John Pombe  Magufuli aliturahisishia sana,  tuliona jinsi alivyokuwa na mchango mkubwa wa kuitangaza lugha hii Duniani, na Dunia wanatambua mchango wake” amesema.

 Ameitaka BAKITA kutoa mafunzo ya lugha ya Kiswahili na istilahi zake kwa watu wa fani za ushereheshaji na ukalimani ambao wanaweza kutumika katika kuikuza lugha hiyo huku akisisitiza uharakishaji wa uagizaji wa vifaa vya kutafsiria lugha mbalimbali za kimataifa kwenda katika lugha ya Kiswahili.

 “Mlisema mnaagiza vyombo ambavyo vitawasaidia katika tafsiri ya lugha mbalimbali, harakisheni hilo, pia ni vyema mkaanzisha mafunzo kwa washereheshaji wetu na wakalimani, hawa wanatumia Kiswahili zaidi na wanaweza wakatumika katika kukikuza zaidi Kiswahili, wanaweza kuwa kwenye matukio ya kiserikali au ya kijamii, wapewe mafunzo na istilahi mbalimbali za kuwawezesha kukitangaza Kiswahili” amesema Gekul.



NAIBU SPIKA AZINDUA UMOJA WA WATU WA MBEYA NA SONGWE UWAMBESO DODOMA



Mbunge wa Mbeya Mjini ambaye ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Mbeya, Dkt. Tulia Ackson akishirikiana na wabunge kutoka Mbeya na Songwe kuzindua Umoja wa Watu wa Mbeya na Songwe wanaoishi Dodoma (UWAMBESO) jijini Dodoma. Umoja huo ambao umesajiliwa rasmi Oktoba 2021 una wanachama 142.

Kutoka kushoto ni  Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Songwe, Neema Mwandabila, Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi na kutoka kulia ni Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Wazazi, Bahati Ndingo, Katibu Mkuu wa Uwambeso, Baleke Moses na Mwenyekiti wa  umoja huo, Nsubi Bukuku. 

Wabunge kutoka mikoa hiyo wamehidi kuchangia sh. mil. 9 kutunisha mfuko wa Uwambeso pamoja na kujiunga uwanachama. 

Katika hafla hiyo uongozi uliwakabidhi vyeti waasisi na na viongozi waanzishilishi wa umoja huo ikiwa ni shukrani ya kutambua mchango wao uliofanikisha uwepo wa umoja huo muhimu.

Dkt. Tulia licha ya kuwapongeza kuanzisha umoja huo ameutaka uongozi ktanua wigo wa umoja huo kwa kuanzisha matawi katika wilaya zote za mkoa wa Dodoma pamoja na kuanzisha Uwambeso katika mikoa mingine nchini. PICHA ZOTE  NA RICHARD MWAIKENDA
Mwenyekiti wa Uwambeso, Nsubi Bukuku akimkabidhi cheti Mbunge wa Mbeya Mjini na Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson ikiwa ni shukrani ya kutambua mchango wake katika umoja huo.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanznania, Dkt. Tulia Ackson (katikati) wabunge na viongozi wa Uwambeso wakikata keki wakati wa uzinduzi wa umoja huo wa watu kutoka mikoa ya Mbeya na Songwe wanaioshi Dodoma.
Dkt. Tulia akimlisha keki Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya ambaye ni Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi.
Mbunge wa Viti Maalumu, Wazazi Taifa,  Bahati Ndingo (kushoto) akifurahia na wajumbe baada ya kukabidhiwa keki iliyonunuliwa na wabunge kutoka Mkoa wa Mbeya.
Dkt. Tulia akihutubia na kuwaambia wajumbe kuwa amefrahishwa na uanzishwaji wa  umoja huo na kwamba wabunge wote kutoka mikoa hiyo wako tayari kujiunga. Pia wabunge hao waliahidi kuuchangia umoja huo sh. mil. 9.
Dkt. Tulia akimlisha keki Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga.
Mbunge wa Viti M aalumu (CCM Wazazi Tanzania Bara), Bahati Ndingo kutoka Mkoa wa Mbeya akilishwa keki na Dkt. Tulia.
Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Songwe, Neema Mwandabila akilishwa keki
Mmoja wa wanachama wa Uwambeso akilishwa keki kwa kuchangia fedha za kutunisha mfuko wa umoja huo.
Ni furaha iliyoje wakati wa hafla hiyo
Wanachama wa Uwambeso wakigongeana glasi na viongozi walio meza kuu kwa kutakiana heri

Wanachama wa Uwambeso wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni Rasmi Dkt Tulia.



 

WAZIRI PROF MKENDA APIGA MARUFUKU POLISI KUKAMATA WAFANYABIASHARA WA MAHINDI

 

Waziri wa Kilimo Prof. Aldof Mkenda amepiga marufuku kwa jeshi la polisi kukamata wafanyabiashara ya mahindi wakati wanapeleka bidhaa yao sokoni kwani hali hiyo inakatisha tamaa wakulima.

Prof.Mkenda ametoa Kauli  wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua na kujionea  Mashamba ya Kilimo cha mkataba wa zao la mtama wilayani Kongwa.

Waziri Mkenda amesema kuwa anatarajia kuzungumza na Mkuu wa Jeshi
la Polisi nchini (IGP) kuhakikisha Jeshi hilo linaachana na tabia ya kukimbizana na wafanyabiashara hao wakati wakipeleka biashara zao sokoni.

"Kuna changamoto kubwa ya masoko inayowakabili wafanyabiashara wa mahindi nchini, wafanya biashara hao wanauhuru wa kufanya biashara eneo lolote nchini kwa kuwa wanakuwa wakitafuta masoko, hivyo kuwazuia na kuwanyang’anya mazao yao wakati wakipeleka sokoni ni kuwavunja moyo na kuwakatisha tamaa,”amesema Prof.Mkenda.

Hata hivyo Prof. Mkenda amewataka askari wa Jeshi la Polisi nchini kuacha tabia hiyo ya kuwanyanyasa na kuwasumbua wakulima na wafanyabiashara wa zao hilo ambao
wanakuwa wakipambana kujikwamua na umaskini na kuchangia pato la taifa.

“Hiki kitu kwa kweli sio kizuri hawa ni watanzania ambao wanatafuta masoko ya zao hilo ni vema wakaachiwa ili kuendelea na biashara hiyo”amesema Prof. Mkenda

Aidha Waziri Mkenda amewataka maafisa ugani kuendelea kutoa elimu kwa wakulima wa mazao mbalimbali wilayani humo ili wafanye kilimo chenye tija ambacho kitaleta matokeo chanya kwao na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Dk. Seleman Serera, amesema wakulima
wa Kongwa wanashauku kubwa ya kuendesha kilimo cha mkataba cha zao la mtama pamoja na kilimo cha mazao mengine kitaalamu ili kusonga mbele katika kilimo.

Hivyo  Dk. Serera amesema ujio wa wawekezaji hao wa ndani kutawafanya wakulima wa Kongwa kufanya kilimo cha kisasa ambacho kitaleta manufaa makubwa kwa wakazi wa eneo hilo na taifa.


Awali  Mwenyekiti wa kijiji cha Sagara B, kilichopo wilayani Kongwa Bw.Gilbert Mlwande amemshukuru Waziri huyo huku akisema amewasaidia wakulima na wafanyabiashara kutatua changamoto ya kukimbizana na Jeshi la Polisi Barabarani.



UWEKAJI VINASABA KWENYE MAFUTA UFANYIKE KWENYE MATENKI - DKT.KALEMANI


 

Na Teresia Mhagama, Dar es Salaam

Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani ameliagiza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuhakikisha kuwa uwekaji wa vinasaba kwenye mafuta kama vile petroli na dizeli unafanyika kuanzia kwenye matenki yanayohifadhi mafuta hayo badala ya magari ili kuhakikisha kuwa mafuta yote yanayosambazwa nchini yanakuwa na ubora na Serikali inapata kodi stahiki.

Dkt.Kalemani alitoa agizo hilo tarehe 28 Aprili, 2021 mara baada ya kufanya ziara kwenye maghala ya mafuta ya kampuni za Camel Oil na Oil Com, Kurasini mkoani Dar es Salaam na kukuta wataalam kutoka TBS wakifanya kazi ya uwekaji wa vinasaba kwenye magari ya kusafirisha mafuta ya kampuni tajwa.

“Nataka muanze kupima mafuta kuanzia kwenye matenki yenyewe, hadi kwenye vituo, siyo tu kusubiri pale wanapopakia kwenye magari, Je ikitokea wamepakia wakati hampo, mtajuaje kuwa mafuta husika yana ubora?”Alisema Dkt.Kalemani

Dkt.Kalemani alieleza kuwa, amefanya ukaguzi wa kazi ya uwekaji wa vinasaba kwenye mafuta ili kujiridhisha kama TBS wanafanya kazi husika kwa ufanisi baada ya kukabidhiwa kutekeleza jukumu hilo ambalo awali lilikuwa likifanywa na mkandarasi binafsi ambaye alikuwa akilipwa takriban shilingi Bilioni Tano kwa mwezi.

Aliongeza kuwa, Serikali imekuwa ikipoteza fedha nyingi kumlipa mkandarasi binafsi kuweka vinasaba kwenye mafuta badala ya TBS ambayo ndiyo yenye dhamana ya kuhakikisha kuwa mafuta yanayouzwa nchini yanakuwa na ubora stahiki.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa, mafuta yanakuwa na ubora, kodi zinapatikana na pia tunajenga uwezo wa watu wetu kufanya kazi husika na Taasisi zetu zisimamie kazi hii badala ya kutegemea watu kutoka nje ya nchi.” Alisisitiza Dkt.Kalemani

Katika ukaguzi huo, Dkt.Kalemani aliiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), kuhakikisha kuwa, wanasimamia kikamilifu kazi ya uwekaji wa vinasaba kwenye mafuta nchini kwani TBS ina jukumu la kupima mafuta hayo na EWURA ndiye mwenye jukumu la kumsimamia mpimaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Athuman Ngenya alimhakikishia Waziri wa Nishati kuwa, TBS ina uwezo wa kufanya kazi ya uwekaji vinasaba kwenye magari na kwamba mafuta yote yanayosambazwa nchini yanakuwa na vinasaba.

Katika ziara yake kwenye maghala hayo ya mafuta mkoani Dar es Salaam, Waziri wa Nishati aliambatana na Kaimu Kamishna wa Petroli na Gesi, Sebastian Shana, na Wakuu wa Taasisi za Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), TBS na EWURA.

Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani (wa Pili kushoto) akikagua kazi ya uwekaji vinasaba kwenye ghala la mafuta la kampuni ya Camel Oil mkoani Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Athuman Ngenya

Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani (wa Tatu kushoto) akiwa katika ghala la mafuta la kampuni ya Camel Oil wakati alipofika kukagua kazi ya uwekaji vinasaba kwenye ghala hilo mkoani Dar es Salaam. Wa Pili kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Athuman Ngenya.

JAFO AKUTANA NA MAWAZIRI WANNE KUJADILI CHANGAMOTO ZA UCHAFUZI WA MAZINGIRA KUTOKANA NA KELELE

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo akiongoza kikao cha kujadili changamoto za uchafuzi wa mazingira kutokana na shughuli za kiuchumi zinazosababisha kelele na mitetemo kilichofanyika Dodoma  Aprili 28, 20021.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Geofrey Mwambe, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dorothy Gwajima, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa na Mkurugenzi wa Mazingira Dkt. Andrew Komba wakiwa katika kikao cha kujadili changamoto za uchafuzi wa mazingira kutokana na shughuli za kiuchumi zinazosababisha kelele na mitetemo kilichofanyika Dodoma  Aprili 28, 20021.

 

Kuanzia kulia ni Waziri Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Hamad Hassan Chande, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga na Naibu Naibu Katibu Mkuu Mohammed Abdallah Khamis wakiwa katika kikao cha kujadili changamoto za uchafuzi wa mazingira kutokana na shughuli za kiuchumi zinazosababisha kelele na mitetemo kilichofanyika Dodoma  Aprili 28, 20021.


Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samwel Gwamaka akiwasilisha taarifa kuhusu hali ya uchafuzi wa mazingira kutokana na kelele na mitetemo na hatua zilizochukuliwa kukabiliana na changamoto hizo.


  

Washiriki wakiwa katika kikao cha kujadili changamoto za uchafuzi wa mazingira kutokana na shughuli za kiuchumi zinazosababisha kelele na mitetemo kilichofanyika Dodoma  Aprili 28, 20021.

(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)