Matokeo chanyA+ online




Wednesday, January 22, 2020

WAZIRI KAIRUKI APONGEZA KIWANDA CHA TOFALI CHA SHAFA KWA UZALISHAJI WAKE


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji Mhe. Angellah Kairuki ametembelea na kukagua mazingira ya uendeshaji wa kiwanda cha vifaa vya ujenzi cha SHAFA na kupongeza uzalishaji wa tofali kiwandani hapo na kusema ni wa kuridhisha.
Ametoa pongezi hizo alipotembelea kiwandani  Januari 20, 2020 ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Pwani ili kukagua mazingira ya wawekezaji,  kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili ili kuendelea kuwa na mazingira mazuri ya wafanya biashara na wawekezaji nchini.
Meneja uendeshaji wa Kiwanda cha kuzalisha tofali cha SHAFA Bw. Suleiman Amour akimuonesha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki matofali yanatengenezwa na kiwanda hicho wakati wa ziara yake ya kikazi tarehe 20 Januari, 2020 Wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani.

Aidha katika ziara yake aliambatana na Watendaji kutoa Ofisi yake, Uongozi wa Mkoa wa Pwani, Watendaji kutoka Wilaya ya Mkuranga pamoja na watendaji wa Taasisi za Serikali ikiwemo TANESCO, TARURA, TRA, na Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC).
Akizungumza na waandishi wa habari kiwandani hapo, alisema amevutiwa na uwekezaji katika kiwanda hicho kwa kuwa na matofali bora kwa kuzingatia muhimu wa mahitaji ya ujenzi katika kuhakikisha kuna kuwa na majengo bora, kiasa na imara kwa matumizi mbalimbali.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akiwa katika ziara yake ya kikazi katika kiwanda cha kutengeneza matofali cha SHAFA kilichopo Wilaya ya Mkuranga Pwani
“Vipo viwanda zaidi ya vitatu vinavyotengeneza tofali nchini ingawa hiki kinaongoza kwa kuwa na mitambo ya kisasa aina ya  MASA yenye uwezo wa kuzalisha tofali 10,000, vigae vya sakafuni  zaidi ya 10,000 kwa siku ukilinganisha na viwanda vingine na kwa nchi za Afrika Mashariki ni kiwanda cha mfano kwa kutoa matofali yenye ubora wa hali ya juu,”alesisitiza Waziri Kairuki.
Alieleza kuwa, ipo haja ya kuunga mkono jitihada za wawekezaji wa viwanda kama hivyo ili kuendelea kujieletea maendeleo ya nchi kwa ujumla kwa kuzingatia mchango wake katika ngazi zote kuanzia Kijiji, Taifa hadi nje ya nchi.
Meneja uendeshaji wa Kiwanda cha kuzalisha tofali cha SHAFA Bw. Syleiman Amour akimuonesha Waziri wa Nchi Ofiis ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki namna matofali yanavyotengenezwa katika kiwanda hicho.
Aliongezea kuwa , furaha yake ni kuona kiwanda kinaweza kuzalisha kwa haraka, ubora na idadi kubwa kwa siku ili kuhakikisha kuna kuwa na majengo salama na yenye kudumu hadi vizazi vijavyo.
Akiwasilisha taarifa ya kiwanda kwa waziri, Afisa Mahusiano wa kiwanda hicho Bw. Agrey Roodluck alieleza malengo ya mradi ni pamoja na kuongeza wigo katika sekta ya ujenzi kwa kuzingatia uzalishaji wake unalenga kuwa na aina tofauti tofauti za matofali yenye ubora na kuweza kukidhi mahitaji kwa gharama nafuu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akioneshwa mtaambo maalum wa kutengeneza matofali na Meneja uendeshaji wa Kiwanda cha kuzalisha tofali cha SHAFA Bw. Suleiman Amour wakati wa ziara yake kiwandani hapo.
“Mradi umezingatia changamoto zilizopo za ukosefu wa matofali bora katika maeneo mengi yanayohitajika katika ujenzi wa maegesho ya magari, bararaba, maeneo ya viwanja vya ndege pamoja na majengo makubwa na madogo,”alieleza Roodlucky
Aidha alitoa omba kwa waziri kuendelea kuhamasisha ujenzi salama wa majengo ya taasisi, nyumba ndogo na kubwa kwa kuendelea kutumia tofali za kiwanda hicho na kueleza kuwa ni sehemu ya kuunga mkono maendeleo ya nchi kwa kuzingatia malighafi zinazotumika zinatoka nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki  akiuliza jambo kuhusu namna matofali yanavyosafirishwa katika kiwanda cha kutengeneza tofali cha SHAFA kwa Meneja uendeshaji wa Kiwanda cha kuzalisha tofali cha SHAFA Bw. Suleiman Amour akimuonesha
“Hadi kukamilika kwa mradi huu utatumia jumla ya Tshs Bilioni 15.3  na tayari zaidi ya asilimia 90 zimeshatumika na asilimia 99.9 za malighafi za kiwanda zinatoka hapa hapa nchini ikiwemo saruji, mchanga, kokoto na maji,”alisisitiza
Sambamba na hilo alisema, lengo kuhakikisha kiwanda kinatoa mchango katika pato la taifa katika kuhakikisha kinalipa kodi zote zinazotakiwa na kuendelea kuzalisha ajira zaidi ya 100 zitakazozingatia kundi kubwa la vijana wazawa ili kuweza kuendesha mitambo iliyopo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akizungumza na watumishi wa kiwanda cha kutengeneza tofali cha SHAFA (hawapo pichani) wakati wa ziara yake kiwandani hapo.
(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Filberto Sanga alimshukuru waziri kwa kutembelea mradi huo, na kueleza kuwa, ni mradi wenye faidi katika Wilaya yake kwa kuzingatia mchango wa mradi na namna walivyojikita katika kuhakikisha wanakuwa wenye bidhaa bora na kukidhi mahitaji ya wateja wake.

MV - MWANZA KUSTAWISHA BIASHARA KANDA YA ZIWA, NA NCHI JIRANI ZA KENYA NA UGANDA.

Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mingi ya kuimarisha miundombinu katika sekta mbalimbali ikiwemo mradi ya umeme (JN HPP-Julius Nyerere Hydropower project) kwa gharama ya shilingi trilioni 6.5, Ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR kwa gharama ya shilingi trilioni 7 na miradi mingine ambayo itaweka mazingira wezeshi kwa wananchi kufanya biashara na uwekezaji.

Mnamo Desemba 8, 2019, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli alizindua ujenzi wa mradi mwingine mkubwa wa ujenzi wa meli kubwa ya abiria na mizigo ya MV. Mwanza, ukarabati wa meli za MV. Victoria na MV. Butiama pamoja na ujenzi wa chelezo katika lango la biashara na uchumi kanda za ziwa ambao utekelezaji wake unaendelea vizuri na utakapokamilika utakuwa umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 153.7.


Meneja wa mradi huo, Mhandisi Abel Gwanafyo ameeleza kuwa, meli kubwa ya “MV Mwanza, Hapa Kazi Tu” itakayogharimu shilingi bilioni 89.76 ambayo ujenzi wake unatekelezwa na kampuni ya ujenzi ya GAS ENTEC wakishirikiana na KANG NAM kutoka Korea Kusini pamoja na SUMA JKT kutoka Tanzania, itakuja kuwa mbadala ya Meli ya MV Bukoba ambayo ilizama miaka 23 ilipita.

 Katika kampeni za uchaguzi mkuu wa 2015, Rais wa Awamu ya Tano, Dkt John Pombe Magufuli aliwaahidi wananchi wa kanda ya ziwa kuwa atajenga meli kubwa kuwaenzi waliokufa kwenye ajali hiyo lakini pia kuimarisha usafirishaji katika ukanda huo wa Tanzania kwani kuna fursa nyingi za biashara.

“Ni miaka 23, tangu kuzama meli ya MV. Bukoba mwaka 1996, miaka mingi imepita, lakini pia kuharibika kwa meli ya mizigo kumekuwa na tatizo kubwa kwa sekta ya usafarishaji kwa wananchi wanaioshi kuzunguka ziwa Victoria na hivyo kuathiri shughuli za uchumi na uzalishaji Kanda ya Ziwa”, Rais Dkt. John Magufuli.

Mradi huo mkubwa utakwenda sambamba na miradi mingine ya ukarabati wa meli ya Mv Victoria utaogharimu shilingi bilioni 22.71, Mv Butiama bilioni 4.9, ambazo ujenzi wake unatekelezwa na kampuni ya ujenzi ya KTMI kutoka Korea Kusini huku ujenzi wa chelezo utakaogharimu shilingi bilioni 36.4, unatekelezwa na kampuni ya Stx Engine ikishirikiana na SAE Kyong kutoka Korea Kusini.

MV Mwanza Hapa Kazi Tu, itakuwa na urefu wa mita 92, na uwezo wa kubeba abiria 1,200, mizigo tani 400, magari makubwa 3 na magari madogo 20, huku Mv Victoria ikibeba abiria 1,200, mizigo tani 200 na Mv Butiama abiria 200, tani 100, na kuwezesha zaidi ya abiria 2,600 na tani 700 za mizigo kwa wakati mmoja hivyo kusadia kupunguza adha ya usafiri na usafirishaji kwa abiria na mizigo katika ukanda huo wa ziwa.

“Ni wazi kuwa utekelezaji wa miradi hii utakaogharimu shilingi bilioni 153.7 utasaidia sana kutatua tatizo la usafiri na usafirishaji kwa wananchi wanaoishi kando ya ziwa Victoria, siyo tu hapa nchini bali hata kwa jirani zetu Kenya na Uganda kwa hiyo ni miradi ambayo ina manufaa kwa uchumi wetu”, amesema Rais Magufuli.

Aidha kukamilika kwa mradi huu kutaondoa kwa kiasi kikubwa tatizo la usafiri kwa abiria katika ukanda huo wa ziwa ikiwa ni pamoja na usafirishaji wa mizigo na mazao mbalimbali ya biashara na kuzalisha ajira kwani meli hii itahitaji wafanyakazi wa aina mbalimbali. Kwa upande wa nchi jirani za Kenya na Uganda , hii pia itakuwa fursa kwao kusafirisha mazao ya biashara na chakula kupitia ziwa Victoria badala ya kutegemea usafiri wa aina moja wa barabara au wa anga.

 Katika uzinduzi wa ujenzi wa mradi huo ambao utafungua ukanda wa kibiashara na kusaidia kukuza pato la taifa, Rais Magufuli alieleza dhamira kubwa ya Serikali ya Awamu ya Tano kuwa ni kufanya mabadiliko makubwa kwa kuleta miradi wezeshi kwa wananchi bila kutegemea misaada yenye masharti lukuki na ufadhili.

Sekta hii ya usafirishaji kwa njia ya maji ni muhimu sana na Serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzani (TPA), pamoja na Shirika la Huduma za Meli imekuwa na usimamizi madhubuti ili kukuza  na kuimarisha sekta hiyo ambayo ni nyenzo kubwa katika uchumi.
Kampuni ya Huduma za meli iliyoanzishwa na Baba wa Taifa, Mwl. Julius Nyerere kwa sasa inafanya kazi kubwa baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani na kuelekeza nguvu katika kuimarisha bandari nchini. Hapo awali ziwa Victoria lilikuwa meli 14 ikiwemo meli ya utalii, lakini meli hiyo iliacha kufanya kazi kutokana na uongozi mbovu, ikiwa ni pamoja na vitendo vya wizi na ubadhilifu wa mali za umma  na hatimaye meli zote 14 ziliisha na kubaki moja tu.

“Nawapongeza Kampuni ya Huduma za Meli kwa kuboresha utendaji kazi katika kampuni hii, kwani miaka ya nyuma hata mishahara mlikuwa hamuwezi kulipa wafanyakazi wenu, lakini kwa sasa utendaji kazi uko vizuri na umeimarika ambapo mpaka sasa meli nne zipo na zinafanya kazi. Meli hizo ni Mv Clarius, Mv Umoja, Mv Sangara na Mv Wimbi, kwa hiyo ujenzi wa meli mpya na ukarabati wa meli hizi mbili utasaidia kukuza huduma zenu”, alisema,Rais Magufuli.


Mamlaka ya Bandari imekuwa ikiendelea na upanuzi na ujenzi wa bandari mbalimbali nchini zikiwemo bandari ya Dar es Salaam, Mtwara, Tanga, Mwanza na bandari zake ndogondogo za Kemendo, Bukoba, Kwemukwikwi na Nyamirembe kwa upande wa kanda ya ziwa.

 Mhandisi,Gwanafyo ameeleza kuwa ujenzi wa meli mpya “Mv Mwanza Hapa Kazi Tu” umefikia asilimia 52 tofauti na mwezi Desemba 2019 ambapo ulikuwa asilimi 50, huku ukarabati wa Mv Victoria ukiwa asilimia 75 badala ya 65, Mv Butiama asilimi 70 badala ya 60 huku ujenzi wa chelezo ukiwa ni asilimia 80 badala 68 za mwezi Desemba 2019.

Miradi hiyo imeweza kutoa fursa nyingi kwa wananchi wa mkoa wa Mwanza ikiwemo fursa za biashara na ajira kwani mpaka sasa kuna ajira zaidi ya 1,000 na bado zinaongezeka kwa kadri siku zinavyoongezeka.

Ujenzi wa meli hii kubwa ni utekelezaji wa ahadi na kutimiza maono ya Baba wa Taifa Mwl.Julius Nyerere aliyetaka kuwepo na meli kubwa katika ukanda huo wa kiuchumi wa Tanzania, ambapo mwaka 1979, alisimamia kuundwa kwa  meli ya MV Bukoba ambayo  ilizama mwaka 1996 na kuleta ugumu wa usafiri na usafirishaji katika ziwa Victoria ambalo ni tegemeo kwa wananchi wa kanda hiyo pamoja na nchi jirani. Uamuzi wa  Rais Magufuli wa kujenga meli hiyo kubwa ‘Mv Mwanza, Hapa Kazi Tu’ na kukarabati meli nyingine unaonyesha jinsi alivyodhamiria kuyaishi na kuyatekeleza maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwa vitendo.
Na.Paschal Dotto-MAELEZO

MAKAZI BORA KUWA AGENDA YA KITAIFA - WAZIRI UMMY

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jmaii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu amesema Serikali imeichukua Kampeni ya kuhamisha wananchi kujenga nyumba bora iitwayo “Piga Kazi: Boresha Makazi” kuwa Agenda ya kitaifa kwa miaka mitatu ijayo.  
Waziri Ummy ameyasema hayo leo jijini Ddooma mara baada ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu na Bajeti kwa kipindi cha nusu Mwaka (Julai-Disemba 2019) kwa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa upande wa Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jmaii, Jinsia,  Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu na Bajeti kwa kipindi cha nusu Mwaka (Julai-Disemba 2019) kwa upande wa Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii kwa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii jijini Dodoma.

Waziri Ummy amesema kuwa Kampeni ya Makazi Bora ni jambo ambalo Wizara imelihamasisha katika kipindi cha nusu mwaka na katika utekelezaji walichagua baadhi ya mikoa kuanza kwa mfano kujenga nyumba bora kwa wasiojiweza na kuhamasiaha wanaojiweza kujenga na kuisambaza nchini nzima ili kuwezesha wananchi kuboresha makazi yao.
“Kampeni hii yenye Kauli mbiu “Piga Kazi: Boresha Makazi”  inalenga kupunguza Kaya zenye makazi duni kwa silimia 50 kutoka asilimia 15.9 ya sasa hadi kufikia asilimia 8 ifikapo mwaka 2022” alisema Waziri Ummy 
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jmaii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Faustine Ndugulie akifafanua jambo kuhusu jitihada za Wizara katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa majukumu na Bajeti kwa kipindi cha nusu Mwaka (Julai-Disemba 2019) kwa upande wa Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii kwa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii jijini Dodoma.
Aidha Waziri Ummy amesema wananchi wakiboresha makazi itasaidia kuondokana na maradhi mablimbali ikiwemo kifua kikuuu na kuwezesha jamii kuwa na sehemu salama za kulala hivyo kupunguza magonjwa yanayotokana na uchafu na kukosa hewasafi.
“Nisema tu tatizo sio wananchi kuwa masikini ila bado hatujapanga kuwa na vipaumbele gani sisi kama Wizara tutahamasisha suala la ujenzi wa Nyumba Bora kuwa kipaumbele kwa wananchi katika maeneo yao.” Alisema Waziri Ummy.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe. Peter Serukamba akitoa maelekozo kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jmaii, Jinsia, Wazee na Watoto upande wa Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa majukumu na Bajeti kwa kipindi cha nusu Mwaka (Julai-Disemba 2019) kwa upande wa Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii kwa Kamati hiyo leo jijini Dodoma.
Akifafanua kuhusu Kampeni ya kuhamasisha Makazi Bora kwa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Katibu Mkuu Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. John Jingu amesema kuwa kampeni hiyo ikibebwa na viongozi wa mikoa na wilaya husika itasaidia kuhamaisha wananchi walio wengi katika kuboresha makazi yao kwani viongozi hao wanazungumza na wananchi kila siku.
“Agenda hii ya ujenzi wa Makazi Bora tutaipeleka hadi kwa viongozi wa dini ili wawe wanahubiri kwa waumini faida za kuwa na nyumba bora itasaida kubadilisha wananchi na tutafanikiwa katika hili” alisema Dkt. Jingu
Katibu Mkuu Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. John Jingu akifafanua jambo kuhusu jitihada za Wizara katika kuhamisha wananchi kujenga nyumba bora katika Kampeni iitwayo “Piga Kazi: Boresha Makazi” wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa majukumu na Bajeti kwa kipindi cha nusu Mwaka (Julai-Disemba 2019) kwa upande wa Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii kwa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii leo jijini Dodoma.
Kwa upande wake Mbunge wa Temeke Mhe. Abdallah Mtolea amesema kuwa Tanzania ya Viwanda na Uchumi wa kati itawezekana ikiwa wananchi watahamasishwa kujenga nyumba bora kwani uchumi wa viwanda na wa kati unaanza na wananchi kuwa katika mazingira bora ya malazi.
Naye Mbunge wa Chemba Mhe. Juma Nkamia alisisitiza Serikali kuipa nguvu Kampeni hii ya kuboresha makazi kwani wananchi walio wengi wamekuwa na kipato kizuri ila bado hawana elimu ya umuhimu wa kuwa na nyumba bora.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na Menejimenti ya Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii wakifuatilia maelezo ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jmaii, Jinsia,  Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu (aliyesimama) wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa majukumu na Bajeti kwa kipindi cha nusu Mwaka (Julai-Disemba 2019) kwa upande wa Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii kwa Kamati hiyo.
Kampeni ya kuboresha makazi imewezesha kufikia wakazi wa Kata ya Mzenga Kisarawe mkoa wa Pwani , Mpandandogo na Kabungu mkoani Katavi, Ikungi na Chibumagwa mkoani Singida na imelenga kufikia mikoa 26 ya Tanzania Bara.

STAMICO KUANZISHA MRADI WA KUSAFISHA DHAHABU MWANZA

Waziri wa Madini Doto Biteko akiieleza jambo Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini wakati wizara ilipowasilisha kwa kamati hiyo  Taarifa  kuhusu Utekelezaji na Hali ya Upatikanaji wa Fedha za Maendeleo ya STAMICO kwa  Kipindi cha Nusu Mwaka, kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020.

Imeelezwa kuwa, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) lipo katika hatua za awali za uanzishwaji wa Mradi wa Kusafisha Dhahabu (Gold Refinery) na tayari kampuni ya ubia ijulikanayo kama Mwanza Precious Metals Refinery Company Limited imeanzishwa.
Hayo  yamebainishwa leo Januari 21, 2020 na Kaimu Mtendaji Mkuu wa (STAMICO) Dkt. Venance  Mwase wakati  akiwasilisha kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Taarifa  kuhusu Utekelezaji na Hali ya Upatikanaji wa Fedha za Maendeleo ya shirika hilo kwa  Kipindi cha Nusu Mwaka, kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 kwa niaba ya Waziri wa Madini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dustan Kitandula akieleza jambo baada ya Wizara kuwasilisha kwa kamati hiyo  Taarifa  kuhusu Utekelezaji na Hali ya Upatikanaji wa Fedha za Maendeleo ya  STAMICO hilo kwa  Kipindi cha Nusu Mwaka, kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020.
Dkt. Venance ameileza kamati hiyo kuwa,  mradi huo utaendeshwa kwa ubia ambapo STAMICO itakuwa  na hisa asilimia 25 na mwekezaji asilimia 75, huku ikilelezwa kwamba, mradi huo  utakaojengwa jijini Mwanza utahusisha kujenga mtambo wenye uwezo wa kusafisha wastani wa kilo 200 hadi 500 kwa siku.
Ameongeza kuwa, makadirio ya fedha zinazohitajika ni Dola la Marekani Milioni 58.204 ambazo zimepangwa kwa ajili ya ununuzi wa mtambo wa kusafishia dhahabu, gharama za awali za mradi, kununua dhahabu kutoka katika masoko pamoja na gharama zaza uendeshaji na kuongeza‘’ Mheshimiwa Mwenyekiti tumepanga uwe mtambo wa viwango vya kimataifa,’’.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini (mstari wa mbele) na Maafisa kutoka Wizara ya Madini na Taasisi zake wakifuatilia uwasilishaji wa Taarifa ya STAMICO kwa kamati hiyo.
Aidha, Dkt. Mwase amesema kwamba katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2019, tayari mradi umetekeleza majukumu kadhaa ikiwemo kupata leseni ya kujenga na kuendesha mtambo huo, kusainiwa mkataba wa ubia pamoja na kuanza taratibu za uanzishwaji wa kampuni ya ubia na kupata eneo la ujenzi wa mtambo chini EPZA.
Ameongeza majukumu mengine yaliyotekelezwa ni pamoja na kufanyika kwa Athari kwa Mazingira (EIA) kwenye eneo la mradi upembuzi yakinifu pamoja na kukusanya taarifa za upatikanaji wa dhahabu katika maeneo mbalimbali yanayokusudiwa.
Waziri wa Madini Doto Biteko akiieleza jambo Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini wakati wizara ilipowasilisha kwa kamati hiyo  Taarifa  kuhusu Utekelezaji na Hali ya Upatikanaji wa Fedha za Maendeleo ya STAMICO kwa  Kipindi cha Nusu Mwaka, kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020.

Akizungumzia shughuli nyingine zinazoendeshwa na Shirika hilo amesema linaendelea kutoa huduma za Kibiashara za uchorongaji miamba wa biashara katika sekta ya mafuta na gesi ambapo katika Mwaka wa Fedha 2019/20  ambapo limefanikiwa kupata kandarasi 4 za uchorongaji kupitia zabuni mbalimbali  zenye thamani ya shilingi bilioni 2.2 .
Kuhusu Mgodi wa Stamigold ambao ni Kampuni Tanzu ya Shirika hilo ameieleza kamati hiyo kuwa, kuanzia Julai hadi |Desemba, 2019, mgodi huo umezalisha na kuuza wakia 7,133.00 za madini ya dhahabu na wakia 879.19 za madini ya fedha, vyote vikiwa na thamani ya shilingi 24,172,700,255.34.
‘’ Mhehimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hicho, mgodi umelipa jumla ya shilingi 1,712,455, 550.91 kwa ajili ya malipo ya mrabaha, ada ya ukaguzi na kibali cha kusafirisha madini nje ya nchi,’’ ameeleza Dkt.  Venance.
Waziri wa Madini Doto Biteko akiieleza jambo Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini wakati wizara ilipowasilisha kwa kamati hiyo  Taarifa  kuhusu Utekelezaji na Hali ya Upatikanaji wa Fedha za Maendeleo ya STAMICO kwa  Kipindi cha Nusu Mwaka, kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020.


Kuhusu mradi wa makaa ya mawe katika Mradi wa Kabulo na Kiwira, amesema jumla ya tani 4,359.10 ziliuzwa na kulipatia Shirika kiasi cha shilingi 17,558,184.76 na kuongeza kuwa, ‘’ shirika lilifanikiwa kulipa mrabaha, ada ya ukaguzi na tozo ya Halmashauri ya jumla ya shilingi 23,645,000.62
Aidha ameongeza kuwa Mgodi umeendelea kutoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 400.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini Doto Biteko wakati akitoa ufafanuzi wa hoja zilizoibuliwa na kamati, amewatoa Hofu Wajumbe wa kamati hiyo kuhusu Maendeleo ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambapo ameeleza pamoja na changamoto zinazolikabili, linakua na linafanya vizuri.
Waziri Biteko ameiomba Kamati hiyo kuendelea kuilea na kuishauri STAMICO  kwa kuwa mwelekeo wake ni mzuri na kwamba hivi sasa lina uwezo wa kuzalisha hadi shilingi Bilioni 20 tofauti na ilivyokuwa awali na kuongeza kuwa, Watendaji na Bodi ya Shirika hilo mara zote wanafanyia kazi ushauri unaotolewa na Kamati pamoja na Wizara.
‘’Mheshimiwa Mwenyekiti, itakuwa bahati mbaya sana kulifuta shirika hili. Linakua, wanaendelea vizuri na Wana Bodi nzuri, watendaji wanasikiliza ushauri na kuufanyia kazi na mapungufu yanafanyiwa kazi, naomba muendelee kuilea na kuishauri STAMICO,’’amesisitiza Waziri Biteko.

Tuesday, January 21, 2020

TANZANIA IMEPIGA HATUA KUBWA KATIKA KUTEKELEZA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO YA MWAKA 2025 - RAIS MAGUFULI


 Rais Magufuli amesema miaka 4 ya tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani Tanzania imepiga hatua kubwa katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 – 2020, mipango ya kimataifa na kikanda na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka 5 (2016/17 – 2020/21) iliyolenga kujenga uchumi wa viwanda utakaochochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu.
Rais Dkt. John Magufuli amesema hayo tarehe 21 Januari, 2020 katika hafla ya kuukaribisha Mwaka Mpya aliyowaandalia Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa (Sherry Party) na kufanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, Waakilishi wa Mashirika ya kimataifa katika Sherehe za Mwaka mpya 2020 kwa Mabalozi hao (Diplomatic Sherry Party

Rais ametaja baada ya mafanikio  yaliyopatikana ni pamoja na kulinda na kudumisha amani na usalama wa nchi, kuimarisha Muungano ambao Aprili 2020 utatimiza miaka 56, ukuaji mzuri wa uchumi wa wastani wa asilimia 7, kudhibiti mfumuko wa bei hadi kufikia asilimia 3.5 na kuongeza akiba ya fedha za kigeni kutoka Dola za Marekani Bilioni 4.123 hadi kufikia Dola za Marekani 5.579 zinazotosheleza kuagiza bidhaa na huduma kwa kipindi kisichopungua miezi 6.3.
Kiongozi wa Mabalozi (Dean of Diplomatic Corps) Mhe. Ahamada El Badaoui Mohamed Fakih akizungumza

Mafanikio mengine ya kiuchumi ni kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato kutoka wastani wa shilingi Bilioni 850 kwa mwezi hadi kufikia shilingi Trilioni 1.5 (ambapo Desemba 2019 ilifikia shilingi Trilioni 1.9), kuvutia uwekezaji wenye thamani ya shilingi Trilioni 30 uliozalisha ajira laki 1, kuogeza biashara ya nje kutoka shilingi Trilioni 11.5 hadi kufikia shilingi Trilioni 16.6, kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara kutoka tani 796,512 hadi kufikia tani 1,141,774 (ongezeko la asilimia 43.3) na kujenga viwanda vipya 4,877.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, Waakilishi wa Mashirika ya kimataifa katika Sherehe za Mwaka mpya 2020 kwa Mabalozi hao (Diplomatic Sherry Party

Aidha, katika kipindi hicho mauzo ya dhahabu nje ya nchi yameongezeka kutoka Dola za Marekani Bilioni 1.469 hadi kufikia Bilioni 1.743, mapato ya Serikali kutokana na madini yameongezeka kutoka shilingi Bilioni 168 hadi kufikia shilingi Bilioni 346, idadi ya watalii imeongezeka kutoka watalii Milioni 1.1 hadi kufikia Milioni 1.5 na mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka Dola za Marekani Bilioni 1.9 hadi kufikia Bilioni 2.488.
 Rais Magufuli ameongeza kuwa katika kipindi hicho Serikali imetekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge railway) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma utakaogharimu zaidi ya shilingi Trilioni 7, ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 za umeme utakaogharimu shilingi Trilioni 6.5, ujenzi wa kilometa 2,500 za barabara za lami na nyingine 2,400 zikiendelea kujengwa, kilometa 7,087 la barabara za lami zikiwa katika maandalizi ya kuanza kujenzi na kukamilisha ujenzi wa madaraja makubwa 8.
Miradi mingine ni kufufua reli ya Dar es Salaam – Tanga – Moshi iliyokuwa haitoi huduma tangu miaka zaidi ya 20 iliyopita, kupanua bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga, kukarabati meli 7 katika maziwa makuu, kukamilisha ujenzi wa jengo la 3 la abiria katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam (Terminal III), kujenga viwanja vya ndege 11, kununua rada 4, na kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) baada ya kununua ndege mpya 11.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, Waakilishi wa Mashirika ya kimataifa katika Sherehe za Mwaka mpya 2020 kwa Mabalozi hao (Diplomatic Sherry Party

Kwa upande wa huduma za kijamii amesema mbali na kujenga Bwawa la Mwalimu Nyerere, Serikali imejenga njia ya umeme ya Iringa – Shinyanga, Makambako – Songea na Lindi – Mtwara, kupeleka umeme vijijini ambapo idadi ya vijiji vilivyofikiwa na umeme imeongezeka kutoka 2,018 hadi kufikia 8,587, kujenga vituo vya afya 352 na Hospitali za Wilaya 69, kuajiri watumishi wa afya 8,000 na kuongeza bajeti ya dawa na vifaa tiba kutoka shilingi Bilioni 31 hadi kufikia shilingi Bilioni 270 kwa mwaka.
Amebainisha kuwa Serikali inatoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari ambapo imeshatumia shilingi Trilioni 1, mikopo ya elimu ya juu imeongezeka kutoka shilingi Bilioni 341 hadi kufikia shilingi Bilioni 450, imetekeleza miradi ya maji yenye thamani ya shilingi Trilioni 3 na hivyo kuongeza upatikanaji wa maji kutoka wastani wa asilimia 56 hadi kufikia asilimia 71, kuongeza mapambano dhidi ya rushwa na Serikali kuhamia Dodoma.
Mhe. Rais Magufuli amesema kwa kuongozwa na sera ya diplomasia ya uchumi, Tanzania imeendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na nchi mbalimbali duniani ambapo pamoja na kufanya ziara katika nchi mbalimbali, Balozi mpya 7 zimefunguliwa na kushiriki katika shughuli na mipango mbalimbali ya kimataifa ikiwemo ulinzi wa amani ambapo kwa sasa askari 2,297 wa Tanzania wapo katika ulinzi wa amani katika nchi mbalimbali.
Baadhi ya  Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, Waakilishi wa Mashirika ya kimataifa katika Sherehe za Mwaka mpya 2020 kwa Mabalozi hao (Diplomatic Sherry Party)

Ameahidi kuwa katika mwaka 2020 Serikali imejipanga kuendelea kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, kudumisha amani na usalama, kukuza zaidi uchumi, kuimarisha akiba ya fedha za kigeni, kuongeza ukusanyaji wa mapato, kukuza sekta kuu za uzalishaji yaani kilimo, viwanda, ujenzi, madini na utalii pamoja na kuboresha mazingira ya kufanyia biashara ambapo amewaomba Mabalozi hao kuwashawishi wafanyabiashara wa nchi zao kuja kuwekeza nchini Tanzania.
Pia, amewahakikishia kuwa katika mwaka 2020 ambapo Tanzania inafanya Uchaguzi Mkuu, Serikali imejipanga kuhakikisha unafanyika kwa misingi ya kidemokrasia na katika mazingira ya amani, uhuru na haki, na amezikaribisha nchi na taasisi mbalimbali kuja kuangalia jinsi Tanzania ilivyokomaa kidemokrasia pindi wakati ukifika.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini kabla ya chakula cha jioni alichowaandalia Mabalozi hao katika Sherehe za Mwaka mpya 2020 kwa Mabalozi hao (Diplomatic Sherry Party) zilizofanyika katika Ukumbi wa Kikwete Ikulu jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Maguful katika   Sherehe za Mwaka mpya 2020 kwa Mabalozi hao (Diplomatic Sherry Party) zilizofanyika katika Ukumbi wa Kikwete Ikulu jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU 


Ameahidi kuwa Tanzania, itaendelea kukuza ujirani mwema, kushirikiana na nchi mbalimbali na kutekeleza majukumu ya kimataifa ikiwemo kuwahudumia wakimbizi na kuwarejesha makwao kwa hiari, lakini ameeleza kusikitishwa na hujuma na propaganda zinafanyika kwa lengo la kukwamisha zoezi hilo.
Akizungumza kwa niaba ya Mabalozi hao, Kiongozi wa Mabalozi (Dean of Diplomatic Corps) Mhe. Ahamada El Badaoui Mohamed Fakih amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi mzuri aliouonesha katika kipindi cha miaka minne ambapo miradi mikubwa ya maendeleo imetekelezwa, kukua kwa uchumi, ustawi wa watu na ameahidi kuwa Mabalozi wataendelea kutoa ushirikiano wowote utakaohitajika.