Matokeo chanyA+ online




Saturday, March 13, 2021

CHUO CHA ARDHI MOROGORO CHAFANYA MAGEUZI MAKUBWA KATIKA KASI YA UPIMAJI ARDHI

 

Katika kipindi kuanzia mwezi Desemba 2020 hadi mwezi Februari 2021 Chuo cha Ardhi Morogoro kimefanya upimaji wa viwanja elfu arobaini mia nane kumi na tatu (40,813), kati ya hivyo viwanja 19,102 vipo Jijini Arusha katika Mitaa ya Mlimani (9,420), Msasani (1,349), Muriet (5,820), Mtaa wa Mashariki (1,041) pamoja na Mtaa wa FFU (1,552). Viwanja vingine ni Manispaa ya Iringa viwanja 2,385 Halmashauri ya Rombo viwanja 1,523 Halmashauri ya Wilaya Same viwanja 176, Halmashauri ya Wilaya ya Moshi viwanja  1,076.


Kwa upande wa Dar es salaam, Chuo cha Ardhi Morogoro kimepima Halmashauri ya Jiji (Ilala) viwanja 5,981. Manispaa ya Temeke viwanja 1,112. Manispaa ya Kigamboni viwanja 2,675. Pamoja na Manispaa ya Kinondoni viwanja 1,000. Mkoa wa Mtwara, Chuo cha Ardhi Morogoro ndani ya muda huo kimepima viwanja 1,084 katika Halmashauri ya Nanyumbu, huku viwanja 4,699 vikiwa katika eneo la Manispaa ya Morogoro.

Ni mara ya kwanza katika shughuli za urasimishaji makazi, kampuni binafsi au taasisi kufanya upimaji mkubwa kiasi hicho kwa kutegemea michango ya wananchi. Mkuu wa Chuo hicho Bw Huruma Lugalla amesema kwamba huo ni mwanzo tu kwani mpango mkakati mpya wa Chuo wa miaka mitano kuanzia 2021 – 2024 umejaa maboresho makubwa na kasi ya ajabu kuhakikisha Taasisi hii pekee ya serikali inayozalisha wataalamu wa upimaji na ramani katika ngazi ya cheti na Diploma na kwamba Watanzania wategemee mambo makubwa katika sekta ya Ardhi. Bw Lugalla ameongeza kwamba yote haya yamewezekana chini ya uongozi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi



Aidha, Makamu Mkuu wa Chuo hicho Bw Charles Saguda, ambae pia ni msimamizi mkuu wa Miradi ameongeza kwamba chuo kimeandaa mpango kabambe wenye kuleta matokeo chanya katika miradi yote inayosimamiwa na chuo, amesema wameanza na Mkoa wa Arusha na Sasa ni zamu ya Dar es salaam na baadae nguvu kazi kuhamia Mkoa wa Morogoro. Bw Saguda alisema kwamba lengo kubwa ni kuongeza wigo wa walipa kodi ya ardhi, ambapo kwa mchanganuo huo tayari kanzidata ya walipa kodi ya ardhi imeongezeka na serikali inaongeza mapato. 

Chuo cha Ardhi Morogoro kimepitia mabadiliko makubwa ya kiutawala baada ya miradi kudhoofu kwa kipindi cha nyuma, kwa sasa mabadiliko na hatua mbalimbali zilizochukuliwa kwa baadhi ya watumishi zinaonekana kuleta tija na ufanisi zaidi katika utendaji.







Tuesday, March 9, 2021

MBUNGE CHALINZE ATEMBELEA WANANCHI WALIOPATA MAAFA YA KUBOMOKA KWA NYUMBA ZAO KITONGOJI CHA PINGO

                        Na. Andrew Chale, Chalinze

Mbunge wa  Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete amewatembelea  kuwafariji Wananchi wa Kitongoji cha Pingo  eneo la Mbiki katika Kata ya Pera  walioezuliwa na kuangushwa nyumba zao kutokana na mvua iliyoambatana na upepo mkali, iliyotokea Machi Mosi mwaka huu.

Katika ziara hiyo 6 Machi, Ridhiwani Kikwete aliambatana na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze,  Geoffrey Kamugisha na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Ramadhani Possi pamoja na viongozi mbalimbali wakiwemo wa Chama cha Mapinduzi (CCM)  na wa Kata na  Kijiji ambapo walitembea kujionea athari za mvua hiyo.

Wakiwa katika eneo hilo la Pingo Mbiki, waliweza kushuhudia nyumba na miti ya mikorosho na ile ya mazao ikiwa imeangushwa pamoja na nyumba zingine kuezuliwa mapaa.

Baada ya kushuhudia tukio hilo,  Mbunge Ridhiwani Kikwete alisema kuwa wamefika maeneo hayo  kuwafariji na kuona namna ya kuwasaidia kwa kushirikiana na Serikali.

"Baada ya viongozi wa Kijiji kutujulisha tukio hili, tukaona tuje maeneo haya kuja tuyaone.

Sisi kwa upande wetu kama Halmashauri tumeona yapo mambo ambayo tutaenda kushahuriana na Mkurugenzi na Mwenyekiti ilikuona ndani ya Halmashauri tunayabebaje." Alisema Mbunge na kuoongeza:

"Lakini pia yapo mambo ambayo tunasema yapo juu ya Halmashauri yale ambayo ya kupeleka ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, lakini pia ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha Maafa ilikuona pia nao kwa Serikali kwa ukubwa wake wanatusaidiaje hii hali". Alisema Mbunge, Ridhiwani Kikwete.

Hata hivyo Mbunge alibainisha kuwa, ameona hali halisi na hivyo watakavyorejea Ofisini wataona namna ya kupanga ilikuwasaidia Wahanga hao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Geoffrey Kamugisha alibainisha kuwa, wamefika hapo ikiwemo kuwapa pole kwa tukio hilo.

"Tunaenda kukaa pamoja na Mbunge na Mwenyekiti kuona namna ya kutatua hali hii ya athari". alisema Mwenyekiti Kamugisha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Ramadhani Possi alisema licha ya kuona hali halisi, yupo tayari kupokea maelekezo ya viongozi hao ikiwemo kufanyia kazi yale yote aliyoyaona katika tukio hilo na kuona jinsi watakavyochukua hatua za haraka.

Kwa upande wao baadhi ya wahanga wa tukio hilo walipongeza kwa kitendo cha Mbunge Ridhiwani Kikwete kufika eneo hilo ba kuwafariji huku wakimuombea baraka katika uongozi wake.

Bi. Mariam Salehe  ambaye ni mmoha wa Wahanga wa tukio hilo la kubomolewa nyumba yake, alimshukuru Mbunge kwa kuwatembelea ambapo wanaamini watapata msaada wa haraka.

Kwa upande wake, Muhidin Rashid alimshukuru Mbunge kwa kufika eneo hilo huku akimuombea dua kuendelea kuwatumikia wananchi usiku na mchana.

"Ujio wa Mbunge na viongozi wengine kutufariji sisi ni heshima kubwa hivyo tunawaombea wazidi kututumikia wananchi wao hasa sisi tuliopo huku vijijini.

Tunamuombea kwa Mungu Mbunge wetu katika uongozi wake". Alimalizia Muhidin Salehe.


Mnamo Machi Mosi mwaka huu mvua hiyo kubwa yenye upepo mkali iliweza kusababisha athari kwa nyumba zaidi ya 39  kuangushwa na zingine kuezuliwa paa zake huku nyumba za ibada mbili nazo zikikumbwa na athari hizo.

ULEGA: USIKIVU WA TBC UNAENDELEA KUIMARIKA

 

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo  Abdallah Ulega amesema kwamba Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) linaendelea kuimarisha usikivu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa studio za Televisheni ya TBC, Mikocheni Dar es Salaam.

 Ulega ameyasema hayo leo Bungeni Jijini Dodoma wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya jamii ilipopokea taarifa kuhusu mradi wa ujenzi wa studio hiyo pamoja na ujenzi wa Redio ya Jamii Makao Makuu Jijini Dodoma.

“Taarifa inayowasilishwa kwenu leo itawezesha kupatikana uelewa wa hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi hii na mtakapoitembelea mtapata fursa ya kuona hali halisi ya utekelezaji” alisema Mhe.Ulega.

Akiwasilisha taarifa hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania  Dkt. Ayoub Ryoba ameeleza kuwa  katika bajeti ya miradi ya maendeleo ya takriban Shilingi milioni 900 iliyoidhinishwa, pamoja na shilingi bilioni 1 kutoka Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) zilitekeleza uboreshaji wa mfumo wa umeme na ufungaji wa “AVR na UPS,” ununuzi na ufungaji wa mitambo na vifaa vya redio pamoja na ukarabati wa jengo la studio.

“Baada ya uboreshaji kupitia fedha hizo manufaa mbalimbali yamepatikana ikiwemo kuaandaa na kurusha vipindi vya redio na televisheni kutokea Dodoma, matangazo ya televisheni ya kipindi cha ARIDHIO na Jambo Tanzania yamekuwa yakirushwa kutokea Dodoma” Alisema Dkt.Ryoba.

Dkt. Ryoba aliongeza kuwa, manufaa mengine yaliyotokana na mradi huo ni kurushwa mbashara vipindi vinavyohitaji ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kitaifa kutoka kwa viongozi wa Serikali muda wote inapohitajika kufanya hivyo pamoja na redio jamii kuhusika kurusha habari za kikanda hivyo kuleta uelewa kwa wananchi kuhusiana na kazi wanazofanya.

 

Monday, March 8, 2021

TSC YAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

Wafanyakazi wanawake wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Makao Makuu Dodoma, wakiwa katika picha ya pamoja, muda mfupi kabla ya kushiriki katika maandamano wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Machi 8, 2021.



Wafanyakazi wanawake wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Makao Makuu Dodoma, wakishiriki katika maandamano wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Machi 8, 2021.



Na Veronica Simba - TSC

 

Wafanyakazi wanawake wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Makao Makuu Dodoma, wameadhimisha siku ya wanawake duniani kwa ufanisi.

Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika leo, Machi 8, 2021 jijini Dodoma, Wafanyakazi hao wameshiriki katika maandamano yaliyoshirikisha Taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi, yaliyoanzia Uwanja wa Jamhuri hadi katika Uwanja wa ‘Nyerere Square.’

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wanawake wa TSC, Mwenyekiti wao, Catherine Kamili ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwathamini wanawake na kuwapatia nafasi za uongozi katika nyanja mbalimbali nchini.

Aidha, amewataka wanawake wote nchini, hususani watumishi wa TSC, kuendelea kuchapa kazi kwa weledi na kujituma katika kuhakikisha, wanakuwa sehemu ya waleta maendeleo ya jamii na Taifa.

Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kitaifa, mwaka huu ni “Wanawake katika Uongozi, Chachu kufikia Dunia yenye Usawa.”

Friday, March 5, 2021

WAZIRI MKUU: NIMERIDHISHWA NA KAZI YA KUPAMBANA NA NZIGE

 

 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia nzige walioteketezwa kwenye kijiji cha Engaruka, wilayani Monduli, mkoani Arusha, Machi 4, 2021.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiangalia ndege inayotumika katika zoezi la kuteketeza nzige kwenye kijiji cha Engaruka wilayani Monduli mkoani Arusha, Machi 4, 2021.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiongea wananchi katika kijiji cha Engaruka wilayani Monduli mkoani Arusha mara baada ya kukagua shughuli ya udhibiti wa nzige katika kata ya Engaruka, wilayani Monduli mkoani Arusha, Machi 4, 2021.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akifafanuliwa jambo na Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda, wakati alipokagua shughuli ya udhibiti wa nzige katika kata ya Engaruka, wilayani Monduli mkoani Arusha, Machi 4, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).



Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na kazi kubwa ya kupambana na makundi ya nzige yaliyovamia nchini iliyofanywa na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana mashirika mawili ya kupambana na nzige barani Afrika.

 

Kazi hiyo inafanywa na Shirika la Kudhibiti Nzige wa Jangwani la Afrika Mashariki (Desert Locust Control Organisation for Eastern Africa-DLCO EA) na Shirika la Kudhibiti Nzige Wekundu la Kusini na Kati mwa Afrika (International Red Locust Control Organisation for Central and Southern Africa-IRLCO CSA).

 

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Machi 4, 2021) wakati akizungumza na wananchi katika kijiji cha Engaruka, wilayani Monduli mkoani Arusha mara baada ya kukagua shughuli ya udhibiti wa nzige katika kata ya Engaruka.

 

Amesema ameridhishwa na kazi nzuri ya kupambana na nzige iliyofanyika tangu makundi hayo yalipongia nchini, ambapo amesisitiza licha ya kazi nzuri iliyofanyika ni muhimu kwa Wizara ya Kilimo ikaweka mikakati ya kukabiliana na makundi hayo pindi yatakapoingia tena.

 

“Lazima tuwateketeze, nzige ni hatari na hawapaswi kupewa nafasi hata ya dakika moja kuingia kwenye mashamba yetu. Nzige hawa wana uwezo wa kusafiri umbali wa kilomita 200 kwa siku na kuteketeza zaidi ya hekta mbili kwa siku, hivyo ni lazima tuwateketeze.”

 

“Muhimu zaidi ni kujipanga vizuri kukabiliana nao, ni lazima tuendeleze kazi nzuri tuliyoianza. Hawa wadudu ni hatari na wanazaliana mno. Ukimuona, kawaida anakuwa na rangi nyekundu lakini ukimuona ana rangi ya njano huyo amebeba mayai tuwatekeze ili wasizaliane.”

 

Waziri Mkuu amesema watalaamu wa Tanzania na wataalamu kutoka Zambia, Zimbabwe, Uganda na Kenya wanashirikiana kupambana na nzige kwa kutumia vifaa mbalimbali kama ndege, helikopta na mitambo ya kupulizia kwa mikono.

 

Amewapongeza wananchi kwa ushirikiano wanaoutoa kwa wataalamu kwa kutoa taarifa pale wanapoona makundi ya nzige na kwenda kuwaonesha wataalamu na amewasihi waendelee kupambana na makundi hayo. “Watanzania na Wana-Engaruka tuendelee kutoa taarifa na kujitokeza kwa wingi kushirikiana na wataalamu wetu kuteketeza makundi hayo.”

 

Pia, Waziri Mkuu amewatahadharisha wananchi waishio karibu na maeneo yaliyopulizwa dawa wasiokote kitu chochote na kula kwa sababu ya uwepo wa sumu, na wasiende kulisha mifugo yao kwenye maeneo hayo hadi baada ya siku saba.

 

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa kundi lililoenda Simanjiro limeshateketezwa, Siha nako wameshateketezwa na sasa hakuna nzige, wilaya ya Mwanga ambako walikuwa wapite kuelekea Simanjiro nako kwa sasa hakuna nzige.

 

“Tuliamua kupiga kambi hapa Engaruka ambako kulikuwa na makundi matatu makubwa jana na leo asubuhi ndege ya Shirika la Kupambana na Nzige wa Jangwani ambalo sisi ni wanachama, lilishambulia makundi hayo na helikopta ya kupambana na nzige wekundu nayo ilipulizia dawa pamoja na vijana waliokuwa wakipuliza.”

 

Prof. Mkenda amesema wataendelea kufuatilia maeneo ambayo nzige wametua na kuangalia kama wametaga mayai ili wayateketeze. 

 

Nzige walianza kuingia nchini Januari 8, 2021 na makundi makubwa yalionekana katika wilaya za Simanjiro kwenye vijiji vya Olchorinyori, Landanai, kitongoji cha Dodoma, Sokoni B na Naberera. Wilaya ya Longido nzige walivamia kijiji cha Tingatinga, Nondoto, Orbomba na Komakowa. Wilaya ya Siha walivamia kijiji cha Namwai na wilaya ya Monduli walivamia vijiji vya Engaruka, Mfereji na Ererendeni.

 

MAKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR ASEMA MSHIKAMANO NDIO NJIA YA KUMUENZI MAALIM SEIF


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mh. Othman Masoud Othman ametoa kauli hio tarehe 04/03/2021 alipokuwa akizungumza na Waumini wa Dini ya kiislamu waliojitokeza katika Hitma (Dua) ya kumuombea Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad aliefariki dunia mwezi uliopita.

Dua hio iliyoandaliwa na Uongozi wa Chama cha ACT Wazalendo Mkoa wa Mjini Kichama ilifanyika katika Mskiti wa Muembe Tanga Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharib Unguja, ambapo pia ilihudhuriwa na viongozi wa wakuu wa Chama cha ACT Wazalendo pamoja na viongozi wa Kiserikali.


Akimkaribisha Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar kwa niaba ya Chama cha ACT Wazalendo Makamu M/Kiti wa Chama hicho kwa upande wa Zanzibar Mh. Juma Duni Haji amesema Maalim alikuwa anawapenda sana Wazanzibari na alikuwa na lengo kubwa la kuwaunganisha, sasa kwavile ameshatangulia na kwasababu  ameshapatikana  kiongozi mwengine Mh. Othman basi wampe mashirikiano na wawe pamoja nae, nahii ndio njia ya kumuenzi  Maalim Seif.

Mh.Othman amesema sio jambo rahisi kuvaa viatu vya Marehemu  Maalim Seif ila kwasababu Wazanzibari ni wamoja na wanaamini katika ushirikiano itakuwa rahisi kwake kufanikisha majukumu yake.


Mh. Othman amesema Maalim Seif alikuwa ni muumini wa umoja na mshikamano hivyo  Wananchi kwa pamoja wakisimamia misingi hio watakuwa wamemtendea haki, na kwake ni faraja.

”Jambo muhimu kuliko yote ni kusimamia Umoja na Mshikamano baina yetu, kwani hilo ndio jambo kubwa ambalo Kiongozi wetu Maalim Seif alikuwa analihubiri, hivyo njia adhwimu ya kumuenzi  ni kukiendeleza  alichokiacha” Amesema Mh.Othman

Makamo wa Kwanza wa Rais amesisitiza tena kwa kusema kwahakika ni ngumu kuwa kama Maalim Seif, kwani Maalim ni Kitabu kilichokamilika na amefanya mengi sana enzi za uhai wake, lakini jambo kubwa linalompa moyo na faraja  nikwamba wapo viongozi wenzake ambao anaamini watashikamana na kushirikiana ili kuhakikisha mambo yanakwenda sawa, kwani Wazanzibari kwa sasa wanapigania mustakbali wa Nchi yao, na katika hilo Mungu hutia baraka na nguvu.

Mh. Othman amesema “kwasasa Wazanzibari tumepata fursa ya kuwa na Rais ambae amejipambanua katika kuikwamua Zanzibar kutoka  hapa ilipo sasa, hivyo ipo haja mahususi  Wananchi wote kwa pamoja kutazama mbele na kuisaidia Nchi yetu ili tuweze kukwamuka kwa kumuunga mkono Mh.Rais na Serikali kwaujumla’’

Mwisho Mh. Othman alitoa shukrani tena kwa waandaaji wa shughuli hio na kuwataka Wananchi kila wanapopata fursa basi kuendelea kumuombea dua Maalim Seif Sharif Hamad

 

RAIS DK. MWINYI AZUNGUMZA NA UONGOZI WA WIZARA YA KILIMO UMWAGILIAJI, MALIASILI NA MIFUGO IKULU ZANZIBAR

 

Mkurugenzi wa Wakala wa Serekali wa huduma za matrekta na Zana za Kilimo Zanzibar Ndg. Affan Othman Maalim, akizungumza wakati wa mkutano wao na Rais wa Zanziubar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani)  wakati wa mkutano huo kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Rais aliyoyatoa wakati wa kuapishwa kwa Mawaziri na Makatibu Wakuu katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar, mkutano huo umefanytika leo katika ukumbi wa Ikulu.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Umwagiliaji Maliasi na Mifugo Zanzibar Bi.Maryam Juma Sadala akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Rais aliyoyotowa wakati wa kuwaapisha Mawaziri na Makatibu Wakuu katika viwanja vya Ikulu Zanzibar, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar na (kulia kwa Rais) Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said.

Baadhi wa Wakuu wa Idara za Wizara ya Kilimo,Umwagiliaji,Maliasili na Mifugo Zanzibar wakifuatilia mkutano wa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Rais aliyoyatoa wakati wa kuapishwa kwa Mawaziri na Makatibu Wakuu katika viwanja vya Ikulu Zanzibar, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Zanzibar Dkt.Kassim Gharib akitowa ufafanuzi wakati wa mkutano wa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Rais aliyoyatowa wakati wa kuwaapisha Mawaziri na Makatibu Wakuu katika viwanja vya Ikulu Zanzibar, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar

 

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Umwagiliaji Maliasili na Mifugo Zanzibar.Bi. Maryam Juma Sadala, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Rais aliyoyatoa wakati wa kuapishwa kwa Mawaziri na Makatibu Wakuu katika viwanja vya Ikulu Zanzibar, mkutano huo umeongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) uliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo,Umwagiliaji,Maliasili na Mifugo Zanzibar. Bi. Maryam Juma Sadala, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji maagizo ya Rais aliyoyatoa wakati wa kuapishwa kwa Mawaziri na Makatibu Wakuu. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar, na (kulia kwa Rais) Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said na (kushoto kwa Rais) Waziri wa Kilimo Umwagiliaji Maliasili na Mifugo Mhe. Dkt.Soud Nahoda Hassan.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake na Uongozi wa Wizara ya Kilimo Umwagiliaji Maliasili na Mifugo Zanzibar, wakati wa kuripoti taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Rais aliyoyatoa wakati wa kuwaapisha Mawaziri na Makatibu Wakuu, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar, na (kulia kwa Rais) Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said na (kushoto kwa Rais) Waziri wa Kilimo Umwagiliaji Maliasili na Mifugo Zanzibar Mhe.Dkt.Soud Nahoda Hassan, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu)



NAIBU WAZIRI ULEGA AITAKA TASCA KUBADILI KATIBA YAO ILI KUNUFAIKA NA FURSA ZILIZOPO



 

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Abdallah Ulega amewaelekeza viongozi wa Umoja wa Vituo na Shule za kuvumbua, kulea na kuendeleza Michezo kwa Watoto na Vijana Tanzania (TASCA) kufanya marekebisho ya Katiba yao ili waweze kutambulika na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania  (TFF) ili kunufaika na fursa zake za kuendeleza programu mbalimbali za wa watoto na vijana.

 

Akifanya mazungumzo na viongozi hao leo Dar es salaam Naibu Waziri Ulega amewashauri viongozi hao kujisajili vitambulike kama Umoja wa Kuvumbua, Kulea na kuendeleza Mpira wa Miguu kwa Watoto na Vijana Tanzania (TAFOCA)  ili waweze kutambulika na TFF na kunufaika na fursa zake.

 

“Sasa usajili wa TASCA unawatambua kama Umoja wa Vituo na Shule za Kuvumbua, Kulea na kuendeleza Michezo kwa Watoto na Vijana jambo linalowakosesha fursa ya kutambuliwa na TFF,” alisema Naibu Waziri Ulega

 

Aidha, Naibu Waziri Ulega amewahakikishia viongozi wa TASCA kuwa Serikali imepokea mawazo yao yote ikiwa ni pamoja na mapendekezo ya kuboresha Kanuni za BMT ili kuweka utaratibu wa wachezaji wa timu B za Vijana za vilabu vya Ligi Kuu na wanaofanya vizuri kwenye timu za Taifa za U17 na U20 wapewe nafasi ya kucheza kwenye michuano ya ligi Kuu badala ya kubakia kwenye timu za vijana za vilabu hivyo ili kuwaongezea uzoefu na kuendeleza vipaji vyao kwa manufaa ya Taifa.

 

Pia Naibu Waziri Ulega amewaahidi viongozi wa TASCA kuwa Serikali italifanyia kazi ombi lao la kushirikiana na Taasisi mbalimbali za Umma kama Vyuo na Shule ili kutumia miundombinu iliyopo katika Taasisi hizo kwa shughuli mbalimbali za kukuza na kuendeleza michezo nchini.

Wednesday, March 3, 2021

MKUTANO WA SITA WA TUME YA PAMOJA YA KUDUMU KATI YA TANZANIA NA BURUNDI KUFANYIKA MKOANI KIGOMA


Tanzania na Burundi zimejipanga kuutumia Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kama njia mojawapo ya kuhamasisha wananchi wa pande zote mbili kuchangamkia fursa mbalimbali za uchumi zinazopatikana katika nchi hizi ili kunufaika nazo.

Kauli hiyo imetolewa kwa pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali, Wilbert Ibuge na mwenzake kutoka Burundi, Mhe. Isidore Ntirampeba walipokutana na Waandishi wa Habari leo mjini Kigoma kwa ajili ya kuwajulisha kuhusu mkutano huo utakaofanyika mjini humo kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021.

Balozi Ibuge alieleza kuwa, Tanzania na Burundi zimeendelea kuwa na ushirikiano wa kihistoria na kindugu kwa muda mrefu huku kila nchi ikinufaika kwa kiasi kikubwa na ushirikiano huo. Hata hivyo alieleza kuwa, bado upo umuhimu mkubwa wa kuendelea kuwahamasisha wananchi wa Tanzania na Burundi kuchangamkia fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye nchi hizo ili ziwanufaishe kiuchumi. Fursa hizo ni pamoja na biashara na uwekezaji.

“Mikutano ya Tume za Pamoja za Kudumu pamoja na mambo mengine inaangalia namna ya kuhakikisha kila mwananchi kutoka nchi husika ananufaika na fursa zilizopo na jukumu letu ni kuendelea kuwahamasisha kuzichangamkia fursa hizo” alisema Balozi Ibuge.

Akizungumzia ukuaji wa sekta ya uchumi kati ya Tanzania na Burundi, Balozi Ibuge alisema pamoja na changamoto mbalimbali,  biashara kati ya Tanzania na Burundi imeendelea kukua mwaka hadi mwaka na kutoa mfano wa kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi 2019 ambapo Tanzania na Burundi zilifanya biashara zenye thamani ya shilingi Bilioni 619.9 ukiwa ni  wastani wa Shilingi Bilioni 123.9 kwa mwaka.  Katika kiasi hicho, Tanzania iliuza nchini Burundi bidhaa zenye thamani ya shilingi bilioni 604.9 na Burundi iliuza Tanzania bidhaa zenye thamani ya Shilingi Bilioni 7.4.

Aidha, akizungumzia huduma ya wakimbizi, Balozi Ibuge alieleza kuwa, Tanzania imeendelea kuhifadhi wakimbizi kutoka Burundi huku Serikali ya Burundi ikiendelea kuwahimiza wakimbizi hao kurejea nchini kwao kwa hiari kutokana na kuimarika kwa hali ya amani na utulivu nchini humo.

“Tanzania imeendelea kuhifadhi wakimbizi kutoka Burundi, hata hivyo kutokana na kuimarika kwa hali ya amani na usalama nchini kwao Serikali yao imeendelea kuwahimiza kurejea ili kwenda kushiriki katika shughuli za ujenzi wa Taifa lao. Itakumbukwa kuwa, zoezi la kuwawezesha wakimbizi hao kurejea kwa hiari Burundi limeendelea kuratibiwa na Kamati ya Utatu inayojumuisha Tanzania, Burundi na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ambapo kati ya mwezi Septemba 2017 na Februari 2021, jumla ya wakimbizi 113,488 wamerejea nchini Burundi kwa hiari” alifafanua Balozi Ibuge.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje kutoka Burundi, Mhe. Isidore Ntirampeba alisema tume ya pamoja ya ushirikiano ni nyenzo muhimu katika kuimarisha ushirikiano baina ya nchi na nchi kwani hutoa nafasi kwa nchi mbili kutathmini mafanikio yaliyofikiwa kupitia ushirikiano uliopo, kutafuta suluhu kwa changamoto mbalimbali na kuainisha hatua imara zaidi za kufikia malengo kusudiwa. Alieleza kuwa, mikutano hii ni fursa nzuri kwa pande zote mbili kujipanga na kuboresha utendaji kulingana na mabadiliko mbalimbali yanayotokea duniani na katika nchi yakiwemo yale ya kisera na kimazingira.

Kadhalika, alitumia fursa hiyo kuishukuru na kuipongeza Tanzania na kuitaja kama nchi ya kupigiwa mfano katika kuhudumia wakimbizi wakiwemo wale wa kutoka Burundi ambao wamekuwa wakipokelewa tangu mwaka 1972. Aliongeza kuwa, Burundi inajivunia mchango wa Tanzania kwenye ustawi wa nchi hiyo na kwamba nchi hiyo inavutiwa na uongozi imara wa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao unalenga kuwaletea wananchi wote maendeleo.

Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi ambao unafanyika miaka 15 baada ya Mkutano wa Tano uliofanyika jijini Dar es Salaam mwaka 2006 unalenga kuendeleza, kuimarisha na kudumisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Burundi. Mkutano huu ambao utaanza kwa ngazi ya wataalam kutoka Tanzania na Burundi tarehe 3 Machi 2021utahitimishwa na Mkutano wa Mawaziri kutoka nchi hizo tarehe 5 Machi 2021.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Burundi, Mhe. Isidore Ntirampeba.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Burundi, Mhe. Ntirampeba akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara wa Tanzania, Prof. Riziki Shemdoe (katikati) pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji wa Tanzania, Mhandisi Nadhifa Kemikimba wakiwa kwenye Mkutano kati ya Balozi Ibuge na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Rashid Mchata (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi  wakiwa kwenye Mkutano kati ya Balozi Ibuge na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Burundi, Mhe. Isidore Ntirampeba naye akizungumza  wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Rashid Mchata naye akizungumza wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021

Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Dkt. Jily Maleko akifuatilia  Mkutano kati ya Balozi Ibuge na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Frank Mwega akifuatia Mkutano kati ya Balozi Ibuge na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021

Sehemu ya wadau kutoka sekta mbalimbali za Tanzania na Burundi walioshiriki mkutano kati ya Baloiz Ibuge na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi utakaofanyika mkoani Kigoma kuanzia tarehe 3 hadi 5 Machi 2021

Sehemuu nyingine ya wadau

Sehemu ya wadau wakifuatilia mkutano

Wadau wa Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Burundi

Mkutano ukiendelea