Matokeo chanyA+ online




Tuesday, August 11, 2020

WAZIRI HASUNGA ATUA MKOANI TABORA NA SINGIDA, AAGIZA KUFANYIKA MAGEUZI MAKUBWA SEKTA YA KILIMO

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akishiriki zoezi la upimaji wa Pamba ya wakulima katika Kijiji cha Malendi kilichopo Wilaya ya Iramba wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya ukaguzi wa msimu wa ununuzi wa Pamba Mkoani Singida jana Tarehe 10 Agosti 2020. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akizungumza na wakulima wa Pamba katika Kijiji cha Ipumbulya kata ya Bukoko Wilaya ya Igunga wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya ukaguzi wa msimu wa ununuzi wa Pamba Mkoani Tabora jana Tarehe 10 Agosti 2020. 
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Igunga Mhe John Mwaipopo wakishuhudia Pamba ya wakulima ikishushwa kabla ya kupimwa na hatimaye kupatiwa malipo yao Wilaya ya Igunga wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya ukaguzi wa msimu wa ununuzi wa Pamba Mkoani Tabora jana Tarehe 10 Agosti 2020. 
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akishiriki zoezi la upimaji wa Pamba ya wakulima katika Kijiji cha Malendi kilichopo Wilaya ya Iramba wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya ukaguzi wa msimu wa ununuzi wa Pamba Mkoani Singida jana Tarehe 10 Agosti 2020.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Shinyanga

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga jana tarehe 10 Agosti 2020 amefanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora na Wilaya ya Iramba Mkoani Singida ambapo amekagua na kuridhishwa na hali ya ununuzi wa msimu wa Pamba kwa mwaka 2020/2021.

Waziri Hasunga amesema kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli imedhamiria kuhakikisha kuwa wakulima wanaondoka katika dhana ya kilimo cha kujikimu badala yake kuwa kilimo cha kibiashara.

Amesema kuwa ili kusimamia jambo hilo kwa vitendo tayari serikali imeanza kutoa elimu kwa wakulima kupitia Maafisa ugani na wataalamu mbalimbali wa kilimo kuhusu namna bora ya kuzingatia mbinu bora za kilimo ili kuongeza tija na uzalishaji.

Katika ziara hiyo akiwa katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora Waziri Hasunga amewahakikishia wakulima kuwa serikali inasimamia kwa weledi mkubwa sekta ya kilimo ambacho ndicho muhimili mkubwa wa maendeleo ya wananchi na ikichangia kwa asilimia kubwa uchumi wa nchi.

Hasunga amesema kuwa ili kuboresha kilimo na maisha ya wakulima ni dhahiri kuwa serikali lazima ifanye mazungumzo na Benki mbalimba ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Mfuko wa Pembejeo za Kilimo AGITF kwa ajili ya kupunguza riba na masharti magumu kwa wakulima ili waweze kukopa kwa ajili ya kuboresha kilimo chao.

Akiwa katika ziara ya Kikazi Wilaya ya Iramba mkoani Singida Waziri Hasunga ameipongeza kampuni ya ununuzi wa Pamba ya Biosustain kwa kuhakikisha kuwa imemaliza madeni yote ya wakulima wa Pamba kwa msimu wa mwaka 2018/2019 mkoa wa Singida.

Amesema kuwa pamoja na changamoto iliyojitokeza ya Ugonjwa wa Mapafu-COVID 19 lakini kampuni hiyo imehakikisha kuwa wakulima wote wanalipwa fedha zao kwa wakati.

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga jana tarehe 10 Agosti 2020 amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku mbili katika mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Tabora na Singida.


Monday, August 10, 2020

WAZIRI MKUU APONGEZA UJENZI WA MRADI WA KUONGEZA UWEZO WA KUHIFADHI NAFAKA UNAOTEKELEZWA NA NFRA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua mfano wa gunia la mahindi wakati alipotembelea Banda la Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA ametoa leo tarehe 8 Agosti 2020 kabla ya kuhitimisha maadhimisho ya sherehe za wakulima Nanenane katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Afisa Mtendaji Mkuu wa NFRA Ndg Milton Lupa akitoa maelezo ya kuhusu uhifadhi wa nafaka mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati alipotembelea Banda la Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA ametoa leo tarehe 8 Agosti 2020 kabla ya kuhitimisha maadhimisho ya sherehe za wakulima Nanenane katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu. 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua mfano wa gunia la mahindi wakati alipotembelea Banda la Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA ametoa leo tarehe 8 Agosti 2020 kabla ya kuhitimisha maadhimisho ya sherehe za wakulima Nanenane katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu. 

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Simiyu

Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa amepongeza ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa Mradi unaotekelezwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).

Waziri Mkuu ametoa pongezi hizo leo tarehe 8 Agosti 2020 wakati alipotembelea Banda la NFRA kabla ya kuhitimisha maadhimisho ya sherehe za wakulima Nanenane katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu. 

Waziri Mkuu amesema kuwa ujenzi huo ni mahususi kwa ajili ya Kuongeza Uwezo wa Kuhifadhi Nafaka kutoka tani 251,000 hadi tani 501,000. 

Akitoa taarifa ya Mradi huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa NFRA Ndg Milton Lupa amesema Mradi huo unajumuisha ujenzi wa vihenge 56 na maghala ya kisasa 9 ambavyo kwa pamoja vinaongeza uwezo wa kuhifadhi kwa tani 250,000. Kwa sasa Mradi huu umefikia umefikia asilimia 75 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2020/2021.

Amesema Uhifadhi wa nafaka kwa kutumia maghala ya kawaida, akiba inaweza kuhifadhiwa kwa takriban miaka mitatu tu kabla ya kuanza kupoteza ubora. Kwa kutumia vihenge vya kisasa, akiba inaweza kuhifadhiwa hata kwa zaidi ya miaka mitano bila kupoteza kiwango cha ubora

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ni Taasisi ya Umma chini ya Wizara ya Kilimo iliyoanzishwa chini ya Sheria za Wakala wa Serikali Na. 30 ya mwaka 1997 na kuanza kazi rasmi tarehe 1 Julai, 2008.

NFRA ina jukumu kuu la kuhakikisha usalama wa chakula ndani ya nchi kwa kununua, kuhifadhi na kutoa chakula katika maeneo yenye upungufu na kwa waathirika wa majanga mbalimbali. 


NAIBU WAZIRI ULEGA - WITO WANGU KWA WATANZANIA NI MUHIMU SANA KUNUNUA BIDHAA ZETU SISI WENYEWE TUNAZOZALISHA


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi ,Abdalah Ulega akizungumza jambo alipotembelea kiwanda cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro 
 
Serikali imesema ipo kwenye mchakato wa kutengeneza sera itayowezesha wanafunzi Mil 10 hadi Mil  20 wa shule za msingi na Sekondari wanaoanza masomo yao kutumia viatu vitakavyozalishwa na Kampuni ya bidhaa za Ngozi ya Kilimanjaro iliyopo mjini Moshi .

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdalah Ulega wakati ya ziara ya siku moja  mkoani Kilimanjaro  ambapo ametembelea  mradi wa ujenzi wa viwanda vya kuchakata bidhaa za ngozi vilivyopo chini ya kampuni ya Kilimanjaro Leather Industries Co Ltd.
 
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvivi ,Abdalah Ulega akipokea maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bidhaa za ngozi ya Kilimanjaro Mhandisi Masud Omari  wakat wa ziara yake ya siku moja kiwandani hapo.
 
Akizungumza mara baada ya kujionea hatua za ujenzi zilipofikia Naibu Waziri Ulega alisema katika kuunga Mkono Jitihada za Rais Wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dk John Joseph Pombe Magufuli za kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa viwanda, Mfuko Wa PSSSF umewekeza katika Mradi wa ujenzi wa Kiwanda kipya cha Bidhaa za Ngozi Mkoani Kilimanjaro .

“Wito wangu tu ni kwamba taasisi za serikali ,ni muhimu sana zikanunua bidhaa zetu sisi wenyewe tunazozalisha hapa sisi wenyewe hapa nyumbani ,kwa mfano watu wengi hawajaamini kama vitu vinavyotengenezwa na wajasiliamali wadogo wadogo na viwanda vyetu kama kweli ni ngozi .álisema Ulega.
 
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi ,Abdalah Ulega akitembelea maeneo mbalimbali ya kiwanda hicho.
 
“Tunalo tatizo la bidhaa hizi za plastiki yaliyokarabatiwa karabatiwa ,yameingia kwa wingi sana ,yamefanya hata wajasilia mali wetu hapa zile bidhaa wanazotengeneza sio ngozi ,lakini zile ni ngozi na watanzania tuamini kwamba zile ni ngozi.”aliongeza Ulega .

Alisema serikali inakusudia kuanza na watoto  katika mashule ya msingi na Sekondari baada ya kukubaliana na watungaji sera na viongozi katika wizara mbalimbali ambapo watoto kati ya Mil 10 na 20 watapata viatu
 
Moja ya majengo ya kiwanda hicho yaliyojengwa katika awamu ya kwanza ya mradi huo
 
Mkurugenzi mtendaji wa kiwanda hiki Mhandisi Masud Omar amesema Kampuni hiyo  pamoja na kampuni za Italia ,TMC na ITALPROGETTI wapo kwenye taratibu za mwisho za kuanza kazi ya kusimika mitambo na kwamba  janga la virusi vya Corona vimechangia kuchelewa kwa kazi hiyo.

“Ili kutekeleza agizo la Serikali, Kampuni ijulikanayo kwa jina la “Karanga Leather Industries Co Ltd” (KLICL) ilianzishwa mnamo tarehe 30 Mei, 2017 kwa lengo la kuanzisha mradi wa viwanda vya bidhaa za ngozi katika eneo la Gereza la Karanga, Moshi, Kilimanjaro kwa lengo la kuboresha kiwanda cha ngozi kilichopo na baadae kujenga kiwanda kipya cha kisasa cha utengeneaji wa ngozi na bidhaa zake. “alisema Mhandisi Omari .
 
Sehemu ya mashine zilizofika kwa ajili ya kusimikwa katika kiwanda hicho.
 
Mhandisi Omari alisema kampuni hiyo ilianzishwa kwa ubia kati ya uliokuwa Mfuko wa Pensheni wa PPF, ambao kwa sasa majukumu yake yamechukuliwa na PSSSF pamoja na Jeshi la Magereza kupitia kampuni yake ya Prisons Corporation Sole.

“Hatua ya kwanza (LOT 1) ya utekelezaji wa mradi inayohusisha ujenzi wa kiwanda cha viatu yaani ujenzi wa jengo ya Ukataji na ushonaji, umaliziaji, ghala na nyumba ya umeme yamekamilika na mmiliki ameanza kuyatumia kwa matumizi ya kiofisi.

Alisema ujenzi huu umeenda sambamba na uwasilishwaji wa mitambo ambapo mitambo yote kwaajili ya kiwanda hivi vilivyokamilika vishawasili katika eneo la kiwanda huku zikisubiria wataalamu kutoka Italia kuja kuzifunga.
 
Awamu ya pili ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakta ngozi ukiendelea katika eneo lililopo jirani na Gereza la Karanga mjini Moshi.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi ,Abdalah Ulega akitizama mashine za kuchakata ngozi alipotembelea kiwanda cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro .
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bidhaa za Ngozi ya Kilimanjaro Mhandisi Masud Omari akiumuonesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi moja ya mashine zitakazotumika katika kuchakata ngozi katika kiwanda hicho .
Mashine kwa ajili ya kuchakata Ngozi ambazo zinatarajiwa kufungwa katika kiwanda cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro .

Na Dixon Busagaga ,Kilimanjaro

Kiwanda kipya kimejengwa katika eneo  la hekari 25  lililotengwa katika Gereza la Karanga Manispaa ya Moshi Mjini huku uzalishaji wa kiwanda hiki ukitazamiwa kuzalisha jozi 4,000 za viatu kwa siku sawa na jozi 1,200,000 kwa mwaka.

MAKAMU WA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AFUNGUA MKUTANO WA BARAZA KUU LA WANAWAKLE TANZANIA (UWT)

 



Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akihutubia Wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Baraza hilo uliofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Jijini Dodoma leo Agostui 10,2020. 

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akimtunuku Tuzo Maalum Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kwa kutambua mchango wake na kuwawakilisha Wanawake Vizuri katika majukumu yake, wakati  wa Ufunguzi wa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT uliofanyika leo Agosti 10,2020 katika Ukumbi wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Jijini Dodoma. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa jukumu la kulainisha mitambo ya uchaguzi kwa upande wa Chama cha Mapinduzi imekabidhiwa kwa Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT) 

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akihutubia Baraza kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) katika ukumbi wa White House mjini Dodoma, amesema kuwa jukumu la kampeni ni jukumu zito.

"Jukumu hili ukilichambua kiundani ni jukumu zito sana kujitoa na kujitolea kwa sababu kazi tunayokwenda nayo kuanza ya kampeni si kazi nyepesi" Makamu wa Rais

Makamu Rais amesema kuwa inahitaji uadilifu na umakini mkubwa  kwani Chama Cha Mapinduzi ni kikubwa na kinahitaji ushindi mkubwa.

WAZIRI HASUNGA AANZA ZIARA YA UKAGUZI WA MSIMU WA UNUNUZI WA PAMBA SIMIYU NA SHINYANGA

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akizungumza na viongozi wa Chama cha Ushirika cha Ngolomamali kilichopo Wilayani Itilima leo Tarehe 9 Agosti 2020 wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Simiyu kukagua msimu wa ununuzi wa Pamba mwaka 2020/2021. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akizungumza na viongozi wa Chama cha Ushirika cha Maendeleo kilichopo Wilayani Itilima leo Tarehe 9 Agosti 2020 wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Simiyu kukagua msimu wa ununuzi wa Pamba mwaka 2020/2021

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akizungumza na viongozi wa Chama cha Ushirika cha Maendeleo kilichopo Wilayani Itilima leo Tarehe 9 Agosti 2020 wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Simiyu kukagua msimu wa ununuzi wa Pamba mwaka 2020/2021

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa  Chama cha Ushirika cha Malita kilichopo Wilayani Maswa leo Tarehe 9 Agosti 2020 wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Simiyu kukagua msimu wa ununuzi wa Pamba mwaka 2020/2021

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Simiyu

Baada ya kumalizikia kwa Sherehe za Wakulima (NANENANE) Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga leo Tarehe 9 Agosti 2020 ameanza ziara ya kikazi katika Mikoa ya Simiyu na Shinyanga ambapo pamoja na mambo mengine atakagua msimu wa ununuzi wa Pamba mwaka 2020/2021.

Ktiaka ziara hiyo Waziri Hasunga amemuagiza Mrajis wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt Benson Ndiege kwa kusaidiana na Warajis wasaidizi wa Ushirika wa mikoa kuhakikisha kuwa wanatoa elimu ya kutosha kwa wanachama wa vyama vya Ushirika ili kuwa na elimu ya kutosha kuhusu usimamizi wa mali za ushirika, kadhalika umuhimu Ushrika.

Kutokana na Wakulima kulalamikia mfumo wa kuwalipa fedha wakulima wa Pamba kupitia kwenye Account za Benki, Waziri wa Kilimo amemuagiza Mrajis Msaidizi wa Vyama Vya Ushirika Mkoa wa Simiyu Ndg Ibrahim Kadudu kuzielekeza kampuni zinazonunua Pamba kuwalipa fedha taslimu wakulima wenye kiasi kidogo cha Pamba.

Agizo hilo limetokana na malalamiko ya viongozi wa vyama vya Ushirika alivyotembelea na kukagua msimu wa ununuzi wa Pamba ambavyo ni Maendeleo AMCOS na Ngolomamali AMCOS za Wilayani Itilima pamoja na Malita AMCOS kilichopo Wilayani Maswa.

Waziri Hasunga amesema kuwa Wizara yake imejipanga kufanya mazungumzo na Benki mbalimbali nchini pamoja na kampuni za simu ili kujadili uwezekano wa kupunguza bei za makato ya wakulima. “Dhamira yetu sisi kama serikali tunataka mkulima apate kiasi anachostahili kutokana na jasho lake makato makato sio sawa” Alisema

Pia, Waziri Hasunga amewataka wakulima wa Pamba nchini ambao hawajalipwa fedha zao kuwa wavumilivu wakati huu ambapo serikali inaendelea kulitafutia ufumbuzi jambo hilo ili kulitatua.

Katika Mkoa wa Simiyu wakulima wanadai Bilioni 2.9 ambapo tayari imeshawalipa wakulima kiasi cha takribani Bilioni 414.4 kati ya Bilioni 419 zilizokuwa zinadaiwa na wakulima wa Pamba kote nchini.


Sunday, August 9, 2020

NAIBU WAZIRI DKT ANGELINE MABULA AMTEMBELEA MJANE WA BABA WA TAIFA BUTIAMA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimsikiliza mjane wa Baba wa Taifa Hayati Mwl Julius Kambarage Nyerere Bi Maria Nyerere alipomtembelea nyumbani kwake Butiama mkoa wa Mara jana wakati akiwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi.


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiagana na  mjane wa Baba wa Taifa Hayati Mwl Julius Kambarage Nyerere Bi Maria Nyerere alipomtembelea nyumbani kwake Butiama mkoa  wa Mara jana wakati akiwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amemtembelea Mjane wa Baba wa Taifa Julius Kambarage Nyerere Mama Maria Nyerere nyumbani kwake Butiama mkoa wa Mara.

Dkt Mabula alikuwa katika ziara ya siku moja wilayani Butiama kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi sambamba na kugawa hati za ardhi kwa wananchi wa Butiama mkoani Mara waliopimiwa na kumilikishwa maeneo yao.

Naibu Waziri mbali na kutembelea wilaya ya Butiama pia alitembelea wilaya za Musoma, Rorya na Tarime ambako alizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi, alikagua mfumo wa ukusanyaji kodi ya pango la ardhi na kufuatilia maelekezo aliyoyatoa kuhusiana na masuala ya ardhi.

 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na wananchi wa Butiama mkoa wa Mara baada ya kuwakabidhi Hati ya Ardhi jana  wakati wa  ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi mkoa wa Mara (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).

WAFANYABIASHARA WADOGO MWANZA WANUFAIKA NA MIKOPO NBC

Mfanya biashara wa jijini Mwanza Grace Meshaki maarufu kama Mama Kweka (katikati) akitoa ushuhuda mbele ya Mkurugenzi wa Benki ya NBC, Theobald Sabi (Kulia) akieleza namna Benki ya NBC ilivyompatia mkopo mpaka sasa anamtaji wa Zaidi ya milioni 250 kutoka milioni 17 katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa kutoa mikopo kwa wafanya biashara wadogo na kati iliyofanyika Gold Crest jijini Mwanza mwishoni mwa wiki. Kushoto ni Meneja wa Tawi la NBC Mwanza, Rodgers Masolwa.
Mkurugenzi mtendaji wa Benki ya taifa ya NBC hapa nchini Theobard Sabi akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa benki ya NBC Mkoa wa Mwanza katika hafla ya uzinduzi wa Mradi kutoa mikopo nafuu kwa wafanya biashara wadogo na wakati jijini Mwanza

Mfanyabiashara wa jijini Mwanza, Grace Kweka, ambaye amenufaika kupitia Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) amewataka watanzania kutoogopa kwenda kukopa benki kwa sababu taasisi hizo zimeanzishwa kwa ajili ya wananchi kukuza uchumi wao.

Akizungumza jijini hapa jana katika hafla maluum iliyoandaliwa na NBC na kukutanisha wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa kutoka mikoa ya kanda ya ziwa ambao ni wanufaika wa benki hiyo, Kweka alisema alianza na mkopo wa Sh milioni 17 mwaka 2005 sasa amefikia kiwango cha Sh milioni 300.

Alisema baadhi ya wafanyabiashara hasa wanawake wamekuwa wakiogopa kukopa katika taasisi za kifedha hivyo kujikuta wanashindwa kukuza mitaji yao wakati ipo benki maalum iliyolenga kuwainua wafanyabiashara wa ngazi zote.

“NBC ni benki yetu wafanyabiashara tuitumie vizuri ili tunufaike nayo riba zake ni rafiki, mimi nilianza nikiwa mjasiriamali lakini sasa ni mfanyabiashara wa kati, kikubwa ambacho nawasihi wafanyabiashara wenzangu ni uaminifu na kufanya biashara kwa kujituma ili kuweza kurejesha mkopo kwa wakati,”alisema na kuongeza.

“NBC ni benki inayosikiliza wateja wake, binafsi nimenufaika sana kupitia benki hii, hata kipindi cha corona niliwafuata nikawaeleza kwamba sasa sijaagiza mzigo kutoka nje tukazungumza wakanipunguzia riba kitendo hiki kinaonyesha kweli wamedhamiria kutuinua wafanyabiashara,”alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, alisema lengo la benki hiyo ni kuhakikisha sekta binafsi inaendelea kupata sapoti ya kifedha kama mikopo na huduma za kibenki ili kuongeza uwezo wao wa kiuchumi na kukuza shughuli zao za uzalishaji hivyo kuwezesha uchumi wa nchi kuwa wa ushindani na kulifanya taifa kufikia uchumi wa kati.

Mkurugenzi wa Kitengo cha biashara kwa wateja wadogo na wakati kutoka NBC, Elvis Ndunguru, alisema lengo lakukutana na wafanyabiashara hao ni kuzungumza nao kuhusu bidhaa za kibenki ambazo benki hiyo inazitoa ili kuwawezesha wajasiriamali kukuza shughuli zao za kiuchumi.

“Leo tutawaeleza wafanyabiashara kuhusu bidhaa za mikopo tunazozitoa ambazo zimeondolewa dhamana kwa wafanyabiashara wanaofanya biashara na makampuni makubwa,” alisema.

Friday, August 7, 2020

SERIKALI YATEKELEZA AHADI YA RAIS MAGUFULI MBALIZI MKOANI MBEYA


Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) akiwa kwenye moja ya vituo 10 vya Mradi wa Maji wa Shongo-Mbalizi katika Kitongoji cha Usahandeshi kwenye Mji mdogo wa Mbalizi, mkoani Mbeya.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga akimtua ndoo kichwani mmoja wa akina mama katika Kitongoji cha Usahandeshi kwenye Mji mdogo wa Mbalizi, mkoani Mbeya.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga akikagua chanzo cha maji cha Mradi wa Maji wa Shongo-Mbalizi unaohudumia Mji mdogo wa Mbalizi, mkoani Mbeya.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga akiongoza timu ya wataalam wa Mkoa wa Mbeya wakitoka kukagua chanzo cha Mradi wa Maji wa Shongo-Mbalizi katika Wilaya ya Mbeya Mjini, mkoani Mbeya.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga akipokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji vijijini ya Mkoa wa Mbeya kutoka kwa Katibu Tawala wa Mkoa Mbeya, Mariam Mtunguja.
Ujenzi wa tenki la maji la Mradi wa Maji wa Shongo-Mbalizi ukiwa katika hatua za mwisho kukamilika katika Wilaya ya Mbeya Mjini, mkoani Mbeya.


Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya UWASA) kwa kutekeleza kwa haraka ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ya kufikishia huduma ya majisafi na salama kwa wananchi wa Mji Mdogo wa Mbalizi, mkoani Mbeya.

Ametoa pongezi hizo mara baada ya kutembelea mradi wa Maji wa Shongo-Mbalizi katika Wilaya ya Mbeya Mjini ikiwa ni ufuatiliaji wa utekelezaji wa maelekezo ya Rais Magufuli ya kuwaondolea kero ya ukosefu wa majisafi na salama wananchi wa Mbalizi aliyoitoa Aprili 27, 2019 kwa Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa.

Mhandisi Sanga amefurahishwa kuona ahadi ya Rais Magufuli kwa wananchi wa Mbalizi imetekelezwa, kwa mradi kufanya kazi na wananchi wameanza kunufaika kufuatia maelekezo aliyoyatoa wakati alipopita katika mji wa Mbalizi akiwa ziarani mkoani Mbeya ya kuhakikisha wananchi hao wanapata huduma ya majisafi na salama haraka.

Awali akiwasilisha taarifa ya mradi huo wa Sh. bilioni 3.3, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya UWASA), Mhandisi Ndele Mengo alisema ulianza kujengwa Julai 1, 2019 na kazi imefikia asilimia 98 na huku idadi ya wananchi waliounganishwa na huduma wamefikia 108 pamoja na vituo 10 vya kuchotea maji, ukiwa na uwezo kuzalisha kiasi cha lita milioni 10 kwa siku ukilinganisha na maji yanayotumika kwa sasa ya kiasi cha lita milioni nne kwa siku kutokana na maunganisho yaliyokwisha fanyika.

Mhandisi Sanga ameitaka Mbeya UWASA kuhakikisha inaongeza mtandao wa maji na kufikia wateja wengi zaidi, akisema ipo haja ya kuwafikia wananchi wengi zaidi kutokana na ukubwa wa mradi na kutimiza dhamira ya Rais Dkt. Magufuli ya wananchi wote kufikiwa na huduma ya majisafi na salama.

Akizungumza mbele ya Katibu Mkuu, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Usahandeshi, Joster Mwalingo alimshukuru Rais Magufuli kwa kutimiza ahadi yake kwa wananchi wa Mbalizi na kuipongeza Wizara ya Maji kwa kukamilisha haraka mradi huo kwa kuwa tangu kuanzishwa kwa kitongoji hicho kianzishwe hakijawahi kuwa na huduma ya maji.

SERIKALI YATOA ML 200 KUBORESHA HUDUMA YA MAJI MBINGA

 Meneja Ufundi wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira manispaa ya Songea(Souwasa)Jafari Yahaya aliyenyoosha mkono akitoa maelelezo kwa wajumbe wa bodi ya mamlaka hiyo waliotembelea mradi wa maji Myangayanga Halmashauri ya mji Mbinga.


Wizara ya Maji  imetoa  shilingi milioni 200,135,522.40 kujenga tenki kubwa la maji linalojengwa na Mamlaka ya maji safi na Usafi wa mazingira manispaa ya Songea(Souwasa)  ikiwa ni mwendelezo wa mkakati wake  kuboresha  huduma ya maji kwa wananchi wa mji  wa Mbinga.

Meneja wa Souwasa Mhandisi Patrick Kibasa alisema, kati ya fedha hizo  milioni 120,000,000.00 zimetolewa na wizara ya maji kwa ajili kutekeleza mradi huo ambao utakapoanza kutoa huduma utamaliza kero ya  maji kwa wakazi  takribani elfu kumi na mbili wa kata tatu ya Matarawe , Bethlehem na Ruhuwiko katika Halmashauri ya mji Mbinga.

Hata hivyo, fedha zilizosalia milioni 80,135,522.40 bado hazijatolewa na zinahitajika sana kumalizia kazi zilizosalia katika ujenzi wa tenki hilo ambalo hadi sasa  ujenzi wake umefikia asilimia 95 na kwa upande wa malipo yaliyotolewa na  asilimia 60.

Alisema, katika mradi huo kazi zilizopangwa kufanyika ni kusafisha eneo,kuchimba msingi,kumwaga zege la msingi wa tenki,kusuka nondo kwa ajili ya msingi na kusuka nondo za ukuta wa tenki.

Kibasa alitaja kazi nyingine kumimina zege la ukuta wa tenki,kumimina zege la ukuta wa paa la tenki,kufunga bomba za kuingiza na kutolea maji, na kujenga uzio na kwa mujibu wake, kazi zilizofanyika katika mradi huo ni kusafisha eneo,kuchimba msingi  na kumwaga zege la msingi wa tenki.

Aidha, kazi  zilizofanyika ni kusuka nondo kwa ajili ya msingi,kusuka nondo za ukuta,kumimina zege la ukuta,kumimina zege la paa na kupiga plasta katika ukuta wa tenki na mradi  umekamilika kwa shughuli za ujenzi(civil works) hivyo kazi zilizosalia zinahitaji fedha ili kukamilisha ujenzi wake.

Alisema, kwa sasa tenki hilo haliwezi kutumika mpaka kazi ya  usambazaji na ulazaji mabomba ukamilike katika eneo la Lusaka na Mamlaka imeomba  shilingi milioni bilioni 1,271,810,561.00 kwa ajili ya ujenzi wa bomba kuu la kusafirisha maji kutoka Kipunga hadi  eneo la Mahela.

Kwa upande wake meneja ufundi wa Souwasa Jafari Yahaya alisema, mamlaka hiyo inatekeleza miradi ya maji katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Ruvuma na miradi hiyo inafadhiliwa moja kwa moja Serikali ya Tanzania.

Alitaja miradi hiyo,ujenzi wa mradi mkubwa wa maji katika mji wa  Namtumbo unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi ml 863,046,567.70 ulioanza kutekelezwa  mwezi Oktoba mwaka jana  ambao unatarajia kuhudumia wakazi 10,738 wanaoishi katika vitongoji vya mji  huo.

Mradi mwingine unaotekelezwa ni wa vijiji vinne vya Litowa,Litisha,Nakahuga na Peramiho B  katika halmashauri ya wilaya Songea  kwa gharama ya shilingi bilioni 2,457,267,930.00 ambapo mpaka sasa fedha zilizotolewa shilingi 420,000,000.00.

Meneja wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mji wa Mbinga(Mbiuwasa)ambao ni wasimamizi wa mradi huo Patrick Ndunguru alisema, mradi wa tenki la maji utakapoanza kutoa huduma utasaidia kumaliza kero ya maji kwa wakazi takribani 12,500 kutoka kata tatu za Ruhuwiko,Bethlehem na Matarawe.

TANZANIA YASAINI MKATABA WA MAPITIO WA GEORGETOWN WA JUMUIYA YA NCHI ZA AFRIKA, CARIBBEAN NA PACIFIC

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


TANZANIA  YASAINI MKATABA WA MAPITIO WA GEORGETOWN WA JUMUIYA YA NCHI ZA AFRIKA, CARIBBEAN NA PACIFIC

 

Dodoma, 06 Agosti 2020

Tanzania imesaini Mkataba wa mapitio wa Georgetown unaosimamia  mahusiano na uendeshaji wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Caribiani na Pasifiki ambayo zamani ilikuwa ikiitwa  ACP na sasa Organisation of African, Carribean and Pacific States (OACPS) iliyo na nchi wanachama 79.


Mkataba huo ulisainiwa na balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji,  Mhe. Jestas Abuok Nyamanga kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Brussels, Ubelgiji tarehe 31 Julai 2020. Hivyo Tanzania inakuwa nchi ya 42 kati ya nchi 79 kusaini Mkataba wa mapitio wa Georgetown.


Mkataba wa Georgetown umefanyiwa mapitio ili uweze kuendana na wakati kwa kuzingatia mabadiliko makubwa yanayoendelea kutokea duniani katika nyanja za  kisiasa, kiuchumi, kijamii na kimazingira tangu kuanzishwa kwa ACP mwaka 1975. Mchakato wa kufanya mapitio ya mkataba huu ulianza mwezi Machi 2013 kupitia timu maalum iliyoanzishwa kukusanya maoni na kuleta mapendekezo chini ya Uenyekiti wa Rais Mstaafu wa Nigeria, Mhe. Olusegun Obasanjo.


Aidha, Mwaka 2019 mchakato wa mapitio hayo ulihitimishwa kwa  kuridhiwa na Wakuu wa Nchi na Serikali wa nchi za OACPS katika mkutano wao uliofanyika mwezi Desemba 2019 jijini Nairobi, Kenya.


Mkataba wa Georgetown ndiyo ulianzisha ACP mwaka 1975 katika mji wa Georgetown nchini Guyana.  Tanzania ilisaini Mkataba huo wa awali tarehe 11 Desemba 1975 na imedumu ikiwa mwanachama wa ACP tangu wakati huo.


Pamoja na kuwa mwanachama Tanzania imekuwa ikinufaika katika masuala ya kiuchumi, kijamii, biashara, na uwekezaji kupitia ushirikiano maalum baina ya nchi za ACP na Umoja wa Ulaya unaosimamiwa na mikataba ya Lome na Cotonou. Vilevile miradi ya ubia wa maendeleo na ile ya mtangamano wa nchi za ACP chini ya ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo wa Ulaya. Pia ushirikiano katika masuala ya kubadilishana ujuzi na uzoefu na nchi za ACP, mshikamano wa kisiasa na kidiplomasia katika kutetea maslahi ya Tanzania kimataifa kupitia jukwaa la ACP.

 

Imetolewa na;

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali

Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga akisaini Mkataba wa Mapitio wa Georgetown  mjini Brussels – Ubelgiji tarehe 31 Julai, 2020.
Nyamanga (katikati), Maafisa wa Ubalozi, na Mwanasheria wa Jumuiya ya OACPS, Dr Emmanuel Opoku wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukamilisha zoezi la utiaji saini Mkataba huo. 

 

Thursday, August 6, 2020

WANANCHI WA MKOA SIMIYU WAMERIDHISHWA NA ELIMU INAYOTOLEWA NA MAMLAKA YA USIMAMIZI WA WANYAMAPORI TANZANIA TAWA

IMG-20200805-WA0025.jpg

Baadhi ya maafisa wa TAWA wakiwa nje ya banda la mamlaka hiyo katika viwanja vya maonyesho ya Kilimo nane nane yanaoendelea  katika viwaja vya  Nyakabindi  mkoani Simiyu.
IMG-20200805-WA0010.jpg

Wananchi wakipata elimu katika banda la TAWA atika viwanja vya maonyesho ya Kilimo nane nane yanaoendelea  katika viwaja vya  Nyakabindi  mkoani Simiyu.


Wananchi  wa Mkoa Simiyu wamesema kuwa wameridhishwa na elimu inayotolewa na Mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori Tanzania TAWA katika maonyesho ya Kilimo nane nane  yanayoendelea katika viwaja vya  Nyakabindi  mkoani humo.

Hayo yamebainika mara baada ya wanachi hao kufika katika Banda la TAWA na kupatiwa elimu masuala mbalimbali hasa ya ufugaji wa wanyamapori kufuatia agizo la Mhe   Rais Dakta  John Pombe Magufuli kuwataka wananchi kufuga wanyamapori.

Akitoa maelezo kwa wananchi hao Mkuu wa kitengo cha habari wa TAWA Twaha Twaibu amewaeleza wananchi hao utaratibu wa kuanzisha mashamba,bustani na ranchi za wanayamapori  kwa mujibu wa sharia.

Twaha amesema kuwa mambo ya msingi wa kuzingatia wakati wa kuhitaji kufungua maeneo ya ufugaji wa wanyamapori  ni pamoja na kuwa na eneo la mradi,kuwa na andiko la mradi,kupata ushauri wa wataalamu kuhusu mradi uliopendekezwa .

Mengine ni pamoja kusajili mradi kwa BRELA jina la biashara au kampuni pamoja na kuhakiki eneo ikiwa ni pamoja na kufanya tathimi ya athari ya mazingira ya mradi pendekezwa.

Sanjari na hayo amesema kuwa baada ya kupewa leseni,mradi wa ufugaji wa wanayamapori unatakiwa kusajiliwa uhai wa usajili wa miaka 15

Aidha TAWA katika maonyesho hayo imetoa elimu kuhusu uanzishwa wa mabucha ya kuuza nyamapori.

Hata hivyo Mkuu wa kitengo cha habari wa Mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori Tanzania TAWA Twaha Twaibu amewataka wananchi kuwa na utarabu wa kutembea vivutio hasa vinavyosimamiwa na mamlaka hiyo.