Matokeo chanyA+ online




Friday, December 20, 2019

KATIBU MKUU MWALUKO AWATAKA WATAALAM WA MAAFA KUTUMIA FURSA ZA MAFUNZO KWA MATOKEO CHANYA


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu na Uwekezaji, Dorothy Mwaluko amewataka wataalam wa masuala ya Maafa nchini kutumia fursa za mafunzo ya masuala ya maafa kwa kuhakikisha wanaleta tija katika kukabili majanga ya mafuriko na ukame.
Ametoa kauli hiyo Desemba 18, 2019 alipokuwa akifungua warsha ya mafunzo ya siku tatu kuhusu upunguzaji wa madhara ya janga la mafuriko na ukame yaliyofanyika Jijini Dodoma iliyoandaliwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza Madhara ya Maafa ya kwa kushirikiana na Idara ya Menejimenti ya maafa Ofisi ya ofisi hiyo.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji) Bi. Dorothy Mwaluko akihutubia wakati wa warsha ya mafunzo kuhusu upunguzaji wa madhara ya janga la mafuriko na ukame iliyofanyika kuanzia tarehe 18 hadi 20 Desemba, 2019 katika Ukumbi wa Mikutano wa Dodoma Hotel Jijini Dodoma. 
Mwaluko aliwataka wataalam hao kutumia fursa za mafunzo kuhakikisha wanaandaa taarifa za wasifu wa nchi utakao bainisha maeneo yenye mafuriko na ukame ili kuwa msaada kwa vizazi vijavyo.
 “Taarifa hizi mnazoandaa hakikisheni mnawafikia walaji kwa kuzingatia matumizi sahihi ya lugha rahisi yenye kueleweka kwa walengwa ili kuwa na taarifa sahihi kuhusu masuala ya menejimenti ya maafa,”alieleza Mwaluko.
Aliongezea kuwa, wanapaswa kuifikia jamii kwa vitendo na si kushiriki katika vikao na warsha zisizoleta tija kwa kukosa matokeo chanya.
 “Hakikisheni mnatumia fursa ya warsha hii kuchakata vyema taarifa hizi ili kuleta matokeo chanya katika jamii yenye matarajio makubwa na Serikali yake,”alisisitiza Mwaluko.

Mwezeshaji wa masuala ya maafa kutoka Taasisi ya Tafiti ya CIMA Bw. Roberto Rudari akiwasilisha mada kuhusu masuala ya menejimenti ya maafa wakati wa mafunzo hayo.

Aidha alifafanua kuwa, wataalam hao wanawajibu wa kutumia ujuzi wao katika kutoa taarifa sahihi kwa wakati kwa kuzingatia athari za ukame na mafuriko nchini na kuwataka kuacha kutumia majukwaa ya makongamano kujifunza pekee pasipo kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi.
“Ni Lazima tufike mahali tuwe watekelezaji na si wazungumzaji, kwa kukaa kwenye viti vizuri wakati watumiaji wanaangamia hivyo ni lazima mkitoka katika mafunzo haya mje na mikakati inayofikika katika kukatua changamoto hizi za majanga nchini,”Alisisistiza
Kwa upande wake mwakilishi kutoka Taasisi ya Utafiti ya CIMA Bw. Roberto Rudari alieleza lengo la kuwakutanisha wataalam hao ni kuhakikisha wanawajengea uwezo juu ya masuala ya kuzuia madhara yatokanayo na majanga ya ukame na mafuriko kwa kuzingatia Tanzania ni miongozni mwa nchi zinazokubwa na aina hizo za majanga.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji) Bi. Dorothy Mwaluko (wa tatu kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya upunguzaji wa madhara ya janga la mafuriko na ukame yaliyoandaliwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza Madhara ya Maafa ya UNDRR kwa kushirikiana na Ofisi yake Jijini Dooma. 
Alifafanua kuwa, taarifa hizi zitaisaidia nchi kuhakikisha wanaweka mazingira rafiki yenye lengo la kuratibu na kukakikisha majanga hayo yanapungua nchini.
Naye mtaalam wa masuala ya maafa kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. James Hela alieleza ni vyema taarifa za masuala ya majanga zikatolewa kwa wakati ili kusaidia kujipanga na kuhakikisha jamii haipati madhara ya majanga hayo.
“Kwa sasa kuna mabadiliko ya tabia nchi na ni vyema taarifa hizi zikaandaliwa kwa lugha rafiki na kuhakikisha inawafikia walengwa ili kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya Tano katika kuwatumikia Watanzania,”alisema Hela.
Aidha, Mhadhiri kutoka Idara ya Jiografia na Stadi za Mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma Dkt. Wilhelm Kiwango alipongeza jitihada za ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuandaa mafunzo hayo kwani yameongeza uelewa wa jumla juu ya vihatarishi na maeneo yanayoathiriwa na maafa na kutoa wito kwa Serikali kuendelea kutoa elimu hiyo katika ngazi zote na umma kwa ujumla.
“Mafunzo haya yametufaa, ni vyema yakatolewa katika ngazi zote na kusaidia kuongeza uelewa hususan kuimarisha mtaala wa elimu ya maafa ngazi zote hadi vyuo vikuu,”alieleza Dkt. Kiwango

DKT KALEMANI AITAKA TANESCO KUBAINI VYANZO VIPYA YA UMEME

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani  (katikati) akiwa kwenye kikao chake na  Bodi/Menejimenti ya TANESCO kilichofanyika jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu na kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Dkt. Alexander Kyaruzi.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ameiagiza Bodi na Menejimenti ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha kuwa wanafanya tafiti kubaini vyanzo vipya vya uzalishaji umeme ili kuongeza kiasi cha nishati hiyo nchini na kuweza kufikia lengo la kuwa na megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu na Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga wakiwa kwenye kikao chao na Bodi na Menejimenti ya TANESCO kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
“Lazima tufanye tafiti kubaini vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme ukiacha hivi vilivyopo, hata kama tusipotekeleza leo, vizazi vijavyo vitatekeleza miradi hiyo, mfano tafiti za mradi wa umeme wa Julius Nyerere (MW 2115) zilifanyika miaka mingi iliyopita, lakini mradi tunautekeleza sasa, hivyo nasi hatuna budi kuibua vyanzo vingine.” Alisema
Aidha, Dkt Kalemani aliiagiza Bodi na Menejimenti ya TANESCO kuhakikisha kuwa maeneo yote nchini yanaunganishwa na umeme wa Gridi ifikapo mwezi Juni 2022 ili wananchi wapate umeme wa uhakika na pia Serikali kuokoa fedha zinazotumika kununulia Mafuta ili kuendesha mitambo ya umeme kwenye baadhi ya maeneo nchini.
Kuhusu kazi ya usambazaji umeme vijijini, alisisitiza kuwa lengo la Serikali ni kufikisha umeme kwenye vijiji vyote ifikapo mwezi Juni mwaka  2021 na asilimia 85  ya wananchi wanapata umeme hivyo TANESCO ina jukumu la kuhakikisha kuwa lengo hilo linafanikiwa.
Vilevile, Dkt Kalemani aliiagiza TANESCO kuhakikisha kuwa, kila kiwanda au Taasisi ya umma inapojengwa, inafikishiwa umeme lengo likiwa ni kuongeza mapato ya Shirika na pia kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii nchini.
Aidha, aliiagiza Bodi na Menejimenti ya TANESCO kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Shirika kutoka shilingi Bilioni 46 zinazokusanywa sasa kwa wiki hadi kufikia Bilioni 52 kwa Wiki.
Dkt. Kalemani aliongeza kuwa, Shirika hilo pia linapaswa kumaliza madeni yake ifikapo mwaka 2026, linaboresha nidhamu ya watumishi ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi na kuhakikisha kunakuwa na mpango wa ukarabati wa miundombinu ya umeme kwenye maeneo yote nchini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, pamoja na kuipongeza TANESCO kwa majukumu mbalimbali wanayofanya, aliiagiza Bodi kujielekeza pia kwenye ukusanyaji wa madeni ya TANESCO kutoka kwa wateja mbalimbali zikiwemo Taasisi za umma kwani fedha zitakazopatikana zitasaidia Shirika kuweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani  (katikati) akiwa kwenye kikao chake na  Bodi/Menejimenti ya TANESCO kilichofanyika jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu na kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Dkt. Alexander Kyaruzi.
Aidha, aliiagiza TANESCO kuangalia suala la malipo ya huduma ya umeme ili kuwe na utaratibu wa malipo hayo kufanyika kwa awamu ili kuweza kuunganishia umeme wananchi wengi zaidi na hivyo miradi hiyo ya umeme kuleta tija.
Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga, alisema kuwa, hali ya umeme nchini imeimarika hivyo TANESCO inapaswa kujikita pia kwenye kazi ya kuongeza wateja wa nishati hiyo ili kuongeza mapato.
Vilevile, alisisitiza kuhusu suala la mikoa yote nchini kuunganishwa na gridi ya Taifa ili kuimarisha hali ya umeme kwenye mikoa hiyo.

Thursday, December 19, 2019

SIMBACHAWENE ATEMBELEA OFISI ZA MAKAMU WA RAIS ZA ZANZIBAR

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene akipokewa na Mratibu wa shughuli za Muungano Ofisi ya Makamu wa Rais Othman Kassim Haji mara baada ya kuwasili katika Ofisi za Makamu wa Rais zilizopo Tunguu, Zanzibar ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo Pemba.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili Ofisi ya Makamu wa Rais iliyopo Tunguu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene (katikati) akiongozwa na Afisa Utumishi, Bakari Maulid Bakari (kulia) kutembelea Ofisi za Makamu wa Rais  zilizopo Tunguu, Zanzibar ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo Pemba. Kushoto ni Mhasibu kutoka Ofisi hiyo Mohamed Said Mwinyi.

Afisa Utumishi Ofisi ya Makamu wa Rais ya Zanzibar Bakari Maulid Bakari (wa pili kushoto) akitoa maelezo kuhusu shughuli za ofisi hiyo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene. Wengine kushoto ni Mhasibu Mohamed said Mwinyi na kulia ni Mratibu Othman Haji.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene akiagana na baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais iliyopo Tunguu, Zanzibar kabla ya kuelekea Pemba kwa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo.

MHANDISI NYAMUHANGA APONGEZA KITUO CHA AFYA MAZWI SUMBAWANGA

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamuhanga amepongeza juhudi zinazofanywa na watumishi kituo cha afya cha Mazwi, Manispaa ya Sumbawanga baada ya kuona namna wanavyokabiliana na ongezeko la wateja wanaohitaji huduma za afya katika kituo hicho ambacho huzalisha wajawazito wapatao 373 kwa mwezi.
Amesema kuwa kabla ya hapo kituo hicho kilikuwa kidogo sana na kushindwa hata kutoa huduma za upasuaji jambo ambalo lilipelekea hospitali ya rufaa ya mkoa kuzidiwa na wagonjwa lakini hali hiyo kwa sasa ni tofauti baada ya upanuzi wa kituo hicho ambacho kutokana na huduma zake wateja wengi huvutiwa kufika na kupata huduma.
 Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamuhanga

Amesema kuwa serikali inatoa fedha nyingi kupata dawa pamoja na vifaa tiba hivyo kinachotegemewa katika kituo hicho ni huduma bora ya afya na kuongeza kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli imejenga vituo vya afya zaidi ya 352 ambapo mojawapo ya vituo hivyo ni kituo cha afya cha Mazwi katika Makispaa ya Sumbawanga ambapo walipatiwa shilingi milioni 500 na sasa kituo hicho kimekamilika na kuanza kutoa huduma.
“Nimefurahishwa kwa upanuzi ambao umefanyika katika kituo hiki cha Mazwi, kilikuwa kituo kidogo tu nakumbuka siku za nyuma lakini kimekarabatiwa kimekuwa kituo kizuri na kinapendeza lakini kitu cha kufurahisha ni kwamba kinahudumia wateja wengi lakini na huduma inayotolewa hapa nimetoka kukagua katika maeneo mbalimbali katika wodi kwakweli nimeridhika na huduma ambazo zinatolewa, changamoto ni kwamba wameongezeka wateja baada ya ukarabati kufanyika, tunashukuru wataalamu wetu wanajitahidi kuwahudumia,” Alisema.
Wakati akitoa taarifa ya kituo cha Afya cha Mazwi Mganga Mkuu wa halmashauri ya manispaa ya Sumbawanga Dkt. Archie Hellar alisema kuwa kuanzia mwezi Januari hadi Novemba kituo hicho cha afya kimezalisha wajawazito 4,103 na kati ya hao waliofanyiwa upasuaji ni wajawazito 426 na kupatikana vifo viwili kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo katika harakati za kuwafanyia wajawazito hao upasuaji..
“Kwajhiyo changamoto tunazozipata ni kwamba wateja ni wengi zaidi wanaichukulia hospitali hii ni kama ya mkoa na wengine wanatoka nje ya manispaa n ahata nje ya Wilaya nyingine kuja kujifungua hapa, sasa ukilinganisha watumishi pamoja na rasilimali fedha unakuta kituo kinaelemewa, lakini hata hivyo tunajitahidi kwa kushirikiana na Mkurugenzi wetu wa manispaa Jacob Mtalitinya kwakweli anatiupa nguvu na kutusaidia sana kufanikisha kutoa huduma,” Alisema.
Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga ilipata shilingi milioni 500 za kupanua ujenzi wa kituo cha Afya cha Mazwi pamoja na kupewa shilingi milioni 400 kwaajili ya ujenzi wa kituo cha Afya kipya kilichopo katika kata ya Katumba azimio ikiwa ni kilometa 12 kutoka katika kituo cha afya cha Mazwi.

HOSPITALI ZA WILAYA 67 KUFANYIWA TATHMINI JUU YA MAENEDELEO YA UJENZI WAKE

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamuhanga amesema kuwa  Ofisi ya Rais inaendelea kufanya tathmini kwa hospitali zote 67 kuhakikisha kwamba shilingi bilioni 100.5 ambazo zilitolewa kwa ujenzi wa hospitali hizo kuwa zimetumika vizuri.
Haya ni baadhi ya majengo yaliyojengwa katika hospitali ya wilaya ya kilolo mkoani Iringa ambayoWaziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo ameridhishwa na kasi ya ujenzi wake

Alisema kuwa serikali ya awamu ya tano imejenga hospitali 67 nchini na mkoa wa Rukwa umejengewa hospitali tatu za wilaya ambapo Mhandisi Nyamuhanga aliweza kutembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kalamnbo, katika mji mdogo wa Matai iliyopokea shilingi Bilioni 1.5 lakini hakuridhishwa na ujenzi wa hospitali hiyo.
 “Kwa halmashauri ambazo fedha hizi zitakuwa hazijatumika vizuri kwakweli tutachukua hatua na katibu tawala wa mkoa kama nilivyoagiza jana, najua kuna vifaa ambavyo tayari vimeshanunuliwa pale ambavyo bado havijawekwa, havijajengwa kwa mfano maru maru na vifaa vingine uhakikishe kwamba kazi hiyo inaendelea ili vifaa hivyo vikishawekwa tuvitathmini sasa kiwango cha ukamilishaji wa hospitali ile ya halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kabla hatujafikiria kutoa fedha nyingine za kukamilisha,” Alisema.
Ameongeza kuwa halmashauri hiyo ya Kalambo imetaja mahitaji ya shilingi milioni 700 ili kuweza kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo jambo ambalo Mhandisi Nyamuhanga hakukubaliana nalo kutokana na tathmini iliyofanywa ya mahitaji ya fedha walizotoa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hizo kuwa yangebaki mambo machache ambayo yasingeweza kuzidi shilingi milioni 300 na kuongeza kuwa anahitaji maelezo ya ziada kutoka katika halmashauri hiyo ambayo hospitali yake imefikia ukamilifu wa asilimia 76 ambacho ni kiwango cha chini cha ukamilishaji.
Katika hatua nyingine amesema kuwa mwezi Aprili mwaka 2019 Ofisi ya Rais TAMISEMI ilitoa shilingi milioni 400 kwaajili ya upanuzi wa Zahanati ya Kijiji cha Samazi katika halmashauri ya Wilaya ya Kalambo ambapo zahanati hiyo inapandishwa hadhi na kuwa kituo cha Afya lakini amesikitishwa na malumbano yanayoendelea katika kijiji hicho juu ya eneo la ujenzi wa kituo hicho jambo lililopelekea kushindwa kuanza kwa ujenzi huo.
“Ofisi ya Rais TAMISEMI imetoa maelekezo kwamba upanuzi ufanyike katika eneo la zahanati iliyopo iongezewe majengo ili kiwe kituo cha afya cha Samazi kiweze kukamilika ili kiweze kufanya kazi, tusiendelee na malumbano tena tumeshatoa maamuzi kwamba upanuzi ufanyike pale kwenye zahanati ili tukipandishe hadhi ikiwe kituo cha afya, tunategemea kazi hiyo ianze mara moja na ikamilike ndani ya miezi mitatu,” Alisisitiza.

TANZANIA MBIONI KUPATA CHETI CHA NCHI ZENYE VIGEZO VYA KUDHIBITI RASILIMALI KUTOTUMIKA KUENDELEZA MACHAFUKO

Imeelezwa kwamba ndani ya Miaka miwili ijayo Tanzania inatarajiwa  kupata Cheti Maalumu kitakachoitambulisha kuwa ni nchi iliyokidhi Vigezo vya nchi! zinazotumia rasilimali zinazopatikana nchini kuepusha machafuko kwa nchi wanachama. 

Cheti hicho kitaiwezesha nchi kutathmini na kuruhusu Madini ya Bati (tin), dhahabu kuuzwa nje ya nchi yakiwa yametambuliwa na kuthaminiwa
 
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akiongoza Sekretarieti iliyofanya tathmini ili kujiridhisha na endapo Tanzania inaweza kupewa cheti ili kuwa miongoni mwa nchi zinazokidhi vigezo kuwa miongoni mwa nchi zinazotekeleza makubaliano ya kutokuruhusu rasilimali za nchi kutumika kuchochea maasi wakiendelea na mazungumzo baada ya taarifa ya tathmini kuwasilishwa Jana usiku tarehe 18 Desemba, 2018 jijini Dar es Salaam 



Hayo yamebainishwa wakati wa kikao kilichoongozwa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo  tarehe 18 Desemba,  2019 jijini Dar es Salaam,  kilicholenga  kupokea ripoti juu ya tathmini iliyofanywa kwa lengo la kujiridhisha endapo Tanzania inakidhi vigezo vya kupewa cheti cha nchi wanachama zilizokidhi matakwa ya kutunza rasilimali za nchi ili zisitumike katika kusababisha na kuendeleza machafuko kwa nchi wananchama. 

Ripoti hiyo iliwasilishwa na wajumbe kutoka kwa viongozi wa sekretariati ya Jumuiya ya Nchi zilizo kwenye Maziwa Makuu wenye nchi wanachama 12 ulioundwa kwa lengo la kulinda rasilimali zinazopatikana katika nchi zao ili zisitumike katika kusababisha na kuendeleza machafuko katika nchi wanachama. 

Akizungumza katika kikao hicho,  Naibu Waziri Stanslaus Nyongo alisema anatarajia nchi za Rwanda, Uganda na Kongo zitafanya kazi kwa pamoja ili kuiwezesha Tanzania kupata cheti hicho. 
Wajumbe wakiendelea na majadiliano

Nyongo alisema kwa tathmini iliyofanywa na Sekretarieri wakati ilipokuwa  nchini, imewaonesha wazi namna Serikali ya Tanzania inavyoendesha biashara ya Madini na kuomba taarifa hiyo itumike kuharakisha mchakato wa nchi kupewa cheti hicho. 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Madini, Prof. Simon Msanjila aliwataka wajumbe kukamilisha kazi hiyo kabla ya Mwaka kuisha ili kuiwezesha Tanzania kupata cheti hicho.

Akizungumza mchakato huo, Gerard Nayuburundi mmoja Kati ya wajumbe wakiokuwa wakifanya tathmini nchini kutoka Burundi alisema wako tayari kuandaa kikao ili kuwasilisha na kujadili matokeo waliyoyapata ili kuiwezesha Tanzania kupata cheti hicho. 

Aliongeza kuwa, wamejiridhisha na namna Tanzania inavyolinda na kuwasaidia wawekezaji ili kile  walichowekeza nchini kiwe na matokeo chanya.Na Nuru Mwasampeta, DSM

Wednesday, December 18, 2019

HUU NDIO MUONEKANA WA KITUO CHA ABIRIA SOGA CHA SGR - KIMEKAMILIKA Watan...

WARATIBU WA MTUHA WATAKIWA KUIMARISHA UPATIKANAJI WA TAKWIMU SAHIHI


Waratibu wa Mfumo wa Taarifa za Utoaji wa Huduma za Afya (MTUHA) nchi wametakiwa kuimarisha upatikanaji wa takwimu sahihi za sekta ya afya  katika maeneo yao ya kazi.
Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali.Dkt. Saitole Laizer akifungua kikao kazi cha waratibu wa mfumo wa taarifa wa ufuatiliaji wa huduma za afya wa mikoa na halmashauri unaofanyika chuo cha mipango jijini Dodoma 
Rai hiyo imetolewa leo na Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali ambaye pia ni mkurugenzi wa mafunzo na rasiliamali watu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Saitole Laizer wakati akifungua  kikao kazi cha waratibu MTUHA wa mikoa na halmashauri Tanzania kinachofanyika jijina hapa.

Dkt. Saitole amesema kuwa Wizara imeboresha mfumo wa takwimu kulingana na mahitaji  ya sasa na zinaingizwa na kuchanganuliwa kwa kutumia program maalum ya kompyuta katika ngazi ya wilaya ijulikanayo  kama ‘District health information software-DHIS 2’, hivyo ana imani  watasimamia na kuratibu kwa umakini.
Waratibu hao wakimsikiliza mgeni rasmi(hayupo pichani)  wakati wa ufunguzi wa kikao kazi hicho.kinachofanyika chuo cha mipango Dodoma

Waratibu wa mfumo wa taarifa wa ufuatiliaji wa huduma za afya wakiwa kwenye makundi wakiandaa mpango kabambe wa utekelezaji
“Matarajio ya wizara ni kuwa takwimu  zinazopatikana kutoka katika program hii zitakuwa sahihi  na mtatengeneza  orodha ya kielekroniki ya vituo vya kutolea huduma  za afya  ili kusaidia  katika mipango na kutoa maamuzi katika Sekta ya Afya”.

Vile vile Dkt. Saitole aliwataka waratibu hao kuweka mipango kabambe ili kuhakikisha mrejesho wa zoezi la uhakiki  wa ubora wa takwimu za afya  uliofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali pamoja  na kutoa mafunzo ya mrejesho katika meza maalum zitakazoandaliwa ili kutoa msaada wa watumishi ambao wanahitaji kujifunza,kupata ufafanuzi au kuuliza na kupata majibu ya masuala ya MTUHA yanayowasumbua  katika maeneo ya kazi .
Mwenyekiti wa waratibu hao Dkt. Ally Msoke akitoa neno la shukrani wakati wa ifunguzi wa mkutano huo

Kaimu mkurugenzi msaidizi ufuatiliaji na tathimini kutoka wizara ya afya Tumainiel Macha  akiongea kwenye kikao kazi hicho

Picha ya pamoja ya watumishi kutoka wizara ya afya na OR-TAMISEMI na mgeni rasmi


Hata hivyo aliwataka waratibu hao kuhakikisha  halmashauri zinatenga fedha kwa ajili ya  MTUHA katika mpango kabambe wa  halmashauri(CCHP) na timu za  za afya za mikoa na halmashauri na Wadau wa Maendeleo wanashiriki kikamilifu katika kuimarisha  upatikanaji wa takwimu sahihi za Sekta ya Afya.

Mfumo wa taarifa za utoaji wa huduma za afya nchini umesaidia kuwezesha sekta ya afya kupata takwimu sahihi na kwa wakati zinazowezesha kufanya maamuzi sahihi katika kupanga na kutekeleza malengo yake ili hatimaye kufikisha huduma bora kwa wananchi kutoka asilimia 43 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 85 mwaka 2019. Na. Catherine Sungura, Dodoma

MIFUMO IKOLOJIA BORA INASAIDIA KUHIMILI MABADILIKO YA TABIANCHI – BALOZI SOKOINE


Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira Faraja Ngereageza akiongea wakati akimkaribishaMgeni Rasmi kufungua warsha hiyo ya mafunzo kuhusu kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwakutumia mifumo ya ikolojia iliyoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais na kufanyika katika ukumbi wa chuo cha Mipango jijini Dodoma
 
Mifumo ikolojia yenye afya ndio inaweza kutupatia huduma za uhakika kama chakula, maji safi na salama, kutuepusha na magonjwa, mafuriko, uharibifu wa ardhi na wakati huo huo kutuwezesha kuhimili athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu kuu Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi Joseph Sokoine ambaye alikua mgeni rasmi katika ufunguzi wa warsha ya mafunzo kuhusu kuhimili mabadiliko ya tabia Nchi kwa kutumia mifumo yaikolojia iliyofanyika katika ukumbi wa chuo cha Mipango jijini Dodoma.
 
Mgeni Rasmi katika warsha hiyo Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Balozi Joseph Sokoine akiwa katika picha ya pamoja na Washiriki waliohudhuria warsha hiyo ya mafunzo kuhusu kuhimili mabadiliko ya tabia Nchi kwa kutumia mifumo ya ikolojia iliyoandaliwa na Ofisiya Makamu wa Rais na kufanyika katika ukumbi wa chuo cha Mipango Dodoma.
 
Alisema kuwa Kukosekana kwa huduma hizo kutapelekea kushindwa kufikia malengo ya maendeleo ya milenia (Sustainable Development Goals). Hivyo mradi huu umekuja wakati muafaka wakati pia Serikali ikiendelea kukuza uchumi katika njia endelevu.

“Kama mnavyo fahamu mabadiliko ya tabianchi yameleta athari mbalimbali kwenye mazingira yetu hapa nchini. Kati ya madhara hayo ni kuharibika kwa kanda za Ikolojia Kilimo (Agro Ecolojical Zones) ambazo kwa mujibuwa tafiti kanda hizi ziko saba. Tafiti zinaonyesha kwamba ni rahisi kuhimili (Adaptation) kuliko kukabili (Mitigation)”. Alifafanua Balozi Sokoine.
 
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Balozi Joseph Sokoine ambaye ni mgeni Rasmiakiongea wakati wa ufunguzi wa Warsha ya mafunzo kuhusu kuhimili mabadiliko ya tabianchikwa kutumia mifumo ya ikolojia iliyoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais na kufanyika katikaukumbi wa Chuo cha Mipango jijini Dodoma.
Meneja wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini Bwana George Kafumu akitoa maelezo mafupi kuhusiana na mradi huo pamoja na lengo warsha hiyo iliyoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais na kufanyika jijini Dodoma.


Akimkaribisha Mgeni Rasmi Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira Bwana Faraja Ngerageza alisema kuwa warsha hiyo itawawezesha washiriki kufahamu zaidi kuhusiana na kuhimili mabadiliko ya tabia nchi kwa kutumia mifumo ya ikolojia iliyopo vijijini.

Warsha hiyo ya mafunzo ya siku tatu imeandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia mifumo ya ikolojia vijini (EBARR). Mradi huu unatekelezwa na Ofisi yaMakamu wa Rais. Warsha hiyoimehudhuriwa na Washiriki kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali, inafanyika katika ukumbi wa Mikutano wa chuo cha Mipango jijini Dodoma.
 
 
 

RAIS MAGUFULI AFUNGUA MRADI WA VISIMA VIREFU PAMOJA NA UJENZI WA MADARASA SHULE YA MSINGI CHATO A-B MKOANI GEITA



Sehemu ya Madarasa ya Shule ya Msingi Chato A-Bkama yanavyoonekana mara baada ya ujenzi wake kukamilika.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na viongozi mbalimbali akifungua moja ya mradi wa Kisima kirefu kilichojengwa katika Shule ya Msingi Chato A-B kwa ufadhili wa Emirates Red Crescent-UAE kwa usimamizi na Utekelezaji wa Balozi wa Falme za Kiarabu nchini Tanzania katika sherehe zilizofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Chato A-B Chato mkoani Geita.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi waChato katika sherehe za Ufunguzi wa Madarasa yaliyojengwa kwa mchango wake Mhe. Rais Dkt. Magufuli pamoja na mradi wa Visima virefu vya Maji vilivyojengwa na Emirates Red Crescent-UAE kwa usimamizi na Utekelezaji wa Balozi wa Falme za Kiarabu nchini
Tanzania zilizofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Chato A-B Chato mkoani Geita.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa TanzaniaMheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na walimu wa Shule ya Msingi Chato A-B mara baada ya kufungua Madarasa pamoja na Ofisi zilizojengwa kwa Mchango wake mwenyewe katika shule hiyo ambayo alisoma elimu yake ya Msingi.
PICHA NA IKULU

WAZIRI KAIRUKI AIPONGEZA TIRDO KUSAIDIA WAWEKEZAJI WADOGO


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki (kushoto) akitazama bidhaa ya nyama inavyochakatwa na kuwa soseji inayozalishwa na Kiwanda cha ORI Meat Product Ltd kilichopo Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kutembelea kiwanda hicho leo Jumatano (Desemba 18, 2019) na kujionea uzalishaji. Katikati ni Meneja Uzalishaji wa ORI Meat Product Ltd, Mitesh Dhokie.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki amelipongeza Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) kwa kuweka msukumo na mkakati endelevu wa kuwaendeleza na kuwasaidia wafanyabiashara na wawekezaji wadogo nchini.

Akizungumza na Uongozi na Wafanyakazi wa Kiwanda cha kuchakata nyama cha ORI Meat Product Ltd leo Jumatano (Desemba 18, 2019), Waziri Kairuki alisema TIRDO imeendelea kutekeleza vyema majukumu kupitia shabaha iliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika ujenzi wa viwanda unaochochea katika kukuza mnyororo wa thamani na kuleta tija iliyokusudiwa.
 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kariuki akizungumza jambo na Viongozi wa Kiwanda cha ORI Meta Product Ltd kinachochakata bidhaa ya nyama na kuwa soseji wakati alipofanya ziara yake katika Kiwanda hicho leo Jumatano (Desemba 18, 2019). Kushoto ni Meneja Uzalishaji wa Kiwanda hicho, Mitesh Dhokie na katikati ni Mkurugenzi Mtendaji, Goodluck Hussein.
Aliongeza kuwa msukumo uliowekwa na Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) ni kuhakikisha kuwa wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo wanakuwa na fursa kuwa katika kukuza uchumi kwa kuwawezesha kujenga viwanda vidogo vidogo na kuchakata bidhaa zenye ubora.

‘’Niwapongeze TIRDO kwa kutambua wajibu wenu katika masuala ya utafiti na viwanda lakini pia kutoa eneo lenu lenye ukubwa square (mraba) mita 600-700 na ghorofa moja na kukodisha kwa kiwanda cha ORI na kwa msukumo huu tutaweza kuwasaidia wajasiriamali, wafanyabiashara na wenye viwanda vidogo kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa’’ alisema Waziri Kairuki. 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki (kushoto) akitazama bidhaa ya nyama inavyochakatwa na kuwa soseji inayozalishwa na Kiwanda cha ORI Meat Product Ltd kilichopo Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kutembelea kiwanda hicho leo Jumatano (Desemba 18, 2019) na kujionea uzalishaji. Katikati ni Meneja Uzalishaji wa ORI Meat Product Ltd, Mitesh Dhokie.
 

Aidha Waziri Kairuki aliitaka TIRDO kuhakikisha kuwa mpango huo unakuwa endelevu ili kuwafanya wafanyabiashara, wawekezaji na wajasiriamali wadogo wanaendelea kupata maeneo makubwa zaidi kupitia miradi yake hatua itakayowawezesha kuweza kuongeza mnyororo wa thamani ya uzalishaji na hivyo kuleta tija kwa taifa.

Waziri Kairuki pia aliipongeza Kampuni ya ORI Meat Product Ltd kutokana na juhudi na ubunifu mkubwa walioufanya katika kuchakata bidhaa za nyama kupitia soseji za ng’ombe na kuku, na kuongeza kuwa Ofisi yake itawasiliana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kuona namna bora mauzo na uzalishaji wa bidhaa za kampuni hiyo.
 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kariuki akionja bidhaa ya nyama iliyochakatwa na kuwa soseji soseji inayozalishwa na Kiwanda cha ORI Meat Product Ltd kilichopo Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kutembelea kiwanda hicho leo Jumatano (Desemba 18, 2019) na kujionea uzalishaji. Kushoto ni Mfanyakazi wa Kiwanda hicho, Martha Gwali na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho Goodluck Hussein.
 

‘’Ndani ya muda mfupi wa kipindi cha mwaka mmoja vijana hawa wa Kitanzania wameweza kuwekeza mtaji wa Tsh Bilioni 1.1, walianza na wafanyakazi 50 lakini sasa wapo 64 lakini pia wameweza kuongeza mnyororo wa thamani kupitia label (alama), vifungashio vya plastiki, wazalishaji wa kuku ambapo wajasiriamali wanaweza kuuza kuku katika kiwanda hiki’’ alisema Waziri Kairuki.

Akifafanua zaidi Waziri Kairuki aliitaka Kampuni hiyo kuendelea kupanua shughuli zake ikiwemo kuimarisha mtandao wa masoko ya ndani na nje ya nchi, ikiwemo soko la Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na kuzalisha bidhaa zenye viwango na ubora unaostahiki.
 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki akitazama bidhaa ya nyama iliyochakatwa na kuwa soseji inayozalishwa na Kiwanda cha ORI Meat Product Ltd kilichopo Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kutembelea kiwanda hicho leo Jumatano (Desemba 18, 2019) na kujionea uzalishaji. Kushoto ni Mfanyakazi wa Kiwanda hicho, Martha Gwali.  (PICHA NA MAELEZO)

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO, Humphery Ndossi Ofisi yake imeendelea kufanya kazi na wawekezaji wa ndani kwa kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara zao, na miongoni mwao ni Kiwanda cha ORI Meat ambapo wamekuwa wakitoa msaada mbalimbali ikiwemo upimaji wa ubora wa bidhaa za kiwanda hicho.

Aliongeza kuwa TIRDO imeendelea kusimamia wajibu wa msingi wa majukumu yake kwa kuwasisitiza wafanyabiashara kuzingatia ubora wa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini ili kuweza kuliepusha taifa na mlundikano wa bidhaa bandia na zisizo na ubora na kuzuia matumizi yake ili kulinda afya za wananchi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ORI Meat Product Ltd, Goodluck Hussein alisema Ofisi yake imeendelea kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa Serikali na imeweza kuuza pakiti 1200-1500 kwa mwaka, jambo ambalo lilikuwa gumu kwa miaka ya nyuma kutokana na uwepo wa bidhaa nyingi za nyama kutoka nje ya nchi.