Matokeo chanyA+ online




Friday, June 7, 2019

BENKI YA AKIBA YAKABIDHI VIFAA VYA USAFI KUADHIMISHA SIKU YA MAZINGIRA 2019

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG

Katika kuadhimisha kilele cha Siku ya Mazingira Duniani Juni 05, 2019, benki ya Akiba (Akiba Commercial Bank) imekabidhi vifaa vya usafi kwa uongozi wa Soko Kuu jijini Mwanza ili kuimarisha huduma ya usafi sokoni hapo.

Hafla ya kukabidhi vifaa hivyo imeambatana na zoezi la kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya Soko Kuu jijini Mwanza ambapo wafanyakazi wa benki ya Akiba wamejumuika pamoja na wafanyabiashara sokoni hapo kufanya usafi huo.

Meneja wa benki ya Akiba tawi la Mwanza, Herieth Bujiku amesema lengo ni kuhakikisha kunakuwa na zoezi endelevu la kufanya usafi katika soko hilo na kuweka mazingira katika hali ya usafi ili kuzuia magonjwa ya milipuko huku akitoa pongezi kwa Serikali kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki.

Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba aliyepokea vifaa hivyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mwanza, John Mongella na kuvikabidhi kwa uongozi wa Soko Kuu jijini Mwanza, amesema vifaa hivyo vina umuhimu mkubwa wa kuimarisha usafi na hivyo wafanyabiashara kufanya shughuli zao katika mazingira safi na salama kiafya.

Naye Mwenyekiti wa Soko Kuu jijini Mwanza, Hamad Nchola ameishukru benki ya Akiba kwa kutoa vifaa hivyo na kuomba liwe zoezi endelevu huku akitoa rai kwa wafanyabiashara sokoni hapo kuvitumia vyema kuimarisha usafi kama ilivyo desturi yao ya kufanya usafi kila jumamosi.
Meneja wa benki ya Akiba (Akiba Commercial Bank) tawi la Mwanza, Herieth Bujiku (kulia) akimkabidhi Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba (wa pili kushoto) vifaa vya usafi vilivyotolewa na benki hiyo ili kuimarisha hali ya usafi eneo la Soko Kuu jijini Mwanza. Zoezi hilo limeambatana na shughuli ya usafi sokoni hapo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2019.
Meneja wa benki ya Akiba (Akiba Commercial Bank) tawi la Mwanza, Herieth Bujiku (kulia) akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi vifaa vya usafi ili kusaidia huduma ya usafi katika Soko Kuu jijini Mwanza. Hafla hiyo imeambatana na zoezi la usafi sokoni hapo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2019.
Vifaa vilivyokabidhiwa na benki ya Akiba ni pamoja na mifagio, mapipa ya kutunzia taka, koleo, reki, buti za usafi, glovusi, toroli na maski.
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba (katikati) akimkabidhi Mwenyekiti wa Soko Kuu jijini Mwanza, Hamad Nchola (kushoto) vifaa vya usafi vilivyotolewa na benki ya Akiba. Kulia ni Meneja wa Benki ya Akiba tawi la Mwanza, Herieth Bujiku.
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba (wa tatu kulia) akimkabidhi Mwenyekiti wa Soko Kuu jijini Mwanza, Hamad Nchola (wa pili kushoto) vifaa vya usafi vilivyotolewa na benki ya Akiba.
Meneja wa benki ya Akiba tawi la Mwanza, Herieth Bujiku akisoma taarifa fupi kuhusu vifaa vilivyotolewa na benki hiyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2019.
Meneja wa benki ya Akiba tawi la Mwanza, Herieth Bujiku akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba akizungumza kwenye hafla hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mwanza, John Mongella.
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba amehimiza vifaa vya usafi vilivyotolewa na benki ya Akiba kutumika vyema kuimarisha usafi katika Soko Kuu jijini Mwanza ambalo amesema miezi michache ijayo litaanza kujengwa upya kuwa la kisasa zaidi.
Mwenyekiti wa Soko Kuu jijini Mwanza, Hamas Nchola akitoa salamu za shukrani kwa benki ya Akiba baada ya kupokea vifaa vya usafi.
Afisa Mazingira (Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mwanza), Mangabe Mnilago akitoa salamu zake kwenye hafla hiyo.
Baadhi ya wafanyakazi wa benki ya Akiba jijini Mwanza wakijumuika na wafanyabiashara Soko Kuu jijini Mwanza kufanya usafi katika maeneo ya soko hilo. 
Wafanyakazi wa benki ya Akiba wakifanya usafi katika eneo la Soko Kuu jijini Mwanza ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira duniani 2019.
Baadhi ya wafanyakazi wa benki ya Akiba wakiwa kwenye usasi katika eneo la Soko Kuu jijini Mwanza.
Baadhi ya wafanyakazi wa benki ya Akiba jijini Mwanza wakijumuika na wafanyabiashara Soko Kuu jijini Mwanza kufanya usafi katika maeneo ya soko hilo. 
Wafanyakazi wa benki ya Akiba wamejumuika na wafanyabiashara katika Soko Kuu jijini Mwanza kufanya usafi sokoni hapo ikiwa ni sehemu ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira duniani, Juni 05, 2019.
Wafanyakazi wa benki ya Akiba wakiendelea na usafi eneo la Soko Kuu jijini Mwanza.
Wafanyakazi wa benki ya Akiba (Akiba Commercial Bank) wakiondoa uchafu katika eneo la kukusanyia uchafu lililopo Soko Kuu jijini Mwanza.

Tazama video hapa chini

HII NDIYO MIRADI YA KIMKAKATI MKOANI MWANZA

Halmashauri ya Jiji la Mwanza inatarajia kuanza utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo ni pamoja na ujenzi wa soko kuu, stendi ya mabasi Nyegesi pamoja na kituo cha maegesho ya magari makubwa Buhongwa ambapo miradi hiyo itaongeza ukusanyaji wa mapato ya halmashauri hiyo.

Hayo yalisemwa jana Juni 05, 2019 na Mkurugenzi wa Jiji hilo, Kiomoni Kibamba wakati akizungumza kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika eneo la Soko Kuu.

"Kutakuwa na "parking" ya magari zaidi ya 500 kwa wakati mmoja chini ya ardhi...ukiingia na hela unatumbukiza kwenye mashine, inakupa chenchi..." alisema Kibamba.
Tazama video hapa chini

Wednesday, June 5, 2019

TATIZO LA MAJI NANDAGALA LAWA HISTORIA

Wananchi washangilia, waishukuru Serikali kwa kuwasogezea huduma

Changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama iliyokuwa inawakabili wananchi wa vijiji vya Nandagala ‘B’ na Ingawali wilayani Ruangwa imekuwa historia baada ya Ubalozi wa Uturiki kupitia taasisi yake ya Diyanet kuwachimbia visima virefu.

Visima hivyo viwili vimekabidhiwa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo (Jumatatu, Juni 3, 2019) na Muambata wa Ubalozi wa Uturuki anayeshughulikia masuala ya jamii nchini, Muhammed Cicek. Hafla hiyo imefanyika katika kijiji cha Nandagala ‘B’.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu amesema Tanzania na Uturuki ni nchi rafiki na kwamba Serikali ya Uturuki imekuwa ikishirikiana na Serikali ya Tanzania katika uboreshaji wa huduma za jamii zikiwemo za afya, elimu na maji.

Waziri Mkuu baada ya kuvipokea visima hivyo amewataka wananchi wa vijiji hivyo kupitia kamati zao za maji zihakikishe zinaisimamia vizuri miradi hiyo na pia wawe wanatoa taarifa za mapato na matumizi ya kila mwezi.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amemuagiza Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wilaya ya Ruangwa, Samwel Pyuza ahakikishe huduma ya umeme inafikishwa katika mradi huo kwa ajili ya kusukuma maji badala ya kutumia jenereta.

Kwa upande wake, Muambata wa Ubalozi wa Uturuki anayeshughulikia masuala za jamii nchini, Muhammed Cicek amesema Watanzania na Waturuki ni ndugu, hivyo amefurahi baada ya wananchi wa vijiji hivyo kupokea zawadi ya visima hivyo walivyowakabidhi.

Wakizungumza baada ya makabidhiano hayo, baadhi ya wakazi wa kijiji cha Nandagala ‘B’ wameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kuwasogezea huduma ya maji karibu na makazi yao.

Mmoja wa wakazi hao Safina Angulupele (63) amesema awali kabla ya kisima hicho walikuwa wanapata maji kutoka katika kijiji kingine na pia hayakuwa na uhakika, hivyo uwepo wa kisima kwenye kijiji chao ni mkombozi kwao.

Naye mkazi mwingine wa kijiji hicho Zainab Issa amesema huduma ya maji safi na salama ni muhimu kwa maendeleo ya jamii, hivyo anaipongeza Serikali kwa kuwafikishia huduma karibu na makazi. “Sasa hata sisi wazee tunaweza kwenda kisimani na kuchota maji.”

Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo, imedhamiria kuwafikishia wananchi wote huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
4406
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua maji baada ya kukabidhiwa kisima cha maji cha kijiji cha Nandagala ‘B’ kilichojengwa kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uturuki nchini Juni 3, 2019. Kulia ni Muambata wa Ubalozi wa Uturuki anayeshughulikia masuala ya jamii nchini, Muhammed Cicek na kushoto ni Mkurugenzi Mkazi wa Turkish Maarif Foundation, Oguz Hamza Yilmaz. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

PROF. KABUDI AZUNGUMZA NA IDARA YA ITIFAKI YA WIZARA YAKE.

Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb.) akizungumza na Watumishi wa Idara ya Itifaki katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (hawapo pichani) alipokutana nao kwa mara ya kwanza baada ya kuteuliwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye nafasi hiyo tarehe 3 Machi 2019. 
 
Pamoja na mambo mengine, Mhe. Prof. Kabudi aliwataka Watumishi wa Wizara kubadilika na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu miongozo na maelekezo mbalimbali pamoja na kuwa wazalendo na kufanya kazi zao kwa kushirikiana na kwa weledi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa. Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. 
 
Faraji Kasidi Mnyepe, Mkurugenzi wa Idara ya Itifaki katika Wizara ya Mambo ya Nje Mhe. Balozi Grace Martin na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Katika Wizara ya Mambo ya Nje. Aidha, mazungumzo hayo ni mwendelezo wa Vikao vya Prof. Palamagamba John Kabudi na Watumishi wa Wizara yake, ambapo yamefanyika katika Ofisi ndogo jijini Dar es Salaam tarehe 04 Juni, 2019 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akutana kwa mara ya kwanza na kiting cha Itifaki cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki 
Mkuu wa Kitengo cha Itifaki cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Grace Martini akitoa maelezo ya majukumu ya kitengo hicho kwa Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi alipokutana na Kitengo hicho kwa mara ya kwanza katika ofisi ndogo za Wizara hiyo jijini Dar es Salaam. 
Sehemu ya Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Idara ya Itifaki wakimsikiliza Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi ambaye hayupo pichani alipozungumza nao 
Sehemu nyingine ya Watumishi wakifurahia jambo wakati wakimsikiliza Mhe. Prof. Kabudi (hayupo pichani) 
Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakiwa kwenye mkutano wao na Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (hayupo pichani). 
Mhe. Prof. Kabudi akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Idara ya Itifaki wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 

Tuesday, June 4, 2019

DKT. GWAJIMA AWAKUMBUKA YATIMA, AWAPA MKONO WA EID

 Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Dorothy Gwajima akiwa katika picha ya Pamoja na watoto wa kituo cha matumaini kilichopo Miuji Jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Doroth Gwajima amewataka wazazi na walezi kuwa makini na kuimarisha ulinzi na usalama wa mtoto wakati wa msimu sikukuu ya Eid.
Dr.Gwajima ameyasema hayo alipotembelea kituo cha kulelea watoto cha Nyumba ya matumaini kilichopo Kata ya Miuji Jijini Dodoma na kutoa misaada ya vitu mbali mbali kwa ajili ya sikukuu.

Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Dorothy Gwajima akifurahia kumbeba mtoto Queen wakati alipotembelea kituo cha kwatoto cha matumaini kilichopo Miuji Jijini Dodoma
“Ni wajibu wa kila mzazi kutekeleza jukumu lake la msingi la kuhakikisha mtoto yuko salama na anasherekea sikukuku katika mazingira rafiki na yenye kumjenga kimwili na kiakili zaidi bila kupata dhahama ya aina yeyote” Alisema Gwajima.
 Aidha Dr. Gwajima amekipongeza kituo hicho kwa jukumu kubwa walilo nalo lakuhakikisha watoto waliopo hapo wanapata malezi bora huku akiwaasa watoto kuzidisha upendo na mshikamano miongozi mwao.
  

Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na mtoto wakati akikagua kituo wakati wa ziara yake katika kituo cha matumaini kilichopo Miuji Jijini Dodoma
“Tunatekeleza hili kwakuwa ni wajibu wetu kuwalea watoto kwani hata sisi leo tumekuwa watu wazima kwa sababu ya juhudi za wakubwa zetu, nanyi watoto mtakuwa wakubwa kama sisi na mtakuja  kuwa viongozi wa taifa hili katika nyanja mbali mbali, hivyo pendaneni na kuishi kwa amani na msome kwa bidii” alisema Gwajima.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia masuala ya ustawi wa Jamii, OR-TAMISEMI, Rashed  Maftah, alisema zoezi hilo ni moja ya majukumu yao ya msingi na wajibu wao katika kuzihudumia Mamlaka zote 184 nchini katika kuhakikisha watoto waliokatika mazingira magumu wanapata  vituo vya kuwalea katika misingi bora na usalama wao unaimarika.

 Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Dorothy Gwajima akifurahi  katika picha ya Pamoja na mtoto Maria wa kituo cha matumaini kilichopo Miuji Jijini Dodoma
“Dini iliyosafi ni yenye kuwajali Yatima na wenye uhitaji kwa kuunganika na kushiriki nao katika mahitaji yao ya Msingi, aidha Sheria ya mtoto  namba 21 ya mwaka 2009 kanuni ya 12 inahimiza suala la kulelea watoto” Alisema Maftah.
Akizungumza kwa niaba ya Walezi wa kituo hicho, mmoja ya walezi, Sister Urea, alisema kituo hicho kina jumla ya watoto 63 na kimekuwa kikifanya kazi zake toka mwaka 1995 kwa kuhudumia watoto wanaopatikana katika mazingira magumu na ukatili wa kijinsia kutoka mikoa ya Dodoma na Singida.

Afisa Ustawi wa Jamii toka OR-TAMISEMI anayeshughulikia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi Nkinda Ziada Shekalaghe akizungumza wakati wa ziara ya Naibu Katibu Mkuu Dr.Dorothy Gwajima
Akishukuru kwa niaba ya wenzake mtoto Mariah Zahoro, alimshukuu Naibu Katibu Mkuu na ujumbe wake huku akiomba zoezi hili lisiwe la mwisho bali liwe endelevu kwani wanapopata wageni wanao watembelea wanafarijika sana.
“Tunawashukuru sana kuja kutuona na kutupatia misaada, lakini msiishie kuja kuleta misaada tu, hata kama hamna kitu msisite kuja kutusalimia na kuongea na sisi, tunaomba Mungu awazidishie pale mlipotoa na siku nyingine tena mtukumbuke” alisema Mariah.

Baadhi ya watoto katika picha ya pamoja wakimskiliza Dr.Dorothy Gwajima wakati wa ziara yake katika kituo cha matumaini kilichopo Miuji Jijini Dodoma
Kwa Mujibu wa Afisa Ustawi wa Jamii kutoka jijini Dodoma, kituo cha Nyumba ya Matumaini kilichopo Kata ya Mihuji ni moja kati ya vituo vinane vilivyopo ndani ya Halmashauri hiyo ambavyo vimekuwa mstari wa mbele kulinda haki za watoto.

SIMANJIRO YATOA MKOPO WA SH. 230.8 MILIONI KWA VIKUNDI 71

Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, imevipatia vikundi 71 vya wanawake, vijana na walemavu, sh230.8 milioni ya mikopo kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ili kuwanyanyua kiuchumi.

Ofisa maendeleo ya jamii wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Asia Ngalisoni akizungumza jana alisema vikundi hivyo ni vya kata 14 vilivyonufaika na mkopo huo.

Ngalisoni alisema mkopo huo umenufaisha vikundi 71, ambapo 59 ni vya wanawake 1,531, vikundi tisa vya vijana 238 na vikundi vitatu vya walemavu 57.

Alisema hadi mwezi Mei mwaka huu halmashauri hiyo imekusanya sh1.7 bilioni ikiwemo mapato ya ndani na marejesho ya fedha za vikundi vilivyokopeshwa awali.

"Mfuko huu unawanufaisha wananchi waliojiunga katika vikundi vyenye shughuli za ujasiriamali au vinavyokusudia kuanzisha shughuli za ujasiriamali mdogo au wa kati," alisema Ngalisoni.

Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula alisema fedha hizo zinazotolewa hazina riba hivyo vikundi hivyo vinapaswa kuchukua mikopo hiyo na kurejesha kiasi kile kile walichokopa.

"Nitoe wito kwa vikundi vyote vilivyokopeshwa na halmashauri virejeshe fedha hizo kwa wakati ili wengine nao waweze kukopa na kujikwamua kiuchumi," alisema Chaula.

"Mfuko huu unawanufaisha wananchi waliojiunga katika vikundi vyenye shughuli za ujasiriamali au kinakusudia kuanzisha shughuli za ujasiriamali mdogo au wa kati," alisema Chaula.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Jackson Sipitieck alimpongeza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri yake Yefred Myenzi kwa kusimamia ipasavyo mapato hadi kufanikisha utolewaji wa mikopo hiyo.

"Wakati halmashauri nyingine zikisuasua kufanikisha mikopo sisi Simanjiro tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani tunatoa mikopo hadi fedha nyingine zimebaki," alisema Sipitieck.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Yefred Myenzi alitoa wito kwa vijana wa eneo hilo kuchangamkia fursa hiyo kwani mwitikio wao bado ni mdogo.

"Zile fedha zenu vijana za asilimia nne mnazopaswa kupewa hamjazichukua hivyo vijana wa Simanjiro mnapaswa kubadilika ili mnufaike kupitia mikopo hii tunayoitoa," alisema Myenzi.

Katibu wa walemavu mji mdogo wa Mirerani, William Orata alisema kupitia mkopo waliopata wamefanikisha uanzishwaji wa mashine ya kusaga nafaka.

Mmoja kati ya wanawake walionufaika na mkopo huo, Susan Alanyamuna alisema wameweza kutengeneza sabuni aina ya Sidai.
IMG_20190531_114812
 Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mhandisi Zephania Chaula (kushoto) akipokea mfano wa hundi kutoka benki ya NMB.
IMG_20190531_114915
 Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mhandisi Zephania Chaula (kushoto) akipeana mkono na viongozi wa vikundi vya wanawake, vijana na walemavu baada ya kupokea mkopo uliotolewa na Halmashauri ya Wilaya hiyo
IMG_20190531_103338
 Baadhi ya vikundi vya wajasiriamali, wanawake, vijana na walemavu waliopatiwa mkopo wa sh 230.8 milioni na Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara.