Matokeo chanyA+ online




Sunday, May 3, 2020

SERIKALI YAFANYA UCHUNGUZI WA VIFAA VYA UCHUNGUZI VYA UGONJWA WA CORONA


Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mbunge wa Iramba Magharibi) akila kiapo mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Hafla iliyofanyika Wilayani Chato Mkoani Geita , , Mei 03, 2020.
 
Rais Dkt. John  Magufuli amemuapisha Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Chato Mkoani Geita.
Rais Magufuli amemtaka Waziri Nchemba kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na mtangulizi wake Marehemu Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga aliyefariki dunia tarehe 01 Mei, 2020 na pia kushirikiana na viongozi wenzake katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya Serikali.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mbunge wa Iramba Magharibi) kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Hafla iliyofanyika Wilayani Chato Mkoani Geita , Mei 03, 2020.

“Nimekuteua kwa mara ya pili kwa sababu naamini unaweza kutekeleza jukumu hili vizuri, na bahati nzuri vijana wengi niliowateua hawajaniangusha, kwa hiyo nakutakia heri katika kazi zako na Mungu akutangulie” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amerejea kauli yake ya kuwataka Watanzania kutokuwa na hofu kubwa dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19) na badala yake waendelee kuchukua tahadhari kama zinavyoelekezwa na wataalamu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisaini hati ya kiapo ya Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mbunge wa Iramba Magharibi) kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Hafla iliyofanyika Wilayani Chato Mkoani Geita , Aprili 22, 2020.
Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mbunge wa Iramba Magharibi) akizunguma mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya kuapishwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Hafla iliyofanyika Wilayani Chato Mkoani Geita , , Mei 03, 2020.
 
Amefafanua kuwa kumekuwa na upotoshaji mkubwa ambao unasambazwa na baadhi ya watu kupitia mitandao ya kijamii na kusababisha hofu kubwa kwa wananchi, hali ambayo haisadii kupunguza tatizo bali kuliongeza na kutengeneza sintofahamu kubwa.
Rais Magufuli amewahakikishia Walimu ambao ni asilimia 49 ya wafanyakazi wote hapa nchini pamoja na wafanyakazi wengine kuwa licha ya changamoto za kiuchumi zinazosababishwa na ugonjwa wa Corona, Serikali imejipanga kuhakikisha wanalipwa mishahara yao kama kawaida na ametoa wito kwa taasisi za kifedha za kimataifa zilizoonesha nia ya kusaidia uchumi wa nchi zinazoendelea, kusamehe mikopo badala ya kutaka kuzikopesha mikopo mipya.
 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza mara baada ya kumuapisha Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mbunge wa Iramba Magharibi) kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Hafla iliyofanyika Wilayani Chato Mkoani Geita , Aprili 22, 2020.
Rais Magufuli amempongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe (aliyeteuliwa kushika wadhifa huo hivi karibuni) kwa kuchukua hatua ya kufanya uchunguzi wa vifaa vya uchunguzi wa ugonjwa wa Corona na ameagiza maabara kuu ya Taifa inayofanya uchunguzi wa ugonjwa huo ichunguzwe vizuri ili kujiridhisha juu ya usahihi wa majibu ya sampuli zinazopelekwa kuchunguzwa.
Amewataka Watanzania wote hasa wanasiasa pamoja vyombo vya habari kuacha kueneza taarifa zinazowajaza watu hofu ama kutumia ugonjwa huu kwa manufaa ya kisiasa na badala yake waungane kutoa elimu sahihi na kuhimizana kuchukua tahadhari za kutoambukizwa.
 
Mwigulu Lameck Nchemba (Mbunge wa Iramba Magharibi) akisaini hati ya kiapo mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya kuapa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Hafla iliyofanyika Wilayani Chato Mkoani Geita, Mei 03, 2020.
 
Rais Magufuli amewapongeza Madaktari, Wauguzi, Wafanyakazi wa Afya na wadau mbalimbai walio mstari wa mbele katika kuwahudumia watu wanaopatwa na maambukizi ya ugonjwa wa Corona na amewahakikishia kuwa Serikali inachukua hatua madhubuti za kukabiliana nao ikiwemo kupata dawa kutoka mahali popote itakapopatikana.
Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mbunge wa Iramba Magharibi) mara baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Hafla iliyofanyika Wilayani Chato Mkoani Geita. Mei 03, 2020.
PICHA NA IKULU

Ameelezea kushangazwa kwake na viongozi ambao wanazuia watu wanaofariki dunia kusafirishwa kwenda kuzikwa nyumbani kwao, na Viongozi wa Dini walioonesha kutetereka kiimani, hivyo ametoa wito kwa viongozi wote kusimama imara, kuonesha uongozi wa kweli na kuwapa matumaini wananchi badala ya kuwajaza hofu.
Rais Magufuli amempongeza Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zubeiry bin Ally na Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga pamoja na viongozi wengine wa Dini waliosimama katika imani na kuwataka Waumini waendelee kusali, kufunga na kumuomba Mwenyezi Mungu aepushe ugonjwa huu.

Friday, May 1, 2020

WAZIRI KALEMANI - TANESCO KATENI UMEME KWA WADAIWA SUGU MUONGEZE MAPATO


Vijana wakiendelea na kazi ya ujenzi katika kituo cha kupoza na kusambaza na umeme cha Zuzu jijini Dodoma, wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani na Wajumbe wa Bodi ya wakurugenzi ya TANESCO ya kukagua ujenzi wa upanuzi wa kituo hicho Aprili 30,2020.
 
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani ameliagiza Shirika la Umeme nchini( TANESCO) kuendelea kukata umeme kwa wadaiwa sugu ili kukusanya mapato zaidi na kulipa madeni ya shirika hilo.

Dkt. Kalemani alisema hayo, Aprili 30, 2020, Jijini Dodoma, alipokutana na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO, kuzungumzia tathimini ya miaka mitano ya utekelezaji wa miradi mbalimbali, baada ya kufanya ziara ya kukagua ujenzi wa upanuzi wa kutuo cha kupoza na kuzambaza umeme cha Zuzu.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) pamoja na Wajumbe wa Bodi ya wakurugenzi ya TANESCO wakipata maelezo kutoka kwa msimamizi mkuu wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Zuzu jijini Dodoma, baada ya kufanya ziara ya kukagua ujenzi wa upanuzi wa kituo hicho, Aprili 30,2020.


Katika kikao hicho, mambo mbalimbali yalijadiliwa kuhusiana na nishati ya umeme inayozalishwa nchini kwa lengo la kuleta manufaa makubwa zaidi kiuchumi kwa nchi, Shirika na watumiaji wa umeme huo ikiwemo viwanda, wafanyabiashara na matumizi mengine.

Dkt. Kalemani aliiagiza TANESCO, kulipa madeni yote inayodaiwa na kutoongeza madeni mapya, vilevile wadaiwa sugu wakumbushwe madeni yao,na endapo hatawalipa, TANESCO iwakatie umeme, kwa kufanya hivyo kutamaliza tatizo la wadaiwa sugu. 

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani( pili kulia) aliyeambatana na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, akipita kukagua shughuli za ujenzi wa upanuzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Zuzu jijini Dodoma, Aprili, 30,2020, katikati ni Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu.

“TANESCO inadaiwa madeni makubwa, pia ina wateja wengi sana ambao ni wadaiwa sugu wanaodaiwa fedha nyingi sana na hawalipi ,zimo Taasisi, Mashirika ya Umma na binafsi, pamoja na watumiaji wa kawaida, ninawaagiza nendeni mkawakatie umeme! narudia tena mkakate umeme! mkishaukata, wahusika watalipa na wataonyesha ushirikiano mkubwa, tofauti na kumdai kawaida tu”, alisema Dkt. Kalemani.

Kuhusu wizi na uhujumu wa miundombinu ya umeme, Dkt. Kalemani, aliitaka TANESCO, Bodi ya TANESCO na Watendaji wa Wizara ya Nishati, kushirikiana kwa pamoja kutafuta njia sahihi naya kisasa zaidi ya kubaini wizi wa umeme,unaofanywa na watu wasiowaaminifu na kusababisha hasara kwa shirika na kupoteza mapato ya taifa.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani(,( mwenye kofia nyeupe) akiwa na Wajumbe Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO) akimueleza jambo Mwenyekiti wa bodi hiyo, Dkt, Alexander Kiyarunzi (kushoto) walipotembelea eneo la kuhifadhi nguzo wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa upanuzi wa kituo cha kupoza na kufua umeme cha Zuzu jijini Dodoma, Aprili 30,2020. 
 
“Wizi wa umeme upo na haukubaliki, tuweke mfumo sahihi wa kisasa kubaini wahusika, tuache na hii tabia ya kukimbizana kimbizana na wezi, pia sisi watumishi tuwe wazalendo,na wasimamizi wazuri wa miundombinu yetu,vilevile tuwe na walinzi wenye weledi katika miradi yetu bila kujali niya serikali au mtu binafsi, jukumu la ulinzi ni letu sote faida ya Taifa kwa jumla”,alisisitiza Dkt. Kalemani.

Aidha aliwataka kuendelea kufanya tathmini na uwiano wa gharama za kutengeneza nguzo za Zege na nguzo zinazotumika sasa,ili kuangalia uwezekano wa kutumia nguzo za zege katika maeneo yote nchini lakini kwa gharama nafuu, kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya kuoza ama kuungua kwa nguzo katika maeneo mbalimbali. 
 
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani( katikati) akizungumza na Wajumbe wa Bodi ya wakurugenzi ya TANESCO wakati wa kikao baada ya ziara ya kukukagua ujenzi wa upanuzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Zuzu jijini Dodoma, Aprili 30,2020, kulia ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu na kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said.

Hata hivyo aliweka wazi kuwa katika baadhi ya maeneo machache ambayo ni korofi nguzo za zege zimeanza kutumika japo ni za gharama kubwa.

Vilevile alitaka kuongezeka kwa idadi ya wateja wa umeme katika kila sekta, kuharakisha uunganishaji wa umeme kwa mteja pale anapomaliza kulipia gharama husika, pamoja na kutatua changamoto za wateja kwa wakati sahihi ili kuvutia wateja wengi zaidi na kuondoa malalaliko.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani( katikati) akizungumza na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO wakati wa kikao baada ya ziara ya kukukagua ujenzi wa upanuzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Zuzu jijini Dodoma, Aprili 30,2020, kulia ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu na kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu aliwataka TANESCO kuangalia uwezekano wa kutoa zawadi kubwa kwa wasamaria wema wanaotoa taarifa za siri kuhusu wanaohujumu na kuiba umeme tofauti na ile inayotolewa sasa, ambayo pia huchukuwa muda mrefu kuikabidhi kwa mhusika.

Mgalu alikitaka kitengo husika kitunza siri za watoa taarifa,pia kifanye uchunguzi wa kina na kutoa adhabu kwa mtumishi yeyote atakayetiliwa shaka, au kuhusika na wizi pamoja na kuhujumu miundombinu ya umeme kama inavyofanywa kwa wahisika wengine wanaobainika.

Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO wakimsilikiza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani,( hayupo pichani) wakati wa kikao baada ya ziara ya kukukagua ujenzi wa upanuzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Zuzu jijini Dodoma,Aprili 30,2020.


Na Zuena Msuya Dodoma,
Vilevile kuwe na uhamasishaji wa kuwavutia watoa taarifa ili kupata matokeo chanya kunusu wizi na uhujumu wa miundombinu ya umeme nchini.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Zena Said, alieleza kuwa ili kukabiliana na changamoto ya wizi na uhujumu wa miundombinu ya umeme, watashirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,(TAMISEMI) kuimarisha ulinzi kuanzia ngazi za Kaya.

Mhandisi Said, alisema kwa kufanya hivyo kutasaidia sana kubaini wezi na wahujumu miundombinu ya umeme kwa kuwa watu hao wasio wazalendo huwa wanaoneka na hata kufahamika katika maeneo yao.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO, Dkt. Alexander Kyaruzi, aliishuruku Wizara ya Nishati kwa kuwapa ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yao na kuyafanyia kazi yale waliokuwa wakiishauri wizara hiyo, katika kipindi chote cha miaka mitano

Dkt.Kiyarunzi, alikiri kwa kuwa kazi ya kusambaza umeme si jambo jepesi, hivyo wanajivunia kuona maendeleo makubwa katika sekta ya nishati ya kuongeza wigo wa usambazaji wa umeme vijijini, kujenga miradi mikubwa ya kuzalisha, njia za kusafirisha na kusambaza umeme pamoja na vituo vya kupoza na kusambaza umeme nchini.

Awali kabla ya kufanyika kwa kikao hicho, Uongozi wa Wizara na Wajumbe wa Bodi hiyo walifanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa upanuzi wa Kituo kikubwa zaidi nchini cha Kupoza na kusambaza umeme cha Zuzu kilichopo jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa Dkt. Kalemani, ujenzi wa kituo hicho utakamilika mwishoni mwa mwezi huu wa Mei, 2020 na kitakuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 648 tofauti na vituo vingine.

Na kituo hicho kitaimarisha upatikanaji wa umeme kwa Jijiji la Dodoma ambalo linaendelea kukuwa kwa kasi na kitakuwa ndiyo kitovu cha vituo vyote vya kupoza kuzambaza umeme katika mikoa yote nchini na kuupeleka nchi jirani pale itakapohitajika kufanya hivyo.

WAZIRI BASHUNGWA AWAPONGEZA MUHIMBILI KWA KUTENGENEZA VAZI MAALUMU LA WAUGUZI.

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa

Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent Bashungwa ameupongeza uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kutengeneza mavazi maalum (coverall) za wauguzi ambayo yanasaidia wahudumu wa afya kujikinga na ugonjwa wa Corona.

“Nawapongeza hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kutengeneza mavazi maalum (coverall) ya wauguzi Mungu awabariki na kuwalinda wauguzi wetu”.

Aidha, amevipongeza viwanda vyote nchini kwa kuendelea kuhakikisha vinatoa mchango mkubwa kwa kipindi hiki cha kupambana na ugojwa wa Corona na ametoa wito kwa viwanda na mtanzania yeyote anaeweza kutengeneza mavazi maalum ya wauguzi ajitokeze na awasiliane na Wizara ya Viwanda na Biashara.

“Viwanda vyetu nchini hamjawahi kuniangusha, yeyote anayeweza kutengeneza awasiliane na Wizara ya Viwanda na Biashara namba ya simu +255784218155"  ili kupata muongozo.

BIL. 33 KUTUMIKA KUIMARISHA HUDUMA ZA KIJAMII NCHINI



Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa akijadiliana jambo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto  Ummy Mwalimu Bungeni

Wizara ya Afya, kupitia Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii inatarajia kutumia Jumla ya shilingi bilioni 33.195 ili kutekeleza shughuli mbalimbali za kijamii hususani zilizopewa kipaumbele kwa mwaka wa fedha 2020/21.
Akiwasilisha Hotuba ya Wizara ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto  Mhe. Ummy Mwalimu amesema katika mwaka wa fedha 2020/21 Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii inatarajia kutumia kiasi hicho cha fedha kwa lengo la kuimarisha huduma na mafunzo kwenye Taasisi za Ustawi na Maendeleo ya Jamii, kukarabati makazi ya wazee, kujenga mahubusu za watoto na kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Alisema kuwa bajeti hiyo itasaidia kuimarisha Kujenga kumbi pacha na hosteli katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru ambapo jumla ya shilingi bilioni 2.7 zimetengwa, pia kuboresha utoaji wa mafunzo ya taaluma ya maendeleo ya jamii ili kukidhi mahitaji ya soko sambamba na kukuza ujuzi wa wahitimu ikiwemo kuwajengea uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa kwa kutenga jumla ya shilingi bilioni 6.6.
Maeneo mengine yaliyotengewa fedha ni pamoja na ukarabati wa majengo na miundombinu katika makazi ya wazee kwa shilingi milioni 400, ujenzi wa Shule ya Maadilisho katika Mkoa wa Geita shilingi milioni 200, kuimarisha ujenzi wa mahabusu ya watoto katika mikoa ya Kigoma na Mtwara shilingi milioni 700 na kuwezesha Taasisi ya Ustawi wa Jamii kuboresha utoaji wa mafunzo yanayokidhi mahitaji ya soko shilingi milioni 250.
Aidha, jumla ya shilingi milioni 827.95 zimetengwa kwa ajili ya shughuli za kutokomeza ukatili wa kijinsia katika jamii.
“Ili kutekeleza vipaumbele vilivyoanishwa kwa mwaka 2020/21, Wizara kupitia Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii imekadiria kutumia kiasi cha shilingi bilioni 33 kwa ajili ya kutekeleza majukumu mbalimbali ya Wizara ikiwa ni pamoja na uendeshaji wa ofisi na miradi ya maendeleo” alisema
 Ummy amesema Wizara imeendelea kukuza ari ya jamii kushiriki katika kujiletea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kutumia nguvu kazi na rasilimali zinazowazunguka na kusimamia masuala yote ya ushirikishwaji wa jamii kwenye sekta mbalimbali.

KAMPUNI YA ASAS IMEKABIDHI (FULL BODY MACHINE) HOSPITALI YA RUFAA IRINGA

 Mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoani Iringa Dr Alfredy Mwakalebela akiwa anapita katikaFULL BODY MACHINE
Afisa Usalama, Afya, Mazingira na Ubora wa kampuni ya Asas Cosmas Charles akiwa anapita katikaFULL BODY MACHINE


 Afisa Usalama, Afya, Mazingira na Ubora wa kampuni ya Asas Cosmas Charles akimkabidhi ndoo maalum kwa mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoani Iringa Dr Alfredy Mwakalebela

NA FREDY MGUNDA,IRINGA.

Kampuni ya Asas ya mkoani Iringa imekabidhi msaada wa mashine ya kutakasa mwili na vifaa vingine vya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona katika hospitali ya rufaa ya Mkoani Iringa.

Akikabidhi msaada huo kwa mganga mkuu wa hospitali ya rufaa mkoani Iringa, kwa niamba ya mkurugenzi  uzalishaji wa kampuni ya Asas ,Afisa Usalama, Afya, Mazingira na Ubora wa kampuni ya Asas Cosmas Charles alisema kuwa lengo LA kutoa msaada huo ni kuhakikisha wananchi wote wanaenda katika hospitali hiyo wanajikinga na maambukizi ya virusi vya Corona ambavyo vimekuwa vinahatarisha maisha ya binadamu kote duniani.

 Alisema kuwa kampuni ya Asas imekuwa ikiwakumbuka mara kwa mara wananchi katika njia tofauti ndio maana baada ya kutokea kusambaa kwa virusi vya Corona Kampuni imekuwa ikijitoa kuhakikisha wananchi wa mkoa wa Iringa wanajikinga vilivyo.

Kampuni imekuwa inaendelea kutoa elimu juu ya maambukizi ya virusi vya Corona katika sekta mbalimbali hapa mkoani Iringa kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanaendelea kuwa salama.

Aidha Charles alivitaji vitu ambavyo kampuni ya Asas imevitoa katika hospitali ya Rufaa ya Iringa ambavyo ni mashine ya kutakasa mwili mzima,ndoo maalum 80 na barakoa 1200

Kwa upande mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoani Iringa Dr Alfredy Mwakalebela aliipongeza kampuni ya Asas kwa msaada huo walioutoa kwa kuwa ni mkubwa kulingana na mahitaji ya kujinga na maambukizi ya virusi vya Corona.

Mwakalebela alisema mashine hiyo ya kutakasa mwili mzima yawezekana nyanda za juu kusini ndio imekuwa ya kwanza kupatikana katika hospitali za rufaa kutoka na uhitaji wake.


"Leo tumepokea mashine hii ambayo ni bora na nzuri katika kuhakikisha tunapambana vilivyo na maambukizi ya virusi vya Corona ambvyo vimekuwa vikishia uhai wa binadamu kote duniani" alisema 

Mwakalebela alisema kuwa licha ya kutoa mashine hiyo lakini kampuni ya Asas imetoa pia ndoo maalum 80 kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona pamoja barakoa 1200.



WAFANYAKAZI WA TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE WAPEWA MAFUNZO YA MARA KWA MARA KUHUSU UGONJWA WA CORONA (COVID – 19)


Utoaji wa mafunzo ya mara kwa mara ya jinsi ya kupambana na  ugonjwa wa Corona  (COVID-19) kwa wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) umewasaidia kuelewa namna ya kujikinga na ugonjwa huo  na kuwahudumia wagonjwa bila ya kupata maambukizi.
 
Mafunzo hayo ambayo yamekuwa yanatolewa  kwa wafanyakazi wa Taasisi hiyo tangu ugonjwa huo ulipotangazwa hapa nchini mwanzoni mwa mwezi wa tatu mwaka huu yamewasaidia  kutokuwa na hofu na kuendelea kutoa huduma ya matibabu kwa wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo kiufanisi zaidi.
Afisa Muuguzi wa chumba cha upasuaji kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Aimana John akiwaelekeza wauguzi wenzake namna sahihi ya kunawa mikono kwa maji safi yanayotiririka na sabuni wakati wa   mafunzo ya jinsi ya kupambana na  ugonjwa wa Corona  (COVID-19) yanayotolewa kwa wafanyakazi wa Taasisi hiyo.
Hayo yamesemwa jana  jijini Dar es Salaam  na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi wakati akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi hiyo waliohudhuria  mafunzo hayo.

Prof. Janabi alisema baada ya wafanyakazi wa JKCI kupewa mafunzo wameweza  kuufahamu vizuri ugonjwa wa Corona, kufahamu njia za kuzifuata ili wasipate maambukizi na wasiwaambukize wengine na  kuondoa unyanyapaa kati yao na wagonjwa kwani ugonjwa wa Corona hauchagui unaweza kumpata mtu yeyote.

“Katika mafunzo tunayoyatoa kwa wafanyakazi wetu tunawafundisha jinsi ya kuwahudumia wagonjwa kipindi hiki Kkigumu ambacho Dunia inapambana na janga la ugonjwa wa Corona. Kwani baadhi ya  dalili za ugonjwa huu zinafanana na magonjwa ya  moyo ambazo ni kushindwa kupumua  na kukohoa  hivyo basi wakifahamu jinsi ya kujikinga kutawasaidia  kuepuka kupata maambukizi’’, alisema Prof. Janabi.

Mkurugenzi huyo Mtendaji alisema ili kuwalinda wafanyakazi wa Taasisi hiyo  wasipate maambukizi wamefunga  mashine ya kutakasa mwili, wametoa vitakasa mikono pamoja na barakoa kwa wafanyakazi wote  pamoja na kuwapima joto la mwili .
Mkurugenzi Mtendaji wa  Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumza na  Wauguzi wa Taasisi hiyo walioshiriki   mafunzo ya jinsi ya kupambana na  ugonjwa wa Corona  (COVID-19) yanayotolewa kwa wafanyakazi wa Taasisi hiyo. Lengo la mafunzo hayo ni kuwafanya wafanyakazi wa Taasisi hiyo  kuufahamu vizuri ugonjwa wa Corona na kufahamu njia za kuzifuata ili wasipate maambukizi na wasiwaambukize wengine.
Picha na JKCI
Aidha kwa wataalamu wa afya ambao wanawahudumia wagonjwa wanaohisiwa kuwa na ugonjwa wa Corona wanavaa vifaa kinga  na kufuata mwongozo wa kuzuia maambukizi wa mwaka 2018 na wa uzuaiaji wa maambukizi ya Virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona (COVID-19) wa  mwezi wa kwanza mwaka 2020 wakati wanawahudumia wagonjwa hao.

Prof. Janabi alisema, “Wagonjwa wanaofika kutibiwa katika  Taasisi yetu wanapimwa joto la mwili kabla ya kuanza kupata huduma ya matibabu pia tumefunga mabomba ya maji pamoja na kuweka vitakasa mikono katika maeneo mbalimbali ya Taasisi yetu hii inawafanya kupata nafasi ya kunawa mikono mara kwa mara”,. 

“Tunatoa elimu ya ugonjwa huu kwa wagonjwa na ndugu wa wagonjwa  kupitia vipindi mbalimbali vinavyorushwa katika Televisheni zilizopo katika Taasisi yetu pia wataalamu wetu wanatoa elimu kila siku kabla ya kuanza kwa kliniki  zetu’’

Prof.Janabi aliongeza kuwa Taasisi hiyo imetenga wodi maalum kwa wagonjwa wanaohisiwa kuwa na dalili za ugonjwa wa Corona ambao baada ya majibu ya vipimo kutoka na kubainika kuwa na ugonjwa huo wanapelekwa katika kituo cha Amana na kuendelea  kupewa huduma za matibabu ya moyo wakiwa huko.

Kwa upande wake mratibu wa mafunzo hayo ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha utafiti na mafunzo  Dkt. Naiz Majani alisema kuwepo kwa mafunzo hayo kumesaidia kwa kiasi kikubwa kuwaondoa hofu wafanyakazi wa Taasisi hiyo kuhusu ugonjwa wa Corona.

Dkt. Naiz ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto alisema mafunzo hayo yanatolewa katika vikundi vichache vya wafanyakazi kutokana na kada zao hali ambayo inawasaidia kuelewa zaidi.

“Katika Taasisi yetu tuna wafanyakazi wa kada ya afya na ambao siyo wa kada ya afya, hata  mafunzo tunayoyatoa tumewagawa kutokana na kada zao na  lugha tunayotumia kufundishia ni tofauti hii yote tunataka wauelewe kwa undani zaidi ugonjwa huu na jinsi ya kujikinga wao na kuwakinga wengine wanaowazunguka”, alisema Dkt.Naiz.

Daktari huyo bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto aliwaomba washiriki wa mafunzo hayo kutoa elimu waliyoipata kwa watu wengine ili wajikinge na ugonjwa huo. Pia wafuate maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya ambayo ni kuvaa barakoa, kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi yanayotiririka na sabuni , kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na kukaa umbali wa zaidi ya mita moja kati ya mtu na mtu.

KAMANDA WA POLISI MKOA WA IRINGA APOKEA VIFAA VYA KUJIKINGA NA VIRUSI VYA COVID 19 KUTOKA KAMPUNI YA AGORA WOOD PRODUCT

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidi wa Polisi (ACP), Juma Bwire kulia(kulia) akipokea vifaa vya kujikinga dhidi ya Virusi ya Covid 19 kutoka Kampuni ya Agora Wood Product vyenye thamani Tsh Milioni 6. 5 kuwasaidia askari Polisi kujilinda afya zao. (Picha na Datus Mahendeka wa Jeshi la Polisi)
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidi wa Polisi (ACP), Juma Bwire kulia(kulia) akipokea vifaa vya kujikinga dhidi ya Virusi ya Covid 19 kutoka Kampuni ya Agora Wood Product vyenye thamani Tsh Milioni 6. 5 kuwasaidia askari Polisi kujilinda afya zao. (Picha na Datus Mahendeka wa Jeshi la Polisi)

SIJARIDHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA CHAMA KIKUU CHA USHIRIKA GEITA - KATIBU MKUU KUSAYA



Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa amepanda juu ya ngazi kutizama mtambo wa kuchambua pamba katika kiwanda cha Matongo Farming Ltd wilaya ya Geita .Kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha robota 450 zenye uzito wa kilo 200 kwa siku. 

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo ametembelea Chama Kikuu cha Mkoa wa Geita (Geita Cooperative Union-GCU) kilichopo Kasamwa wilaya ya Geita na kutoridhishwa na hali ya kiwanda cha kuchambua pamba kushindwa kufanya kazi muda mrefu.

Ametoa kauli hiyo leo (01.05.2020) wakati alipotembelea na kukagua shughuli za taasisi zilizo chini ya wizara yake na kusema kiwanda cha kuchambua pamba (ginnery) Kasamwa kimeshindwa kujiendesha kutokana na mitambo na majengo yaliyopo kuwa ya kizamani yaliyotumika toka mwaka 1956 

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya ( aliyevaa koti la bluu ) akiwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Kiwanda cha Matongo Bw.Mwalida Samson wakitembelea kiwanda hicho mjini Geita leo.

“Nimekagua na sijaridhishwa na jinsi kiwanda (ginnery) hii ya Kasamwa kuona haina hata mtambo mmoja unaofanya kazi hali inayopekea pamba ya ya wakulima kuchakatwa kwenye viwanda binafsi “ alisema Kusaya

Amewaagiza viongozi wa Chama kikuu cha ushirika Geita kushirikiana na serikali ya mkoa na wadau kufufua kiwanda hicho ili kitumike kuongeza thamani ya zao la pamba inayozalishwa wa wakulima wa Geita kwa kutafuta mitambo ya kisasa. 

Majengo ya kiwanda cha kuchambua pamba yanayomilikiwa na Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Geita (GCU) kama yanavyooneka leo wakati Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (hayupo pichani) alipotembelea na kusema hajaridhishwa kuona mali ya wakulima ikiwa haitumiki. 

Awali Katibu Mkuu Kusaya alikagua kiwanda cha Matongo Farming Limited cha Geita na kukuta kimesimama kuzalisha marobota ya pamba kutokana na upungufu wa malighafi.

Kiwanda hicho kinachomilikiwa na Samson Ng’walida kilianzishwa mwaka 2018 na kina uwezo wa kuzalisha marobota 450 kwa siku na kuchambua pamba mbegu tani 270 kwa siku.
 

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa anakagua matrekta yanayotumika kwenye kiwanda cha kuchambua pamba cha Matongo mjini Geita leo. 

“Uwezo wa kiwanda ni kuchambua tani 48,600 kwa mwaka na msimu huu wa 2019/2020 tumefanikiwa kuzalisha jumla ya robota 9,412 za pamba nyuzi sawa na asilimia 19 ya uwezo wa kiwanda” alisema Mwalida Samson ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa kiwanda cha Matongo Ginery.

Kufuatia hali hiyo Katibu Mkuu Kusaya alitoa wito kwa mikoa yote 17 inayozalisha pamba nchini kutengeneza mazingira rafiki kwa wananchi na wawekezaji ili waongeze uzalishaji wa pamba kukidhi malengo ya Serikali ya awamu ya Tano kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda. 

“Napenda kuona uchakataji wa pamba unafanyike mwaka mzima badala ya miezi mitatu au minne ya sasa kutokana na ukosefu wa malighafi hali inayosababisha ajira kupungua na serikali kukosa mapato kutokana na viwanda kutozalisha bidhaa za pamba” alisema Kusaya.  

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (kushoto) akitazama mizani ya kisasa inayotumika na kiwanda cha kuchambua pamba Matongo kupima uzito wa marobota ya pamba leo wilayani Geita.

Amewataka wataalam wa kilimo nchini kuwasaidia wakulima kupata ya mbegu bora za pamba zinazozalishwa kituo cha utafiti TARI Ukiriguru pamoja na matumizi ya pembejeo na mbolea ili kuongeza tija na uzalishaji wa zao hilo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Tanzania Marco Mtunga alisema takwimu zinaonesha mkoa wa Geita umezalisha kilo milioni 33 za pamba katika msimu wa 2019 kiasi ambacho ni kidogo kulingana na mahitaji makubwa ya viwanda vilivyopo mkoani humo.

Aliongeza kusema uwezo wa viwanda vya ndani nchini kwa sasa ni kuchakata pamba ni tani milioni 1.2 wakati uzalishaji umefikia tani 348,910 na kusema bodi yake itaendelea kubuni mikakati mizuri ili uzalishaji pamba uongezeke.