Matokeo chanyA+ online




Tuesday, April 28, 2020

DKT. KALEMANI HARIDHISHWI NA KASI NDOGO YA MATUMIZI YA UMEME TABORA

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani( kulia) akizungumza na Mkazi wa Kijiji cha Busomeke( katikati) wilayani Igunga mkoani Tabora baada ya waziri huyo kuwasha umeme katika nyumba mwanakijiji huyo.
 Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amewataka wakazi wa Mkoa wa Tabora kuongeza kasi ya kutumia umeme unaopatikana mkoani humo kwakuwa matumizi yao yapo chini zaidi kulinganisha na umeme unaozalishwa mkoani humo.

Dkt. Kalemani alisema hayo wakati akikagua shughuli za usambazaji wa umeme vijijini katika Kijiji cha Mizanza na kuwasha umeme katika Kijiji cha Busomeke wilayani Igunga mkoani Tabora, Aprili 27, 2020.

Dkt. Kalemani alisema kuwa mitambo ya kufua umeme iliyopo mkoani humo inauwezo wakuzalisha Megawati 42 za umeme ili itumike mkoa mzima lakini mpaka sasa matumizi ni Megawati 14 tu.
Moja ya nyumba iliyowashiwa umeme katika Kijiji cha Busomeke wilayani Igunga mkoani Tabora baada ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani kufanya ziara ya kukagua shughuli za usambazaji umeme Vijijini wilayani humo Aprili 27, 2020.
 “Kwa nini ninyi wakazi wa Tabora hamtaki kutumia umeme haliyakuwa tayari miundombinu imewafikia na bei ya kuunganisha ni 27,000 tu! mitambo ya hapa Tabora inauwezo wa kufua umeme wa Megawati 42, ninyi matumizi yenu hayafiki hata nusu ya umeme huo,hii si sawa mtaharibu mitambo yetu kwakuwa mingine italazimika kuzimwa na ikizimwa kwa muda mrefu itaharibika na nchi itapata hasara” alisema Dkt. Kalemani.

Aliwataka Viongozi wa Serikali za Vijiji, Mitaa pamoja na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuongeza kasi ya kuhamasisha wananchi wa mkoa huo kuunganisha umeme katika nyumba zao.

Vilevile aliwataka wananchi hao kuongeza shughuli za uzalishaji mali kama vile viwanda vidogo vinavyotumia umeme ili kuongeza idadi ya matumizi ya umeme ambao mwingi hupotea kwa kukosa watumiaji hali yakuwa bado wakazi wengi hawana huduma hiyo.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na Viongozi wa Kijiji cha Busomeke katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, alipofanya ziara ya kukagua shughuli za usambazaji umeme vjijini, Aprili 27, 2020.

Viongozi wa Kijiji cha Mizanza wilayani Igunga Mkoani Tabora wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani, hayupo pichani baada ya kufanya ziara kijijini hapo ya kukagua shughuli za usambazaji umeme vjijini, Aprili 27, 2020. Katika ziara yake hiyo, aliwasha umeme katika Kijiji cha Busomeke na kuwataka wananchi wa eneo hilo kuendelea kulipia shilingi 27,000 ili waunganishiwe umeme.

Akiwa katika Kijiji cha Mizanza, Dkt. Kalemani aliiagiza TANESCO, kuharakisha upelekaji wa nguzo kijijini hapo, ili kuwapa fursa wakazi wa kijiji hicho kuunganishiwa umeme, hivyo amewataka wakazi hao kulipia gharama za uunganishwaji na kutandaza nyaya katika nyumba zao.

Aliendelea kusisitiza kuwa miradi ya usambazi umeme vijiji hauna fidia, hivyo wananchi watoe ushirikiano kwa wakandarasi na TANESCO pindi wanapopitisha miundombinu katika maeneo yao kwa lengo la kurahisisha utekelezaji wa kazi hiyo.


Mbunge wa Manonga, Saif Gulamali (katikati) akizungumza na Viongozi wa Kijiji cha Mizanza katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, alipofanya ziara ya kukagua shughuli za usambazaji umeme vjijini, Aprili 27, 2020. Kulia ni Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.Na Zuena Msuya Tabora,


Hata hivyo aliwataka kutumia wakandarasi walioainishwa na TANESCO na wanaotambulika katika serikali za mitaa na vijiji vyao ili kuepuka vishoka na watu wasiowaaminifu.

Sambasamba na hilo, aliwaeleza kuwa wasikubali kulipia miundombinu ya umeme kama nguzo, nyaya, mashineumba (Transfoma) wala mita za LUKU.

Monday, April 27, 2020

KATIBU MKUU DKT. CHAULA AKABIDHIWA OFISI RASMI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Sekta ya Mawasiliano, Dkt. Zainab Chaula (wa pili kushoto aliyesimama mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na Menejimenti na wawakilishi wa taasisi za Sekta hiyo alipowasili kwa mara ya kwanza Wizarani hapo Mji wa Serikali, Dodoma. Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu anayestaafu, Dkt. Maria Sasabo 
 
Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Sekta ya Mawasiliano, Dkt. Zainab Chaula, amewasili rasmi  Wizarani katika ofisi zilizopo Mji wa Serikali, Mtumba, Dodoma kwa mara ya kwanza tangu alipoteuliwa, baada ya kuhamishwa kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Dkt. Chaula amesema kuwa amefurahi na kumshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa kumhamishia Wizara hiyo  kwa kuwa anafahamu umuhimu na mchango wa Sekta hiyo katika maeneo mengine kwa kuzingatia kuwa amekuwa akitumia TEHAMA katika kutekeleza majukumu yake alipokuwa TAMISEMI na Wizara ya Afya
Katibu Mkuu mstaafu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, (Sekta ya Mawasiliano) Dkt. Maria Sasabo (wa kwanza kushoto) akimkabidhi Katibu Mkuu mpya, Dkt. Zainab Chaula nyaraka mbali mbali kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Sekta hiyo alipowasili ofisini kwenye Mji wa Serikali, Dodoma.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (wa kwanza kushoto) akiwa na Katibu Mkuu wa Sekta ya Mawasiliano wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula alipowasili Wizarani hapo, Mji wa Serikali, Dodoma, kujitambulisha baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Sekta hiyo
“TEHAMA itatutoa kwenye chagamoto, lazima tuwekeze na tuitumie kama fursa, suala sio wingi wa watu, kuwa na watumishi wengi, kwa kuwa mnaweza kuwa wengi ikawa vurugu, ila mnaweza kuwa wachache na mkafanya kazi vizuri, binafsi nimetumia TEHAMA kwenye sekta ya afya na TAMISEMI, nimekuja huku nimefurahi, nitaendelea kujifunza zaidi, nanyi ndio wataalamu, mjiamini, msiwe na hofu, watanzania tuna akili, uwezo tunao,” amesisitiza Dkt. Chaula

Katibu Mstaafu wa Sekta hiyo, Dkt. Maria Sasabo, akizungumza wakati anamkaribisha na kumkabidhi ofisi Dkt. Chaula, Dkt. Sasabo alisema kuwa Sekta ya Mawasiliano ni mtambuka, inategemewa na Serikali, sekta binafsi na wananchi katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu mbali mbali ya kila siku ambapo tayari kuna Sera, sheria, miongozo na kanuni zinazosimamia uendeshaji wa Sekta ikiwa ni pamoja na miundombinu ya mawasiliano ambayo inawezesha utendaji kazi wa mifumo ya kielektroniki nchini
 
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Sekta ya Mawasiliano, Dkt. Jim Yonazi, akimpongeza Katibu Mkuu wa Sekta hiyo anayestaafu, Dkt. Maria Sasabo (aliyeketi katikati) na kumkaribisha Katibu Mkuu mpya ofisini, Dkt. Zainab Chaula (wa kwanza kulia) Mji wa Serikali, Dodoma
 Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye akizungumza na Katibu Mkuu mpya wa Sekta ya Mawasiliano, Dkt. Zainab Chaula alipofika ofisini kwake, Mji wa Serikali, Dodoma kujitambulisha baada ya kuhamishiwa Wizarani hapo
Naye Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe alimweleza Dkt. Chaula kuwa Sekta hii imetekeleza vema majukumu yake katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2019/2020 na sasa wanajiandaa kuwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo kwenye Bunge la bajeti linaloendelea mjini Dodoma

Kamwelwe amemwagiza Dkt. Chaula kuhakikisha kuwa Sera ya Taifa ya Posta inahuishwa ili iweze kwenda na wakati kwa kuwa sekta ya posta imebadilika na Shirika la Posta limebadiilisha namna ya kufanya kazi na kuhudumia wananchi kwa kuwa linatumia TEHAMA kutoa huduma na kusafirisha vifurushi na vipeto kwa wateja
 
 Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Sekta ya Mawasiliano, Dkt. Zainab Chaula, akijadiliana jambo na Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Elius Mwakalinga, alipowasili Wizarani hapo kuwa Katibu Mkuu wa Mawasiliano
 
Akisalimiana na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashata Nditiye mara alipowasili ofisini kwake kujitambulisha, Nditiye alimwarifu Dkt. Chaula kuwa Sekta ya Mawasiliano ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa taifa letu kwa kuwa sasa ni moja ya Sekta tano bora kwa kuongoza kuchangia pato la taifa na hata Bungeni maswali mengi yanayoulizwa ni pamoja na upatikanaji wa huduma za mawasiliano

Naye Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa amemweleza Dkt. Chaula kuwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano viongozi wanafanya kazi kama timu moja bila kujali anasimamia Sekta ipi na mara nyingine amekuwa akishiriki kazi za Sekta ya Mawasiliano ikiwa ni pamoja na kujibu maswali Bungeni
 Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa akizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Sekta ya Mawasiliano, Dkt. Zainab Chaula alipowasili rasmi baada ya kuhamishiwa Wizarani hapo, Mji wa Serikali, Dodoma
 
Na Prisca Ulomi, WUUM, Dodoma

Akizungumza na Menejimenti na wawakilishi wa taasisi za Sekta hiyo Wizarani hapo, Dkt. Chaula amesema kuwa anategemea kupata ushirikiano kutoka kwa viongozi na wafanyakazi kwa kuwa kwenye kazi tunatengeneza upendo, marafiki na kuwa ndugu na sio maadui, tunafungua njia. Hivyo, amewataka kufanya kazi vizuri kama uko nyumbani kwako kwa ajili ya wengine

Pia, amewakumbusha kuendelea kuzingatia miongozo na maelekezo ya Wizara ya Afya ya kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni ili kujilinda na maambukizi ya virusi vya Corona ambavyo ni janga la dunia ambapo kwa Tanzania Serikali imejitahidi na kujidhatiti kuhakikisha kuwa maambukizi yanaendelea kupungua na wagonjwa wanapona na amewataka wasiwe na hofu kwa kuwa Corona ni mafua tu.

SERIKALI YAPOKEA BIL 14.9, ZITATUMIKA KUNUNUA VIFAA KINGA KWA WATUMISHI WA AFYA NA VIFAA TIBA

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akiopokea hundi kutoka Airtel


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akipoea hundi kutoka Kampuni ya Rotary





Na WAMJW-Dar es Salaam
Serikali  imepokea msaada wa shilingi bilioni 14.9 kutoka Global Fund, Airtel Tanzania, Rotary Club Tanzania ambazo sehemu kubwa zitatumika kununua vifaa kinga kwa watumishi wa afya na vifaa tiba kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wenye maambukizi ya COVID-19.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameyasema hayo leo wakati akipokea msaada wa fedha na lita 1,250 za vitakasa mikono ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na maambukizi ya virusi vya Corona.

Waziri Ummy amefafanua kwamba Global Fund imetoa shilingi bilioni 14, Airtel Tanzania shilingi milioni 700 na Rotary Club Tanzania shilingi milioni 250.

“Tumepokea shilingi bilioni 14 kutoka Global Fund, shilingi bilioni 9.6 tumezitoa kwa ajili ya kununua vifaa kinga kwa ajili ya watumishi wa Afya, lakini pia fedha zilizotolewa na Airtel na Rotary Club Tanzania tutazielekeza huko. Kipaumbele chetu ni kuwalinda watumishi wa afya,” amesema Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.

“Natumia fursa hii kuwashukuru watumishi wa afya ambao wamekuwa wakijitoa usiku na mchana katika kutoa huduma kwa watu waliopata maambukizi ya virusi vya Corona (Covid-19) pamoja na wale wahisiwa.

"Kipaumbele cha Serikali ni kuwalinda watumishi wa Afya kwa kununua vifaa kinga kwani fedha tulizozipata hapa tutazielekeza kwenye ununuzi wa vifaa kinga.  Niendelee kuwaisistiza Watumishi wa Afya wazingatie miongozo ya magonjwa ya kuambukiza,” Amesema Waziri Ummy .

Amesema watumishi wa afya ambao wamepatiwa mafunzo katika vituo vya kutoa huduma kwa wenyr maambukizi ya  ugonjwa huo,  hakuna aliyepata maambukizi kwa kuwa wanazingatia miongozo ya Serikali ya kutoa matibabu kwa wagonjwa wa Covid-19 pamoja na miongozo ya magonjwa ya kuambukiza.

Waziri amesema ushiriki wa kila mdau katika mapambano dhidi ya maambikizi ya virusi vya Corona ni muhimu na kwamba msaada uliotolewa na kampuni hizo ni mkubwa katika mapambano ya maambukizi ya ugonjwa wa Corona.

“Napenda kurudia tena kwa niaba Mhe. Rais Dkt. John Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, nawashukuru Airtel Tanzania, Serengenti Breweries na Rotary Club kwa hiki mlichotupatia. Asanteni sana,” amesema Waziri Ummy.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Airtel Tanzania, Bw. Gabriel Malata amesema Airtel Tanzania imetoa shilingi milioni 700 ikiwa ni sehemu ya  kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na janga la Corona.

“Sisi bodi ya wakurugenzi wa Airtel na kwa niaba ya Airtel Tanzania, tunatambua juhudi za Serikali katika kupambana na ugonjwa wa Corona, lakini pia tumejitathimini na kutambua kuwa sisi kama Airtel hatuwezi kuendelea bila kuwepo watu wanaotumia huduma zetu. Watu hawa ndio mtaji wa Kampuni,” amesema Bw. Gabriel.

Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kampuni ya Bia ya Serengenti, Bw. John Wanyancha amesema kuwa kampuni hiyo imetoa lita 1,250 ya vitakasa mikono nyenye thamani ya shilingi milioni 15  kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na maambukiza ya virusi.

Mwenyekiti wa Rotary Club, Bi. Agnes Batenga amesema Rotary imetoa shilingi milioni 250 kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa homa ya mapafu (COVID-19).

“Shilingi milioni 183 zitatumika kutoa msaada wa vifaa vya kujikinga (PPE), vifaa vya maji safi ambavyo vitasambazwa katika vituo maalumu vya kuhudumia wagonjwa wa Corona jijini Dar es Salaam, Hospitali ya Amana, Zanzibar, Hospitali ya Mawenzi na Hospitali ya Mount Meru,” amesema Bi. Agnes.

Amesema shilingi milioni 67 zitatumika katika kutekeleza miradi ya kudhibiti ugonjwa wa Corona nchini kupitia Club za Rotary.

WAZIRI BITEKO AZINDUA VIWANDA VIWILI VYA MFANO VYA UCHENJUAJI DHAHABU NCHINI

Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Geita mara baada ya hafla ya uzinduzi na makabidhiano ya kiwanda cha kuchenjua dhahabu cha Katente na Lwamgasa Mkoani Geita. Kiwanda hicho kimekabidhiwa kwa Shirika la Madini la Taifa (Stamico) ili kukisimamia na kukiendesha.
 
Waziri wa Madini, Doto Biteko amelitaka Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kusimamia ipasavyo Viwanda vya Mfano vya Uchenjuaji wa madini ya dhahabu vya Katente-Bukombe na Lwamgasa-Geita alivyovizindua leo APRIL 26 na kuvikabidhi rasmi kwa shirika la Stamico..

Ujenzi wa viwanda hivyo visivyotumia kemikali hatari ya zebaki ulifanywa na kampuni ya Tan Discovery MineralConsaltancy Limited inayosimamiwa na Rogers Sezigwa iliyoanza ujenzi wa mradi mwezi Disemba, 2016 ikianziaLwamgasanakufuatianaKatentenaItungi- Chunya.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa viwanda hivyo vya Mfano,Waziri Biteko amesema, itakuwa aibu kubwa kwa Stamico endapo Viwanda hivyo vitafia mikononi mwao kwani Serikali imetumia gharama kubwa katika ujenzi wa viwanda hivyo.
 
Mtaalamu wa kuendesha mitambo ya uchenjuaji wa dhahabu kwa kutumia teknolojia ya Kisasa Gabriel Masanyiwa akitoa maelezo ya hatua zinazopitiwa mpaka kupata dhahabu.
“Afe Kipa, afe beki ni lazima viwanda hivi vifanye kazi” Biteko alisisitiza.

Aidha,Waziri Biteko amewahakikishia wananchi na wachimbaji wadogo wa madini nchini kuwa, serikali ya Rais John Magufuli inawajali na itawahudumia kwa gharama nafuu hivyo wasisite kupeleka mawe kiwandani hapo ili waweze kuchenjuliwa dhahabu kwa kutumia teknolojia mpya na ya kisasa na hivyo kuepuka kutumia zebaki na kuachana na utumiaji wa matimba kwenye mashapo.

Amesema matumizi ya matimba wakati wa uchimbaji yanasababisha uharibifu wa mazingira wakati zebaki huathiri afya za wachimbaji hivyo waitikie na kuvitumia viwanda hivyo kwa faida zao.
 
Waziri wa Madini, Doto Biteko akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili kilipojegwa kiwanda cha kuchenjua dhahabu bila kutumia kemikali ya zebaki cha Katente wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho uliofanyika tarehe 26 Aprili, 2020
“Tumetengeneza viwanda hivi kuwavutia ninyi fanyebiashara” Biteko alisisitiza.


Pamoja na hayo, Waziri Biteko alimtaka Mwenyekiti wa Bodi ya Stamico kuhakikisha wanasimamia ipasavyo miradi hii pasipo kucheka na watu wasiotimiza wajibu wao kwenye viwanda hivyo.

Sambamba na hayo amewataka Bodi pamoja na Stamico kuhakikisha wananchi wanaozunguka viwanda hivyo wananufaika na uwepo wa viwanda katika maeneo yao kwa kupata ajira ndogo ndogo kwa kufanya hivyo kutainua uchumi wao.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila akiongea jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa viwanda vya kuchenjua dhahabu vya Katente na Lwamgasa uliofanyika Katente mkoani Geita tarehe 26 Aprili 2020.
 
Akizungumzia faida zitokanazo na uwepo wa viwanda hivyo vya mfano, Waziri Biteko alisema ni pamoja na utoaji wa mafunzo na maarifa kuhusu sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali kwa wachimbaji wadogo, kutolewa elimu ya mfumo wa kuthamini mashapo ya madini yaliyopo ilikufanya uchimbaji wenye tija, kuchenjua dhahabu pamoja na kukodishwa vifaa vinavyotumika katika shughuli za uchimbaji kwa gharama nafuu pamoja na kutolewa elimu juu ya uongezaji thamani madini na upatikanaji wa masoko.
Akizungumzia mchakato wa ujenzi wa viwanda hivi vya mfano, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Augustine Ollal amesema, ujenzi huo nimatokeo ya Utekelezaji wa Sera ya Madini ya mwaka 2009 iliyosisitiza zaidi juu ya uendelezaji wa sekta ya madini hususani wachimbaji wadogo.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idrisa Kikula akizungumza jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha kuchenjua dhahabu cha Katente wilayani Bukombe mkoani Geita tarehe 26 Aprili, 2020.
 
Amesema katika kutimiza azma hiyo, Serikali ilianzisha mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) uliokuwa na awamu mbili, ya kwanza ni kuanzia 2009 hadi 2014 na awamu ya pili mwaka 2015 hadi 2018 ambapo awamuya pili ya mradi ndipo viwanda vitatu vya mfano vya uchenjuaji wa dhahabu vya Katente- Bukombe, Lwamgasa- Geita na Itumbi –Chunya vilipoanza kujengwa baada ya kufanyika kwa utafiti wa kijiolojia chini ya ushirikiano baina ya uongozi wa mradi, Stamico, Taasisi ya Utafiti na Jiolojia Tanzania (GST) na wachimbaji wadogo.
Akizungumzia gharama ya ujenzi wa viwanda hivyo Ollal alisema mradi wa Katente umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.7 na Lwamgasa umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.3 wakati mradi wa Itumba Uligharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.7 na hivyo kufanya miradi yote kutekelezwa kwa kiasi cha shilingi bilioni 4.7.
Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Stamico Lucas Seleli akizungumza jambo mara baada ya uzinduzi na makabidhiano ya Viwanda viwili vya uchenjuaji wa Madini ya dhahabu kisichotumia kemikali ya zebaki vilivyoko Katente na Lwamgasa mkoani Geita.
 
Ollal ameongeza kuwa, uwepo wa tekinolojia hii kwa wachimbaji wadogo itakuwa na manufaa kama vile; kupunguza kwa kiasi kikubwa ajali migodini kwa kutumia sementi katika kuimarisha kuta, kurahisisha utoaji wa mbale mgodini(Haulage system) kupunguza athari za kimazingira kwa kutokata miti hovyo na kurahisisha ufungaji wa migodi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara y aMadini, Prof. Simon Msanjila amelitaka Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kuisaidia jamii inayozunguka viwanda hivyo vya mfano kuondokana na changamoto ya maji kwa kuchimba kisima kiwandani hapo na kuiruhusu jamii kunufaika na huduma hiyo.
Aidha, Prof. Msanjila amewataka Stamico kutoa nafasi za ajira kwa wananchi kutokana na ukweli kwamba wao ndio walinzi wa viwanda hivyo. “Nitashangaa sana kuona wafanyakazi wakawaida wanatoka km 200 kutoka hapa wakati kijiji kimezungukwa na vijana mahiri na wachapa kazi” alisistiza Prof. Msanjila.
Viongozi wa Serikali kuanzia kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel akifuatiwa na Waziri wa Madini, Doto Biteko, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila na mwisho ni Mshauri mwelekezi aliyesimamia ujenzi wa viwanda vya kuchenjua dhahabu Rogers Sezigwa wakiendelea na ukaguzi wa kiwanda hicho kabla ya kukikabidhi rasmi kwa Shirika la Madini la Taifa (Stamico).
 
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel ametoa wito kwa watendaji na wasimamizi wa vituo hivyo kuwa wazalendo katika usimamizi wa Viwanda hivyo vya uchenjuaji wa dhahabu.
Sanjari na hilo, ameelezea mikakati ya mkoa wake kuelekea maonesho ya Tekinolojia ya uchimbaji wa madini kwa mwaka huu kuwa ni pamoja na mkoa wake kuandaa uwanja maalum kwa ajili ya maonesho hayo ambapo tayari ujenzi wa jengo la ofisi mbalimbali ikiwepo ya wataalamu wa Sekta ya madini umefanyika.
Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa wataalamu na timu nzima ya Ujenzi wa viwanda hivi kushiriki kikamilifu katika maonesho hayo ili kuachilia utaalamu wao kwa watanzania wengine wenye nia ya kujiendeleza kupitia sekta ya Madini.

WAZIRI BASHUNGWA ATANGAZA UKOMO WA BEI ZA BARAKOA, AELEKEZA VIWANDA VYA NGUO NCHINI KUTENGENEZA BARAKOA

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Innocent Bashungwa amesema atachukua hatua kwa Taasisi zisizo za kiserikali (NGOs) zinazouza barakoa kwa gharama kubwa.

Bashungwa alitoa taadhari hiyo mkoani Arusha alipotembelea Viwanda vya kuzalisha nguo vya Sunflug na A to Z kuangalia hali ya uzalishaji wa barakoa katika Viwanda hivyo.

Bashungwa alitoa onyo kwa NGOs zilizoomba kibali cha kuzalisha barakoa kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania lakini badala yake wanauza barakoa kwa shillingi 2,500 hadi 3,000  
Waziri wa Viwanda na Bishara Mhe Innocent Bashungwa akitolea ufafanuzi wa bei ya barakoa ambapo ameagiza bei isizizi 1500 badala ya bei ya sasa ilikuwa sokoni ya 2500 ambayo watanzania wengi inawapa changamoto ya kumudu. (Picha Zote Na Eliud Rwechungura, Wizara ya Viwanda na Biashara)

Waziri wa Viwanda na Bishara Mhe Innocent Bashungwa{kulia} akipokea maelezo kutoka kwa Bw. Emmanuel Mgoma{kushoto} muakilishi wa kiwanda cha Sunflug ambacho kwa sasa kinazalisaha barakoa 25,000 kwa siku. {katikati} Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo

Waziri wa Viwanda na Bishara Mhe Innocent Bashungwa akiongea na menejimenti ya kiwanda cha A to Z ambacho kwa sasa kinazalisha barakoa 15,000 kwa siku.
“wamekuwa wakitoa masharti kupitia mitandao ya kijamii kuwa hawauzi barakoa chini ya bei hiyo”.

Sitawataja kwa leo lakini nikiona tu wanauza kwa bei kubwa sitasita kuwachukulia hatua, maana mnakuja kuomba vibali kumbe mnafanya mtaji.

Aliongeza kusisitiza barakoa zote ziuzwe kwa bei isiyozidi 1500 badala ya bei ya sasa ilikuwa sokoni ya 2500 ambayo watanzania wengi inawapa changamoto ya kumudu.

Kwa upande mwingine Mhe. Bashungwa alivipongeza Viwanda nguo vya A-Z na Sunflug kwa kuzalisha barakoa ambazo zinawasaidia watanzania walio wengi, na amewahaidi serikali kuwapati ushirikiano.

Aidha alivitaka Viwanda hivyo kuendelea kuzalisha kwa wingi ili wananchi walio wengi wa vijijini waweze kupata vifaa hivyo vya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa korona.
Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo aliwataka wananchi wote wa mkoa huo kuchukua taadhali zinazotolewa na Wizara ya afya wanapotembelea maeneo yenye mkusanyiko.

Pia, alisisitiza kuwa ni vema sasa wafanyabiashara hao wakatengeneza barakoa kwa bei nafuu ili kuwezesha wananchi kununua.

Wakitoa taarifa kwa Mhe. Waziri, Bw. Emmanuel Mgoma muakilishi wa kiwanda cha Sunflug alisema kiwanda kina uwezo wa kuzalisha barakoa 25,000 kwa siku.

Muakilishi wa A-Z Bw. Slyvester Kazi  alisema kiwanda kina uwezo wa kuzalisha barakoa 15,000 kwa siku.

SERIKALI: UHAI WA BINADAMU UNA THAMANI KUBWA KULIKO UHAI WA WANYAMAPORI

Naibu Waziri Constantine Kanyasu
Serikali imetolea ufafanuzi wa kauli iliyotolewa na  baadhi ya Wananchi  wanaodai kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa ikithamini uhai wa wanyamapori kuliko uhai wa Binadamu.

 Akizungumza na viongozi wa vijiji vitano vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti katika wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Naibu Waziri Constantine Kanyasu amesema  uhai wa binadamu una thamani kubwa na kamwe hauwezi kufananishwa na uhai  wa wanyamapori 

Amesema licha ya  kuwa  Binadamu anaaminika kuwa akili kuliko Wanyamapori hata hivyo Wizara hiyo imekuwa ikifanya kila liwezekalo ili kuondoa migogoro kati ya Wanyamapori na binadamu.

" Tunaamini kila binadamu angetamani kuona yupo salama na ndio madhumuni na matamanio ya serikali" Amesisitiza Naibu Waziri Kanyasu.

 Amesisitiza  kuwa  binadamu ana uwezo wa kukwepa mienendo ya wanyamapori na  kuwa katika mazingira salama kuliko mnyama mwenyewe na ameongeza kuwa  wanyamapori hao wapo kwa ajili ya Binadamu na sio vinginevyo.

Akitaja baadhi ya mikakati iliyochukuliwa na Serikali  ili kunusuru uhai wa binadamu ni pamoja na kuhamisha jumla ya Simba 36 kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kupelekwa katika Hifadhi nyingine lengo likiwa ni kupunguza madhara kwa binadamu wanaoishi karibu na Hifadhi hiyo.

Amesema jitihada hizo zilizochukuliwa na Serikali kufuatia Simba kula  ng'ombe wapatao  360 kwa kipindi cha mwezi Januari na Februari mwaka huu  huku  baadhi ya Wananchi kuuawa na wengine kujeruhiwa na wanyamapori wakali na waharibifu ni mkakati wa kuona maisha ya binadamu yanakuwa salama.

Licha ya jitihada hizo zilizofanywa na Serikali, Mhe.Kanyasu amewataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kujiepusha kulima mazao  pamoja kujenga nyumba karibu na vigingi ili kuepuka athari za wanyamapori hao    kwa vile wanyamapori  wanakapokuja hawajui kuwa wamevuka mpaka.

 Amesema maamuzi hayo ni moja ya jitihada za Serikali kuhakikisha  uhai wa binadamu unalindwa kwa gharama yoyote ile.

Amesema licha ya kuwa moja ya jukumu la msingi la Wizara hiyo ni kulinda na kuendeleza Wanyamapori kwa ajili ya kizazi cha sasa na cha badae lakini hata hivyo thamani ya  Uhai wa binadamu ipo pale pale .

Sunday, April 26, 2020

KATIBU MKUU KUSAYA: VIJANA JIFUNZENI KILIMO BIASHARA

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akikagua kitalu nyumba kilichopandwa nyanya na vijana walliopo katika Kituo Atamizi cha Vijana kujifunza Kilimobiashara chini ya Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine mjini Morogoro.
Kijana Hefsida Olloo (Kushoto)akitoa maelezo ya nanma alivyofanikiwa kuzalisha nyanya katika kitalu kwenye kambi Atamizi ya SUA .Hefsida ni mhitimu wa Shahada ya Sayansi katika Hisabati toka Chuo Kikuu cha Dodoma mwaka 2018 aliyeamua kufanya kilimo biashara.Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya alipotembelea chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine hivi karibuni.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa ameshika hoho za rangi zinazozalishwa na vijana katika kituoo atamizi cha mafunzo kwa vitendo chini ya SUA.Kulia kwake ni Msimamizi wa kituo hicho Zebedayo Sanga na kushoto kwake ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine Prof.Raphael Chibunda.


Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akikagua kitalu kinachozalisha hoho za rangi katika kituo atamizi cha vijana kujifunza kilimobiashara chini ya Chuo Kikuu cha Sokoine mjini Morogoro hivi karibuni.Jumla ya vjana wahitimu wa kozi mbalimbali wapatao 40 wanapata mafunzo kwa mwaka mmoja kwenye kituo hicho .
Sehemu ya vijana wanaopata mafunzo kwa vitendo katika kituo atamizi Chuo Kikuu cha Sokoine kujifunza kilimobiashara wakimsikiliza Katibu Mkuu wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (hayupo pichani) wakati alipowatembelea hivi karibuni mjini Morogoro.
(Picha na habari Wizara ya Kilimo)


Vijana wahitimu wa vyuo mbalimbali nchini wameshauriwa kujitokeza na kupata mafunzo kwa vitendo kuhusu kilimo biashara kwa ajili ya kujipatia ujuzi na ajira toka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine.

Wito huo umetolewa jana na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya wakati akiongea na vijana wanaondelea na mafunzo kwa vitendo kuhusu kilimo biashara katika Kituo Atamizi cha Vijana cha Kilimobiashara (SUA-AIC Youth Agribusiness Incubators) mjini Morogoro

“Vijana tunatambua uwepo wenu hapa kituoni,jitahidini kujifunza mbinu bora za kilimo mkilenga kujiajili na mwisho wa mafunzo yenu mrudi vijijini na mijini kuwa walimu kwa vijana wenzenu” alisema Kusaya

Katibu Mkuu Kusaya aliwapongeza vijana hao kwa kuamua kujiunga na kambi atamizi kwani wanatekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya Rais Dkt.John Pombe Magufuli ya kuwataka vijana kujiajili kupitia kilimo.

“Lengo la serikali ya Awamu ya Tano ni kukifanya kilimo kuwa ni ajira na kazi inayochangia kukuza uchumi wa nchi,ndio maana nimekuja kuwatembelea na kuwatia moyo “ alisisitiza Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo

Akitoa taarifa ya kituo hicho,Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine Prof. Raphael Chibunda alisema kituo atamizi kinafundisha vijana wahitimu wa vyuo mbalimbali wanaopenda kufanya kilimo biashara .

Alisema kwa sasa kuna vijana wapatao 40 wanaoendelea na mafunzo kwa vitendo kwa mwaka mmoja wakizalisha mazao ya mboga mboga kama hoho za rangi,matango na nyanya kwa usimamizi wa wataalam wa chuo.

Akielezea manufaa ya kituo hicho Hefsiba Olloo kutoka Kilimanjaro alisema ameweza kuzalisha nyanya kwenye kitalu nyumba na kuvuna kilo 1,318 za nyanya zilizompatia shilingi milioni 4 ndani ya kipindi cha miezi minne .

Mafanikio aliyopata mwaka huu Januari alivuna kilo (338) Februari (400),Machi (400) na Aprili amevuna (180) ambazo ameuza kwa bei ya shilingi 2500 hadi 3000 kwa kilo moja .

“ Kwa muda mfupi tangu nimejiunga na kambi atamizi hapa SUA mwezi Septemba 2019 tayari nimeona manufaa yake kwa kuwa na uhakika wa kipato kupitia kilimo cha nyanya .Nilipanda nyanya mwezi Octoba mwaka 2019 na sasa naendelea kuvuna” alisema Hefsida

Hefsida alihitimu shahada ya Sayansi katika Hisabati (Bachelor of Science in Mathematics) Chuo Kikuu cha Dodoma mwaka 2018 na hakuweza kupata ajira hivyo akaamua kuanzisha kilimo cha mboga

Kwa upande wake msimamizi wa kituo atamizi Zebedayo Sanga ambaye ni mhitimu wa digrii ya Horticulture mwaka 2018 toka SUA aliwahamasisha vijana wengi zaidi waliopo mitaani kuja kujifunza kilimobiashara na kuwa na uhakika wa kipato na ajira .

GGM KUANZA KUTUMIA UMEME WA GRIDI YA TAIFA MWEZI JUNI MWAKA HUU

Muonekano wa sehemu ya mitambo ya katika kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Mponvu kinachotarajiwa kukamilika mwishoni mwa Mwezi Mei, 2020.  

Waziri wa Nishati, Dkt. Medrad Kalemani, ( katikati) akitoa maelekezo kwa wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Mponvu mkoani Geita baada ya kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa kituo hicho alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akikagua mashine zilizofungwa ndani ya jengo la kuendeshea mitambo (Control room) katika Kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Mponvu mkoani Geita baada ya kufanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho.                                                                            Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema kuanzia Mwezi Juni mwaka huu, Mgodi wa kuchimba dhahabu wa Geita (GGM) utaanza kutumia umeme wa Gridi ya Taifa kuendesha shughuli zake baada ya Kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Mponvu mkoani Geita kukamilika mwishoni mwa Mwezi Mei, 2020.

Aidha alisema ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa kituo hicho ambacho awali kilipangwa kukamilika mwezi Juni lakini kutokana na kasi ya ujenzi wake kitakamilika mwishoni mwa Mwezi Mei na kuanza kusambaza umeme kwa wateja ikiwemo GGM.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani( kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel (kulia) wakipita katika tope wakikagua eneo la ujenzi wa kituo cha kuchenjua dhahabu cha Geita, huku kukiwa na mvua kubwa.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto)akizungumza na baadhi ya Viongozi kijiji cha Buyagu,( hawapo picha )ili wakawaeleze wananchi wao kulipia gharama za umeme ili waunganishiwe huduma hiyo, baada ya kuwasha umeme katika kijiji hicho. Uwepo wa virusi vya Corona nchini kumezuia mikusanyiko ya watu kwa lengo la kujikinga na kuchukuwa tahadhari.katikati ni Mbunge wa Busanda, Lolensia Bukwimba.

Dkt. Kalemani alisema hayo, alipofanya ziara ya kikazi Aprili 25, 2020, mkoani Geita ya kukagua ujenzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Mponvu, Kituo cha kuchenjua dhahabu cha Geita na kuwasha umeme katika Kijiji cha Buyagu na Zahanati ya Musasa.

“kituo hiki cha Mponvu kitakuwa mkombozi mkubwa wa nishati ya umeme ya kutosha na kwa gharama nafuu kwa wakzi wa Mkoa wa Geita na mikoa jirani,pia Mgodi wa GGM utajiendesha kwa faida zaidi na kuliongezea mapato taifa kwa sababu wataacha kutumia majenereta kuzalisha umeme ambao ni wa gharama kubwa sana ukilinganisha na umeme unaozalishwa hapa nchini” alisema Dkt. Kalemani.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani( katikati) na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel (kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Josephat Maganga( kushoto) wakiwa katika eneo linalojengwa jengo la utawala la eneo la uwekezaji mkoani Geita.

Dkt. Kalemani alifafanua kuwa, mgodi wa GGM utatumia umeme wa gridi ya taifa kutoka kituo cha Mponvu ambacho kitapokea umeme wa njia ya kusafirisha umeme wa Kilovolti 220 kutoka kituo cha Bulyanhulu mkoani Shinyanga hadi mkoani Geita yenye urefu wa kilomita 55.

Vilevile alieleza kuwa tayari njia ya kusafirisha umeme wa Kilovolti 33 utakaotumiwa na mgodi huo yenye urefu wa Kilomita 6.5 kutoka katika kituo hicho hadi ndani ya mgodi huo imekamilika na kinachosubiriwa sasa ni kuunganisha umeme punde kituo hicho kitakapokamilika.

Dkt. Kalemani pia aliwasha umeme katika Kijiji cha Buyagu,ambacho ni moja ya vijiji vinavyopitiwa na njia ya kusafirisha umeme wa Kilovolti 220 kutoka Bulyanhulu hadi Geita ikiwa ni ishara ya kukamilika kwa njia hiyo kwa asilimia 80.
Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani( kushoto) akipata maelezo ya ufungaji wa Mashineumba( Transfoma) katika kituo cha kuchenjua dhahabu cha Geita kutoka kwa Kaimu Meneja wa Shirika la Umeme nchini( TANESCO) mkoani Geita, Charles Msangi(katikati).

Na Zuena Msuya, Geita

Katika kukagua maendeleo ya usambazaji umeme vijijini, aliwasha umeme katika zahanati ya Musasa na kuwataka wananchi wa eneo hilo kuendelea kulipia ili waunganishiwe umeme.

Hata hivyo aliliagiza Shirika la Umeme Nchini, ( TANESCO) kuharakisha ufungaji wa Mashineumba( Transfoma) katika kituo cha kuchenjua dhahabu mkoani Geita ambacho kiko katika hatua za mwisho kukamilika.

Dkt. Kalemani alirejea kusema kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa wachimbaji wote nchini wanaendesha shughuli za uchimbaji kwa kutumia nishati ya umeme unaozalishwa nchini kwa gharama nafuu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel alisema kuwa kituo hicho kikikamilika kitakuwa uwezo wa kuchenjua dhahabu inayotakiwa katika ubora wa kimataifa na kitawasaidia wachimbaji wadogo kunufaika zaidi na shughuli zao za uchimbaji tofauti na ilivyo sasa.

Gabriel aliwaomba wawekezaji kwenda kuwekeza zaidi katika mkoa huo wa Geita kwa kuwa kuna umeme mwingi wa kutosha na gharama nafuu kuendesha shughuli mbalimbali vikiwemo viwanda.

Vilevile aliishukuru Wizara ya Nishati kwa kuhakikisha kuwa mkoa huo unakuwa na umeme wa kutosha ili kuvutia wawekezaji wengi, kuwaunganishia umeme wa bei nafuu wananchi wa mkoa huo pamoja na kujengwa kwa kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Mponvu ambacho kitawezesha migodi yote katika mkoa huo kutumia umeme, na kuugawa katika mikoa jirani.