Idara ya Uhamiaji ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejikita kwa nguvu kubwa katika kuzuia mianya yote inayoweza kutumiwa na wasafirishaji wa dawa za kulevya kuingia au kutoka nchini. Kwa kushirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Idara hii imeongeza ulinzi na ufuatiliaji katika mipaka ya nchi, viwanja vya ndege, bandari, vituo vya mabasi, na njia zote za nchi kavu zinazotumiwa na wasafiri.
Katika jitihada hizi, Uhamiaji hutekeleza ukaguzi wa kina kwa abiria, mizigo na nyaraka ili kuzuia watuhumiwa wa biashara ya dawa za kulevya kuingia au kutoka nchini. Hatua hizi pia hujumuisha kuzuia utoaji wa hati za kusafiria kwa watuhumiwa na kuwazuia wanaojaribu kuingiza dawa hizo nchini. Lengo kuu ni kuhakikisha Tanzania inasalia kuwa nchi salama, isiyokuwa na nafasi kwa biashara haramu ya dawa za kulevya.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameonyesha msimamo thabiti dhidi ya dawa za kulevya, akisisitiza kuwa biashara hiyo haramu huathiri uchumi wa taifa kwa kuficha fedha nyingi ambazo zingesaidia kwenye maendeleo ya jamii.
Kupitia ushirikiano huu wa kimkakati kati ya Uhamiaji na DCEA, Tanzania inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha usalama wa raia na mustakabali wa taifa unalindwa kwa nguvu zote dhidi ya janga la dawa za kulevya.
Kauli mbiu: "Wekeza kwenye Kinga na Tiba dhidi ya dawa za kulevya"
No comments:
Post a Comment