Matokeo chanyA+ online




Tuesday, April 20, 2021

VIONGOZI WA SERIKALI WAPIKWE NA TAASISI YA UONGOZI - WAZIRI MCHENGERWA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mohamed Mchengerwa amezitaka  Wizara, idara na taasisi za Serikali kuhakikisha zinapitisha viongozi wake katika mafunzo yanayoandaliwa na kutolewa na Taasisi ya UONGOZI.   
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mohamed Mchengerwa amezitaka  wizara, idara na taasisi za Serikali kuhakikisha zinapitisha viongozi wake katika mafunzo yanayoandaliwa na kutolewa na Taasisi ya UONGOZI.

Mchengerwa ameyasema hayo Aprili 19,221  wakati wa ziara yake katika taasisi hiyo ambapo amesema taasisi zote hapa nchini ambazo zina watumishi wa umma wajipange, watenge bajeti zao kuhakikisha kwamba wanapita kwenye taasisi hii ili tuweze kupikana zaidi.

"Na wale ambao tunaamini wanaweza kutusaidia, tuwatumie. Tunao Wakuu wa Mikoa ambao wana uzoefu zaidi, waiteni na kuwatumia ili kuendelea kutoa elimu. Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambao ni vijana na pengine wanadhani wao wakishateuliwa ndiyo wameshamaliza, kwamba hakuna mamlaka ya kuwachunguza na kuwafuatilia, ni lazima tuzingatie sana,” amesema Waziri huyo.

Aidha, Waziri Mchengerwa ametoa  msisitizo kuhusu suala la utendaji kazi kwa wizara, idara na taasisi zote za serikali; ikiwemo kuhakikisha kwamba stahiki za watumishi wa umma zinapatikana kwa wakati na kwa mujibu wa sheria, kuhakikisha  watumishi wanaokaimu nafasi mbalimbali kwa muda mrefu waweze kuthibitishwa katika nafasi hizo.

Endapo wana sifa zinazostahili, na kuhakikisha maadili na taratibu za utumishi wa umma zinazingatiwa ili kuleta ufanisi katika kazi na huduma zitolewazo kwa wananchi.

Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI Kadari Singo, akimkaribisha Waziri Mchengerwa kuongea na watumishi wa Taasisi hiyo.
Waziri Mchengerwa (Kushoto) akisikiliza wasilisho juu ya programu za Taasisi ya UONGOZI, pembeni yake ni Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo.
Waziri Mohamed Mchengerwa akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Taasisi ya UONGOZI.

RAIS SAMIA AFANYA UTEUZI WA VIONGOZI 8

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali kama ifuatavyo;

1.  Amemteua Dkt. Richard J. MASIKA kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT). Uteuzi huu umeanza tarehe 16 Aprili, 2021.  Dkt. MASIKA anachukua nafasi ya Marehemu Prof. Apollinary Elikana PELEKA.

 

2.  Amemteua Prof.  Joseph J. MSAMBICHAKA kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC).  Uteuzi huu umeanza tarehe 15 Aprili, 2021.  Prof. MSAMBICHAKA anachukua nafasi ya Prof. Manase Peter SALEMA.

 

3.   Amemteua Dkt. Revocatus Petro MUSHUMBUSI kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI).  Uteuzi huu umeanza tarehe 16 Aprili, 2021.  Dkt. MSHUMBUSI anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Ladislaus NSHUBEMUKI ambaye amestaafu.

 

4.  Amemteua Prof. John W.A. KONDORO kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) baada ya kumaliza muda wa kipindi cha kwanza. Uteuzi huu umeanza tarehe 15 Aprili, 2021.

 

5.  Amemteua Dkt. Mboni A. RUZEGEA kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB). Uteuzi huu umeanza tarehe 16 Aprili, 2021.  Dkt. RUZEGEA anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Ali MCHARAZO ambaye amestaafu.

 

6.  Amemteua Prof. Esther Hellen LUGWISHA kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali baada ya kumaliza muda wa kipindi cha kwanza. Uteuzi huu umeanza tarehe 15 Aprili, 2021.

 

7.  Amemteua Kept. Ernest Mihayo BUPAMBA kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Bahari Dar es Salaam (Dar es Salaam Maritime Institute – DMI) baada ya kumaliza kipindi cha kwanza. Uteuzi huu umeanza tarehe 15 Aprili, 2021.

 

8.  Amememteua Prof. Makenya MABOKO kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) baada ya kumaliza muda wa kipindi cha kwanza. Uteuzi huu umeanza tarehe 15 Aprili, 2021.

 

RAIS SAMIA AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA SPIKA WA BUNGE JOB NDUGAI

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwa katika mazungumzo na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Yustino Ndugai leo tarehe 20 Aprili, 2021 Ikulu Jijini Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiagana na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Yustino Ndugai mara baada ya mazungumzo yao leo tarehe 20 Aprili, 2021, Ikulu Jijini Dodoma.

WAZALISHAJI WA DAWA NCHINI WATAKIWA KUONGEZA KASI


Na.WAMJW- Dar es Salaam.

Wazalishaji wa  dawa na vifaa tiba wote nchini wametakiwa kuongeza kasi ya uzalishaji dawa kwa kushirikian na Bohari ya Dawa(MSD) ili kuondokana na changamoto ya bidhaa hizo nchini.

Rai hiyo ilimetolewa Leo na  Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto- Afya Prof. Abel Makubi wakati alipotembelea Bohari ya Dawa na kuongea na wazalishaji wa dawa na vifaa tiba nchini.

"Tunawashukuru kwa uzalendo wenu wa kuwekeza nchini, pokeeni  salamu kutoka kwa  Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima na Manaibu Waziri".

Hata hivyo Prof. Makubi amewataka wazalishaji hao kushirikiana na MSD katika kuhakisha dawa zao zinawafikia wananchi wa vijijini ili kuweza kutatua changamoto ya Dawa Kwenye vituo vya kutolea Huduma za afya nchini.

Aidha, Katibu Mkuu huyo  amewahakikishia Wazalishaji hao kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana nao na  kuhakikisha eneo la  uzalishaji dawa linakua ili kupunguza utegemezi wa dawa kutoka nje ya nchi.

"MSD ni chombo chetu Cha kuwatumikia wananchi hivyo ni vyema kukipa ushirikiano ili upatikanaji wa dawa,vifaa na vitendanishi ziwepo wakati wote".Alisisitiza Prof. Makubi.

Aliongeza kuwa ni wakati Sasa wa kuanza ukurusa Mpya kati ya Wazalishaji na MSD kwani utawala Bora  unajengwa kwa misingi ya Uzalendo, Uaminifu, na Kuaminiana .

Kwa upande wa Bei za bidhaa za Dawa, Katibu Mkuu huyo aliwataka Wazalishaji kukaa pamoja na MSD kupitia upya bei za bidhaa ili ziwe na uhalisia wa soko bila kuumiza Wananchi.

Licha ya hayo Prof. Makubi  amewaahidi kuwa  Serikali itawalipa kwa wakati Wazalishaji wote ambao watatoa ushirikiano wa kuleta dawa na vifaa kwa wakati na kwa ukamilifu.

Nao Wazalishaji hao ambao ni wamiliki  wa viwanda vya dawa na bidhaa nyinginezo za afya nchini wameahidi kutoa ushirikiano kwa Serikali katika kuboresha upatikanaji wa dawa nchini na kuuunga mkono Serikali iliyoko madarakani inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.





 

Friday, April 16, 2021

TANZANIA ITAENDELEA KUSHIRIKIANA NA INDIA KATIKA KUHAKIKISHA MAZINGIRA BORA YA KIBIASHARA KWA WAFANYABIASHARA


Waziri wa Viwanda na Biashara Prof, Kitila Mkumbo amesema Tanzania itendelea kushirikiana na India katika kuhakikisha mazingira bora ya kibiashara kwa wafanyabiashara pamoja na kuendeleza za uhusiano wa kidplomasia kijamii na kiuchumi  katika nchi hizo.


Prof Mkumbo ameyasema hayo alipokuwa akishiriki katika mkutano kibiashara  kwa njia ya mtandao  kati ya India na Tanzania uliofanyika katika ofisi za Wizara zilizopo Mtumba jijini Dodoma.

Mkutano huo umelenga kujadiliana kuhusu fursa za biashara zilizopo, kuimarisha ushirikiano wa kibiashara, kubadilishana uzoefu na kuonyesha   maeneo muhimu ya biashara kati ya India na Tanzania.

Akiongea katika kikao hicho kilichohudhuriwa na Balozi wa India nchini Tanzania na Balozi wa Tanzania nchini India, pamoja na wenyeviti wa wafanyabiashara katika nchi hizo, Waziri Prof Mkumbo amewashauri wawekezaji kutoka India kuwa wakiwekeza Tanzania wataweza kuuza bidhaa na huduma zao katika nchi za Afrika Mashariki (EAC) na nchi za Jumuiya  ya Maendeleo kusini mwa Afrika(SADC) bila ushuru wa forodha na ukomo wa kiwango cha bidhaa kama ilivyo kwa kwa wafanyabiashara wa Tanzania.

Akiwahimiza wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania, amesema kuwa Tanzania ni mwananchama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yenye ukubwa wa soko lenye idadi ya watu wasiopungua milioni 177. Pia Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Maendelea Kusini mwa Afrika yenye  ukubwa wa soko lenye idadi ya watu  zaidi  milioni 300. Vilevile Tanzania iko katika hatua za mwisho za kukamilisha majadiliano ya uanzishaji wa Eneo huru la Biashara Afrika litakalokuwa na ukubwa wa soko lenye idadi ya watu isiyopungua bilioni 1.5.


“Hivyo, kwa kuzingatia jinsi India ilivyoendelea katika Sekta ya Viwanda na Biashara, nawahimiza wafanyabiashara wa India kuja hususani wenye Viwanda kuja kuwekeza katika maeneo ya fursa zilizopo Tanzania hasa katika uongezaji wa thamani wa mazao ya kilimo, ngozi na madini”.

Aidha, Prof Mkumbo alizisihi taasisi za Serikali Tanzania na India kufanyia kazi vikwazo  vya kibiashara hususan vikwazo visivyo vya kiushuru (non- tariff barriers) ili kurahisisha upatikanaji wa bidhaa na huduma  baina ya nchi hizo huku wakizingatia ushindani katika biashara. Pi aliainisha kuwa  kwa sasa Tanzania inatekeleza Mpango wa “Blue Print” unaolenga kuboresha mazingira  ya biashara ili kuvutia biashara na uwekezaji.

“ Nafikiri hatutakubaliana kuwa mazao ya kilimo kutoka Tanzania kama viungo, mbaazi za kijani, korosho  na ufuta  ambavyo vinahitajika zaidi India  lakini havina soko la kuaminiaka," Amesema Prof Mkumbo.

Vilevile, Waziri amesema ili kutimiza azma hiyo ya kuendeleza biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo, Serikali ya Tanzania na India imeanzisha Tume ya pamoja ya Biashara ( Joint Trade Commission (JTC)) inayokutana mara moja  ambapo mkutano wa JTC unatarajiwa kufanyika hivi karibuni nchini Tanzania.

WAZIRI MKUU MAJALIWA: WATENDAJI JIEPUSHENI NA RUSHWA


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka watendaji wajiepushe na vitendo vya kuomba rushwa na urasimu usiokuwa wa lazima katika kuwahudumia wawekezaji ili kujenga imani baina ya sekta binafsi na sekta ya umma

 

Pia, Waziri Mkuu amezitaka Wizara na taasisi zote zinazohudumia wawekezaji kuhakikisha wanawezesha wawekezaji katika maeneo yao kwa kutoa huduma na taarifa muhimu kwa wakati.

 

Ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Aprili 16, 2021) wakati akihitimisha hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka wa 2021/2022 mwaka wa Fedha 2021/2022, Bungeni jijini Dodoma.

 

Waziri Mkuu amesema tarehe 6 Aprili 2021, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan Tanzania akiwaapisha Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Wakuu wa baadhi ya Taasisi za Serikali alisisitiza masuala mbalimbali ikiwemo uwekezaji na vibali vya kazi.

 

“Mheshimiwa Rais aliielekeza Ofisi ya Waziri Mkuu kuimarisha huduma za pamoja (One Stop Centre), kushughulikia malalamiko kuhusu kodi, kuondoa vikwazo katika uwekezaji, kuhamasisha uwekezaji kupitia mazungumzo, ushawishi, kudhibiti rushwa na kuondoa urasimu kwenye maombi ya vibali vya kazi”.

 

Amesema maelekezo hayo ya Mheshimiwa Rais yenye kujali maslahi mapana ya nchi hii yalikwenda sambamba na uamuzi wake wa tarehe 31 Machi 2021 wa kuunda rasmi Wizara ya Uwekezaji chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa lengo la kuhakikisha kuwa Wizara hiyo inasimamia kikamilifu masuala ya uwekezaji.

 

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kueleza hatua mbalimbali za utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia kuhusu Wizara ya Uwekezaji ambazo tayari zimechukuliwa kuwa ni pamoja na pamoja na kuandaa Muundo wa Wizara ambao utaainisha majukumu na mgawanyo wa Idara na Taasisi zitakazokuwa chini ya uwekezaji.

 

“Hatua ya pili ni kupitia Sera ya Uwekezaji ya mwaka 1996 na Sheria ya Uwekezaji ya mwaka 1997 ili kubainisha maeneo yenye kuhitaji maboresho ambapo tayari tathmini ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka 1996 imekamilika na kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Maendeleo ya Uwekezaji ili kuimarisha uratibu, usimamizi, uhamasishaji na ufuatiliaji wa masuala ya uwekezaji nchini”.

 

Waziri Mkuu amesema kukamilika kwa hatua hizo kutaiwezesha Serikali kushiriki kikamilifu katika mikutano na majadiliano ya jumuiya za kikanda yanayohusu masuala ya uwekezaji ikiwemo maandalizi ya Sera ya Uwekezaji ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

Pia, Waziri Mkuu ameongeza kuwa hatua hizo zitaiwezesha Serikali kushiriki katika utungaji wa Sera za Uwekezaji kwa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Itifaki ya Uwekezaji ya Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika.

 

“Kujenga  mazingira rafiki ya uwekezaji na uchumi shindani nchini kwa kutekeleza programu mbalimbali za kuimarisha mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi na kuandaa mfumo wa kielektroniki wa kupokea na kushughulikia malalamiko ya wawekezaji (Online Investors Feedback Platform)”.

 

“Kutatua changamoto za wafanyabiashara kupitia Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) kwa kuratibu majadiliano ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, kutoa elimu na hamasa kuhusu huduma zitolewazo kwenye Kituo cha Huduma za Mahala Pamoja (One Stop Facilitation Centre-OSFC).”

 

Amesema kupitia hatua hizo, Serikali itaweza kuimarisha mifumo ya usajili wa miradi na kutoa Cheti cha Vivutio (Certificate of Incentives), kuunganisha mifumo inayotumika TIC na makao makuu ya Taasisi na kuboresha mfumo wa kuchakata rufaa za vibali vya kazi na ukaazi kwa njia ya mtandao.

 

“Nitumie fursa hii tena kuwakumbusha watendaji wenzangu wakiwemo Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu kuhakikisha kuwa muundo na mifumo ya masuala ya uwekezaji inakamilika ndani ya muda ulioelekezwa na Mheshimiwa Rais”.

Monday, April 12, 2021

RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AWASILI UGANDA KWA ZIARA YA KIKAZI YA SIKU MOJA

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akilakiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda Mhe Sam Kutesa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe alipowasili nchini Uganda kwa ziara ya kikazi ya siku moja  Jumapili Aprili 11, 2021
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza jambo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda Mhe Sam Kutesa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe alipowasili nchini Uganda kwa ziara ya kikazi ya siku moja  Jumapili Aprili 11, 2021


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na baadhi ya Mawaziri wa Tanzania katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe alipowasili nchini Uganda kwa ziara ya kikazi ya siku moja  Jumapili Aprili 11, 2021


RAIS SAMIA AKARIBISHWA NA MWENYEJI WAKE RAIS MUSEVENI WA UGANDA IKULU YA ENTEBBE ALIPOWASILI KWA ZIARA YA KIKAZI YA SIKU MOJA



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akiwa katika mazungumzo na mwenyeji wake Rais Yoweri Museveni wa Uganda alipowasili katika Ikulu ya Entebbe  Jumapili Aprili 11, 2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akikaribishwa na  mwenyeji wake Rais Yoweri Museveni wa Uganda alipowasili katika Ikulu ya Entebbe leo Jumapili Aprili 11, 2021

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akitambulishwa kwa viongozi mbalimbali na mwenyeji wake Rais Yoweri Museveni wa Uganda alipowasili katika Ikulu ya Entebbe  Jumapili Aprili 11, 2021
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akitambulisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula kwa mwenyeji wake Rais Yoweri Museveni wa Uganda alipowasili katika Ikulu ya Entebbe Jumapili Aprili 11, 2021
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akitambulisha ujumbe wa Tanzania alioongozana nao kwa mwenyeji wake Rais Yoweri Museveni wa Uganda alipowasili katika Ikulu ya Entebbe Jumapili Aprili 11, 2021
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akitambulisha Mkurugenzi Mkuu wa TPDC Dkt Mataragio kwa mwenyeji wake Rais Yoweri Museveni wa Uganda alipowasili katika Ikulu ya Entebbe Jumapili Aprili 11, 2021

Wednesday, April 7, 2021

VIJANA IKUNGI WAONESHA UZALENDO WACHANGIA MADAWATI SHULE YA MSINGI MWISI


Viongozi pamoja na wananchi wa Kijiji cha Mwisi wilayani Ikungi mkoani Singida wakiwa katika picha ya pamoja baada ya hafla ya makabidhiano ya madawati Shule ya Msingi Mwisi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Justice Kijazi akizungumza na viongozi pamoja na wananchi wa Kijiji cha Mwisi kwenye shughuli za kukabidhi madawati.

Afisa Maendeleo Wilaya ya Ikungi  Haika Masawe akizungumza jambo kwenye hafla hiyo.


Afisa Mtendaji Kata ya Ndung'unyi, Yahaya Njiku ambaye pia ni mdau wa maendeleo akizungumza kwenye halfa hiyo ya kukabidhi madawati Shule ya Msingi Mwisi.

Wananchi wa Kijiji cha Mwisi wakiwasikiliza kwa makini viongozi kwenye halfa hiyo.

Madawati yakikabidhiwa. Kushoto ni Diwani wa Kata ya Lighwa Borgius Ntandu.

 Saimon Philipo mmoja wa vijana waliochangia madawati hayo akielezea namna walivyoguswa na kuamua kutoa msaada wao.

Viongozi wakiwa meza kuu.

Na Dotto Mwaibale, Singida.

Vijana wazalendo kutoka Kijiji cha Mwisi Kata ya Lighwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wametoa Madawati kwenye Shule ya Msingi Mwisi kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha watoto wote wanakaa kwenye madawati wakati wa masomo yao.

Vijana hao ambapo kwa sasa wako maeneo mbalimbali,wameona vema kuunga mkono juhudi za Serikali na wameamua kuanzia nyumbani kwenye Shule walikosomea ambapo wamechangia madawati 37.

Akikabidhi Madawati hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Justice Kijazi amewapongeza Vijana hao ambapo amesema amefarijika kuona wazalendo wanaokumbuka kurudisha fadhila nyumbani.

"Hongereni sana ni watu wachache sana wanaokumbuka kurudisha fadhila,hivyo endeleeni kuchangia mnapoona kuna changamoto katika kijiji chenu.Na mimi nachangia madawati 20." alisema Kijazi na kuongeza.

"Vijana kwenye risala yenu mumesema kuna uhitaji wa kukarabati chumba cha Darasa katika Shule hii ambalo litatumika kama Ukumbi, nachangia mifuko 30 ya Saruji pamoja na kumlipa fundi,hivyo mtakapoanza mipango niambieni." alisema.

Kijazi aliwataka Vijana kubuni Miradi mbalimbali ili kufungua fursa za ajira zitakazopelekea maendeleo ya Elimu na mambo mengine ambapo aliwaahidi kuwa Halmashauri kupitia asilimia 10%  zinazotengwa itatoa mikopo hiyo kwa Vijana watakao anzisha miradi ya maendeleo.

Aidha mmoja wa vijana hao waliounda umoja wa wanadarasa waliohitimu Shule ya Msingi Mwisi Mwaka 2007,Saimon Philipo alisema waliona zawadi pekee ya kulipa nyumbani ni kutengeneza madawati ili wadogo zao wasome kwenye mazingira mazuri.

"Sisi tuliamua kuanzisha umoja wetu ili tuweze kuchangia shughuli za maendeleo,Sio tu hapa tutafanya hata maeneo mengine lakini tuaona tuanzie kwanza nyumbani." alisema Saimon.

Naye Diwani wa Kata hiyo Borgius Ntandu aliwataka Vijana wa Kata hiyo kuwa chachu ya maendeleo kwa kuiga mfano wa Vijana wengine wazalendo wanaunga mkono juhudi za Serikali.

Hata hivyo Diwani huyo aliwapongeza wananchi wa kijiji cha Mwisi kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha inawaletea maendeleo wananchi wake.

Kwa upande wake Mdau wa maendeleo wilayani humo Yahaya Njiku ambaye pia ni Afisa Mtendaji Kata ya Ndung'unyi alisema uzalendo wa vijana utapimwa kwa utendaji kazi wao na sii vingine,hivyo akawaomba vijana wengine kuwa wazalendo kwa kushiriki shughuli za maendeleo katika maeneo yao.

"Huyu Saimon mmoja waliochangia madawati haya nimesoma naye kidato cha tano na sita na amekuwa rafiki yangu sana,nimeona nimuunge mkono katika hili na hata mengine.Nachangia sh.elfu Hamsini." alisema Njiku.