Matokeo chanyA+ online




Friday, April 15, 2022

DIASPORA AWAVUTIA WATAFITI WA MALIGHAFI ZA UJENZI WA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM

 Mtanzania anayeishi nchini Canada, ambaye ameonesha nia ya kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya barabara nchini, Bw. Joseph Katallah amewavutia watafiti wa malighafi za ujenzi ambao ni wahadhiri katika fani za kemia, mazingira, sayansi na uhandisi wa raslimali za ujenzi kutoka Kampasi mbalimbali za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).


Haya yamejiri leo terehe 14 Aprili 2022 wakati wa kikao kilichoongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Tagie Daisy Mwakawago katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaaam. Kikao hicho kilitokana na ombi la watafiti hao kutaka kukutanishwa na Diaspora huyo ambaye ameleta teknolojia ya “geopolymer” inayoweza kutumika katika ujenzi wa barabara.

Watalaamu hao kutoka UDSM wamejikita katika kutafiti malighafi za udongo wa mfinyanzi (clay), miamba madini, hewa ya ukaa (CO2) na taka za viwandani na sekta ya kilimo ambazo wanazitumia kuzalisha bidhaa na vifaa mbalimbali vya ujenzi bila kuhusisha matumizi ya saruji (Portland cement). Teknolojia hiyo ambayo ni asili ya “geopolymer” imepata mapokezi mazuri miongoni mwa wataalamu wa sekta ya ujenzi kupitia uwekezaji wa Bw. Katallah, inatajwa kuwa ni rafiki wa mazingira, inazalisha bidhaa za bei nafuu, zinazodumu kwa muda mrefu zikiwa pia na uwezo wa kukabiliana na madhara ya chumvi na fangasi vinayoathiri majengo mengi yaliyojengwa kwa saruji.

Akizungumza katika kikao hicho kwa niaba ya timu ya watafiti wenzake, Dkt. Aldo Kitalika ambaye pia aliongoza ujumbe wa Wataalamu hao kwenye mazungumzo, alieleza jinsi alivyovutiwa na uzoefu na ujuzi wa Bw. Katallah katika sekta ya ujenzi na kueleza utayari wao wa kushirikiana naye kupitia tafiti ili kuongeza tija zaidi katika sekta ya ujenzi.

“Tumevutiwa sana na teknolojia ya geopolymer ambayo kimsingi ni sehemu ya tafiti zetu tulizozifanya kwa kupima aina tofauti za malighafi za ujenzi ikiwemo udongo wa mfinyanzi (clay), madini ujenzi na taka za mimea kutoka maeneo mbalimbali ya nchi yetu kama vile mikoa ya Iringa, Njombe, Dodoma, Pwani, Manyara, Kilimanjaro, Mwanza, Ruvuma, Tanga, Morogoro na mingine mingi.” amesema Dkt. Kitalika.

Timu hiyo ya watafiti ilionesha wasilisho lenye bidhaa kifani (prototypes) kama vile matofali ya ujenzi wa aina mbalimbali, matofali yanayohimili joto kali (refractory bricks), vigae (tiles), vyungu vya maua, vyungu kwa ajili ya matumizi ya viwandani (crucibles), na meza za jikoni (kitchen counter tops).

Bw. Katallah amekuwa nchini kwa wiki kadhaa kwa madhumuni ya uwekezaji kwa kushirikiana na Kampuni ya Geopolymer Solutions LLC ya nchini Marekani inayomilikiwa na Bw. Rodney Zubrod, ambaye ni mbunifu wa teknolojia ya geopolymer.Teknolojia hiyo hutumia mabaki ya uchafu wa viwanda na migodi yenye kutengeneza alumina na vioo. Uchafu huo hujulikana kitaalamu kama matope mekundu.

Umoja wa watafiti hao unaundwa na Dkt. Aldo Kitalika (DUCE), Dkt. Makungu Madirisha (Mwalimu Nyerere, Mlimani), Bw. Said Abeid (MRI, Dodoma), Dkt. Regina Mtei (Mwalimu Nyerere, Mlimani), Dkt. Petro Mabeyo (DUCE), Dkt. Silvia Mushi (DUCE) na Dkt. Elianaso Elimbinzi (MUCE). Mazungumzo hayo ni sehemu ya muendelezo wa utekelezaji wa mikakati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Kitengo cha Diaspora ya kuhamasisha Diaspora wenye malengo ya kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini ili kutekeleza diplomasia ya uchumi.

Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Tagie Daisy Mwakawago akisitiza jambo kwenye kikao kilichoratibiwa na Wizara baina ya Bw. Joseph Katallah (Mwekezaji, Mtanzania anayeishi nchini Canada) na timu ya watafiti kutoka UDSM kilichofanyika katika ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaaam.
Timu ya watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakifuatalia mada iliyokuwa ikitolewa na Daipora (Mtanzania anayeishi nchini Canada) Bw. Joseph Katallah (hayuko pichani) kwenye mazungumzo yaliyofanyika katika ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaaam.

 Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Tagie Daisy Mwakawago (watano kushoto) na Bw. Joseph Katallah (wane kulia) Mtanzania anayeishi nchini Canada na Timu ya watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakiwa katika picha ya pamoja. Waengine (wapili na watatu kulia) ni Maafisa wa Kitengo cha Diaspora

No comments:

Post a Comment