Matokeo chanyA+ online




Thursday, April 22, 2021

MIGOGORO NDANI YA KAMPUNI ITATULIWE KWA KUFUATA MISINGI YA SHERIA NA KANUNI - MHE KITILA MKUMBO



 Migogoro ndani ya kampuni itatuliwe kwa kufuata misingi ya taratibu, sheria na kanuni na kama migogoro hiyo ipo mahakamani basi iachiwe mahakama kufanya maamuzi yake na sio kuingiliwa kwenye maamuzi hadi hapo itakapokamilika na kuletwa kwenu rasmi kwa taratibu zinazotakiwa kufuatwa.   

Kauli hiyo imetolewa na Mhe Kitila Mkumbo, Waziri wa Viwanda na Biashara alipofanya ziara ya kikazi katika taasisi ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) leo tarehe 21 Aprili, 2021 mkoani Dar es Salaam.  

“Unaweza kukuta kwenye kampuni wamegombana kutokana na hisa au mmoja anataka kuzidisha hisa kwenye kampuni kinyemela, hayo yatatuliwe kisheria na kikanuni na sio kutumia busara sana ili kuweza kupunguza migororo mingi” amesema Mkumbo 

Pia, Mhe Mkumbo ametoa wito kwa wafanyabiashara kuwa na muamko wa kusajili biashara kwasababu kurasimisha biashara inaanza na kusajili, hivyo Watanzania na  Wafanyabiashara waitumie Brela katika kurasimisha biashara ili wapate faida za kutambulika wanapofanya biashara na uzuri taratibu za urasmishaji umerahisishwa kwa njia ya mtandao

Pia, Mhe Mkumbo amesema kuwa taasisi ya Brela imepewa jukumu la kuwezesha ufanyaji biashara nchini na sio kudhibiti biashara, hivyo katika utekelezaji wa majukumu amewaelekeza watumishi wa Brela kila wanapopokea taarifa kutoka kwa mfanyabaishara kutaka kufunga biashara au kampuni afuatiliwe kwa ukaribu ili kujua changamoto iliyopelekea kufungwa kwa kampuni hiyo,

“Kama taasisi yenye jukumu kubwa tusione sifa kumhudumia mfanyabiashara anayetaka kufunga biashara labda ufungaji huo utokane na migogoro ndani ya kampuni” amesisitiza Mhe Mkumbo 


Nae, Afisa Mtendaji Mkuu wa Brela, Bw Godfrey Nyaisa amesema kuwa hadi sasa kwa mwaka huu wa fedha, kampuni zilizosajiliwa ni 7148 na malengo ya taasisi ni kufikia usajili wa makampuni 9528 ambapo hadi sasa usajili umefikia asilimia 75 ongezeko hili limetokana na matokeo ya uboreshaji wa mfumo wa usajili kwa njia ya mtandao

Bw Nyaisa ameeleza kuwa kwa sasa usajili wa kampuni unakamilika ndani ya siku moja, changamoto hutokea endapo anayesajili  amewasilisha nyaraka zenye kutiliwa mashaka na wataalam kutoka kwetu au kuwasilisha nyaraka zisizokamilika

Pamoja na kuongea na wafanyakazi Mhe Kitila Mkumbo ametembelea jengo jipya linalotarajiwa kuwa makao makuu ya Brela, ukarabati wa jengo linategemea kumalizika mwishoni mwa mwezi Juni mwaka 2021

Wednesday, April 21, 2021

DKT. MWIGULU - ADA YA TATHMINI YA MIKOPO KWENYE BENKI YA MAENDELEO YA KILIMO NI HALALI


Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alipokuwa akijibu swali bungeni kuhusu kigezo cha tozo ya asilimia moja kwa mkopaji wa Benki ya Kilimo Tanzania, bungeni jijini Dodoma. 

Na Saidina Msangi, WFM, Dodoma

 Serikali imesema kuwa ada ya tathmini ya mikopo inayotozwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ni kwa ajili ya kulipia gharama za uchambuzi wa maombi ya mkopo ambayo ni pamoja na shajala, uhakiki wa mradi na dhamana ya mkopo.

Hayo yamebainishwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Halima Mdee, aliyehoji kigezo cha tozo ya asilimia moja kwa mkopaji wa Benki ya Kilimo ambapo asilimia 50 inalipwa kabla ya kuanza kufanya tathmini na asilimia 50 inalipwa baada ya mkopo kuidhinishwa.

Dkt. Mwigulu amesema kuwa kigezo kinachotumika kutoza ada ya uchambuzi wa maombi ya mikopo ni gharama halisi za uchambuzi wa maombi hayo zinazotokana na nguvu ya soko kwa wakati husika, utaratibu huo ni wa kawaida kwa taasisi za fedha kutoza ada ya uchambuzi wa maombi ya mikopo.

“Endapo mkopo hautaidhinishwa, asilimia 50 ya asilimia moja iliyolipwa hairejeshwi kwa mwombaji wa mkopo kwa kuwa kiasi hicho kimetumika kulipa gharama za uchambuzi wa mkopo”, alifafanua Dkt. Mwigulu.

Aidha alisema kuwa Sekta ya kilimo inapata mikopo kidogo kutokana na changamoto ya mikopo chechefu kama ilivyobainishwa katika ripoti ya Mdhibti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambapo kiasi cha Sh. Bilioni 129 kilirekodiwa huku Sh. bilioni 2.1 tu iliweza kurejeshwa.

Alisema kuwa Serikali inampango wa kubadilisha sekta ya kilimo kuwa ya uhakika ili kuwezesha wakulima kurejesha mikopo, matumizi ya mbegu bora, kilimo cha umwagiliaji, uhifadhi na masoko ambayo yatamuwezesha mkulima kuwa na uhakika wa kurejesha mkopo na hata benki kuwa na uhakika wa makusanyo na riba kuwa rafiki.

Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali itaendelea kuiangalia benki hiyo kuona namna ya kuiwezesha kimtaji ili kuwezesha kukuza uchumi wa viwanda na kukuza kipato cha wananchi kwa ujumla ili kusonga mbele kiuchumi.


MBUNGE MAVUNDE AGAWA MIFUKO YA SARUJI YENYE THAMANI YA SH MILIONI 10 KUSAIDIA SEKTA YA ELIMU JIJINI DODOMA

 






Charles James, Michuzi TV

Katika kuunga mkono juhudi  za Serikali za kutoa elimu bure, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde amekabidhi mifuko ya Saruji 580 yenye thamani ya Sh Milioni 10 yenye lengo la kusaidia ujenzi wa madarasa na matundu ya vyoo kwenye Shule za Msingi na Sekondari ndani ya jimbo hilo.

Mbunge Mavunde amekabidhi mifuko hiyo kwa Afisa Elimu Msingi, Joseph Mabeyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma ikiwa ni ahadi yake aliyoitoa muda mrefu ya kuendelea kukamilisha maeneo mengi yenye upungufu wa madarasa na yale ambayo hayakua na shule za msingi na sekondari.

Amesema Saruji hiyo aliyokabidhi itakwenda kutumika kama chachu katika maeneo hayo yote ambayo wanakwenda kuanza ujenzi wa shule za msingi na sekondari lakini pia kuongezea madarasa na matundu ya vyoo kwa shule ambazo zina upungufu.

" Nichukue fursa hii kuwapongeza Afisa Elimu Msingi na Sekondari kwa mchango wenu mnaoutoa kwenye sekta ya elimu na ndio maana na mimi nawiwa sana kuendelea kuchangia kwani napata mchango mkubwa kwenu, lengo letu ni kuendelea kutatua changamoto kwenye sekta ya elimu na mimi sitochoka kwani ndio kazi ambayo niliomba kwa wananchi.

Matumaini yangu ni kwamba ndani ya kipindi hiki kifupi tutakua tumeanza ujenzi wa Shule nyingi za Msingi na Sekondari, lengo langu ni kuwaona watoto wa Dodoma wanasoma katika mazingira rafiki.

Leo tumeanza na hatua ya kwanza ya kukabidhi Saruji hii yenye thamani ya Sh Milioni 10 lakini tutaendelea na utaratibu mwingine hatua kwa hatua na ninayo furaha kwamba zile fedha tulizoomba kwa Waziri Mkuu Sh Bilioni 1.9 sasa zitaanza kufanya kazi katika baadhi ya Shule kwenye Jiji letu la Dodoma na wanaanza ujenzi muda sio mrefu na pia kuna fedha zingine kama Milioni 46, 46 kwa zaidi ya Shule Nane katika Jimbo letu hili," Amesema Mavunde.

Ametoa rai kwa Madiwani wa Jiji la Dodoma kutumia Saruji hizo kama ilivyokusudiwa kwa kuwaandaa wananchi na yeye akiahidi kushirikiana nao kwa pamoja pindi ujenzi utakapoanza.

MSIGWA: TUTILIE MKAZO MASLAHI YA WAANDISHI WA HABARI

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Nd. Gerson Msigwa

 

Na Ahmed Sagaff - DODOMA

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Nd. Gerson Msigwa  ameomba ushirikiano kutoka kwa uongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)  katika kutetea maslahi ya waandishi wa habari kwenye vyombo wanavyofanyia kazi ili kuinua hadhi zao.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii leo jijini Dodoma mara baada ya kukutana na uongozi huo, Msigwa amesema anafahamu changamoto zinazowakabili waandishi wa habari nchini tangu alipokuwa akifanya kazi hiyo mkoani, hivyo anafahamu kwamba hali ya wanahabari haifurahishi na kwamba anataka kuona wanahabari wananufaika na kazi wanazozifanya.

“Kwa hiyo tumekubaliana kwamba tufanye kazi kubwa ya kuhakikisha tunanyanyuana, tunawekana sawa na tunashirikiana, hatuna muda kwa ajili ya kuvutana, tuna muda kwa ajili ya kushirikiana na kuijenga nchi yetu”,  ameeleza Msigwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TEF, Nd. Deodatus Balile amewataka wanahabari kujiendeleza kielimu ili kukidhi vigezo vya kisheria vilivyowekwa miaka mitano iliyopita ambavyo vinainua hadhi ya taaluma ya habari kwa kumtaka mwandishi wa habari kuwa na elimu ya fani hiyo kuanzia stashahada na kuendelea.

“Waandishi ambao watakuwa wamesahau kidogo kwamba Novemba tutakuwa tunafikia muda wa kuanza kutumika ile kanuni ambayo inataka kila mwandishi wa habari kuwa na elimu ya kuanzia stashahada ya uandishi wa habari kwenda juu, kwa hiyo kanuni hiyo inaanza kutekelezwa mwaka huu hivyo ambao hawajaenda kusoma, waende”, amesema Balile.

Kwa mujibu wa kanuni 17 (2) ya Huduma za Habari 2017, anayetaka kusajiliwa kama mwandishi wa habari anapaswa kuwa na stashahada au shahada ya uandishi wa habari kutoka kwenye chuo kinachotambuliwa na Serikali.

Aidha, Serikali ilitoa muda wa miaka mitano ili wanahabari ambao hawana sifa zilizoainishwa kwenye kanuni hiyo, wajiendeleze kitaaluma ili kuendana na matakwa ya kisheria.

 

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA BUNGENI LEO JIJINI DODOMA


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama (kushoto), Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi (wa pili kushoto) na  Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, Bungeni jijini Dodoma, Aprili 21, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro, Bungeni jijini Dodoma, Aprili 21, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi, Bungeni jijini Dodoma, Aprili 21, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

MKUTANO WA KAWAIDA WA 20 WA BARAZA LA MAWAZIRI LA KISEKTA LA AFYA UNAENDELEA KUFANYIKA JIJINI ARUSHA, TANZANIA.

 

Mkutano wa Kawaida wa 20 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya umeendelea kufanyika kwa siku ya tatu leo, katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha, Tanzania. 

 

Mkutano huu ambao utafanyika kwa siku tano kuanzia tarehe 19 hadi 23 Aprili 2021,una lenga kufanya mapitio ya hatua ya maendeleo iliyofikiwa katika utekelezaji wa maamuzi na maagizo yaliyotolewa na Mkutano uliopita wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na la Kisekta. Vilevile mkutano huu ataangazia masuala mengine muhimu katika Sekta ya Afya ndani ya Jumuiya. 

 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huu katika ngazi ya wataalamu Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayesimamia Sekta za Uzalishaji na Jamii, Mhe. Christophe Bazivamo amewashukuru wataalamu wa Sekta ya Afya kwa juhudi zao za kutatua changamoto mbalimbali na kutoa mapendekezo na ushauri wa kitaalamu kwa ngazi za maamuzi ambayo yamepelekea utekelezaji wa mipango ya ubunifu katika sekta ya Afya na kuunganisha vipaumbele vya uwekezaji kwenye sekta hiyo katika Jumuiya.

 

Katika ngazi ya Wataalamu mkutano huu unafuatilia na kutathimini maendeleo ya utekelezaji wa masuala mbalimbali katika sekta ya afya kama ilivyoelekezwa na Mkutano uliopita wa Baraza la Mawaziri na la Kisekta, ikiwemo; maendeleo ya utekelezaji wa mikakati ya pamoja ya kukabiliana na Ugonjwa wa Homa kali ya Mapafu unaosababishwa na Virusi vya Korona (UVIKO-19), usalama wa dawa na chakula, masuala ya afya ya uzazi, Watoto na Lishe na hali ya utekelezaji wa miongozo na taratibu za  taaluma na huduma za afya katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano katika ngazi ya wataalamu Dkt. Leonard Subi Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto ameeleza kuwa; Tanzania imeendelea kuongeza mikakati ya kuzuia na kudhibiti janga la UVIKO-19 tangu lilipozuka katikati ya Machi 2020.

 Ameongeza kusema kuwa UVIKO-19 ni ugonjwa mpya wa aina yake kwani tumeshuhudia tishio la ukuaji wa uchumi wa ulimwengu na umegharimu maisha ya watu wengi sehemu mbalimbali duniani, hivyo mshikamano ni muhimu ili kuukabili.

 

 “Tanzania tunadhamini juhudi zinazofanywa na Wanasayansi mbalimbali ulimwenguni katika kupata suluhisho la kudhibiti ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na mshikamano ulioonyeshwa na WHO, GAVI na Taasisi zingine zinazounga mkono jitihada hizo.

 

Tanzania haikatai chanjo ya UVIKO-19, isopokuwa tunafanya tathmini thabiti kabla ya kukubali matumizi ya chanjo nchini. Mathalani, Tanzania nyakati zote imekuwa na rekodi za juu kwenye matumizi ya chanjo kwa watoto wachanga walio chini ya miaka 5 hivyo tutaendelea kutoa ushirikiano mzuri kwa wadau wa ndani na  Wakimataifa katika mapambano dhidi ya janga la COVID-19. ” Ameeleza Dkt.Subi

 

Mkutano huu unaofanyika kwa njia mbili ya ana kwa ana na video, umehudhuriwa na nchi zote Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Aprili 22, 2021 watakutana Makatibu Wakuu na Aprili 23, 2021 watakutana Mawaziri wanaosimamia masuala ya Afya kutoka nchi Wanachama.

 

RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AKUTANA NA VIONGOZI WA JUMUIYA YA WAFANYABIASHARA WA CHINA NCHINI TANZANIA IKULU JIJINI DODOMA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa China hapa nchini, (Chinese Business Chamber of Tanzania) Janson Huang wakwanza kulia kutoka kwa Mhe. Rais, ambaye aliambatana na Viongozi wenzake wenzake Ikulu Jijini Dodoma leo tarehe 21 Aprili, 2021.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 21 Aprili, 2021 amekutana na viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa China nchini Tanzania (Chinese Business Chamber of Tanzania) na kuzungumzumza nao kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu biashara na uwekezaji hapa nchini.

Viongozi hao wakiongozwa na Bw. Janson Huang wamempa pole Mhe. Rais Samia kufuatia msiba mkubwa wa Kitaifa wa kuondokewa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na wamempongeza kwa kupokea kijiti cha Urais katika Serikali ya Awamu ya Sita.

Wamemhakikishia kuwa Wafanyabiashara wa China wapo tayari kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Sita katika kukuza uchumi na kuinua ustawi wa wananchi kupitia uwekezaji mkubwa wanaokusudia kuufanya kupitia kampuni zaidi ya 800 za China zilizotayari kuwekeza Tanzania.

Viongozi hao wametaja maeneo ambayo kampuni zao zipo tayari kuwekeza kuwa ni viwanda vya kutengeneza simu, dawa za binadamu, magari, kuanzisha maeneo maalum ya viwanda (Industrial Parks) na kuwawezesha watanzania kupata ujuzi kupitia mpango wa elimu utakaotoa fursa kwa Watanzania kusoma vyuo vya Tanzania na China katika masuala mbalimbali yakiwemo uhandisi na utalii kwa ufadhili wa Serikali ya China na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa China. 

Akizungumza na viongozi hao, Mhe. Rais Samia amewashukuru kwa salamu zao za pole na pongezi na amewahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itashirikiana nao katika uwekezaji na itaboresha zaidi mazingira ya biashara na uwekezaji ili matokeo ya uwekezaji huo yanufaishe pande zote mbili.

Rais Samia amewahakikishia kuwa Serikali itafanyia kazi changamoto mbalimbali zinazokwamisha uwekezaji ikiwemo upatikanaji mgumu wa vibali vya kazi, kodi, ucheleweshaji wa malipo, urasimu, kushughulikia changamoto zinazojitokeza kwa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini na zinazoingizwa kutoka nje ya nchi na kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa korona (Covid-19).

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa China hapa nchini, (Chinese Business Chamber of Tanzania) Janson Huang akizungumza na Wanahabari mara baada ya mazungumzo yao Ikulu Jijini Dodoma leo tarehe 21 Aprili, 2021.  PICHA NA IKULU



DKT. NDUGULILE AITAKA TCRA KUELIMISHA UMMA NA KUBORESHA MIFUMO YA MALALAMIKO




Na Faraja Mpina, WMTH, Dodoma

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA-CCC) kuboresha vitengo vyao vya mawasiliano ili kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya huduma za mawasiliano kwa kuzingatia haki na wajibu pamoja na matumizi sahihi ya simu janja na mtandao.


Dkt. Ndugulile amezungumza hayo mbele ya waandishi wa habari baada ya kikao chake cha kazi cha Wizara na taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo cha kujadili na kufanya mapitio ya taarifa za mapato na matumizi za taasisi hizo kwa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2020/2021 Kilichofanyika katika Ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.


Aidha Dkt. Ndugulile ameziagiza taasisi hizo kuboresha mifumo ya wananchi kutolea malalamiko yanayohusu huduma za mawasiliano na kushughulikia malalamiko hayo kwa wakati na taarifa ya malalamiko hayo itakuwa ni ajenda ya kudumu katika vikao vya kila robo mwaka baina ya Wizara hiyo na taasisi zake.


Ameongeza kuwa elimu kwa umma ikitolewa kwa kiwango kinachojitosheleza kitapunguza baadhi ya malalamiko ya wananchi kwa mfano malalamiko ya vifurushi vya data kuisha haraka ambapo kwa namna moja ama nyingine inasababishwa na settings za simu janja kuruhusu programu zake kujiboresha zenyewe (automatic Updating).


“Kuna mambo ambayo ni muhimu wananchi kuyafahamu kwa mfano matumizi makubwa ya data yanayosababishwa na settings za simu janja ambazo zinaruhusu baadhi ya programu kujiboresha zenyewe nazo zinachangia vifurushi vya data kuisha haraka”, alizungumza Dkt. Ndugulile


Aliongeza kuwa Serikali inatengeneza mazingira wezeshi ya kuhakikisha mawasiliano yanafika kwa wananchi wote lakini kumekuwa na changamoto ya baadhi ya watu kutokuwa na matumizi sahihi ya huduma hii, hivyo wananchi wanahitaji kuelemishwa ili kuhakikisha wanajua wajibu wao na haki zao na kuwa na matumizi sahihi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).


Akizungumzia kikao cha Wizara na taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo cha mapato na matumizi Dkt. Ndugulile amesema kuwa lengo ni kusimamia nidhamu na matumizi ya fedha za taasisi hizo badala ya kusubiri mpaka mwisho wa mwaka CAG aje kuhoji.


“Sisi kama Wizara tunajipanga kuhakikisha fedha zinazopatikana zinaelekezwa katika kute

keleza majukumu ya msingi ya Wizara na taasisi zake ikiwa ni pamoja na kwenda kutekeleza miradi ya maendeleo.


Dkt. Ndugulile amezielekeza taasisi zilizo chini ya Wizara yake kutolea ufafanuzi maeneo ambayo yaliguswa katika taarifa ya CAG na kama kuna hoja zozote ziliyojitokeza zijibiwe kikamilifu na kuwasilishwa ndani ya wiki ijayo na taasisi ambazo hazikuwasilisha hesabu zao kwa CAG watoe maelezo kwa nini hawakuziwasilisha kwa mujibu wa taratibu za Serikali


Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Kundo Mathew amezitaka taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano kwa kutambua kuwa Wizara inayowasimamia ipo makini kuhakikisha taasisi hizo zinatimiza wajibu wake wa kuhudumia wananchi na yeye kama msaidizi wa Waziri mwenye dhamana atashirikiana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Naibu wake kuhakikisha kuwa Wizara na taasisi zake zinafanya kazi zenye ubora na kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuandaa taarifa zinazojitosheleza bila kusubiri maelekezo.


Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula, Naibu wake Dkt Jim Yonazi, Wakuu wa taasisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Tume ya Taifa ya Tehama (ICTC), Shirika la Posta Tanzania (TPC), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA-CCC), Menejimenti ya Wizara pamoja na baadhi ya watendaji wa taasisi zake.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza katika kikao chake na Wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo cha kujadili taarifa za mapato na matumizi na utekelezaji wa majukumu kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2020/2021 katika ukumbi wa Hazina, Dodoma.

Tuesday, April 20, 2021

WAZIRI MKUU MAJALIWA: SERIKALI IPO IMARA NA MIRADI YOTE YA KIMKAKATI INAENDELEA KUJENGWA

 

 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akifafanuliwa jambo na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo nchini (TBA,) Mbunifu Majengo. Daud Kondoro, wakati alipokagua nyumba za Magomeni Quarters Aprili 20, 2021, jijini Dar es salaam. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiangalia moja ya chumba, wakati alipokagua mradi wa nyumba za makazi ya waliyokuwa wakazi wa eneo hilo, Magomeni Quarters Aprili 20, 2021, jijini Dar es salaam. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ipo imara na miradi yote ya kimkakati inaendelea kujengwa, hivyo Watanzania waendelee kuwa na imani nayo.

Amesema Serikali inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ipo makini na inaendelea kuwatumikia Watanzania. ”Tuendelee kuchapa kazi”.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Aprili 20, 2021) baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni Kota, Dar es Salaam.

”Siri ya kuwepo mafanikio na maendeleo nchini ni utulivu na amani. Tulianza vizuri tangu Serikali ya Awamu ya kwanza, tutaendelea kuimarisha amani na utulivu.”

Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwaasa Watanzania watumie muda mwingi kufanya shughuli za maendeleo kuliko mambo mengine yasiyo na tija.

Akizungumzia kuhusu mradi huo, Mheshimiwa Majaliwa amesema amefurahi kukuta majengo yamekamilika na kwamba ameridhika na maendeleo ya ujenzi wake.

Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wahakikishe wanakamilisha kazi iliyosalia haraka ili mwaka huu wananchi waanze kuishi hapo.

Naye, Mtendaji Mkuu wa TBA, Bw. Daud Kondoro amesema mradi huo una jumla ya block tano na ambazo zinauwezo wa kuchukua familia 656.

Amesema mbali na ujenzi wa nyumba hizo za makazi pia katika eneo hilo wanajenga maduka makubwa pamoja na vizimba kwa ajili ya wajasiriamali kufanya biashara.

Mradi ulianza kutekelezwa mwaka 2016 na unatarajiwa kukamilika Mei 2021. Hadi sasa umefikia asilimia 94 ya utekelezaji wake na gharama yake ni shilingi bilioni 50.

Baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba za makazi za Magomeni Kota, Waziri Mkuu alikagua kituo cha Reli ya Kisasa cha Tanzanite jijini Dar es Salaam

WAZIRI NDUMBARO: HATUWEZI KUWAUA NYANI WANATULETEA DOLA


Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro amekataa  ombi la Wakazi wa Rombo  la kutaka  kuwaua nyani na tumbili   wanaodaiwa  kuvamia makazi yao na kuharibu mazao kwani wanaleta fedha (dola)

Baadala yake Waziri Ndumbaro amemuagiza Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Dkt. Maurus Msuha kwa kushirikiana na  Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) kuwahamisha nyani hao kwa kuwapeleka katika Hifadhi zilizo mbali na makazi ya Watu.

Waziri Ndumbaro ametoa agizo hilo jana wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro baada ya kupata malalamiko hayo kutoka kwa Wananchi,

Amefafanua kuwa Wizara haiwezi kuwaua nyani hao kwa kuwa nyani na tumbili  ni moja ya vivutio vya Utalii vinavyotuletea pesa nyingi nchini kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Aidha, Dkt. Ndumbaro ameiagiza Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) kuanza kufanya utafiti wa kuwapeleka nyani hao katika mazingira ambayo yatakuwa sawa na ya Rombo ili wasiweze  kupata shida yoyote kutokana na kubadailisha mazingira.

Nyani hao wanadaiwa kuvamia makazi na kuanza kung'anganiana chakula pamoja na kudaiwa kuwachukua Watoto wadogo wa Binadamu na kuanza kukimbia nao porini ambako wakati mwingine huwajeruhi.

Awali Mbunge wa Rombo ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Adolf Mkenda alisema licha ya nyani hao kuwasumbua Wapiga kura wake lakini Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro imekuwa ikifanya jitihada ya kuwaondoa nyani hao.

Hata hivyo, Prof, Mkenda ameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Taasisi zake jinsi inavyowasaidia Wananchi wa Rombo katika maendeleo kwa kuwajengea shule pamoja na Zahanati.

Kwa upande wake Diwani wa  Katangara Mrere,  Mallel Venance amesema nyani hao wamekuwa tatizo sio katika kata yake tu bali ni Wilaya nzima

''Wanakuja katika makazi yetu wakiwa katika makundi kati ya 40 na 100 na katika baadhi ya vijiji wamekuwa wakiharibu mazao hali inayopelekea sisi kama wazazi kushindwa kuchangia chakula katika shule ambako watoto wetu wanasoma, Tukuomba Mhe. waziri tusaidie tunakuwa masikini kwa ajili ya nyani hawa.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro ( wa kwanza kushoto) akiwa na  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja wakizungumza na baadhi ya Watumishi wa Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro mara baada ya kufanya mkutano wa hadhara na Wananchi wa kata ya Mashati iiliyopo katika wilaya ya  Rombo mkoani Kilimanjaro ambapo Waziri Dkt. Ndumbaro  ameagiza nyani hao wanaovamia makazi ya watu wahamishiwe katika Hifadhi zilizo mbali na makazi ya Watu. Watatu kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Allan Kijazi
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro akizungumza na baadhi ya Watumishi wa Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro mara baada ya kufanya mkutano wa hadhara na Wananchi wa kata ya Mashati iliyopo katika wilaya ya  Rombo mkoani Kilimanjaro ambapo Waziri Dkt. Ndumbaro  ameagiza nyani hao wanaovamia makazi ya watu wahamishiwe katika Hifadhi zilizo mbali na makazi ya Watu. Watatu kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Allan Kijazi

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro akihutubia mkutano wa   hadhara uliofanyika katika Kata ya Mashati iliyopo katika wilaya ya  Rombo mkoani Kilimanjaro ambapo amewahakikishia Wananchi hao wanaolalamikia Nyani na Tumbili kuvamia makazi yao kuwa watahamishiwa katika Hifadhi zilizo mbali na makazi ya Watu

SERIKALI IPO TAYARI KUKIDHI MAHITAJI YA WAWEKEZAJI - WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewahakikishia wawekezaji wote nchini kuwa Serikali itakidhi mahitaji yao ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuweka sera bora na mazingira wezeshi kwa kuhakikisha uwepo wa huduma muhimu za maji, umeme, ardhi na barabara na kuwataka kuwaalika marafiki katika nchi zao na nje ya mipaka kuja na kuwekeza nchini kwa kuwa sera na mazingira ya uwekezaji ni rafiki zaidi.

Akizungumza leo mara baada ya kutembelea na kukagua kiwanda cha kuunganisha magari cha GFA Assemblers kilichopo Kibaha mkoani Pwani Majaliwa amesema Serikali inatambua mchango wa wawekezaji nchini na itawaunga mkono kwa kuhakikisha changamoto zilizopo ndani ya uwezo wa Serikali zinapatiwa ufumbuzi.

"Mkoa wa Pwani una viwanda vya kutosha na bado maeneo yapo mengi, Mkuu wa Mkoa yupo na wawekezaji wenye uhitaji wa maeneo Serikali ipo kwa ajili yenu na tunawaunga mkono wakati wote." Amesema Majaliwa.

Waziri Majaliwa ameupongeza Mkoa wa Pwani kwa kuwa kinara na kutumia fursa ya kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wenye viwanda.

Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi. Evarist Ndikilo amesema, Mkoa wa Pwani una viwanda 1438 huku viwanda vikubwa vikiwa 82 kikiwemo kiwanda cha GFA Assemblers.

"Mwaka 2015 tulikuwa na viwanda 300, hadi sasa tumefikia idadi ya viwanda 1438 kwa ongezeko la viwanda 3100 ambavyo vimetengeneza ajira za moja kwa moja 50,0000 na ajira za muda 10,0000." Amesema Ndikilo.

Aidha amesema kuwepo kwa viwanda hivyo katika mkoa huo umepaisha mapato ya Mkoa huo hadi kufikia bilioni 147 na bado uwekezaji wa viwanda mkoani humo unashika kasi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kiwanda hicho Aljawad Karimal ameiomba Serikali kutoa vipaumbele zaidi kwa sekta binafsi hasa katika masoko na sera za uwekezaji ili kuendelea kujenga taifa la viwanda.

Aljawad amesema wanajivunia uwekezaji walioufanya nchini hasa kwa kuwa kiwanda cha kwanza cha kuunganisha magari ya aina zote na kuiomba Serikali kuwapa masoko kupitia Halmashauri na taasisi zake ikiwemo jeshi na hospitali kwa kuwapa kazi za kuunganisha magari ya kutolea huduma.
Waziri mkuu Kasimu Majaliwa akisikiliza maelekezo kutoka kwa, Elizabert Mwaya wakati alipofanya ziara ya kutembelea Kiwanda cha kutengeneza Magari GFA-Vehicle Assembling kilichopo Kibaha mkoani Pwani jana.kulia ni Mkurugenzi wa kiwanda hicho Ally Jawad Karmali.Picha na Said Khamis
Waziri mkuu Kassimu Majaliwa akizungumza na Mkurugenzi wa kiwanda cha kutengeneza magari cha GFA-Vehicle Assembling,Aljawad Karimal kilichopo Kibaha wakati wa ziara ya kukagua kiwanda hicho. Kulia ni Mkuu wa mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo.Picha na Said Khamis
Waziri mkuu Kasimu Majaliwa akisikiliza maelekezo kutoka kwa Baraka Samson ,wakati alipofanya ziara ya kutembelea Kiwanda cha kutengeneza Magari GFA-Vehicle Assembling kilichopo Kibaha mkoani Pwani jana. Wa pili kulia ni Mkurugenzi wa kiwanda hicho Ally Jawad Karmali.

MAKAMU WA RAIS DKT. MPANGO AKUTANA NA KATIBU MKUU KIONGOZI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, akisalimiana kwa Ishara maalum na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Hessein Katanga walipokutana na kufanya mazungumzo Ofisini kwa Makamu wa Rais Ikulu Chamwino Jijini Dodoma leo April 20,2021.