Matokeo chanyA+ online




Wednesday, September 29, 2021

SINGIDA DC YAPONGEZWA KWA UELEWA WA UHAMASISHAJI CHANJO YA UVIKO 19

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI) Idara ya Jamii  na Lishe, Dinah Atinda, akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Afya ya Msingi Wilaya ya Singida DC      katika kikao kilichoketi mkoani hapa jana.    
Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Mkuu wa Wilaya hiyo Mhandisi Paskas Muragili, akizungumza kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
Picha ya pamoja.

 Picha ya pamoja.

Na Dotto Mwaibale, Singida.1

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI) Idara ya Jamii  na Lishe, Dinah Atinda amewapongeza wajumbe wa Kamati ya Afya ya Msingi Wilaya ya Singida DC kwa kuwa na uelewa mpana wa uhamasishaji wa chanjo ya Uviko 19 ambao unaendelea nchini kote.

Atinda alitoa pongezi hizo jana kwa niaba ya wenzake katika semina ya siku moja iliyokuwa ikitolewa kwa wajumbe hao wilayani humo.

" Tunapita katika Halmashauri zote kuangalia namna kinavyofanyankazi hiki kikao cha PHC lakini napenda kusema kikao hiki ni tofauti kidogo na vikao tulivyo vipitia ndugu mwenyekiti wa kikao 'Mkuu wa wilaya' inaonekana wajumbe wa kikao hiki wamepata elimu ya kutosha na wapo vizuri kabisa hivyo tunawapongeza sana,". alisema Atinda.

Alisema Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na TAMISEMI na wadau mbalimbali baada ya kuona hali ya nchi sio nzuri ugonjwa wa Uviko 19 unaendelea na watu wanakufa tukaona kuna haja ya kuanzisha  mpango mkakati shirikishi na harakishi kwa ajili ya kuhamasisha na kuelimisha jamii ili wote waweze kupata chanjo na kupunguza madhara yanayotokana na ugonjwa huo.

Alisema zoezi la mtu kuchanja ni la hiyari hivyo lifuate maagizo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuwa vituo vya chanjo sasa vimeongezwa hadi kufikia zaidi ya 6,500 na vinatoa huduma.

Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Mkuu wa Wilaya hiyo Mhandisi Paskas Muragili alisema changamoto kubwa iliyopo kwa Watanzania ni kuwa hawajapewa elimu ya kutosha kuhusu chanjo na hawajui umuhimu wa chanjo hiyo lakini wanauelewa mkubwa wa mambo mbalimbali hivyo ni wajibu wa kamati hiyo kwenda kuwaelimisha na wakielewa watachanja.

Wakizungumza baada ya kupata mafunzo hayo wajumbe wa kamati hiyo walisema sasa wanakwenda kufanya uhamasishaji wa nguvu wakianzia kwenye familia zao.

Walisema uhamasishaji huo wataufanya kwenye nyumba za ibada, magulio, mashuleni, na kwenye mikusanyiko ya watu.

Wajumbe hao walisema wataenda kutoa elimu hiyo kwa viongozi mbalimbali wa vijiji wakiwemo wa Serikali na vyama vya siasa lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wana elewa na kujitokeza kwa wingi kwenda kupata chanjo hiyo.

MSD KUANZISHA KIWANDA CHA DAWA ZA NGOZI NCHINI


Mkurugenzi Mkuu Bohari ya Dawa (MSD), Meja Jenerali Gabriel Mhidze akizungumza na  waandishi wa habari kwenye semina ya  siku moja iliyoandaliwa na MSD iliyokuwa na lengo la kutoa taarifa ya mafanikio na mwelekeo wa MSD,  jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa MSD Erick Mapunda.
Wafanyakazi wa MSD wakiwa kwenye semina hiyo.
Waandishi wa Habari wakiwa kwenye semina hiyo.
Semina ikiendelea.


Na Dotto Mwaibale

Mkurugenzi  Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Meja Jenerali Gabriel(Dkt) Mhidze amesema MSD iko mbioni kuanzisha kiwanda cha dawa za ngozi,ikiwemo mafuta maalumu ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Meja Jenerali Mhidze aliyaeleza hayo jana  mbele ya waandishi wa habari alipokuwa akizungumzia kuhusu majukumu na maboresho ya MSD.

Alisema kiwanda hicho, ambacho mashine zake zimeshafika kitazalisha pia dawa za meno na dawa za macho.

Aidha Mkurugenzi Mkuu huyo wa MSD ameeleza kuwa kiwanda cha  MSD cha kuzalisha mipira ya mikono kilichopo imIdofi, Makambako mkoani Njombe kinatarajiwa kuanza uzalishaji mwezi Novemba mwishoni,huku akisema viwanda vingine vya dawa za rangi mbili, vidonge na dawa za maji maji za watoto mashine zake zimeshaanza kuwasili.

Tayari ina viwanda vya kuzalisha barakoa na dawa Keko jijini Dar es Salaam,ambavyo vinauwezo wa kuzalisha aina 10 za dawa na barakoa.

Tuesday, September 28, 2021

KATIBU MKUU WA CHAMA CHA MAPINDUZI DANIEL CHONGOLO APOKEA UGENI WA KATIBU MKUU WA CHAMA CHA FRELIMO PAMOJA NA WAJUMBE WA KAMATI KUU YA CHAMA HICHO KWA ZIARA YA SIKU TANO

 


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg Daniel Chongolo (Kushoto) akiwa na mgeni wake Katibu Mkuu wa Chama Cha Frelimo Nchini Msumbiji Ndg Roque Sliver Samweli ,mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Mwl Julius Nyerere Jijini Dar Es Salaam.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg Daniel Chongolo (Kushoto) akizungumza Katibu Mkuu wa Chama Cha Frelimo Nchini Msumbiji Ndg Roque Sliver Samweli ,mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Mwl Julius Nyerere Jijini Dar Es Salaam.
Wajumbe wa Sekretariet ya Chama Cha Mapinduzi Taifa wakimpokea Katibu Mkuu wa Chama Cha Frelimo Nchini Msumbiji Ndg Roque Silver Samweli mara baada ya kuwasili  Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM Lumumba Jijini Dar Es Salaam.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Frelimo Nchini Msumbiji Ndg Roque Silver Samweli  akivishwa Skafu na kijana wa Hamasa mara baada ya kuwasili  Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM Lumumba Jijini Dar Es Salaam.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg Daniel Chongolo (Kulia) akiwa na mgeni wake Katibu Mkuu wa Chama Cha Frelimo Nchini Msumbiji Ndg Roque Sliver Samweli ,alipowasili katika Ofisi ndogo za makao makuu ya CCM Lumumba  Jijini Dar Es Salaam.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg Daniel Chongolo (Kulia) akiwa na mgeni wake Katibu Mkuu wa Chama Cha Frelimo Nchini Msumbiji Ndg Roque Sliver Samweli ,wakikagua kikundi cha ngoma  ofisi ndogo ya makao makuu ya CCM Lumumba Jijini Dar Es Salaam.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg Daniel Chongolo (Kulia) akiwa na mgeni wake Katibu Mkuu wa Chama Cha Frelimo Nchini Msumbiji Ndg Roque Sliver Samweli ,wakiingia ndani katika Ofisi ndogo za Mkao Makuu ya CCM Lumumba Jijini Dar Es Salaam.
Picha ya Pamoja ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg Daniel Chongolo (Kulia ) akiwa na mgeni wake Katibu Mkuu wa Chama Cha Frelimo Nchini Msumbiji Ndg Roque Sliver Samweli ,katika Ofisi ya katibu Mkuu wa CCM Lumumba jijini Dar Es Salaam.
Wajumbe wa Sekretariet ya Chama Cha Mapinduzi  wakiongozwa na Katibu Mkuu Ndg Daniel Chongolo pamoja na wajumbe wa kamati kuu ya Chama Cha Frelimo walioongozana na Katibu Mkuu ndg Roque Silver Samwel wakiwakaribisha Viongozi hao katika kikao cha pamoja kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano Ofisi ndogo za Makao makuu ya CCM Lumumba Jijini Dar es Salaam
Katibu Mkuu  wa Chama cha mapinduzi (CCM) Ndg Daniel Chongolo  akizungumza pamoja na wajumbe wa kamati kuu ya Chama Cha Frelimo walioongozana na Katibu Mkuu ndg Roque Silver Samwel katika kikao cha pamoja kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano Ofisi ndogo za Makao makuu ya CCM Lumumba Jijini Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa chama Cha Frelimo Nchini Msumbiji Ndg Roque Silver Samwel akizungumza katika kikao cha pamoja kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano Ofisi ndogo za Makao makuu ya CCM Lumumba Jijini Dar es Salaam
Picha zote na (FAHADI SIRAJI/CCM MAKAO MAKUU)

WATUMISHI WATUME YA UTUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUONGEZA KASI YA UTENDAJI WA KAZI

 

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bwana Mathew Modest  Kirama  amewataka watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma kuongeza kasi ya utendaji  wa kazi ili kufikia malengo yaliyowekwa na Tume.

Bwana Kirama aliapishwa jana tarehe 27 Septemba 2021 na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, amesema haya leo baada ya kufika Ofisini kwake, Ofisi ya Tume iliyopo katika Jengo la Chimwaga, Dodoma na kupokelewa na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma  Jaji (mstaafu) Mheshimiwa Dkt. Steven James Bwana, Wakuu wa Idara na Vitengo na watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma.

“Tume ya Utumishi wa Umma ina jukumu la kuhakikisha Waajiri, Mamlaka za Ajira, Mamlaka za Nidhamu na Watumishi wa umma wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu, Miongozo na Maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Serikali, ninapenda kila mmoja katika nafasi yake ahakikishe anawajibika ipasavyo, anajitoa kadri anavyoweza kuhakikisha tunafikia malengo ya Tume. Mahali tunapofanya vizuri, tuhakikishe tunazidi kufanya vizuri zaidi. Ongezeni kasi ya utendaji wa kazi. Nafahamu Tume kuna changamoto,  kwa pamoja tunapaswa kushirikiana ili kutafuta majawabu ya changamoto hizo” amesema Bwana Kirama.

Bwana Mathew Kirama amewapongeza na kusisitiza uwajibikaji zaidi Watumishi wa Tume kwa namna ambavyo kila mmoja anavyojitoa wakati wa kutekeleza majukumu yake pamoja na changamoto zilizopo kuhakikisha majukumu ya Tume hasa yale ya kisheria ya kushughulikia rufaa na malalamiko na Ukaguzi wa Rasilimali Watu katika Utumishi wa  Umma yanaendelea kufanyika.

Akizungumzia umuhimu wa kutatua kero za watumishi wa Tume, Bwana Kirama amesema ni muhimu Wakuu wa Idara na Vitengo wa Tume kutenga muda wa kukutana na kusikiliza kero na matatizo ya watumishi walio chini yao na kutafutia ufumbuzi.

“Tunapaswa kuendelea kuanzia pale mtangulizi wangu alipoishia, unahitajika utashi wa kila mmoja wetu, kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu, ushirikiano, maelewano, kuheshimina na kutambua nafasi na mchango wa kila mmoja ili  kufanikisha malengo ya Tume” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji (mstaafu) Mheshimiwa Dkt. Steven James Bwana amempongeza Bwana Kirama kwa kuteuliwa na kuapishwa kuwa Katibu wa Tume.

“Nina matumaini makubwa sana kwako Katibu wa Tume,  Mathew Kirama  naamini ni mtu sahihi  na huu ni wakati sahihi kwako kuiongoza Tume ya Utumishi wa Umma. Nawaomba watumishi wa Tume kutoa ushirikino mkubwa kwako Katibu ili uweze kuifikisha Tume katika malengo yake iliyojiwekea” amesema Mheshimiwa Jaji (Mstaafu) Dkt. Bwana.

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bwana Mathew Modest Kirama ameteuliwa na kuapishwa na Mheshimiwa Rais, kuchukua nafasi ya Bwana Nyakimura Muhoji ambaye amestaafu.

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma,  Bw. Mathew M. Kirama (wa nne kutoka kulia) katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Jaji (mstaafu) Dkt. Steven J. Bwana (wa tano kutoka kulia) na baadhi ya watumishi wa Tume, baada ya Katibu kufika katika Ofisi ya Tume  Chimwaga- Dodoma,  28/09/2021.

Bw. John C. Mbisso (kushoto) Naibu Katibu wa Tume, akifafanua jambo kwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew M. Kirama (katikati) baada ya Katibu wa Tume kufika Ofisi ya Tume, Chimwaga Dodoma  28/09/2021. Kulia ni Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji (mstaafu) Mhe. Dkt. Steven J. Bwana.

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Modest Kirama (kulia) akipokelewa na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji (mstaafu)  Mhe. Dkt. Steven J. Bwan, baada ya kufika  Ofisi ya Tume ya Utumishi wa Umma iliyopo Jengo la Chimwaga, Jijini Dodoma, kushoto ni Bw. John C. Mbisso, Naibu Katibu wa Tume.

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji (mstaafu) Mhe. Dkt. Steven J. Bwana (kushoto) akisalimiana na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Modest Kirama, baada ya kufika katika Ofisi ya Tume iliyopo Jengo la Chimwaga, Jijini Dodoma  tarehe 28/09/2021.

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew M. Kirama akipokelewa  baada ya kuwasili katika Ofisi ya Tume ya Utumishi wa  Umma, Chimwaga – Dodoma,  tarehe 28/09/2021.

Sunday, September 26, 2021

MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR ATOA MAAGIZO KWA TPA KUHUSU UPANUZI BANDARI TANGA,ATAKA IVUTIE KIMATAIFA


 Makamu wa Pili wa Rais Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,Hemed Suleiman Abdulla ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha kuwa wakati upanuzi wa Bandari ya Tanga ukielekea ukingoni wahakikishe kuwa wanaitangaza kimataifa ili kuvutia wateja.


Ametoa agizo hilo leo wakati akifanya ukaguzi wa Bandari ya Tanga ambapo yupo katika ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Tanga,hivyo upanuzi wa bandari hiyo unaotekelezwa na kampuni ya CHEC kutoka China ukielekea ukingoni ni vema mamlaka hiyo ikaanza mikakati ya kuitangaza bandari hiyo wakati ujenzi ukiendelea.


Amesema kuwa katika upanuzi huo, serikali imewekeza zaidi ya kiasi cha Sh.bilioni 400 hivyo lazima kuwe na tija kuona ni namna gani serikali itarudisha hiyo fedha."Serikali imetumia zaidi ya Sh.bilioni 400 katika upanuzi wa bandari hii ambayo ni nguzo muhimu kiuchumi sio kwa mkoa wa Tanga pekee bali hata mikoa ya kanda ya Kaskazini.


"Visiwani na nchi za Rwanda na Burundi,hivyo itangazeni hii bandari kimataifa ili wateja waanze kuja kabla hata ujenzi haujakamilika ikiwemo kuweka promosheni ili kuwavutia wateja na pia wekeni mazingira rafiki kwa wafanyabiashara ili walipe kodi kwa mujibu wa sheria," amesema.



Kwa upande wake,Mkurugenzi Mkuu wa Bandari,Eric Hamisi amekiri mamlaka hiyo kutoitangaza bandari hiyo na kuahidi kutelekeza agizo hilo mara moja ikiwemo kutumia ofisi za balozi za Tanzania zilizopo nje ya nchi kwa kutoa elimu kwa kutumia lugha za asili za nchi husika ili kuwa na uelewa pamoja na kuimarisha ofisi za TPA katika nchi hizo.


" Ni kweli bado bandari hii haijatangazwa sana kimataifa lakini mkakati uliopo ni kuhakikisha tunashirikiana na ofisi za balozi zetu nje ya nchi kwa kutoa elimu,kuanzaa vipeperushi,mawasilisho kwa kutumia lugha za nchi husika pamoja na kuimarisha ofisi zetu katika bandari hizo," alisema.


Wakati huo huo Ofisa Mradi kampuni ya CHEC, Lyu Wei amesema mradi huo umetekelezwa kwa awamu mbili,awamu ya kwanza ambayo imekamilika kwa asilimia 100 tangu Mei 2020,imetumia kiasi cha Sh.bilioni 172 na awamu ya pili imetumia Sh.bilioni 256 , ipo katika hatua ya mwisho ikiwemo kuleta mashine mbili za bandari.


Kwa upande wake,Meneja wa Bandari ya Tanga, Donald Ngaile amesema kuwa kukamilika kwa bandari hiyo kutaondoa msongamano katika Bandari ya Dar es salaam, kupunguza gharama ya kutoa mizigo mara mbili kati ya meli-tishali na kutoka kwenye tishali- nchi kavu kwa asilimia 40.


Pia kupunguza gharama za matumizi ya mafuta zinazotumika katika boti za kuvuta tishali ,kufupisha muda wa kuhudumia meli kutoka siku tano mpaka sita hadi kufikia saa 24 pamoja na kuongeza idadi ya kupokea meli nyingi na kuhudumia shehena kutoka tani 700,000 hadi tani milioni 3.



 

KATIBU MKUU WA WIZARA YA MAJI SANGA AKAGUA UTENDAJI WA SEKTA YA MAJI MTWARA


Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga mwishoni mwa wiki amekagua utendaji wa Sekta ya Maji mkoani Mtwara.

Mhandisi Sanga katika ziara hiyo ya kikazi amewataka watendaji na wataalamu wa sekta ya maji kutumia ubunifu katika kutoa huduma, na kuepuka gharama ambazo hazina ulazima.

Amesisitiza wataalamu kutumia usanifu wa miradi utakaowezesha majisafi kuwafikia wananchi kwa njia ya mserereko, hivyo huduma hiyo kumfikia mlaji kwa gharama ndogo.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga akikagua chanzo cha maji cha Mbwinji kinachotumiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Masasi Nachingwea (MANAWASA) kusambaza huduma ya maji, (kulia) ni Mkurugenzi Mtendaji wa MANAWASA Mhandisi Nuntufye Mwamsojo.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga akitoa maelekezo ya kitaalamu kuhusu ujenzi unaoendelea wa mradi wa maji wa Chipingu, pamoja naye (katikati) ni Mbunge wa  Lulindi Mhe. Issa Ally (Mb) na wataalamu wa sekta ya maji. Chanzo cha maji cha mradi huo ni mto Ruvuma.

WAZIRI MHAGAMA AONGOZA HARAMBEE UNUNUZI VIFAA VYA ELIMU NA SAIDIZI KWA WANAFUNZI WENYE ULEMAVU KATIKA SHULE YA LIBERMANN VISIWI



Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akiwa na watendaji wa Shule ya Viziwi ya Libermann wakionesha Hundi iliyochangiwa na uongozi wa shule hiyo wakati wa Harambee maalum ya kuchangia vifaa vya shule na vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye uziwi wa shule hiyo, Hafla hiyo ilifanyika tarehe 25 Septemba, 2021 katika shule hiyo.




Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akihutubia wakati wa Kilele cha Harambee Maalum ya ununuzi wa vifaa vya kielimu na saidizi pamoja na maadhimisho ya Somo wa Shule za Libermann iliyofanyika Septemba 25, 2021 shule ya Libermann Viziwi iliyopo kata ya Kawe, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam.Shule inamilikiwa na Shirika la Mapadri wa Roho Mtakatifu (Spiritans) Kanda ya Tanzania



Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akikabidhi mchango wake kwa Bw. Karoli Tarimo, Mwenyekiti wa Kamati ya Harambee ya ununuzi wa vifaa vya kielimu na saidizi kwa wanafunzi wenye uziwi katika shule ya Libermann Jijini Dar es Salaam.




Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akiangalia miundombinu ya kufundishia watoto wenye mahitaji maalum wa shule ya Libermann Viziwi alipotembelea kukagua mazingira ya shule hiyo.anayetoa maelezo ni Bi. Neema Shiyo Mnzava, Mwenyekiti wa Kamati ya Shule hiyo.




Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Libermann Viziwi Bi. Neema Shiyo Mnzava akimuonesha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama miundombinu ya kufundishia wanafunzi wenye uziwi alipotembelea shule hiyo.




Baadhi ya wanafunzi wa shule ya Libermann Viziwi wakionesha ndoto zao baada ya masomo kwamgeni rasmi Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa hafla ya Harambee maalumu ya ununuzi wa vifaa vya shule na saidizi kwa wanafunzi hao.



Meneja wa Kampuni ya Jatu PLC Bw. Mohamed Simbano akikabidhi msaada wa mchele kwa uongozi wa Shule ya Libermann Viziwi na katikati ni mgeni rasmi Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama.



Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa Shule ya Libermann Viziwi mara baada ya kumkabidhi zawadi wakati wa hafla hiyo.



Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akicheza wimbo maalum wa Mjomba band wa kuhamasisha harambee hiyo na wanafunzi wa Shule ya Libermann Viziwi wakati wa hafla hiyo.



Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akishiriki maombi maalum ya kuombea Shule ya Libermann Viziwi pamoja na sala maalum ya sikukuu somo wa shule hiyo (Francis Maria Libermann) iliyoambatana na harambee hiyo.



Padre Philip Athanas Massawe C.S.Sp, Mkuu wa Shirika la Roho Mtakatifu (Spiritans) Kanda ya Tanzania, akieleza historia ya Shirika wakati wa Harambee maalum ya kuchangia vifaa vya shule na Vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye uziwi wa shule hiyo.



Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) akitoa burudani ya kuhamasisha uchagiaji wa vifaa vya shule na saidizi kwa wanafunzi wa shule ya Libermann Viziwi.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

…………………………………………………………

NA.MWANDISHI WETU

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameongoza harambee maalumu ya ununuzi wa vifaa maalumu vya kielimu na saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wa shule ya Libermann Viziwi.


Halfa hiyo ilifanyika tarehe 25 Septemba, 2021 iliambatana na kumbukumbu ya Somo wa Shule zetu Mwenyeheri Francis Maria Paul Libermann na pamoja na maadhimisho ya wiki ya Viziwi Duniani.


Waziri alionesha kufurahishwa na hatua ya uongozi wa shule hiyo kwa kuona umuhimu wa kusaidia watoto wenye mahitaji maalum na kuendesha harambee hiyo ili kuwa na vifaa na kuboresha masuala yanayowahusu ili kuwa na mazingira rafiki ya ufundishaji na kuhakikisha wanatimiza ndoto zao.


“Nimefurahishwa sana na uamuzi wenu wa kuadhimisha wiki hii ya Viziwi Duniani kwa kufanya harambee ya kupata fedha za uendeshaji na ununuzi wa vifaa maalumu vya kielimu na saidizi kwa wanafunzi wetu Wenye Ulemavu. Hongereni sana,”alesema Waziri Mhagama.


Waziri alieleza kuwa kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, kwa mwaka 2019/2020, Tanzania inakadiriwa kuwa na idadi ya watu milioni 55.9 ambapo milioni 2.5 kati yao ni Watu wenye Ulemavu. Aidha, kwa kipindi kirefu Watu Wenye Ulemavu wamekuwa wakikutana na changamoto mbalimbali katika kutafuta fursa na huduma za kijamii ikiwemo elimu.


“Watu wenye ulemavu wamekuwa wakiachwa nyuma katika masuala mbalimbali likiwemo hili la elimu, niendelee kuiasa jamii kuwapa kipaumbele na kuwawezesha ili wapate elimu itakayotoa fursa ya kuonesha uwezo walio nao bila kujali hali zao,”alisisitiza Waziri Mhagama.


Akisoma taarifa ya shule hiyo Mwalimu Mkuu Bi.Edister Massawe alisema shule inalenga kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuto elimu bora kwa watoto wa Tanzania hasa wenye mahitaji maalum kama vile viziwi pamoja na kuwapa fursa watoto wenye ulemavu kupata elimu bora, kusaidia familia zao kwa kuwapatia ufadhili na udhamini kwa watoto hao ili wajikwamue kielimu.


“Shule hii ya Viziwi inatoa elimu hiyo bure na imejikita kuwasaidia ili kuwafanya wabadilike wawe wenye kujitambua, kugundua na kuendeleza vipaji vyao na kuwajengea uwezo kwenye nyanja za ufundi na biashara ili waweze kushiriki katika masuala ya ujasiriamali, utunzaji wa mazingira na afya,”alisema Edister.


Akiongoza ibada maalumu ya kuombea shule na kumbukumbu ya Somo wa Shule zetu Mwenyeheri Francis Maria Paul Libermann Padre Philip Athanas Massawe C.S.Sp, Mkuu wa Shirika la Roho Mtakatifu (Spiritans) Kanda ya Tanzania, alisema jamii iwe mstari wa mbele bila uoga kuwainua watu wenye mahitaji maalum kwa kuwajengea ujasiri na kuwatambua kwani kufanya hivyo ni sehemu ya ibada na kujipatia baraka mbele za Mungu kwa kuwaangalia wahitaji.


“Taifa tuondoe uwoga na kuwainua watu wenye ulemavu na kuwaona wanaweza na kuwainua bila kuacha kuwaombea kuyafikia malengo yao,”alieleza Padri Philip


Shule ya Libermann Viziwi inamilikiwa na Shirika la Mapadri wa Roho mtakatifu (spiritans) Kanda ya Tanzania. Shule ipo kata ya Kawe, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam.Shule ilisajiliwa rasmi tarehe 11 Septemba, 2019 na kupewa namba za usajili EM. 17973 yenye kaulimbiu isemayo “Moyo mmoja roho moja (One heart one Soul).Ni shule pekee ya viziwi inayotumia mtaala wa Kingereza kwa kufundishia na kujifunzia na ina uwezo wa kuchukua wanafunzia 210 kuanzia ngazi ya awali mpaka darasa la saba.

SERIKALI YATUMIA SH. BILIONI 52.975 KUTEKELEZA MIRADI MBALIMBALI SINGIDA


Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa akionesha Jarida la Nchi Yetu wakati akitoa taarifa ya wiki ya Serikali kwa waandishi wa habari mkoani Singida.
Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa hiyo.
Taarifa ikitolewa.
Waandishi wa habari wakisikiliza taarifa hiyo.
Waandishi wa habari wakisikiliza taarifa hiyo. Kushoto ni Afisa Habari Msaidizi Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Mwanahabari Elisante Mkumbo akiuliza swali kwenye mkutano huo.
Mwanahabari Damiano Mkumbo akiuliza swali kwenye mkutano huo.
Mwanahabari  Edina Alex akiangalia   Jarida la Nchi Yetu kwenye mkutano huo. 
Waandishi wa habari wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
Kazi ikiendelea,
Katibu Mwenezi na Itikadi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida Ahmed Kaburu akiuliza swali kwenye mkutano huo.


Na Dotto Mwaibale, Singida

Serikali imetoa Sh.Bilioni 52.975  mkoani Singida kwa ajili  ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo barabara, elimu, afya, maji, huduma za utawala na uwezeshaji wa wananchi. 

Hayo yamesemwa na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa wakati akitoa taarifa ya wiki ya Serikali kwa waandishi wa habari mkoani Singida jana.

Alisema Serikali inaendelea kutoa huduma za kiutawala na maendeleo katika Mkoa wa Singida kama kawaida chini ya Mkuu wa Mkoa Dkt. Binilith Mahenge na kuwa hali ya mkoa ni shwari na wananchi wanaendelea na shughuli zao za uzalishaji mali bila bughudha. 

Alisema katika kuimarisha ustawi wa wananchi wa Singida, Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kama ambavyo inafanya katika mikoa mingine hapa nchini na katika kufanikisha utekelezaji huo Serikali inahakikisha inatoa fedha kama ilivyopangwa. 

Msigwa alisema kuanzia Mwezi huu wa tisa, Serikali imeleta Sh. Bilioni 2 na Milioni 275 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Vituo vya Afya 8 (Ntuntu-Ikungi, Mitundu-Itigi, Chibungwa/Sasajila-Manyoni, Ilunda-Mkalama, Iglansoni-Ikungi, Tyegelo-Iramba, Kasisiri-Iramba na Makuro-Wilayani Singida) na kukamilisha vyumba vya madarasa 22 katika shule za Sekondari. Hizi ni fedha ambazo zinakusanywa kutokana na tozo katika miamala ya simu. 

Alisema kuna miradi mbalimbali ya ujenzi wa Barabara na Madaraja inayoendelea kutekelezwa na kati ya Machi na Septemba mwaka huu 2021, Serikali imeleta Singida shilingi Bilioni 21 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja. 

"Mfano mmoja wapo ni ujenzi wa Daraja la Msingi (lenye urefu wa mita 100) katika barabara ya Ulemo-Gumanga-Sibiti. Ujenzi wa daraja hili utagharimu Sh. Bilioni 10.933, hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 69. Daraja hili pamoja na barabara zake unganishi zitakamilika Juni 2022,".  alisema Msigwa.

Msigwa aliongeza kuwa pamoja na miradi hiyo Serikali imeanza  kufanya upembuzi yakinifu na usanifu kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Sabasaba, Sepuka na Ndago Kizaga yenye km 77.6.

Alitaja barabara nyingine kuwa ni ya mchepuo ya Singida (Singida bypass) ya kilometa 46, Barabara ya Mkalama-Gumanga-Nduguti-Iguguno ambayo ni sehemu ya barabara inayoanzia Bariadi mkoani Simiyu ambayo itaunganisha na Iguguno. 

Akizungumzia miradi ya maji alisema Serikali imeleta sh. Bilioni 5 na Milioni 278 kutekeleza miradi hiyo katika vijiji vya Mughamo, Ibaga, Kipumbuiko na Kintinku/Lusilile. Hii yote nijuhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kumtua ndoo ya Maji Mama na kukabiliana na tatizo la maji. 

 Kuhusu umeme kupitia mradi wa usambazaji wa umeme vijijini (REA-III), Serikali imesambaza umeme katika vijiji 274 kati ya vijiji vyote 441 (sawa na asilimia 62.1). Kazi inayoendelea sasa ni kusambaza katika vijiji 167 vilivyobaki. Vijiji hivi vyote vitakuwa vimepata umeme ifikapo Desemba mwakani. 

Pia alisema Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa umeme wa kitaifa unaitwa Backbone Transimission Investment Project (BTIP) na kuwa hapa Singida kuna kituo kikubwa cha kupooza umeme na kinapokea kutoka kituo cha Zuzu – Dodoma umeme wa msongo wa kilovoti 400. Uwezo wake wa juu ni kupokea, kupoooza na kusambaza jumla ya Megawati 600. Kwa sasa tayari kimeanza kuhudumia Mji wa Singida na kazi inayoendelea ni kuunganisha na mitambo ya msongo wa kilovoti 400 na ile ya kilovoti 220 ambayo inatumika kuwapelekea wananchi. 

Alisema mradi huo  ni sehemu ya mradi mkubwa wa kujenga njia kuu ya umeme kutoka Iringa, Dodoma, Singida hadi Shinyanga. Na pia ni sehemu ya mradi wa kuunganisha njia ya umeme kati ya Tanzania na Kenya. Njia hii inakwenda mpaka  Namanga – Arusha hadi kuunganisha na Isinya nchini Kenya. 

Alitaja Gharama za mradi huo kuwa ni  Dola za Marekani Milioni 56 (Bilioni 128.8), hadi sasa umefikia asilimia 99 na unatarajiwa kukamilika kabla ya Desemba mwaka huu 2021.

Akizungumzia mradi wa kimkakati wa kukabiliana na upungufu wa mafuta ya kula nchini alisema nchi yetu inahitaji kama tani 640,000 za mafuta ya kula, uzalishaji wetu ni tani 240,000 tu. Mafuta yanayobaki kiasi cha tani 400,000 tunalazimika kuagiza kutoka nje ya nchi na tunatumiza zaidi ya shilingi Bilioni 500 kuagiza mafuta hayo. 

Alisema Serikali imejipanga kuhakikisha inaleta mbegu za alizeti za kupanda tani 1,194 kwa ajili ya wakulima. Hizi ni mbegu bora ambazo zinatoa mafuta mengi. 

Alisema katika juhudi za kuongeza mbegu za alizeti kwa ajili ya kuzalisha mafuta, tunahitaji tani milioni 2 kwa mwaka lakini tunazalisha tani laki 6 tu. 

"Serikali inawapongeza viongozi na wakulima wa Mkoa wa Singida kwa kujiwekea mpango wa kulima ekari 597,000 na kuzalisha tani 581,986 ambazo zitazalisha tani 242,500 za mafuta. Hii itasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya upungufu wa mafuta ya kula hapa nchini na kupanda kwa bei ya mafuta, alisema Msigwa.

 Msigwa alitumia nafasi hiyo kunatoa wito kwa wakulima wote nchini kuongeza uzalishaji wa alizeti na Serikali itaendelea kutoa huduma za ugani, kutafuta mbegu bora na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kusafisha mafuta. 

Adha Msigwa akizungumzia Mapambano dhidi ya Uviko-19 alisema  janga la ugonjwa  unaosababishwa na Virusi vya Korona (Uviko-19). Serikali kupitia Viongozi wake na Wataalamu imeendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya kujikinga na ugonjwa huo na kupokea chanjo. 

"Kwa kutambua changamoto ya kuhakikisha elimu dhidi ya ugonjwa huu inawafikia wananchi ipasavyo pamoja na kupata chanjo, Wiki hii Serikali imeanza kutekeleza Awamu ya Pili ya utoaji chanjo kwa kupanua uwigo wa vituo vya kutolea chanjo ya Uviko-19, tulianza na vituo 550 nchi nzima na sasa chanjo zinatolewa katika vituo vyote vinavyotoa chanjo zingine nchini. Kuna vituo zaidi ya 6,784 vinatoa chanjo na pia wataalamu wa kutoa chanjo sasa wanakwenda hadi vijijini na maeneo yote yenye mikusanyiko ya watu. Hata juzi kwenye mtanange wa Yanga na Simba, watu wamepata chanjo pale," alisema Msigwa. 

Alisema kwa tulipofikia sasa, hatutaki Mtanzania aliyetayari kupata chanjo apate shida ya kwenda sehemu ya kuchanjwa. Tunaweka vituo vya chanjo kwenye vituo vya mabasi, kwenye masoko, vituo vya kupima uzito magari, Mwenge wa uhuru, tunakwenda mechi ya watani wa jadi na kila mahali ambapo tunaona pana weza kuwarahisishia watu kupata chanjo. Na hii ni kwa sababu, tumeona Watanzania wengi wapo tayari kupata chanjo lakini changamoto imekuwa kuvifikia vituo vinavyotoa chanjo. 

Alisema utoaji chanjo unakwenda vizuri, mpaka leo Watanzania takribani 400,000 wamechanjwa na wengine wanaendelea kupata chanjo dhidi ya uviko-19. Kasi hii imeongezeka sana baada ya Wizara ya Afya, TAMISEMI na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuzindua Awamu ya Pili ya Uhamasisha na utoaji elimu (Sepetemba 15, 2021) ambapo sasa chanjo zinapelekwa hadi vijijini na Wataalamu wetu sasa wameanza kupita nyumba kwa nyumba ili wale ambao wapo tayari kupata chanjo wapate. 

Aliongeza kuwa Serikali inawapongeza Wataalamu wa Afya wote kwa kazi kubwa wanayoifanya, kwanza kwa wao wenyewe kuonesha mfano kwa kupokea chanjo na pili kupeleka huduma za Mkoba kwa wananchi (yaani mwananchi anapata chanjo pale alipo. 

Msigwa alimpongeza kijana Michael Filbert Nondo ambaye ameamua kusafiri kwa baiskeli kutoka Kigoma hadi Dar es Salaam akipita kuhamasisha wananchi kupokea chanjo. Leo amefika Dodoma na kukutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,  Jinsia, Wazee na Watoto lakini kwa bahati mbaya hatoweza kumaliza safari yake baada ya kupatwa na msiba wa kufiwa na mwanae huko Kigoma. Nawaomba vijana wote tuungane kuhamasisha jamii kupata chanjo kama anavyofanya kijana huyo. 

Alisema Serikali inahimiza watu kuchukua tahadhari dhidi ya Uviko-19 na kupata chanjo kwa sababu KINGA NI BORA KULIKO TIBA. Kitengo cha Kinga cha Wizara ya Afya kinachoongozwa na Dkt. Leonard Subi wanafanya kazi kubwa ya kuhakikisha wananchi wanapata elimu na chanjo, na leo hapa nimeongozana na Dkt. Ama Kasangala, yeye ni Kaimu Mkurugenzi wa kitengo cha elimu ya afya kwa Umma cha Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. 

Alisema  kwa kutambua kuwa Waandishi wa Habari wana umuhimu mkubwa katika jukumu la kuwaelimisha Watanzania kukabiliana na Uviko-19 Serikali imeona iongeze ushirikiano nao ambapo alimtambulisha Rais wa Umoja wa Vyama vya Waandishi wa Habari vya Mikoa (UTPC)  Deogratius Nsokolo alikuwa ameongozana naye. 

"Mimi lengo langu Waandishi wa Habari twende pamoja, tufanye kazi zetu kwa kuzingatia weledi, sheria za nchi, kanuni na taratibu lakini muhimu zaidi tuiweke nchi yetu kwanza (Tanzania Kwanza), tuwapiganie Watanzania pamoja. Kwenye hili janga la Korona Watanzania wanakufa kwa sababu ya kutozingatia afua hizi za kukabiliana na virusi vya ugonjwa huu, kutozingatia kuwa KINGA NI BORA KULIKO TIBA," alisema Msigwa. 

Msigwa alihitimisha hutuba yake kwa kuwaomba Waandishi wa Habari kushirikiana na Wataalamu waliopo katika mikoa yote hapa nchini  kuhakikisha elimu kwa wananchi inafika ipasavyo kwa kuwasiliana na Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Waganga wa Hospitali zetu, viongozi wa Mikoa na Wilaya ili Watanzania wapate chanjo na wajikinge na balaa hilo. 

Katika mkutano huo Msigwa alipata fursa ya kujibu maswali mbalimbali ya wananchi waliokuwa wakipiga simu moja kwa moja kwenye mkutano huo.