Na Damian Kunambi, Njombe
Kufuatia
kuwepo kwa changamoto nyingi za maji katika maeneo mbalimbali ya wilaya
ya Ludewa mkoani Njombe imepelekea wizara ya maji hapa nchini kuahidi
kutoa kiasi cha shilingi bilioni moja ndani ya mwezi huu ili kupunguza
changamoto hizo.
Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa maji
Merryprisca Mahundi baada ya kufanya ziara katika kata ya Masasi na
Iwela na kusikiliza changamoto zao pamoja na kukagua mradi wa maji wa
Iwela.
Kabla ya Naibu Waziri huyo kutoa ahadi hiyo mbunge wa
jimbo la ludewa Joseph Kamonga alielezea changamoto wanazozipata
wananchi hao na kusema kuwa wananchi wake wamekuwa wakitembea umbali
mrefu wa zaidi ya masaa mawili kwenda kuchota maji kitu ambacho
kinawaumiza huku miradi mbalimbali ikikwama kwa kukosa maji.
"Mheshimiwa
Naibu Waziri mradi huu wa Iwela ni mkubwa sana! hivyo tunaweza
kusambaza maji ya mradi huu hata katika vitongoji na vijiji vya jirani
kama Kisaula , Lutala na kwingineko",amesema Kamonga.
Aidha kwa
upande wa Naibu Waziri huyo amesema kiasi hicho cha fedha kitagawanywa
katika baadhi ya maeneo yenye shida zaidi ili kuweza kuwapunguzia adha
wanayoipata.
"Mbunge wenu alikuwa akinisumbua sana kwa kunitaka
nifike katika jimbo lake na kuona changamoto hii ya maji inayowapata
wananchi wake, na sasa nimefika nimejionea kwa macho yangu hivyo
serikali haina budi kuleta fedha ili tumtue mama ndoo kichwani", amesema
Mhandisi Mahundi
Hata hivyo Naibu Waziri huyo amemuagiza
mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Iringa
(IRUWASA) David Palangyo kuwasilisha andiko la kuongeza usanifu mpya wa
vitongoji ambavyo vimekosa maji ya mradi wa Iwela.
Naibu Waziri huyo amesema mradi huo umejengwa kwa kutumia 'force account' na kuweza kuokoa milioni 500 mpaka kukamilika kwa mradi hivyo kuna uwezekano wa chenchi kubaki ambayo ndiyo itakayosaidia kuongeza mabomba ya maji.
No comments:
Post a Comment