Matokeo chanyA+ online




Friday, June 27, 2025

ESTHER MORRIS WA NAWEZA TENA AONGOZA MAPINDUZI CHANYA KWA DADA POA NA WARAIBU WA DAWA ZA KULEVYA MWANZA

Mkurugenzi wa Shirika la Naweza Tena, Bi. Esther Morris, ameibuka kama sauti ya matumaini kwa wanawake waliokuwa wakijihusisha na biashara ya ukahaba na matumizi ya dawa za kulevya jijini Mwanza. Kupitia mradi wa kutoa Stadi za Maisha, shirika hilo limekuwa likiwasaidia Dada Poa na waraibu wa dawa za kulevya kuachana na maisha hatarishi na kuingia kwenye njia salama ya kujitegemea kiuchumi.

Bi. Morris amesema kuwa shirika hilo linawafuatilia kwa karibu walengwa wake, kuwafundisha maadili, kazi halali, na kuwajenga kisaikolojia ili waweze kurejea katika hali yao ya kawaida. Miongoni mwa miradi inayowasaidia ni pamoja na ajira katika kituo cha kuoshea magari, hatua inayowapa kipato halali na heshima mpya katika jamii.

Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika kinga na tiba dhidi ya dawa za kulevya. Esther amewataka wadau wote wenye nia ya kusaidia kundi hili kuwasiliana nao kupitia namba 0753 85 85 85, ili kwa pamoja kuendeleza mapinduzi haya ya matumaini.

Kauli mbiu: "Wekeza kwenye Kinga na Tiba dhidi ya dawa za kulevya"

#DCEA
#OktobaTunatiki

MCH. HANANJA ATOA WITO WA KITAIFA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA - TUIMARISHE KINGA, TUOKOE MAISHA

Mchungaji Richard Jackson Hananja ametoa wito kwa jamii na Serikali kuendelea kushirikiana kwa dhati katika mapambano dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya, amesisitiza umuhimu wa kuwekeza zaidi katika hatua za kinga na tiba kwa waathirika. 

Pia, Mch. Hananja ameeleza kuwa Serikali ya awamu ya sita imefanya kazi kubwa kwa kuongeza bajeti ya tiba, ujenzi wa vituo vya afya ya akili na huduma za tiba mbadala kwa waraibu.

Aidha, ametoa wito kwa wazazi, viongozi wa dini, walimu na jamii nzima kushirikiana katika kutoa elimu ya mapema kwa vijana kuhusu madhara ya dawa hizo, akibainisha kuwa kinga ni silaha madhubuti kuliko tiba. “Hatupaswi kusubiri vijana wetu waanguke kwenye janga hili ndipo tuingilie kati elimu, maombi, na ufuatiliaji wa karibu ni njia muhimu ya kuzuia,” amesisitiza.

Mch. Hananja amehimiza ushirikiano baina ya taasisi za dini, mashirika ya kiraia na Serikali katika kuhakikisha Taifa linaibuka na kizazi salama, kisichoathirika na matumizi ya dawa za kulevya.

Kauli mbiu: "Wekeza kwenye Kinga na Tiba dhidi ya dawa za kulevya"

#DCEA
#OktobaTunatiki