Matokeo chanyA+ online




Tuesday, December 17, 2019

WAZIRI KAIRUKI AZITAKA KAMPUNI BINAFSI KUSAIDIA WAFANYAKAZI WAKATI WA MAJANGA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki akizungumza jambo na mmoja wa wafanyakazi wa Kampuni Kioo Ltd, Abdulrahman Rashid wakati wa ziara yake ya kutembelea Ofisi za Kampuni jana Jumatatu (Desemba 16, 2019) Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki amezitaka kampuni binafsi nchini kuweka utaratibu maalum wa kuwasaidia wafanyakazi na familia zao pindi wanapokabiliwa na majanga mbalimbali ya kibindamu ikiwemo ajali na vifo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Wafanyakazi wa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) wakati wa ziara yake ya kutwembelea ofisi za Kampuni hiyo jana Jumatatu (Desemba 16, 2019) Jijini Dar es Salaam

Waziri Kairuki aliyasema hayo jana Jumatatu (Desemba 16, 2019) wakati wa ziara yake ya kutembelea Kampuni ya vinywaji baridi ya SBC Tanzania Ltd inayozalisha vivywaji vya Pepsi, Mirinda, Mountain Dew na 7up, na kusema utaratibu huo utasaidia kuongeza tija, motisha na uzalishaji katika makampuni hayo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki akisalimiana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya SBT Tanzania Ltd inayozalisha vinywaji baridi vya Pepsi, Mirinda, Mountain Dew na 7up, Avinash Jha wakati wa ziara yake ya kutembelea Kiwanda hiyo aliyoifanya jana Jumatatu (Desemba 16, 2019) Jijini Dar es Salaam.
Waziri Kairuki alisema Kampuni ya SBC Tanzania imekuwa ni miongoni mwa makampuni machache nchini yaliyoweka utaratibu wa kusaidia wafanyakazi wake wakati wa majanga, ikiwemo vifo na hivyo kuwataka waajiri wa makampuni mengine kuiga mfano huo kwani wafanyakazi ni kiungo muhimu cha mafanikio ndani ya makampuni hayo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki akitazama moja ya chupa inayozalishwa katika Kiwanda cha Kioo Ltd wakati wa ziara yake ya kutembelea Ofisi za Kiwanda hicho jana Jumatatu (Desemba 16, 2019).

‘Hapa PESPI kuna Mtumishi alifariki akiwa kazini, na kampuni ya SBC ilimchukua mtoto wake na kumuendeleza kielimu kuanzia degree (Shahada) ya kwanza hadi ya pili na yupo katika Idara ya Masoko ya kampuni hii na huu ni mfano mzuri unaopaswa kuigwa na makampuni mengine katika kuendeleza familia za wafanyakazi wao pindi wanapofariki’ alisema Waziri Kairuki.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuniya SBT Tanzania Ltd, Avinash Jha akisoma taarifa ya Kampuni hiyo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki (wa kwanza kulia) wakati wa ziara yake ya kutembelea Ofisi za Kampuni hiyo jana Jumatatu (Desemba 16, 2019) Jijini Dar es Salaam.

Aidha Waziri Kairuki alisema kitendo cha kuweka utaratibu wa kuwasadia wafanyakazi na familia zao wakati wa majanga utasaidia kuendeleza kizazi kinachofuata ndani ya kampuni hizo na hivyo kuwafanya kufurahia kufanya kazi ndani ya kampuni hizo na kuhimiza utaratibu huo kuwa endelevu ili kuzidi kuimarisha ushirikiano baina ya kampuni hizo na familia za wafanyakazi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki akitazama namna uzalishaji wa chupa unavyofanyika ndani ya kiwanda cha kampuni ya Kioo Ltd wakati wa ziara yake aliyoifanya jana Jumatatu (Desemba 16, 2019).

Akizungumzia kuhusu uzalishaji wa Kampuni hiyo, Waziri Kairuki aliupongeza Uongozi wa SBC Tanzania Ltd kutokana na juhudi na jitihada kubwa inazoendelea kuzifanya katika kukuza soko la bidhaa za vinywaji nchini sambamba na kuendelea kutoa ajira kwa Watanzania na hivyo kuchangia katika kukuza uchumi nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji),Angellah Kairuki akipata maelezo kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya SBT Tanzania, Avinash Jha wakati wa ziara ya Waziri Kairuki alipotembelea Ofisi za Kampuni hiyo jana Jumatatu (Desemba 16, 2019) Jijini Dar es Salaam.

Akitolea mfano Waziri Kairuki alisema Kampuni hiyo yenye mtaji wa Dola Milioni 373 imeendelea kukuza mnyoyoro wa thamani wa bidhaa zake nchini, ambapo katika kipindi cha miaka 18 tangu kuanzishwa kwake kiwanda hicho kimeonyesha uhalisia wa kazi kubwa inayofanya, na hilo linadhihishwa na kiwango cha malipo ya kodi kwa Serikali ya Tsh Bilioni 416 iliyolipa kuanzia mwaka 2001.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Karuki akipata maelezo kutoka kwa mmoja wa Viongozi waandamizi wa Kiwanda ya Kioo Ltd kuhusu uzalishaji unaofanywa na kampuni hiyo wakati wa ziara yake ya kutembelea Kiwanda hicho aliyoifanya jana Jumatatu (Desmba 16, 2019) Jijini Dar es Salaam.

‘Kampuni hii ilianza mwaka 2001 ikiwa  wafanyakazi 76 na mtaji wa uwekezaji wenye thamani ya Tsh Bilioni 24.6, lakini kwa sasa ina jumla ya wafanyakazi walioajiriwa katika ajira ya moja kwa moja takribani 1215, na pia wameendelea kuhuisha mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wao kila baada ya miaka 2-3’’ alisema Waziri Kairuki.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Karuki (katikati) akiwa pamoja na watendaji wa Kampuni ya SBT Tanzania Ltd  wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya uzalishaji wa bidhaa za kampuni hiyo aliyoifanya jana Jumatatu (Desemba 16, 2019) Jijini DaR es Salaam.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya SBC Tanzania Ltd, Avinash Jha alisema Kampuni hiyo itaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na serikali katika kufanikisha mikakati mbalimbali ikiwemo sera ya uchumi wa viwanda, hatua inayolenga kuleta maendeleo jumuishi kwa Watanzania wote.
Jha aliongeza kuwa kampuni yake itaendelea kuzingatia sera, miongozo na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Serikali ikiwemo kutoa ajira kwa vijana wengi wa Kitanzania sambamba na kuwajengea uwezo na uzoefu wa kazi ili kumudu changamoto zilizopo katika soko la ajira nchini.

RAIS WA ZANZIBAR DK SHEIN AFUNGUA KONGAMANO LA KITAIFA LA UTAWALA BORA NA HAKI ZA BINADAMU



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akikabidhiwa Tunzo Maalum ya Kusimamia na Muazilishi wa Utawala Bora Zanzibar na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.Haroun Ali Suleiman, wakati wa hafla ya Kongamano la Kuadhimisha Siku ya Maadili na Haki za Binadamu na Utawala Bora lililofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakil Kikwajuni Jijini Zanzibar  16-12-2019.(Picha na Ikulu)

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia wakati wa hafla ya ufunguzi wa Kongamano la Kitaifa la Utawala Bora na Siku ya Maadili na Haki za Binadamu, lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu)
 
 
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba imefanya bidii kubwa kuhakikisha misingi ya utawala bora inafuatwa ili kukuza uchumi na kujenga jamii yenye imani, upendo na mshikamano baina yao, serikali na nchi yao kwa jumla.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa huko katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul Wakili, Kikwajuni mjini Zanzibar katika maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binaadamu.

Baadhi ya Washiriki wa Kongamano la Kitaifa la Utawala Bora na Haki za Binadamu wakifuatilia hutuba ya ufunguzi wa Kongamano hilo wakati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akihutubia (hayupo picha) katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu)


Katika hotuba hiyo, Rais Dk. Shein aliitaja misingi hiyo kuwa ni ushirikishwaji wa umma, utawala wa sheria, haki na usawa kwa watu wote,uwazi katika kuendesha shughuli za maendeleo pamoja na uwajibikaji katika utendaji na uadilifu.

Rais Dk. Shein alieleza hatua mbali mbali zilizochukuliwa na Serikali kuona kwamba utawala bora unaimarika ikiwa ni pamoja na kupitisha Sera ya Utawala bora ya mwaka 2011, ambayo utekelezaji wake unasaidia katika kuyafikia malengo ya mkataba wa haki za binaadamu na ule wa mapambano dhidi ya rushwa.

Alieleza kuwa Tanzania ni nchi ya mwanzo kuanzisha Wizara ya Utawala Bora katika nchi za Bara la Afrika hatua ambayo imeijengea sifa kubwa ndani na nje ya Afrika.

DKT KALEMANI AZINDUA KITUO CHA KUPOKEA NA KUTAWANYANJIA KUU ZA UMEME -SIMIYU

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, amezindua Kituo cha Kupokea na Kutawanya Njia Kuu za Umeme (Switching Station) kilichopo katika kijiji cha Ng’ami, eneo la Viwandani, wilayani Bariadi,  Mkoa wa Simiyu.
Uzinduzi huo umefanyika Desemba 15, 2019 ambapo Kituo hicho kinachukua umeme kutoka Kituo Kikuu cha Mabuki kilichopo Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza umbali wa kilomita 87.2, kupitia Njia ya kusafiri umeme ya Msongo wa kV 33.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ( mwenye shati la bluu) akisalimiana na watumishi mbalimbali wa Mkoa wa Simiyu mara baada ya kufika katika uzinduzi wa Kituo cha Kupokea na Kutawanya Njia kuu za Umeme  kilichopo eneo la Ng’ami wilayani Bariadi mkoani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya uzinduzi huo, Dkt Kalemani, alisema kituo hicho kimezinduliwa rasmi kwa lengo la kuimarisha hali ya upatikanaji umeme katika Mkoa wa Simiyu  ambao umejikita katika uwekezaji wa Viwanda , na hivyo unahitaji umeme wa uhakika.
Kutokana na uwepo wa Kituo hicho, Dkt. Kalemani alisema “natoa agizo kwa Meneja wa Mkoa, mtafute eneo la kiwanja hapa, mjenge eneo la makazi kwa ajili ya mtumishi atakayekiangalia kituo hiki kwa masaa 24, kwa sababu ikitokea dharura haitowezekana mtu kutembea kilomita 10 kuja hapa hivyo ni lazima mtu akae hapa.”

Msimamizi wa cha Kituo cha Kupokea na Kutawanya Njia kuu za Umeme cha Ng’ami, wilayani Bariadi mkoani Simiyu akitoa maelezo kuhusu kituo hicho kwa Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani pamoja wageni alioambatana nao. 

Aidha, Dkt Kalemani alitoa wito kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,  Anthony Mtaka, kuwahamasisha wananchi wa eneo hilo kutunza miundombinu ya  kituo husika ili wananchi wasifanye uharibu wa aina yoyote katika eneo hilo, ambalo ni muhimu kwenye maendeleo ya shughuli mbali mbali za kiuchumi.
Vile vile, alisema ifikapo mwezi Machi mwakani Kituo Kikuu cha Kupoza umeme cha Imalilo kilichopo wilaya ya Bariadi, mkoani humo nacho kitakuwa kimekamilika ambapo kitawezesha wananchi wa Mkoa huo na maeneo ya jirani kupata umeme wa uhakika na wakutosha kwa ajili ya matumiza ya kawaida  na Viwanda vilivyopo mkoani humo.
Aidha, alisema kuwa, Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 4 kwa Mkoa huo ambazo zinatumika kwa ajili ya kufanya ukarabati wa miundombinu ya umeme iliyoharibika na kusambazia umeme katika maeneo ambayo bado hayajapata umeme.
Eneo la Kituo cha Kupokea na Kutawanya Njia kuu za Umeme kilichopo katika eneo la Ng’ami  wilayani Bariadi mkoani Simiyu. 

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka aliishukuru Serikali kwa kazi kubwa inayofanya ili kuhakikisha umeme unapatikana nchi nzima.
 Alisema, Mkoa huo unaenda kwenye Mapinduzi ya Viwanda kwa haraka na ujio wa kituo hicho utaharakisha maendeleo ya Viwanda mkoani humo.
Waziri wa Nishati,  Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nyasosi wilayani Bariadi  kabla ya kuwasha umeme katika eneo hilo.

Aliongeza kuwa, wawekezaji waliofika mkoani Simiyu walitaka wajenge viwanda karibu na eneo ambalo lipo karibu na kituo hicho cha umeme na Serikali imeridhia ombi hilo.
Katika ziara yake mkoani humo, Waziri wa Nishati, alitembelea eneo kutakapojengwa Kituo cha Kupoza Umeme, Imalilo wilayani Bariadi na kuwasha umeme katika kijiji cha Nyasosi kilichopo wilayani humo.

Monday, December 16, 2019

BODI TISA ZA MAZAO KUUNGANISHWA ILI KUUNDA BODI TATU PEKEE - WAZIRI HASUNGA


Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza na viongozi wa vyama vya ushirika katika ukumbi wa Wilaya ya Tandahimba akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Mtwara, tarehe 13 Disemba 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Sehemu ya wakulima wa korosha wakifatilia hotuba ya Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza na viongozi wa vyama vya ushirika katika ukumbi wa Wilaya ya Tandahimba akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Mtwara, tarehe 13 Disemba 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza na viongozi wa vyama vya ushirika katika ukumbi wa Wilaya ya Tandahimba akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Mtwara,  tarehe 13 Disemba 2019.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mtwara

Serikali imedhamiria kuziunganisha Bodi sita za mazao zilizopo chini ya Wizara ya Kilimo na kuwa na Bodi tatu ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo tarehe 13 Disemba 2019 wakati akizungumza na viongozi wa vyama vya ushirika katika ukumbi wa Wilaya ya Tandahimba akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Mtwara.

Waziri Hasunga amesema kuwa kumekuwa na Bodi nyingi lakini matokeo ya kiutendaji hayaakisi wingi huo hivyo ili kuboresha majukumu yake na kuwa na weledi katika kazi Bodi hizo zitaunganishwa.

Amesema kuwa Bodi saba zitaunganishwa na kuunda Mamlaka moja ya kusimamia mazao ya kimkakati ambayo ni pamoja na Kahawa, Pamba, Mkonge, Tumbaku, Pareto, Korosho, Alizeti na zao la mchikichi.

Waziri Hasunga amesema kuwa mabadiliko hayo yatakayozihusisha Bodi hizo yatapelekea kuundwa kwa idara za kusimamia kila zao.

Bodi nyingine ya pili itasimamia mazao ya nafaka, mboga mboga na matunda (Cereal and Horticulture Authority) pamoja na Bodi ya Sukari itakayosalia kujitegemea.

Amesema, kuwa na Bodi nyingi kumepelekea usimamizi kuwa mgumu kadhalika kuwa na Bodi chache kutaimarisha ufanisi na uwezo wa kuwasimamia watendaji wake.

Sambamba na hayo Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amesema kuwa Wizara ya Kilimo ipo katika mchakato wa kupitia upya sheria ya Ushirika pamoja na Shirika la ukaguzi wa vyama vya Ushirika-COASCO ili kuimarisha sheria na kuwa na usimamizi madhubuti wa mali za wananchi kwenye Ushirika.

Waziri Hasunga yupo mkoani Mtwara kwa ajili ya ziara ya kikazi ambapo awali alitembelea mkoa wa Pwani na Lindi kwa ajili ya kukagua hali ya uuzaji wa korosho msimu wa 2019/2020, kukagua hatua zilizofikiwa za malipo ya wakulima wa korosho zilizonunuliwa na serikali msimu wa mwaka 2018/2019 na kukagua skimu za umwagiliaji.


Wednesday, December 11, 2019

WATANZANIA TUNA RAHA SANA: Hotuba ya Rais John Magufuli Watanzania Tunaw...



  • Hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano, N ujenzi wa ukuta kwenye eneo la migodi ya madini ya Tanzanite Mirerani, kuanzishwa kwa masoko ya madini kwenye mikoa na wilaya nchi nzima na kuundwa kwa mifumo ya kisasa ya kijiditali ya kurekodi mapato ambayo licha ya kuongeza mapato, lakini pia imeongeza ufanisi.

  • Mei 2019 sekta ya madini kwa kipindi cha miezi kumi na moja ya mwaka wa fedha 2018/19 mapato yamefikia Shilingi bilioni 302.63 kiasi ambacho ni zaidi ya mapato yote kiasi cha Shilingi bilioni 301.6 yaliyopatikana kwenye mwaka wa fedha 2017/18.

  • Mapato kwenye sekta ya madini katika kipindi cha miaka minne yamekuwa yakiongezeka mfululizo, akitolea mfano amesema mwaka 2016/17 makusanyo ya maduhuli yalikuwa bilioni 214.5 wakati mwaka 2015/16 maduhuli yalikuwa Shilingi Bilioni 210 na mapatao ya mwaka 2017/18 yalikuwa Shilingi bilioni 301.6

Tuesday, December 10, 2019

MHANDISI MTIGUMWE AAGIZA BODI NA WATENDAJI WA SACCOS KUWASILISHA RASIMU ZA TAARIFA ZA FEDHA KWA WAKAGUZI WA NJE COASCO KABLA YA JANUARI 31, 2020


Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe ameiagiza Bodi na Watendaji wa SACCOS kuwasilisha Rasimu za Taarifa za Fedha kwa Wakaguzi wa Nje (COASCO) kabla au ifikapo tarehe 31.01.2020.

MHandisi Mtigumwe ametoa agizo hilo Jijini Dodoma ambapo amesema kuwa ni lazima kuwasilisha mapema taarifa hizo ili Ukaguzi uweze kufanyika kwa wakati na Taarifa za Ukaguzi ziwasilishwe kwa Mamlaka husika ndani ya muda uliopangwa Kisheria.

Amewataka wanachama wote wa SACCOS hususani Bodi na Watendaji wa SACCOS nchini kuwa, matakwa ya Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018 (The Microfinance Act 2018), kuhusu ukaguzi wa nje hivyo ni lazima kutekeleza agizo hilo kwa wakati.

“SACCOS zote zinatakiwa kuhakikisha kuwa Taarifa za Fedha za Mwaka 2019 ziwe zimekaguliwa na kuwasilishwa Benki Kuu au kwa Mamlaka iliyokasimiwa ambayo ni Mrajis wa Vyama Vya Ushirika ifikapo tarehe 30 Aprili, 2020” Alisema .Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma


Sunday, December 8, 2019

WAZIRI MKUU, KASSIM MAJALIWA, AMWAKILISHA RAIS KWENYE MAZISHI YA KAKA WA MAMA MARIA NYERERE MUSOMA


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Mama Maria Nyerere, kwenye mazishi ya Kaka yake, Mzee Inyasi Gabriel, aliyefariki tarehe 4.12.2019, huko Musoma, mkoani Mara, Desemba 7, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akimpa mkono wa pole Mama Maria Nyerere, kwenye msiba wa Kaka yake, Mzee Inyasi Gabriel, aliyefariki tarehe 4.12.2019, huko Musoma, mkoani Mara, Desemba 7, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiweka udongo, kwenye kaburi la Kaka wa Mama Maria Nyerere, Mzee Inyasi Gabriel, aliyefariki tarehe 4.12.2019, huko Musoma, mkoani Mara, Desemba 7, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Thursday, December 5, 2019

TUPO KWENYE MKAKATI WA KUBORESHA KILIMO KUPITIA ASDP II - WAZIRI HASUNGA

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza matumizi ya zana za kilimo wakati akizungumza kwenye Kongamano la tatu la kilimo na mifugo lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Mkoani Morogoro, jana tarehe 4 Disemba 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo mbele ya Ndg Ramadhan Majubwa ambaye ni Mratibu wa shamba la mfano la mafunzo  ya kilimo katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine kwenye Kongamano la tatu la kilimo na mifugo lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Mkoani Morogoro, jana tarehe 4 Disemba 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua shamba la mfano la mafunzo ya kilimo katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine kwenye Kongamano la tatu la kilimo na mifugo lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Mkoani Morogoro, jana tarehe 4 Disemba 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza matumizi ya zana za kilimo wakati akizungumza kwenye Kongamano la tatu la kilimo na mifugo lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Mkoani Morogoro, jana tarehe 4 Disemba 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua Viuatilifu wakati alipotembelea Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine kwenye Kongamano la tatu la kilimo na mifugo lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Mkoani Morogoro, jana tarehe 4 Disemba 2019.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Morogoro

Serikali imesema kuwa imejipanga kuhakikisha kuwa inawawezesha wakulima kuboresha sekta ya kilimo kupitia mpango kabambe uliobuniwa na serikali wa kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili-ASDP II.

ASDP awamu ya pili imejikita katika kuboresha kilimo kuwa chenye tija ili kuimarisha kipato cha wakulima nchini hivyo kupitia programu hiyo wakulima watanufaika na mafunzo yatakayotolewa na wataalamu wa kilimo ikiwa ni pamoja na matumizi sahihi ya zana bora za kilimo

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo jana tarehe 4 Disemba 2019 wakati akihutubia kwenye Kongamano la tatu la kilimo na mifugo lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Mkoani Morogoro.
Amesema kuwa maendeleo ya kilimo katika nchi yoyote Duniani yanategemea teknolojia bora na za kisasa kwani matokeo ya teknolojia duni ndio yaliyopelekea kukosekana kwa kilimo bora.

Amesema kuwa Programu ya kuendeleza kilimo awamu ya pili ASDP II ina malengo matatu mahususi ambayo ni pamoja na kuwa na usimamizi bora wa ardhi, Uongezaji wa thamani wa mazao na Kuongeza tija na uzalishaji ili kuwa na matumizi sahihi ya mbegu bora, Viuatilifu, Mbolea na zana bora za kilimo.

Waziri Hasunga, amesema kuwa zaidi ya asilimia 80 ya watanzania wanalima kilimo cha hasara badala ya kulima kilimo cha kibiashara chenye tija na uzalishaji mkubwa hivyo programu hiyo itakuwa muarobaini wa maboresho ya sekta ya kilimo.

Waziri Hasunga amekipongeza Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Mkoani Morogoro kwa kutoa mafunzo ya teknolojia za kisasa kwa wakulima ambao kwa kiasi kikubwa wakulima wameendelea kunufaika na mafunzo hayo.


WIZARA YAFUNGUA DAWATI MASHULENI MKOANI RUKWA KUTOKOMEZA UKATILI KWA WATOTO

Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na Mkoa wa Rukwa imefungua Madawati ya watoto kwa baadhi ya Shule za Msingi na Sekondari katika Manispaa ya Sekondari kwa lengo la kupambana na ukatili dhidi ya Watoto ikiwemo mimba za utotoni.
Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia masuala ya watoto kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Bw. Sebastian Kitiku akiongea na wanafunzi wa shule za Msingi Chem chem na Lukewile zote Manispaa ya Sumbawanga ameutaja Mkoa wa Rukwa kuwa na changamoto kubwa ya mimba za utotoni.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Watoto kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Bw. Sebastian Kitiku akifafanua jambo kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kilimani Maweni iliyoko nje kidogo ya mji wa Sumbawanga wakati wa ufunguzi wa Dawati la Jinsia Shuleni mapema jana shuleni hapo.

Aidha Bw. Kitiku amewataka watoto shuleni hapo kulitumia Dawati  la Watoto Shuleni hapo ipasavyo ili liweze kuwa masaada mkubwa kwa wanafunzi wanaokumbana na vitendo vya ukatili na kuwataka kutokuwa waoga wa kutoa taarifa ili kuwawezesha walimu wa malezi shuleni hapo kuweza kuangalia namna bora ya kulifanyia kazi taio hilo.
 Bw. Kitiku ameongeza kuwa watoto wanatakiwa kupewa haki zote kama ilivyo kwa watu wazima akizitaja haki hizo kuwa haki ya kulindwa, haki ya kuendelezwa, Afya, kutobaguliwa na kushirikishwa kama ilivyobainishwa katika Sera ya Taifa ya Mtoto ya Mwaka 2008. 

Uongozi wa Shule ya Msingi Chemchem, Wizara pamoja na Mkoa wakiwa katika ya pamoja na wanafunzi wa wateule wa Dawati la Jinsia wakati wa ufunguzi wa Dawati la Jinsia Shuleni mapema jana shuleni hapo.

Aidha Mkurugenzi huyo amewataka watoto hao kutoa taarifa katika Dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi lakini pia kutumia mtandao wa simu ya bure ya 116 ili kuweza kupewa msaada wa haraka pindi watakapobaini kuwa wanafanyiwa vitendo vya ukatili ambavyo amevitaja kuwa ulawiti na ubakaji, kazi ngumu kwa watoto pamoja na utumikishwaji watoto manyumbani kwa maana ya ukatili wa kingono na kimwili.
Dwati la watoto katika shule hizo limefanyika kwa wanafunzi husika kuchagua wawakilishi wao ndani ya Dawati lakini pia wanafunzi hao baada ya kuelimishwa pia wamewachagua walimu ambao wanawaamini kuwa walezi hao ambao kimsingi watafanya kazi kwa karibu sana na Dawati la Jinisia shuleni hapo.
Mkurugenzi Msaidizi  Idara ya Watoto kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Bw. Sebastian akiwa katika picha ya pamoja  na wanafunzi waliochaguliwa kuunda Dawati la Jinsia katika Shule ya Sekondari Kilimani Maweni iliyoko nje kidogo ya mji wa Sumbawanga wakati wa ufunguzi wa Dawati la Jinsia Shuleni mapema jana shuleni hapo.
 Zoezi la uanzishwaji Dawati la Watoto shuleni pia limefanyika shule ya Sekondari Kilimani Maweni iliyoko nje kidogo ya mji wa Sumbawanga na Wizara kwa kushirikiana na uongozi wa shule na mkoa wameongoza wanafunzi shuleni hapo kuchagua wawalilishi wao wa Dawati lakini pia wamechagua walimu wawili kuwa walimu wa malezi shuleni hapo.
Mkurugenzi Msaidizi  Idara ya Watoto kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Bw. Sebastian Kitiku akishirikiana na Mwakilishi wa  Afisa Elimu Mkoa wa Rukwa Bi.Matinda Mwinuka kuunda Dawati la Jinsia la  wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kilimani Maweni iliyoko nje kidogo ya mji wa Sumbawanga wakati wa ufunguzi wa Dawati la Jinsia Shuleni mapema jana shuleni hapo.

Wataalam wa Wizara ya Afya Idara Kuu Mawendeleo ya Jamii wako Mkoani Rukwa kushirikiana na Mkoa huo katika juhudi zake za kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na mkoa ni miongoni mwa mikoa yenye kiwango cha juu Kitaifa kuwa na idadi kubwa ya mimba za utotoni.  

Wednesday, December 4, 2019

UONGOZI WA JIJI LA ZANZIBAR WAJIPANGA KUSIMAMIA VIPAUMBELE VYA USAFI WA MAZINGIRA


Uongozi wa Jiji la Zanzibar umejipanga kusimamia vipaumbele vyote vya usafi wa mazingira ili hadhi ya  kuwa na  jiji liendane na vitendo vya mazingira yalio safi na salama.



 Hayo yameelezwaa na Mkurugenzi wa jiji Ndugu Ali Khamis Juma baada ya shughuli ya uchaguzi wa kumchangua mstahiki Meya wa Baraza la jiji la Zanzibar na Naibu wake.



Hakimu wa mahakama ya mkoa Makame Mshamba amewaapisha wajumbe wa baraza la jiji,mstahiki Meya na naibu meya wa baraza la jiji la Zanzibar hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Karikoo.



Akizungumza mara baada ya hafla hiyo Mkurungezi wa  jiji la Zanzibar amesema  baraza lake litafanya kazi kwa karibu na wajumbe wa baraza hilo ili kuona dhamira na malengo ya kuanzishwa kwake yanafikiwa ikiwa ni pamoja na kuyasimamia mabaraza ya manispaa ya Mkoa wa Mjini Magharibi.



Aidha Mkurugenzi Ali amesema Serikali inamatarajio makubwa na baraza hilo katika kuona yanakuwepo mabadiliko makubwa katika miji na manispaa za Zanzibar hususani katika usafi wa mazingira na miundombinu ikiwemo ya barabara.



Nae mstahiki  Meya wa Jiji la Zanzibar Saleh Juma Kinana amekishukuru Chama Cha Mapinduzi kwa kumuamini na kumpa zamana na ridhaa ya kukiwakilisha chama hicho katika nafasi hiyo mpya ya meya wa jiji la Zanzibar.

 baadhi  ya  wajumbe  wamesema  kuwa  watashirikiana  kwa  pamoja  katika  kufanya  kazi   zenye  maendeleo  hususani  katika  suala  la  kufanya  usafi  wa  mazingira  katika  mji.

WASHIRIKI 225 KUSHIRIKI KONGAMANO LA SITA LA DIASPORA ZANZIBAR


Zaidi ya washiriki 225 wanatarajiwa kuhudhuri  katika kongamano la 6 la Diaspora litakalofanyika terehe 14-15 Disemba 2019 katika   Visiwani Zanzibar .
Akizungumza  na  waandishi wa habari  Waziri  wa  Nchi  Ofisi  ya  Rais  na Mwenyekiti  wa Baraza  la Mapinduzi  Issa  Haji  Gavu  katika  ukumbi  wa  raha leo  mjini  Unguja .
Amesema  Serikali  ya Mapinduzi  ya  Zanzibar  imeeandaa kongamano  kwa  ajili  ya  washiriki  hao  ambapo lengo  kuu ni  kuwashajihisha  watanzania  walipoo nje  kuja  kuwekeza  na  kuleta  maendeleo  katika  nchi yao.
Aidha  Waziri   Gavu  amesema kufanyika  kwa  kongamano  hilo ni kuwepo kwa  amani  na  utulivu na  ushiriki  Zanziabr unaopelekea  kuzidi kufanyika kwa kongamano hilo Visiwani  Zanzibar

Sunday, December 1, 2019

MKOA WA MARA WAJENGA HOSPITALI 4 ZA WILAYA NA VITUO VYA AFYA 13

Serikali imeuwezesha mkoa wa Mara kujenga Hospitali 4 za Wilaya, Vituo vya Afya 13 kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Akizungumza katika kipindi cha ‘TUNATEKELEZA’ Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam Malima amesema mkoa huo umepiga hatua kubwa katika kuimarisha huduma mbalimbali za jamii ikiwemo sekta ya afya kutokana na kutekelezwa kwa ujenzi wa miundombinu ya sekta hiyo kwa ufanisi.

“Mradi wa Hospitali ya Kanda ya Mwalimu Nyerere unaendelea vizuri na utawezesha wananchi kupata huduma za kibingwa ikiwemo za mifupa na nyingine hali itakayoondoa adha ya wananchi kusafiri hadi Hospitali ya Bugando kufuata huduma hizo” Alisisitiza Malima.
Akifafanua amesema kuwa mkoa huo umepata mafanikio makubwa katika sekta nyingine kama vile elimu kwa kujenga miundombinu ya kisasa yakiwemo madarasa na maabara hali iliyochangia kukua kwa kiwango cha elimu katika mkoa huo ikilinganishwa na miaka iliyotangulia kabla ya uwekezaji huo.
Kwa upande wa sekta ya madini amesema kuwa kuwepo kwa sheria nzuri na taratibu zilizowekwa na Serikali ya Awamu ya Tano, mkoa huo umezalisha kilo 130 za dhahabu kufikia Septemba mwaka huu hali inayochangia kukuza sekta ya madini na uchumi kwa ujumla.
Akizungumzia mikakati yake ya kukuza kilimo na uvuvi, Mhe. Malima amesema kuwa dhamira ya mkoa huo ni kuona sekta hizo zinatoa mchango stahiki katika uchumi kutokana na hatua zilizochukuliwa katika kokomesha uvuvi haramu katika mkoa huo.
Aidha, Mhe. Malima amebainisha kuwa wamejipanga kukuza sekta ya utalii katika mkoa huo ili kuongeza pato la mkoa huo hatua itakayowasaidia kuwainua wananchi kiuchumi na Taifa kwa ujumla.
Kipindi cha ‘TUNATEKELEZA’ kinarushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na kuratibiwa na Idara ya Habari MAELEZO ambapo awamu hii inawashirikisha wakuu wa mikoa yote Tanzania Bara.