Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeanza kufanya
ufuatiliaji wa maelekezo yake katika kuboresha huduma za matibabu kwa
wazee kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Hayo
yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Dkt. Dorothy Gwajima alipotembelea
hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma na kujionea jinsi walivyoweza
kutekeleza maagizo ya utoaji wa huduma za afya kwa wazee wanaofika
kupata matibabu hospitalini hapo.
Dkt.
Gwajima amesema mahitaji ya maboresho ni mengi hivyo wizara yake
imeona ianze na vitu vile vya msingi ambavyo wazee wamekuwa
wakiyalalamikia kila siku wanapofika kwenye vituo vya kutoalea huduma
za afya.
Ametaja
malalamiko yanayokuwa yakilalamikiwa na wazee wanapofika kwenye vituo
vya afya ni pamoja na mapokezi yasiyoeleweka na kutokupata huduma
iliyokusudiwa na kuongeza kuwa wazee nguvu zimekwisha hivyo wanahitaji
kuongozwa kwahiyo wizara yake wamefanya maboresho kwa kuwa na watu
maalumu wa kuwapokea wazee hao pale wanapoifika hadi kuondoka na
kuwatambulisha kwa kuvaa sare maalumu.
“Kila
kituo lazima kiwe na nesi mmoja, afisa ustawi wa jamii pamoja na
daktari aliyepangwa zamu na lazima wavae sare ambayo itamtambulisha na
imeandikwa ‘Mzee ni Tunu, Tunakupenda, Tunakuheshimu’ pamoja na kuweka
mabango yanayomuelekeza au kumuongoza mzee wapi atapata huduma
anazozihitaji na ambayo yameandikwa "Mpishe Mzee apate huduma kwanza".
Dkt.
Gwajima amesema maelekezo hayo wameyatoa katika hospitali na vituo vya
afya vyote na kwa hatua hiyo sasa wizara inaenda kutengeneza muongozo
ambao utakua wa uwiano kwa hospitali zote. Hata hivyo ameipongeza
hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma kwa kuanza utekelezaji huo na kuwa
itakuwa ya mfano wengine kujifunza utaratibu unaotumika na kuboresha
kulingana na mazingira yao.
Aidha,
Dkt. Gwajima amewataka hospitali zingine kutokusubiri miongozo katika
kutekeleza maelekezo yanayolewa na kusiwe na visingizio vingi kwamba
haiwezekani kwani maagizo yanayotolewa yanawezekana na utekelezaji wake
ni wa mara moja hususan katika hospitali za kuanzia halmashauri hadi
ngazi ya Taifa.
Naye
Kaimu Mkurugenzi wa huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya Dkt. Vivian
Wonanji amesema idara yake imeandaa mkakati wa huduma wa wazee wa
miaka kumi na ifikapo mwezi Juni mwaka huu wataanza kuandaa mpango wa
utekelezaji wake.
Dkt.
Wonanji amesema mpango mkakati huo utakuwa na mambo makuu yakiwemo
kuzalisha wataalam wa kutoa huduma za wazee,"kama tunavyofahamu wazee
wanahitaji mambo mengi ikiwemo masuala ya lishe na utengamao hivyo
mkakati huo utakua na maono muhimu ambayo yatasaidia kuboresha huduma za
wazee nchini”.
Wakati
huo huo Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma Dkt.
Ernest Ibenzi amesema hospitali yake imejipanga kuwahudumia wazee wa
rika tofauti wakiwemo wenye uoni hafifu na hivyo waratibu wa wazee
huwafuata wazee mara wafikapo hospitalini hivyo wanashukuru mapokeo ya
wazee pamoja na wagonjwa wanaofika kupata huduma.
Mnamo
tarehe 7 Mei, mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Samia Suluhu Hassan wakati akiongea na wazee wa Mkoa wa Dar es salaam
aliahidi kuboresha tiba kwa wazee kwani tiba ni haki yao ya msingi
katika daraja lolote lile watakalokua wanaugua kuanzia vituo vya afya,
zahanati hata hospitali za Taifa.
Waziri Dkt.Gwajima akiangalia mfumo wa kuwahudumia wagonjwa uliopo Kwenye hospitali hiyo.
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy
Gwajima akipima afya Kwenye jengo wa wagonjwa wa nje kwa kutumia
'patient monitor' ambayo unapima Presha,mapigo ya Moyo na wingi wa hewa
ya Oksjeni.
Waziri
wa Afya Dkt.Dorothy Gwajima akiangalia Bango linaloelezea huduma za
wazee wakati wa ziara ya kuona utekelezaji wa maboresho ya Huduma ya
Wazee Kwenye hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma.
Waziri
wa Afya Dkt.Gwajima akiwa Kwenye chumba Cha kuwahudumia Wazee kilichopo
Kwenye jengo la wagonjwa wa nje,mbele yake ni Mganga Mfawidhi wa
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma Dkt.Ernest Ibenzi
Waziri
Dkt.Gwajima akiwa amevalia vazi maalumu la kumtambulisha mtoa huduma
ambaye anawahudumia Wazee kwenye hospitali ya Rufaa ya Mkoa
Dodoma.Mkakati huo itatekelezwa nchi nzima Kwenye vituo vya kutolea
huduma.
No comments:
Post a Comment