Serikali ya Mkoa wa Dodoma imetoa maamuzi matatu katika kuzisaidia Kaya 556 zilizoathirika na mafuriko katika kata ya Nkuhungu jijini Dodoma ikiwemo kutoa viwanja bure vyenye thamani ya Shilingi Shilingi Bilioni mbili.
Akizungumza Mei 9 na wakazi wa eneo la mtaa wa Buchela,Salama,Mnyakongo na Mtube,Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk Binilith Mahenge amesema viwanja hivyo vipo katika eneo la Nala na Mahomanyika Jijini Dodoma.
Jambo la Pili amesema ni kuchimba mitaro miwili Ili kuziba maji toka milimani na kutoa maji katika bwawa lililopo eneo hilo.
"Kazi hii ya mitaro ina gharimu kiasi Cha Shilingi Bilioni 1.3 ,na kazi ya kutoa Maji kwenye bwawa zinahitajika takribani sh bilioni 9.6 sio pesa ndogo,ni lazima tuiombee na kazi yake haiwezi kukamilika kwa haraka,hivyo suluhisho la mapema ni kuwapa viwanja Ili muanze maisha katika maeneo mengine,"alisema.
Ametaja Jambo la tatu kuwa ni Mara baada ya mitaro hiyo kukamilika na Maji kuondoka,wale waliokuwa na makazi katika maeneo hayo wataendelea kuyamiliki.
Uamuzi huo wa serikali ya mkoa wa kutoa viwanja mbadala na kuchimba mitaro kukinga na kuondoa maji kwenye bwawa ulifikiwa baada ya kupokea taarifa ya Kikosi Kazi hicho kilichoundwa na Mkuu wa Mkoa Dk Mahenge mapema Aprili mwaka huu na kilifanya kazi kwa siku 12 na kuja na mapendekezo hayo.
No comments:
Post a Comment