Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) George Simbachawene amesema Serikali imefanya mapitio ya Sera ya
Mazingira ya mwaka 1997 ili kuzingatia changamoto mpya za kimazingira
zinazojitokeza mara kwa mara.
Akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu na Bajeti ya
Ofisi ya Makamu wa Rais na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimazi wa Mazingira
(NEMC) kwa kipindi cha Julai – Desemba 2019 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Viwanda, Biashara na Mazingira amesema Ofisi
imeendelea kuratibu utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 1997
pamoja na Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004.
Simbachawene
amesema Rasimu ya Mwongozo wa mita 60 katika kuhifadhi vyanzo vya maji katika
bahari, maziwa na mito imeandaliwa; Rasimu ya Sera ya Taifa ya Mazingira ya
Mwaka 2020 imeandaliwa na ipo katika hatua ya kuwasilishwa katika vyombo vya
maamuzi; na Itifaki ya SADC ya Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo Endelevu
iliridhiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Rasimu
ya Mwongozo wa Uwekezaji katika usimamizi wa Taka imeandaliwa; Kanuni za
Usumamizi wa Taka za kielekroniki za mwaka 2019 zimeandaliwa; Kanuni za
Usimamizi wa Taka hatarishi za mwaka 2009 zimepitiwa na Mwongozo wa Kitaifa wa kufanya tathmini
ufuatiliaji na utoaji taarifa za hewa ukaa umeandaliwa” Simbachene alisisitiza.
Awali, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi
Joseph Malongo amesema Ofisi hiyo inatarajia kuandaa mkutano mkubwa
utakaowakutanisha viongozi kutoka Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa
kuzungumzia agenda ya Mazingira ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wananchi
kushiriki katika shughuli za utunzaji wa mazingira nchini.
Kwa upande mwingine Mkurugenzi Mkuu wa
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka
amesema Baraza linaendelea na Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria ya Mazingira
kwa kufanya Kaguzi za Mazingira.
“Baraza limefanya ukaguzi katika miradi 870 ili kuhakikisha uzingatiaji wa
Sheria ya Mazingira nchini. Vilevile. Kaguzi hizo zilifanyika katika shughuli
za kiuchumi na kijamii zenye kuweza kuleta athari kwa mazingira” Gwamaka
alisisitiza.
Kuhusu Udhibiti wa Taka Hatarishi, Baraza kwa kushirikiana na
mamlaka nyingine za Serikali lilishiriki katika zoezi la ukaguzi wa makontena 151 ya chuma chakavu yaliyokuwa yanatakiwa
kusafirishwa nje ya nchi ikiwa ni kujua uhalali wa kuendesha biashara hiyo na
kukagua shehena ya makontena hayo ili kubaini aina ya chuma chakavu kilichopo
ndani ya makontena. Aidha, hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa
Mazingira ya mwaka 2004 ikiwemo kutozwa faini, zilichuliwa dhidi ya Makampuni
yaliyokaguliwa na kukutwa na makosa.
Dkt. Gwamaka
amesema kuwa Baraza limesajili jumla ya Miradi 664 (Miradi 387 ya
Tathmini za Athari kwa Mazingira na Miradi 277 ya kufanyiwa Ukaguzi wa Athari
za Mazingira) ikiwa ni asilimia 55 ya miradi ambayo imekusudiwa kufanyiwa
mapitio.
“kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/20.
Kwa kipindi hicho miradi ipatayo 375 imeidhinishwa kupata vyeti, hii ikiwa
miradi 225 kwa ajili ya Tathmini za Athari kwa Mazingira (Environmental Impact Assessment) na Miradi 150 Kwa ajili ya
Ukaguzi wa Athari za Mazingira (Environmental
Audit). Aidha miradi mingine ipo katika hatua tofauti za upembuzi.
Mbunge wa Babati Vijijini Mhe. Jitu Vrajlal
Son ameshauri Serikali kuongeza kasi ya utoaji wa elimu ya mazingira katika
ngazi zote za Serikali na kuhimiza uanzishaji wa Mfuko wa mazingira nchini.
No comments:
Post a Comment