Matokeo chanyA+ online




Sunday, September 26, 2021

SERIKALI YATUMIA SH. BILIONI 52.975 KUTEKELEZA MIRADI MBALIMBALI SINGIDA


Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa akionesha Jarida la Nchi Yetu wakati akitoa taarifa ya wiki ya Serikali kwa waandishi wa habari mkoani Singida.
Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa hiyo.
Taarifa ikitolewa.
Waandishi wa habari wakisikiliza taarifa hiyo.
Waandishi wa habari wakisikiliza taarifa hiyo. Kushoto ni Afisa Habari Msaidizi Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Mwanahabari Elisante Mkumbo akiuliza swali kwenye mkutano huo.
Mwanahabari Damiano Mkumbo akiuliza swali kwenye mkutano huo.
Mwanahabari  Edina Alex akiangalia   Jarida la Nchi Yetu kwenye mkutano huo. 
Waandishi wa habari wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
Kazi ikiendelea,
Katibu Mwenezi na Itikadi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida Ahmed Kaburu akiuliza swali kwenye mkutano huo.


Na Dotto Mwaibale, Singida

Serikali imetoa Sh.Bilioni 52.975  mkoani Singida kwa ajili  ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo barabara, elimu, afya, maji, huduma za utawala na uwezeshaji wa wananchi. 

Hayo yamesemwa na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa wakati akitoa taarifa ya wiki ya Serikali kwa waandishi wa habari mkoani Singida jana.

Alisema Serikali inaendelea kutoa huduma za kiutawala na maendeleo katika Mkoa wa Singida kama kawaida chini ya Mkuu wa Mkoa Dkt. Binilith Mahenge na kuwa hali ya mkoa ni shwari na wananchi wanaendelea na shughuli zao za uzalishaji mali bila bughudha. 

Alisema katika kuimarisha ustawi wa wananchi wa Singida, Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kama ambavyo inafanya katika mikoa mingine hapa nchini na katika kufanikisha utekelezaji huo Serikali inahakikisha inatoa fedha kama ilivyopangwa. 

Msigwa alisema kuanzia Mwezi huu wa tisa, Serikali imeleta Sh. Bilioni 2 na Milioni 275 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Vituo vya Afya 8 (Ntuntu-Ikungi, Mitundu-Itigi, Chibungwa/Sasajila-Manyoni, Ilunda-Mkalama, Iglansoni-Ikungi, Tyegelo-Iramba, Kasisiri-Iramba na Makuro-Wilayani Singida) na kukamilisha vyumba vya madarasa 22 katika shule za Sekondari. Hizi ni fedha ambazo zinakusanywa kutokana na tozo katika miamala ya simu. 

Alisema kuna miradi mbalimbali ya ujenzi wa Barabara na Madaraja inayoendelea kutekelezwa na kati ya Machi na Septemba mwaka huu 2021, Serikali imeleta Singida shilingi Bilioni 21 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja. 

"Mfano mmoja wapo ni ujenzi wa Daraja la Msingi (lenye urefu wa mita 100) katika barabara ya Ulemo-Gumanga-Sibiti. Ujenzi wa daraja hili utagharimu Sh. Bilioni 10.933, hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 69. Daraja hili pamoja na barabara zake unganishi zitakamilika Juni 2022,".  alisema Msigwa.

Msigwa aliongeza kuwa pamoja na miradi hiyo Serikali imeanza  kufanya upembuzi yakinifu na usanifu kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Sabasaba, Sepuka na Ndago Kizaga yenye km 77.6.

Alitaja barabara nyingine kuwa ni ya mchepuo ya Singida (Singida bypass) ya kilometa 46, Barabara ya Mkalama-Gumanga-Nduguti-Iguguno ambayo ni sehemu ya barabara inayoanzia Bariadi mkoani Simiyu ambayo itaunganisha na Iguguno. 

Akizungumzia miradi ya maji alisema Serikali imeleta sh. Bilioni 5 na Milioni 278 kutekeleza miradi hiyo katika vijiji vya Mughamo, Ibaga, Kipumbuiko na Kintinku/Lusilile. Hii yote nijuhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kumtua ndoo ya Maji Mama na kukabiliana na tatizo la maji. 

 Kuhusu umeme kupitia mradi wa usambazaji wa umeme vijijini (REA-III), Serikali imesambaza umeme katika vijiji 274 kati ya vijiji vyote 441 (sawa na asilimia 62.1). Kazi inayoendelea sasa ni kusambaza katika vijiji 167 vilivyobaki. Vijiji hivi vyote vitakuwa vimepata umeme ifikapo Desemba mwakani. 

Pia alisema Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa umeme wa kitaifa unaitwa Backbone Transimission Investment Project (BTIP) na kuwa hapa Singida kuna kituo kikubwa cha kupooza umeme na kinapokea kutoka kituo cha Zuzu – Dodoma umeme wa msongo wa kilovoti 400. Uwezo wake wa juu ni kupokea, kupoooza na kusambaza jumla ya Megawati 600. Kwa sasa tayari kimeanza kuhudumia Mji wa Singida na kazi inayoendelea ni kuunganisha na mitambo ya msongo wa kilovoti 400 na ile ya kilovoti 220 ambayo inatumika kuwapelekea wananchi. 

Alisema mradi huo  ni sehemu ya mradi mkubwa wa kujenga njia kuu ya umeme kutoka Iringa, Dodoma, Singida hadi Shinyanga. Na pia ni sehemu ya mradi wa kuunganisha njia ya umeme kati ya Tanzania na Kenya. Njia hii inakwenda mpaka  Namanga – Arusha hadi kuunganisha na Isinya nchini Kenya. 

Alitaja Gharama za mradi huo kuwa ni  Dola za Marekani Milioni 56 (Bilioni 128.8), hadi sasa umefikia asilimia 99 na unatarajiwa kukamilika kabla ya Desemba mwaka huu 2021.

Akizungumzia mradi wa kimkakati wa kukabiliana na upungufu wa mafuta ya kula nchini alisema nchi yetu inahitaji kama tani 640,000 za mafuta ya kula, uzalishaji wetu ni tani 240,000 tu. Mafuta yanayobaki kiasi cha tani 400,000 tunalazimika kuagiza kutoka nje ya nchi na tunatumiza zaidi ya shilingi Bilioni 500 kuagiza mafuta hayo. 

Alisema Serikali imejipanga kuhakikisha inaleta mbegu za alizeti za kupanda tani 1,194 kwa ajili ya wakulima. Hizi ni mbegu bora ambazo zinatoa mafuta mengi. 

Alisema katika juhudi za kuongeza mbegu za alizeti kwa ajili ya kuzalisha mafuta, tunahitaji tani milioni 2 kwa mwaka lakini tunazalisha tani laki 6 tu. 

"Serikali inawapongeza viongozi na wakulima wa Mkoa wa Singida kwa kujiwekea mpango wa kulima ekari 597,000 na kuzalisha tani 581,986 ambazo zitazalisha tani 242,500 za mafuta. Hii itasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya upungufu wa mafuta ya kula hapa nchini na kupanda kwa bei ya mafuta, alisema Msigwa.

 Msigwa alitumia nafasi hiyo kunatoa wito kwa wakulima wote nchini kuongeza uzalishaji wa alizeti na Serikali itaendelea kutoa huduma za ugani, kutafuta mbegu bora na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kusafisha mafuta. 

Adha Msigwa akizungumzia Mapambano dhidi ya Uviko-19 alisema  janga la ugonjwa  unaosababishwa na Virusi vya Korona (Uviko-19). Serikali kupitia Viongozi wake na Wataalamu imeendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya kujikinga na ugonjwa huo na kupokea chanjo. 

"Kwa kutambua changamoto ya kuhakikisha elimu dhidi ya ugonjwa huu inawafikia wananchi ipasavyo pamoja na kupata chanjo, Wiki hii Serikali imeanza kutekeleza Awamu ya Pili ya utoaji chanjo kwa kupanua uwigo wa vituo vya kutolea chanjo ya Uviko-19, tulianza na vituo 550 nchi nzima na sasa chanjo zinatolewa katika vituo vyote vinavyotoa chanjo zingine nchini. Kuna vituo zaidi ya 6,784 vinatoa chanjo na pia wataalamu wa kutoa chanjo sasa wanakwenda hadi vijijini na maeneo yote yenye mikusanyiko ya watu. Hata juzi kwenye mtanange wa Yanga na Simba, watu wamepata chanjo pale," alisema Msigwa. 

Alisema kwa tulipofikia sasa, hatutaki Mtanzania aliyetayari kupata chanjo apate shida ya kwenda sehemu ya kuchanjwa. Tunaweka vituo vya chanjo kwenye vituo vya mabasi, kwenye masoko, vituo vya kupima uzito magari, Mwenge wa uhuru, tunakwenda mechi ya watani wa jadi na kila mahali ambapo tunaona pana weza kuwarahisishia watu kupata chanjo. Na hii ni kwa sababu, tumeona Watanzania wengi wapo tayari kupata chanjo lakini changamoto imekuwa kuvifikia vituo vinavyotoa chanjo. 

Alisema utoaji chanjo unakwenda vizuri, mpaka leo Watanzania takribani 400,000 wamechanjwa na wengine wanaendelea kupata chanjo dhidi ya uviko-19. Kasi hii imeongezeka sana baada ya Wizara ya Afya, TAMISEMI na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuzindua Awamu ya Pili ya Uhamasisha na utoaji elimu (Sepetemba 15, 2021) ambapo sasa chanjo zinapelekwa hadi vijijini na Wataalamu wetu sasa wameanza kupita nyumba kwa nyumba ili wale ambao wapo tayari kupata chanjo wapate. 

Aliongeza kuwa Serikali inawapongeza Wataalamu wa Afya wote kwa kazi kubwa wanayoifanya, kwanza kwa wao wenyewe kuonesha mfano kwa kupokea chanjo na pili kupeleka huduma za Mkoba kwa wananchi (yaani mwananchi anapata chanjo pale alipo. 

Msigwa alimpongeza kijana Michael Filbert Nondo ambaye ameamua kusafiri kwa baiskeli kutoka Kigoma hadi Dar es Salaam akipita kuhamasisha wananchi kupokea chanjo. Leo amefika Dodoma na kukutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,  Jinsia, Wazee na Watoto lakini kwa bahati mbaya hatoweza kumaliza safari yake baada ya kupatwa na msiba wa kufiwa na mwanae huko Kigoma. Nawaomba vijana wote tuungane kuhamasisha jamii kupata chanjo kama anavyofanya kijana huyo. 

Alisema Serikali inahimiza watu kuchukua tahadhari dhidi ya Uviko-19 na kupata chanjo kwa sababu KINGA NI BORA KULIKO TIBA. Kitengo cha Kinga cha Wizara ya Afya kinachoongozwa na Dkt. Leonard Subi wanafanya kazi kubwa ya kuhakikisha wananchi wanapata elimu na chanjo, na leo hapa nimeongozana na Dkt. Ama Kasangala, yeye ni Kaimu Mkurugenzi wa kitengo cha elimu ya afya kwa Umma cha Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. 

Alisema  kwa kutambua kuwa Waandishi wa Habari wana umuhimu mkubwa katika jukumu la kuwaelimisha Watanzania kukabiliana na Uviko-19 Serikali imeona iongeze ushirikiano nao ambapo alimtambulisha Rais wa Umoja wa Vyama vya Waandishi wa Habari vya Mikoa (UTPC)  Deogratius Nsokolo alikuwa ameongozana naye. 

"Mimi lengo langu Waandishi wa Habari twende pamoja, tufanye kazi zetu kwa kuzingatia weledi, sheria za nchi, kanuni na taratibu lakini muhimu zaidi tuiweke nchi yetu kwanza (Tanzania Kwanza), tuwapiganie Watanzania pamoja. Kwenye hili janga la Korona Watanzania wanakufa kwa sababu ya kutozingatia afua hizi za kukabiliana na virusi vya ugonjwa huu, kutozingatia kuwa KINGA NI BORA KULIKO TIBA," alisema Msigwa. 

Msigwa alihitimisha hutuba yake kwa kuwaomba Waandishi wa Habari kushirikiana na Wataalamu waliopo katika mikoa yote hapa nchini  kuhakikisha elimu kwa wananchi inafika ipasavyo kwa kuwasiliana na Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Waganga wa Hospitali zetu, viongozi wa Mikoa na Wilaya ili Watanzania wapate chanjo na wajikinge na balaa hilo. 

Katika mkutano huo Msigwa alipata fursa ya kujibu maswali mbalimbali ya wananchi waliokuwa wakipiga simu moja kwa moja kwenye mkutano huo.

Friday, September 24, 2021

NAIBU WAZIRI YA MADINI AMALIZA MGOGORO WA UMILIKI MGODI


Naibu Waziri Wizara ya Madini Profesa Shukuru Manya akizungumza na wachimbaji wadogo wa mgodi wa dhahabu wa Kijiji cha Matongo katika mkutano wa hadhara alipokwenda kutatua mgogoro wa umiliki wa mgodi huo jana uliopo wilayani Ikungi mkoani Singida
Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahaman Mwanga akizungumza na wachimbaji wakati wa utatuzi wa mgogoro huo.
Kaimu Afisa  Madini Mkazi Mkoa wa Singida,Chone Malembo akizungumza na wananchi katika mkutano huo.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro akizungumza na wananchi katika mkutano huo.
Naibu Waziri wa Madini Profesa Shukuru Manya (wa nne kulia)akizungumza na wachimbaji wadogo wa mgodi wa dhahabu wa Kijiji cha Matongo wakati akikagua maduara ya uchimbaji.
Wachimbaji wadogo wa mgodi huo wakiwa mkutanoni.
Mchimbaji Abdulkheri Abdulkadir kutoka Geita, akizungumza kero zinazo wasibu wachimbaji kwenye mgodi huo.
Mchimbaji  kutoka Mkoa wa Iringa Geita, akizungumza kero zinazo wasibu wachimbaji kwenye mgodi huo.
Mmiliki wa mgodi huo Richard Lyamuya akizungumza katika mkutano huo
Mbia wa mgodi huo Helena Mtaturu akizungumza  katika mkutano huo


Na Dotto Mwaibale, Ikungi Singida


Naibu Waziri  Wizara ya Madini Profesa Shukuru Manya katika hali ambayo haikutegemewa na wengi ametumia masaa mawili sawa na dakika 120 kumaliza mgogoro wa muda mrefu wa umilikaji mgodi wa uchimbaji dhahabu katika machimbo ya Kijiji cha Matongo yaliyopo wilayani Ikungi mkoani hapa.

Mgogoro huo ambao umemalizwa na Profesa Manya ulikuwa ukimuhusisha mmiliki halali wa mgodi huo Richard Lyamuya na wabia wenzake Israel Njiku na Helena Mtaturu ambaye alikuwa mlalamikaji na mmiliki wa eneo hilo la mgodi lenye ekari 70 ambalo alidai lilichukuliwa na Lyamuya bila ya kufuata taratibu kwa kumuhusisha Mtaturu na ndugu zake.

Kutoka na madai hayo  Mtaturu ambaye ni mjane alimuandikia barua Waziri Wizara ya madini akidai kuwa kwa kificho bila yeye kujua mmiliki wa mgodi huo Richard Lyamuya ambaye ni mkazi wa Singida Mji alikwenda ofisi za madini Mkoa wa Singida ili apewe kibali cha kuchimba dhahabu kwenye eneo lake bila ya kushirikishwa.

Baada ya barua hiyo kufika katika wizara hiyo na kufanyiwa uchunguzi ndipo jana Naibu Waziri Wizara ya Madini Profesa Shukuru Manya alipofika kwenye mgodi huo na kufanya mkutano wa hadhara uliowahusisha wadau wa uchimbaji, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro, Viongozi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi  (CCM) wananchi na wamiliki wa mgodi huo ambao baadhi yao waliweza kuelezea walivyokuwa wakielewa jinsi mmiliki wa mgodi huo alivyopata eneo hilo kwa kufuata sheria za uchimbaji wa madini kwa kumshirikisha Helena Njiku na kuweka kumbukumbu za makubaliano kwa maandishi na kutiliana saini.

Mmoja wa viongozi wa Umoja wa wachimba madini katika wilaya hiyo  (SIREMA) Seleman Omari alisema mbele ya Naibu Waziri Wizara ya Madini kuwa anaujua mchakato mzima wa uanzishwaji wa mgodi huo na kuwa hakukuwa na udanganyifu wowote na wabia hao waliwekeana namna ya kulipana ambapo Mtaturu aliachiwa asilimia 40 huku Richard Lyamuya na Israel Njiku wakichukua asilimia 30 kila mmoja.

Mbali ya Omari kuyasema hayo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro alisema suala hilo alilikuta ofisini kwake baada ya kusikizwa na mtangulizi wake Edward Mpogolo ambaye amehamishiwa Wilaya ya Same ambapo nyaraka zote zinaonesha umiliki wa mgodi huo ni wa watu hao watatu na tayari Serikali imekwisha wapa leseni ya uchimbaji na si vinginevyo.

Baada ya watu mbalimbali kutoa maelezo yao na kubaini kuwa Mtaturu aliandika barua ya madai ambayo sio ya kweli Naibu Waziri Profesa Manya alimwambia asirudie tena kufanya jambo hilo.

Profesa Manya alitumia nafasi hiyo kuwaomba wachimbaji hao kufanya kazi zao kwa upendo na kufuata sheria za uchimbaji.

Mkuu wa wilaya hiyo Jerry Muro aliwaomba wachimbaji hao kudumisha amani na kujikinga na magonjwa ya Corona na ukimwi kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu katika eneo hilo.

Wednesday, September 22, 2021

RAIS DK.HUSSEIN ALI MWINYI AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA MLEZI WA CHAMA CHA MAPINDUZI MIKOA WA KUSINI NA KASKAZINI UNGUJA JOB NDUGAI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, akimsikiliza Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Mlezi wa Chama Cha Mapinduzi Mikoa wa Kusini na Kaskazini Unguja ambae pia ni Spika wa Bunge la Tanzania Job Yustino Ndugai alipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu, akiwa katika ziara yake ya Kichama Zanzibar. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mgeni wake Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa,Mlezi wa Chama Cha Mapinduzi Mikoa ya Kusini na Kaskazini Unguja ambae pia ni Spika wa Bunge la Tanzania Job Yustino Ndugai, alipofika Ikulu kwa mazungumzu, akiwa Zanzibar kwa ziara ya Kichama katika Mikoa wa Kusini na Kaskazini Unguja.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi akifuatana na mgeni wake Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Mlezi wa Chama Cha Mapinduzi Mikoa ya Kusuni na Kaskazini Unguja, ambae pia ni Spika wa Bunge la Tanzania.Mhe. Job Yustino Ndugai, wakitoka katika ukumbi wa baada ya kumaliza mazungumzo yao, akiwa Zanzibar kwa ziara ya Kichama katika Mkoa wa Kusini na Kaskazini Unguja.(Picha na Ikulu)

Thursday, September 16, 2021

SHAKA:SERIKALI HAIJASITISHA MPANGO WA ELIMU BILA MALIPO




Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka amesema hakuna ahadi iliyotolewa kwenye ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025 ambayo haitatekelezwa ikiwemo mpango wa elimu bila malipo na utatuzi wa changamoto za sekta ya elimu nchini.

Amesema hayo wakati akikagua Ujenzi wa shule ya sekondari ya wavulana Nachingwea iliyopo kata ya Chiumbati mkoani Lindi.


 "Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kugharamaia elimu bila malipo. Ikiwa ni utekelezaji wa waraka wa elimu namba 6 wa mwaka 2015 na ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025" Alisema Shaka

Aliwataka wananchi wapuuze taarifa zozote za upotoshaji zinazodai serikali itasitisha mpango wa kugharamia elimu bila malipo.


 "Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Samia imeendelea kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu ikiwemo kuajiri walimu takribani 6,949 na katika bajeti ya 2021/22 imetenga kiasi cha fedha shilingi bilioni 125 za kukamilisha maboma elfu kumi nchi nzima ikiwa ni utekelezaji wa ibara ya 80 ya ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025." Alifahamisha Shaka.

Shaka amewapongeza wananchi wa kata ya Chiumbati, kijiji cha Chiumbati shuleni kwa kutoa eneo la ujenzi wa shule hiyo, kujitolea nguvu kazi na hata kuchangia ujenzi katika hatua za awali kabla ya serikali kuwaunga mkono kuendeleza ujenzi huo.


Hata hivyo  Wananchi wa eneo hilo wamemshukuru Rais Samia katika kuipa kipaumbele elimu na kufanikisha hatua za ujenzi wa shule hiyo ya wavulana  ambayo ilikuwa ni hitaji lao la muda mrefu.

Shaka pia amewataka wananchi kujitokeza kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa ya watu na makazi itakayofanyika mwaka 2022. Alihimiza serikali inatekeleza zoezi hilo kwani taarifa zake zina umuhimu mkubwa katika kuisaidia serikali kupanga rasilimali zake katika maendeleo ya nchi na watu wake hivyo ni muhimu kila mmoja kujitokeza kulishiriki.


Shaka yupo kwenye ziara ya Sekretarieti ya CCM Taifa inayokamilika leo mkoani Lindi ikiongozwa na Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel Chongolo.

KATIBU MKUU WA CCM ASISITIZA SENSA, MIKUTANO YA MASHINA NA KUWAONYA WALIOANZA HARAKATI MAJIMBONI



Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Daniel Chongolo amesisitiza umuhimu wa Sensa, mikutano ya Mashina na kuwaacha waliopata dhamana kufanya kazi.


Amezungumza hayo leo tarehe 15 Septemba, 2021 wakati wa Mapokezi ya ziara yake Mkoa wa Lindi akiambatana na Wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.


Akizungumzia suala la Sensa ya Watu na Makazi, Katibu Mkuu amewataka viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali  kuhakikisha katika maongezi yao na wananchi wanahamasisha zoezi la Sensa lililozinduliwa na Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Mhe. Samia Suluhu Hassani Jijini Dodoma, ambalo linatarajiwa kufanyika Mwaka 2022,  kwani Sensa  ndio msingi wa maendeleo ya nchi na uchumi wetu.


"Sensa katika nchi ndio Uchumi  na ndio Maendeleo, tukitengeneza  mazingira  mazuri  ya kuhamasishana  na kujitokeza  vya kutosha  katika kushiriki Sensa zoezi  ambalo limezinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Dodoma, tutaipa serikali fursa ya kupanga Mipango ya Maendeleo kwa urahisi na kufikia maendeleo yenye usawa na kwa haraka." Katibu Mkuu amesisitiza


Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu amewaonya watu wanaofuatilia nafasi za ubunge na udiwani wanapaswa kuacha mara moja, kwani Uchaguzi umeshapita na CCM haiwezi kuwa Chama cha  Uchaguzi wakati wote badala ya kuwaletea wananchi maendeleo.


"Kama unapenda Ubunge ama udiwani subiri 2025 sasa hivi chokochoko  katika majimbo zinatoka wapi,na chokochoko za nafasi zinatoka wapi..?waacheni wabunge wafanye kazi  wanazofanya, subirini 2025, tukihangaika kuwafuatilia sasa hivi na kuwazushia uongo tutafika mwaka 2025 na majeraha makubwa." Katibu Mkuu ameeleza


Ameongeza kuwa, "Kila mtu anahaki  ya kutumia nafasi yake ya uanachama ndani ya Chama hiki kugombea, lakini hana haki ya kumsumbua aliyeshinda uchaguzi kwa kuwa tuna kazi ya kujenga nchi na  kutekeleza Ilani ya Chama chetu."


Akizungumzia Uhai wa Chama Mashinani, Katibu Mkuu amesema,  katika uchaguzi Mkuu wa ndani ya Chama unaotarajiwa kufanyika mwakani, mtu akitaka kuchagulia kuwa Kiongozi ndani ya Chama ni lazima awe amehudhuria mikutano ya  mashina. Mwanachama hawezi kuwa Kiongozi wa Chama kama hakushiriki mikutano ya Mashina kwa ushahidi wa mihutasari.


Akiendelea na Ziara Wilayani Kilwa Katibu Mkuu ametembelea na kukagua ujenzi wa kituo cha Afya cha Chumo na kuhudhuri mkutano wa Shina namba 3 Tawi la Chumu Kata ya Chumo.


Huu ni muendelezo wa Utekelezaji wa Maelekezo ya Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa cha  tarehe 29 Juni, 2021ikiwa ni  kuimarisha Uhai wa Chama katika ngazi za Mashina pamoja na Kukagua Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 - 2025.




NAIBU KATIBU MKUU WA CCM (BARA), CHRISTINA MNDEME, AMESEMA MWAKANI NI MWAKA WA UCHAGUZI NDANI YA CHAMA NI VYEMA WANACHAMA KUJIPANGA IPASAVYO

 


 

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (Bara), Christina Mndeme, amesema mwakani ni mwaka wa uchaguzi ndani ya chama ni vyema wanachama kujipanga ipasavyo

Amesema chaguzi hizo za Chama ni muhimu, ili kupata viongozi watakaomsaidia Rais Samia Suluhu Hassan, katika kusimamia utekelezaji wa Ilani.

Mama Mndeme amesema hayo jana katika viikao vya shina namba moja na mbili Wilayani Ruangwa Mkoani Lindi katika ziara ya Wajumbe  wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM ikiongozwa na Katibu Mkuu wa Chama Daniel Chongolo.

Ziara hiyo imelenga kuhamasisha uhai wa Chama kwa umma na kusimamia  utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020/2025.

Mama Mndeme alisema wanachama wajiandae na uchaguzi bila kuwapo na mpasuko.

"Leo Rais amesema tumepata Rais mwanamke kwa kudra za Mungu na mfumo wa Katiba yetu mwaka 2025 ndio tunaenda kuchagua Rais mwanamke maandalizi yanaanza sasa ndani ya CCM, ikiwemo kuchagua viongozi wazuri uchaguzi wa mwakani,"alisema.

Alisema ni muhimu kamati za siasa na viongozi wa mashina kukemea kuchafuana na kuweka mazingira rafiki ya ushindi wa CCM.

"2025 tunaenda na Rais Samia tusikubali kupasuka,  sumu haijaribiwi tusiweke mazingira ya kuwapa wenzetu nafasi,"alisema.

Aliongeza kuwa "Hakuna haja ya kusikiliza wenye nia mbaya na taifa, serikali ikisema hivi wao wanageuka na kusema hivi hawaridhiki,"alisema.

Pia alisema ni vyema viongozi wa CCM wasifunge milango katika kusikiliza wananchi, kwa kutambua kuwa  Ruangwa ina heshima yake ni Jimbo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Mama Mndeme alisema ni wakati wa CCM kuhakikisha Chama, kinaheshimiwa na kutekeleza Ibara ya 251 ya Ilani, inayoelekeza kuwapo kwa ukaguzi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ipasavyo.

Alihimiza haja ya kupokea wanachama wapya na kulipa ada, kuimarisha amani na kuwapo huduma muhimu kwa wananchi ikiwemo huduma bora za afya hususani kwa wazee.

Alisema Ibara ya 83 ya Ilani ya CCM inaeleza umuhimu wa kuwapo afya bora na kuwa na dirisha la wazee kwakuwa mchango wao ni mkubwa katika kutumikia taifa.

Mama Mndeme alisisitiza wanachama na wananchi kujipanga kwa ajili ya maandalizi ya sensa ifikapo mwakani, kwakuwa maendeleo yanahitaji watu wake kuhesabiwa.

"Rais amezindua sensa, wakati ukifika tujitokeze huwezi kusonga ugali wa watu watatu ndani kuna watu watano hawatashiba, ni lazima kujua idadi na mahitaji yaliyopo na tujiepushe na wapotoshaji tukahesabiwe,"alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ruangwa Saidi Kaondo alisema chaguzi nyingi zimepita hivyo Chama kisiwe na wasiwasi aliyeamuliwa na Mungu ndio atakayepita.

Alisema CCM Ruangwa haina mwenyewe wala mwenye hati miliki bali Chama kwanza mtu baadaye hivyo hakutakuwa na makundi wala migogoro.

"Tufikishie salamu kwa Rais Samia tumepata viatilifu bure vya korosho, haijawahi kutokea tutampa heshima kwa kuweka maslahi ya Chama mbele,"alisema.


CCM YAWATAKA VIONGOZI , WATENDAJI WA CHAMA NA SERIKALI KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO ZA WANANCH


Katika wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi( CCM) Taifa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka amewaeleza viongozi na watendaji wote ndani ya Chama na Serikali kushughulika na changamoto za wananchi badala ya kukaa ofisini.

Shaka ameyasema hayo  akiwa ziarani  wilayani Nachingwea mkoani  Lindi.

Pamoja na mambo mengine ziara hiyo imelenga kuhamasisha na kuimarisha uhai wa chama kuanzia ngazi ya shina, kuhimiza mahusiano ndani ya chama pamoja na serikali.

Shaka ameendelea kuwahakikishia wananchi kuwa CCM na serikali vipo salama na imara katika mikono ya Mwenyekiti na Rais mahiri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

"Hii ni kwa sababu katika muda mfupi serikali anayoiongoza imetoa mwelekeo wenye matumaini makubwa ya kuimarisha ustawi wa wananchi, uchumi wa nchi yetu, kuvutia uwekezaji zaidi, kuzalisha ajira kwa vijana na kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka ya Nchi yetu na raia wote,"amesema Shaka

Shaka amewataka viongozi na watendaji wote ndani ya serikali kuchapakazi kwani Chama, Rais Samia na wananchi wanataka matokeo yanayoonekana na yanayopimika kutoka kwenye utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM 2020-2025.

Wakati huo huo Shaka ameilekeza Wizara ya Nishati kuhakikisha wanamaliza tatizo la kukatikakati kwa umeme linaloendelea maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Wilaya ya Nachingwea.

Shaka pia amewataka wananchi kujitokeza kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa ya watu na makazi itakayofanyika mwaka 2022. Alihimiza serikali inatumia gharama kubwa kukamilisha zoezi hilo kwani taarifa zake zina umuhimu mkubwa katika kusukuma maendeleo ya nchi mbele zaidi hivyo ni muhimu kila mmoja kulishiriki.

Shaka yupo kwenye ziara ya Sekretarieti ya CCM Taifa iliyopo kwenye ziara mkoani Lindi ikiongozwa na Katibu Mkuu wa CCM  Daniel Chongolo.

MWENYEKITI UWT TAIFA APOKEA WANACHAMA 10 KUTOKA CHADEMA MKOANI SINGIDA


Charles James, Michuzi TV

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Gaudentia Kabaka amepokea wanachama 10 kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambapo amesema kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Samia Suluhu ndio inawavutia wapinzani kujiunga na chama hicho.


Kabaka amesema uwezo wa Serikali ya CCM kushughulikia matatizo na changamoto za watanzania umekua ukiwavutia wapinzani ambapo amesema idadi kubwa ya wanachama wa vyama vya upinzani kujiunga na CCM itaendelea.


Hayo yamefanyika katika ziara ya Mwenyekiti huyo wa UWT Taifa katika Wilaya za Manyoni na Iramba Mkoani Singida ambapo yeye ni mlezi wa kichama wa Mkoa huo.


Akiwa ziarani humo Kabaka amekagua ujenzi unaoendelea  wa nyumba ya Katibu wa UWT wilaya ya Iramba wenye gharama ya Sh Milioni 34 ambapo amefurahishwa kasi inayoendelea katika ujenzi pamoja na thamani ya fedha inayotumika kujenga huku yeye mwenyewe akichangia kiasi cha Sh Milioni Moja kufanikisha ujenzi huo.


Pia Kabaka amekagua  jengo la lishe lililopo katika hospitali ya Kiomboi wilayani Iramba ambalo limegharimu kiasi cha Sh Milioni 150 ambalo nalo ameridhishwa na kasi ya ujenzi huo.


Mwenyekiti Kabaka pia ametembelea kikundi cha wajasiriamali kiitwacho JIPEMOYO ambacho kinajishughulisha na kilimo Cha Alizeti  chenye ukubwa wa ekari 10 na ufugaji wa nyuki mizinga 45.


Kikundi hiki kimenufaika na mkopo usio na riba ulitolewa na Halmashauri ya wilaya ya Iramba ambapo idadi ya kikundi hiko ni watu 20 na wamekopeshwa  kiasi Cha Shilingi Milioni 10.


Aidha Kabaka amewasihi viongozi wa serikali kuhakikisha wanatumia vizuri fedha zinazotolewa na Serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Maendeleo.Pia amewakumbusha kuwa makini katika ujenzi wa miradi inayoendana thamani halisi ya Fedha zinazotolewa na Serikali kuu au  zile zinazotokana na makusanyo ya vyanzo vya mapato ya  Halmashauri husika.

Mwenyekiti wa UWT Taifa akishiriki ujenzi wa Nyumba ya Katibu wa Wilaya ya Iramba ambapo pia amechangia kiasi cha Sh Milioni Moja kufanikisha ujenzi huo.

Wanachama wa Umoja wa Wanawake Tanzania Wilaya ya Iramba na baadhi ya wananchi wakimsikiliza Mwenyekiti wa UWT Taifa alipofika kuzungumza nao na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mwenyekiti wa UWT Taifa, Gaudentia Kabaka akizungumza na wananchi na wanachama wa CCM katika Wilaya ya Iramba alipofika kukagua miradi ya maendeleo Wilayani humo.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania UWT, Gaudentia Kabaka akipokea kadi ya Chadema baada ya mwanachama huyo kuirudisha na kuomba kujiunga na Chama Cha Mapinduzi CCM.

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AWASILI KIGOMA KUKAGUA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO NA SHUGHULI ZA KIJAMII

 

 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Septemba 16, 2021 amewasili mkoani Kigoma kwa ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na shughuli za kijamii,Pichani Waziri Mkuu akipokewa na viongozi mbalimbali wa mkoa huo mara baada ya kuwasili uwanja wa ndege mkoani humo.
 


Wednesday, September 15, 2021

DC MOYO:WAHUDUMU WA AFYA WATAKAO WANYANYASA WAZEE IRINGA KUKIONA CHA MTEMA KUNI


Mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo akisisitiza jambo kwa wahudumu wa afya alipokuwa kwenye moja ya mikutano ya hadhara ambapo ameamua kufanya ziara kijiji kwa kijiji kusikiliza kero za wananchi wa wilaya hiyo


Wananchi wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo  wakati akisisitiza jambo kwa wahudumu wa afya alipokuwa kwenye moja ya mikutano ya hadhara ambapo ameamua kufanya ziara kijiji kwa kijiji kusikiliza kero za wananchi wa wilaya hiyo
Wananchi wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo  wakati akisisitiza jambo kwa wahudumu wa afya alipokuwa kwenye moja ya mikutano ya hadhara ambapo ameamua kufanya ziara kijiji kwa kijiji kusikiliza kero za wananchi wa wilaya hiyo

 Na Fredy Mgunda,Iringa.

Mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo amewaonya wahudumu wa afya wanaokiuka agizo la serikali linalowataka kutoa kipaumbele kwa wazee kutoa huduma za kiafya na kwamba tabia hiyo haivumiliki na watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.

Kauli hiyo imekuja mara baada ya kupokea kero kwenye mikutano ya hadhara katika tarafa ya Kiponzero na Mlolo ambapo baadhi ya wazee wamemlalamikia mkuu huyo wa wilaya kunyanyaswa na wahudumu wa afya wa tarafa hizo.

Wakizungumza kwenye mikutano ya hadhara wazee hao walisema kuwa serikali imewajali kwa kuwapatia kadi za matibabu kwa wazee kwa lengo la kuwawezesha kupata huduma za kiafya bure lakini hali inakuwa tofauti pale wanapokwenye kupata huduma hiyo kwenye vituo vya afya,zahanati,hospitali za wilaya hadi hospitali ya Rufaa ya mkoani Iringa.

Wazee hao walisema kuwa kuwa mara nyingi wamekuwa wakienda kutaka kupata huduma ya afya lakini wamekuwa hawapati huduma inayostahili kama ambavyo serikali imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa wazee wanapaswa kupewa kipaumbele katika huduma za kiafya.

Walimuomba mkuu wa wilaya ya Iringa kuhakikisha kuwa anapeleka kilio chao kwa serikali kuu ili nao waweze kuhudumiwa vizuri kama wananchi wengine wenye kipato kikubwa kwa kuwa wamelitumikia taifa hili kwa miaka yao yote ya maisha.

Aidha wazee hao waliongeza kuwa licha ya kuwa na kadi hizo bado kumekuwa na tatizo la kuzipata dawa ambazo wanakuwa wanaziitaji wakati huo kulingana na magonjwa ambayo wanakabiliana nayo badala yake wamekuwa wakielekezwa kwenda kununua dawa nje ya vituo vya afya.

Akijibia kero hizo za wazee mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo alisema kuwa wazee wote wa wilaya ya Iringa ambao wanaumri wa kuanzia miaka 60 wanatakiwa kupewa kadi za matibabu za wazee kwa kuwa hiyo ni haki yao kwa muji wa sera za serikali ya awamu ya sita.

Alisema kuwa wahudumu wa afya wilaya ya Iringa wanatakiwa kuacha mara moja tabia ya kuwatolea lugha chafu wazee wanapokwenda kupata huduma za kiafya bara yake wanatakiwa kuwahudumia kama wanavyowahudumia wateja wengine wanaokwenda kupata huduma hiyo.

Moyo alisema kuwa akisikia wahudumu wa sekta ya afya wanatoa lugha hizo chafu watachukuliwa hatua kali za kinidhamu kwa lengo la kukomesha tatizo hilo ambalo linaonekama kuwa sugu katika wilaya hiyo.

“Kila zama na kitabu chake mimi sipo tayari kuona wazee hawa wakinyanyaswa bila sababu yoyote ile ya msingi wanapokwenda kupata huduma za kiafya kwa kuwa serikali imeamua kuwadumumia kutokana na mchango wao katika taifa hili hadi hapa lilipofika” alisema Moyo

Moyo amewaomba wananchi na wazee wote wa wilaya ya Iringa kutoa taarifa kwake endapo watatolewa au hawatahumiwa vizuri na watumishi wa sekta ya afya katika wilaya hiyo ili kuondoa kero hiyo na kuboresha huduma kwa wateja ambao wanakuwa wanaenda kupata huduma za afya.

Moyo alimazia kwa kusema kuwa lengo la serikali ya awamu ya sita ni kuboresha sekta ya afya kwa wananchi wa wilaya ya Iringa na Tanzania kwa ujumla hivyo haitaji tena kuona watumishi wa sekta hiyo wakikwamisha juhudi za serikali.