Matokeo chanyA+ online




Tuesday, August 20, 2019

SAA 48 NILIZOISHI NDANI YA SADC - HAFIDH KIDO

Hafidh Kido akihuliza swali katika Mhadhara uliofanyika Chuo Kikuu cha Dar es salaam. #39SADCSummit


Wiki tatu zilizopitita sikuwa na uelewa wowote kuhusu Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa kushirikiana na Idara ya Habari (MAELEZO), ililazimika kutoa semina za siku tatu kwa wanahari mkoani Morogoro.

Semina ile si tu ilinifungua masikio lakini iliniongezea uelewa mpana juu ya jumuiya hii muhimu kwa maendeleo ya Tanzania na nchi nyingine wanachama.

Siku wiki zikakatika, ikafika Agosti na kuanza mchakamchaka wa shughuli za SADC katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam. Wiki ya nne ya viwanda, mikutano ya makatibu wakuu, mawaziri na hatimaye ikafika siku yenyewe ya Agosti 17 na 18. Mkutano wa wakuu wa nchi na serikali wa SADC.

Nilifika nyuma ya ukumbi na kukaguliwa, baadaye nilianza kutembea kutokea usawa wa Uwanja wa Gymkhana kilipo kituo cha polisi. Kulia na kushoto kwangu kulikuwa kumepambwa na mabango makubwa yanayoonyesha utajiri wa mbuga za wanyama na hifadhi za taifa, milima, mabonde na maporomoko ya maji tulivyo navyo nchini.

Kisiwa cha Zanzibar, wanyama kama Mbega na wengine adimu wanaopatikana bara hili tu lililobarikiwa kila utajiri. Nilijihisi kama naingia mlango wa peponi. Mwili ulinisisimka vinyweleo vikanisimama. Nilitamani dunia nzima ijue kuna nchi inaitwa Tanzania na leo ina ugeni kutoka nchi 16 za Afrika.

Nje ya ukumbi nilifurahishwa na ngoma za asili, zilikuwa zimepangiliwa kwa namna ya kipekee kuvutia kila mtazamaji, kinamama na kinababa wa Kimaasai walikuwa wakinema na kuruka kwa sauti zao za kupendeza na kuvutia.

Utasema ni Twiga waliotoroka mbugani, kinamama wa Kimaasai walikuwa wakichezesha shanga walizozizungusha shingoni utasema wanapeta mahindi. Wao hawaruki hawasogei, wanainua visigino na kuvirudisha, mchezo huo ulileta taswira nzuri ya mtibwiriko wa maungo na kelele za polepole lakini zinazofuatana za shanga mwilini mwao. Huku sauti nzito za kiume zikiunguruma kama Simba mzee, zikisikika kwa nyuma kama kuwagombesha wakinamama wanaolalamika kwa sauti tamu na nyororo.

Ratiba ilionyesha shughuli zinaanza saa mbili asubuhi, kwa kawaida sipendi kuwa wa mwisho katika mambo ya msingi. Saa moja kasoro robo nilikuwa ukumbini, moja kwa moja nilifululiza chumba cha habari gorofa ya kwanza upande wa kushoto. Nilijikuta peke yangu, sikushangaa kwa kuwa dhamira yangu haikutaka niwe wa mwisho.

Baada ya kujipanga nilijitoma ukumbini, upande wa juu tulipopangiwa wanahabari. Mwili ulisisimka kwa kuona siku imewadia kuweka historia. Ni historia katika uandishi wa habari kuripoti tukio kubwa namna hiyo. Sikuwahi kufanya hivyo kabla.

Wakati tukipewa semina na Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika ukumbi wa Mikumi miezi kadhaa kabla ya tukio hili, nilivutiwa na mwanahabari mkongwe Deodatus Balile namna alivyoelezea kwa madaha mkutano wa SADC uliofanyika kwa mara ya kwanza nchini mwaka 2003, ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.

Nilimuona kama aliyeshushwa duniani moja kwa moja bila kuzaliwa, nami nikaweka ahadi Mungu anipe pumzi na afya ili nipate cha kuwaelezea wanahabari wenzangu miaka 16 ijayo namna nilivyoshiriki mikutano ya SADC hatua kwa hatua.

Nilitia mguu wangu eneo la wanahabari saa mbili kasoro, nikaanza kuwaona viongozi wastaafu wakiwasili, alianza Mzee Benjamin Mkapa, akafuata Mzee Jakaya Kikwete kisha akaja Mzee Ali Hassan Mwinyi. Walikaa pamoja wakizungumza na kucheka, ishara nzuri kwa wageni.

 Saa nne kamili asubuhi viongozi wa kitaifa wa nchi 16 za jumuiya hii wakaanza kuingia mmoja baada ya mwingine, alianza mwenyeji Rais Dk. John Magufuli wakafuatia viongozi wengine mmoja mmoja kwa mpangilio wa kupendeza. Walisimama kwa muda wakitizama bendera ndogo zilizopangwa mshazari mbele ya meza zao.

Walipangiwa kukaa kwenye viti vya rangi ya maziwa vilivyodariziwa kwa vitambaa vya mahmeli, juu ya meza kulikuwa na vibakuli vidogo vyenye lawalawa za kuwapumbaza wasichoke kuendesha mkutano. Kila mmoja alipangiwa seti ya vifaa maalum vya kufasiri lugha.

Meza yao ilipendeza kweli maana chini kulitandazwa mashada ya maua kuanzia mwanzo hadi mwisho wa meza yenye urefu yapata futi 30, imepindwa kidogo kuleta taswira ya mwezi mchanga ili kuwafanya watazamaji wawaone vizuri.

Marais walikuwa 11 wakiongozwa na Rais Dk. John Magufuli (Tanzania), Rais Cyril Ramaphosa (Afrika Kusini), Rais Edgar Lungu (Zambia), Rais Dk. Hage Geingob (Namibia), Rais Emmerson Mnangagwa (Zimbabwe), Rais    João Lourenço (Angola), Rais Filipe Nyusi (Msumbiji), Rais Danny Faure (Ushelisheli) na Rais Azali Assoumani (Comoro).

Wengine ni Rais Andry Rajoelina (Madagascar), Rais Felix Tshisekedi (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo - DRC), Makamu wa Rais Everton Herbert Chimulirenji (Malawi), Waziri Mkuu Tom Thabane (Lesotho), Waziri Mkuu Ambrose Mandvulo Dlamini (Eswatini), Waziri wa Mambo ya Nje Unity Dow (Botswana) na Waziri wa Mambo ya Nje Nandi Botha (Mauritius).

Baada ya kuimbwa wimbo wa SADC ukafuata wimbo ya AU kisha ukaimbwa wa Tanzania, nilitamani niitoe sauti yangu yote ili ukumbi mzima ujue kuna mtanzania anaitwa Hafidh Kido anaimba wimbo wa taifa lake.

Cheche za machozi zilinitoka pembezoni mwa macho kwa furaha, nilikuwa nimeukumbatia moyo wangu uliofuatisha mdundo wa Brass Band ya Polisi kwa madaha. Hakika kuwa mtanzania kwenye jumuiya hii ya SADC ni heshima kubwa.

Baada ya hapo zilifuata taratibu za kiitifaki na ukafika wasaa wa Rais Magufuli kukabidhiwa kijiti cha uenyekiti kutoka kwa Rais Geingob wa Namibia. Kilikuwa kipindi cha amani na usikivu wa hali ya juu, kila mmoja alitaka kusikia mwenyekiti mpya atasema nini.

Kama ilivyo kawaida yake, Rais Magufuli ni mkweli na hapendi kupamba maneno. Alieleza alivyoumizwa na alivyofurahishwa ndani ya SADC. Akaahidi kuyabadili yaliyomuumiza ndani ya mwaka mmoja, ikiwa atapewa ushirikiano wa kweli.

Siku ya kwanza ikaisha, vikao vya ndani vikahamia Ikulu ya Dar es Salaam. Siku iliyofuata kama kawaida nikawahi nafasi yangu ndani ya ukumbi. Ulijaa kama jana (Jumamosi Agosti 17, 2019).

Kilichonidhihirikia kuwa leo (Jumapili Agosti 18, 2019) ndio tunaikamilisha safari ya mwezi mzima katika hekaheka za SADC ni pale nilipomuona dada yangu Zamaradi Kawawa ambaye alikuwa mwenyekiti wetu kwa upande wa wanahabari kupitia kamati ya kuratibu mkutano huu, ambaye pia ni Naibu Mkurugenzi wa MAELEZO, alikuwa akiingia ukumbini huku akicheza kwa furaha.

Katika maisha yangu tangu nimjue dada Zamaradi sikuwahi kumuona akicheza, alionyesha kazi imekamilika salama na sasa tumekabidhiwa rasmi jukumu la kuiandika vema SADC ikiwa imerejea nyumbani, Dar es Salaam.

Kikao cha kufunga hakikuwa kirefu, itifaki zilifuata kama kawaida na kilipofika kipindi cha kutoa hotuba ya ufunguzi sote tulikaa kimya kumsikiliza mwenyekiti atakuwa na yapi ya kutuambia. Alipoanza kwa kusalimia kwa lugha ya Kiswahili, nilimuonyesha alama ya dole mwanahabari mwenzangu aliyekaa upande wa kushoto ukumbini; ishara ya kuwa Kiswahili kimekubaliwa kuwa lugha rasmi ya nne ya SADC.

Ni kweli, baadaye Mwenyekiti Rais Magufuli aliueleza umma wa wana SADC kuwa Kiswahili kimepitishwa kwa kauli moja kuwa lugha ya nne ya SASDC. Kila mtu alifurahi, hapo ndipo nilipoamini lugha hii ni lugha ya ukombozi.

Mwisho baada ya kufunga, nilitaka kuwahi kuandika stori ili niitume gazetini Jamvi la Habari. Kwa mara nyingine nikakutana na uso wa bashaha wa Dada Zamaradi akiwa amesimama pembeni ya mlango akiwagongea ‘ngumi’ wanahabari wote waliokuwa wakipita kutoka nje. Ushindi! Hakika ulikuwa ni ushindi wetu sote.

Mwandishi wa makala haya ni  Hafidh Kido ambaye ni Mhariri wa gazeti la Jamvi la  Habari
Na Hafidh Kido

No comments:

Post a Comment