Matokeo chanyA+ online




Friday, August 30, 2019

BODI MPYA YA WADHAMINI MOI YAWEKA MIKAKATI YA KUBORESHA HUDUMA ZAIDI

Dar es Salaam, 30/08/2019. 

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MOI Profesa Charles Mkony leo ameongoza kikao cha kwanza cha bodi mpya ya MOI ambapo wajumbe wamepata fursa ya kukutana na menejimenti pamoja na kukagua maeneo ya kutolea huduma.
Prof. Mkony ameongoza wajumbe hao kujadili mipango, mikakati pamoja na kupitia taarifa mbalimbali za Taasisi ambazo zimewasilishwa zinazolenga kuendelea kuboresha utoaji wa huduma bora kwa watanzania.
Pamoja na Mwenyekiti wa bodi hiyo mpya Prof. Charles Mkony na Katibu Dkt Respicious Boniface wajumbe wengine ni Bi Deodatha Makani, Dkt Amani Malima, Bw. Charles Beida, Dkt Pilly Chillo, Dkt Tuhuma Tuli, Dkt Petronila Ngiloi, Dkt Pern Tellya na Dkt Lusisyo Mwakaluka.
Aidha, Prof.Mkony amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa kumuamini na kumpa dhamana ya kuongoza bodi ya wadhamini ya Taasisi kubwa ya MOI.
“Ikiwa ni kikao cha kwanza nimshukuru sana Mh Rais kwa nafasi hii, ameonyesha imani kwangu na kwa wenzangu hivyo ni jukumu letu kufanya kazi kwa bidii na kwa weledi ili Taasisi hii tegemeo iendelee kutoa huduma bora” Alisema Prof. Mkony
Kwa upande wake ,Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface amesema ujio wa bodi mpya wa wadhamini MOI utaleta mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma pamoja na kuendelea kuboresha na kuanzisha huduma mpya sawa na zile za mataifa ya Ulaya na India.
Baada ya kukamilisha ziara ya kukagua maeneo ya kutolea huduma MOI wajumbe wa bodi mpya ya wadhamini MOI wameipongeza Serikali kwa ukwekezaji mkubwa iliyoufanya kwenye miundombinu, vifaa, majengo na wataalamu na kuahidi kuifanya MOI kuendelea kuwa Taasisi bora zaidi barani Afrika.

WADAU WA NAFAKA WAKUTANA DAR KUJADILI FURSA

 Wadau wa mazao ya nafaka, wakimsikiliza Waziri wa Kilimo Mhe. Japhate Hasunga wakati akihutubia mkutano wa siku mbili wa Wafanyabiashara wa Nafaka Ndani na Nje ya Nchi  kwenye ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam 
 
Mkutano  wa siku mbili wa Wafanyabiashara wa Nafaka Ndani na Nje ya Nchi umefunguliwa na Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga kwenye ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo Agosti 29, 2019.

Mkutano huo ambao umewajumuisha wasindikaji, wasafirishaji na wamiliki wa maghala ya nafaka Lengo lake ni kuangalia fursa zilizopo kwenye tasnia ya nafaka na jinsi ya kuzifikia ikiwa ni pamoja na masoko.
 
 Mhe. Waziri Hasunga.


Akizungumza na washiriki wa mkutano huo uliowakutanisha  wadau kutoka mikoa mbalimbali  nchini, Mhe. Hasunga ambaye alifuatana na Manaibu wake, Mhe. Husein Bashe, na Mhe. Omary Mgumba alisema mkutano huo utatoa fursa kwa wajumbe kuelimishwa kuhusu fursa ya biashara ya mazao ya nafaka katika soko la Afrika, uwezo wa Tanzania kuzalisha na nafasi ya wafanyabiashara kushiriki kikamilifu lakini pia washiriki watapata fursa ya kujifunza athari za upotevu wa mazao ya nafaka baada yamavuno na mkakati wa serikali kudhibidi hali hiyo.
 
 Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga akihutubia mkutano huo.
“Kitaalamu wanasema utafiti uliofanyika Tanzania na  nchi nyingi za Kusini asilimia 40 ya mazao yote yakiwemo ya nafaka yanapotea baada ya mavuno kwa kuharibika na matatizo mengine, hii haikubaliki mkulima amewekeza, amevuna halavu mazao yake yanaharibika, lazima tuwe na mkakati wa kuzuia hali hii.” Alitoa hakikisho Mhe. Waziri Hasunga na kuongeza.

Kulingana na uzalishaji uliopo, nafaka nyingi kama mahindi mtama na nafaka nyingine huhifadhiwa katika kiwango kisichoridhisha hali hii huchangia kupoteza ubora wa nafaka na hatimaye huchangia kuzorota kwa ustawi wa afya zetu, alifafanua zaidi Mheshimiwa Waziri.
 
 Mtafiti Mwandamizi wa Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF) Dkt.Hoseana Lunogelo, akiwasilisha mada kuhusu mahusiano kati ya maghala (Storage facilities na upotevu wa mazao baada ya mavuno, post harvest losses).
 
Alisema Agosti 1, mwaka huu kwenye sherehe za Nanenane kwenye viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muunganow a Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alizindua mkakati wa namna ya kupambana na kudhibiti upotevu wa mazao baada ya mavuno.

Katika utafiti wake ilioufanya hivi karibuni Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF) chini ya Mradi wa Rapid Response Implementation Support to the Ministry of Agriculture and Agriculture Sector Lead Ministry (RARIS) unaofadhiliwa na Taasisi ya Bill and Melinda Gates Foundation umebaini kuwa hali ya maghala mengi ya watu binafsi hayatoi taarifa serikalini na hii ni kutokana na mfumo wa sasa wa maghala.
 
 Mtafiti Mwandamizi wa Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF) Dkt.Hoseana Lunogelo, akiwasilisha mada kuhusu mahusiano kati ya maghala (Storage facilities na upotevu wa mazao baada ya mavuno, post harvest losses).
 
Akitoa mada kuhusu mahusiano kati ya maghala (Storage facilities na upotevu wa mazao baada ya mavuno, post harvest losses), Mtafiti Mwandamizi wa Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF) Dkt.Hoseana Lunogelo alisema ESRF ilifanya utafiti wa hali (status) ya maghala nchini na kubaini kuwa maghala ya watu binafsi hayalazimiki kisheria kutoa taarifa serikalini kuhusu nini kimehifadhiwa na kiasi gani cha nafaka kilichohifadhiwa ndani ya maghala hayo na hali hii serikali inategemea tu maghala ya Serikali yaani (Public Storage Facilities ) kupitia Werehouse Reseat Regulatory Board ili kujua takwimu za hali ya chakula nchini.
 Bi. Margareth Nzuki (katikati), akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF akifuatilia kwa makini mada iliyokuwa inawasilishwa na Dkt. Bunogelo kuhusu utafiti ambao ulifanywa na Taasisi hiyo kuhusu mahusiano kati ya maghala (Storage facilities na upotevu wa mazao baada ya mavuno, post harvest losses).

Alisema hii ni changamoto kubwa, kama serikali inapata taarifa kutoka kwenye maghala machache sana nchini na yale mengi haipati taarifa zake, maana yake Serikali haiwezi kufanya maamuzi sahihi kuhusiana na upatikanaji wa chakula nchini na hiyo ina athari mbaya kwenye usalama wa chakula na pia ina athari mbaya pia kwenye biashara.” Alsiema Dkt. Lunogelo.NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID
 Mkuurgenzi Mtednaji wa Benki ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw.Japhet Justine akipiga makofi wakati mkutano huo ukiendelea

“Kwa sasa kuna maghala 3,430 yaliyopo kati ya hayo ni 185 tu ndiyo kuna uhakika wa kupata tawimu endapo zitahitajika lakini yaliyosalia huwezi kupata takwimu hizo kwa sababu hakuna sheria inayowalazimisha kufanya hivyo.” Alifafanua Dkt. Lunogelo.
 
 Mjumbe akifuatilia kwa makini mkutano huo.
  Mjumbe akifuatilia kwa makini mkutano huo.
 Bi.Margareth Nzuki (kushoto), kutoka ESRF akibadilishana mawazo na Bi. Vumilia L. Zikankuba kutoka Wizara ya Kilimo wakati wa mkutano huo.
 Mshiriki akitoa maoni yake.
 Oswald Mashindani (kushoto), kutoka ESRF akizunhumza jambo mbele ya Katibu Mkuu (mstaafu) Wizxara ya Fedha, Bw. Paniel Lyimo (katikati) wakati wa mkutano huo.
 Mhe. Hadsunga (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na manaibu waziri makatibu wakuu na Mwenyekiti wa TPSF.
 Washiriki wakiwa kwenye mkutano huo unaofikia kilele leo Agosti 30, 2019.
 Washiriki wakiwa kwenye mkutano huo unaofikia kilele leo Agosti 30, 2019.
Washiriki wakiwa kwenye mkutano huo unaofikia kilele leo Agosti 30, 2019.

SERIKALI YAFUTA MILIKI YA MASHAMBA YA MOA MKINGA

Serikali imefuta miliki ya Mashamba matatu ya Mkomazi Plantantions maarufu MOA yaliyopo wilaya ya Mkinga mkoani Tanga kutokana na kukiuka masharti ya uendelezaji ikiwemo kutelekezwa bila kufanyiwa maendelezo yaliyokusudiwa  na kutolipiwa kodi ya pango la ardhi.
Uamuzi huo umetangazwa leo tarehe 30 Agosti 2019 na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alipozungumza na wananchi wa Mayomboni wilayani Mkinga mkoani Tanga alipokwenda kutatua mgogoro wa muda mrefu katika eneo hilo.
Mashamba yaliyofutiwa ni lenye hati Na 9780  na ukubwa wa ekari 14,688, shamba  Na 4268  ekari 804 na Shamba lenye Hati Na 9781  ekari 246 ambapo mashamba yote matatu yana ukubwa wa ekari 15,738.
Kufuatia uamuzi huo, jumla ya vijiji kumi vyenye kaya 3,236 zilizo na wakazi 16,450 zitanufaika na uamuzi wa serikali kutokana na wananchi wake kuvamia mashamba hayo na kufanya maendelezo ya kujenga makazi, shule pamoja na kuendesha shughuli za kilimo cha mazao ya kudumu na ya muda mfupi.
Vijiji vilivyonufaika ni uamuzi wa Serikali kufuta mashamba ya Mkomazi Plantations ni kijiji cha Kilulu-Dunga, Zingibari, Mwaboza, Mwakikoya, Mhandakini, Nkanyeni, Sigaya, Mayomboni, Ndumbani pamona na kijiji cha Moa
Akizugumza wakati wa kutangaza uamuzi huo, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema uamuzi wa kufuta mashamba hayo matatu unafuatia maombi yaliyotumwa kwa Raisi John Pombe Magufuli ya kutaka kufutwa mashamba hayo kutokana na kutoendelezwa na wamiliki wake kwa muda mrefu.
Alisema, Rais ameridhia maombi hayo kwa kuwa serikali imekuwa ikisisitiza utekelezwaji wa sheria ya Ardhi Na 4 ya mwaka 1999 ikiwemo uendelezaji wa mashamba ambayo yamemilikishwa sehemu mbalimbali nchini.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliagiza kufanyika upimaji katika vijiji vyote kumi vilivyopo ndani ya shamba hilo sambamba na kuanishwa miapaka ya vijiji hivyo na kupatiwa hati ambapo alitaka wananchi wanaishi kwenye vijiji hivyo kutobughudhiwa.
Aidha, Waziri Lukuvi alitaka maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya uwekezaji katika shamba yaliyofutwa kuachwa kwa ajili ya shughuli hiyo ikiwemo muwekezaji wa Katani Azka International Tanzania mwenye ekari mia tano pamoja na maeneo ya viwanda kama kile cha kuzalisha chumvi na kusisitiza kuwa serikali inataka uwekezaji utakaotoa ajira kwa vijana na wakati huo kupata mapato kupitia kodi ya pango la ardhi.
Katika hatua nyingine Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameagiza kufanyika uhakiki wa mashamba mengine ya Kwa Mtili Estates Co Ltd yaliyopo Mkinga mkoani Tanga ambapo ekari 58 pekee ndizo zilizoombwa kufutwa kwa Rais kutokana na kutoendelezwa huku mmili wake ikidaiwa kumiliki ekari  2,841.
Hatua hiyo inafuatia Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili katika halmashauri ya wilaya ya Mkainga Obed Katonge kueleza kuwa, Kwa Mtili Estates Co Ltd inalo shamba la lenye ukubwa wa ekari 2,841 tofauti na inavyoonekana katika kumbukumbu za ofisi ya Msajili wa Hati Kanda ya Kaskazini ambazo ni 58.
Lukuvi aliagiza wataalamu wa ardhi kutoka Kanda ya Kaskazini kufanya uhakiki huo katika kipindi cha mwezi mmoja na kumpa taarifa ya uhakiki huo mwisho wa mwezi Septemba 2019 na kufafanua kuwa pale itakapothibitika kuna ujannja uliofanyika wa kumuongeza mmiliki wa shamba hilo hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wahusika.
Mbunge wa Jimbo la Mkinga mkoani Tanga Dustan Kitandula aliishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kusikiliza kilio cha muda mrefu cha wananchi wanaoishi eneo la shamba lililofutwa la kutaka kurejeshewa ardhi yao waliyokuwa wakiutumia kwa shughuli mbalimbali.
Alisema, mgogoro wa ardhi baina ya wananchi wa mkinga na wamiliki wa mashamba ya Mkomazi Plantantions Co Ltd umekaa kwa muda mrefu na kuwafanya wananchi kuwa na ndoto isiyokuwa na majibu lakini uamuzi uliotolewa na Serikali umewafanya kuishi kwa furaha na amani .

MFUKO WA MAZINGIRA KUTATUA CHANGAMOTO ZA MABADILIKO YA TABIANCHI



Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima akitolea ufafanuzi hoja mbalimbali katika Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira
Serikali imesema Mfuko wa Dhamana ya Mazingira ulioanzishwa na Ofisi ya Makamu wa Rais utasaidia katika kutatua changamoto mbalimbali za kimazingira zikiwemo mabadiliko ya tabianchi.
Hayo yamesemwa leo Agost 30, 2019 na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima wakati akiwasilisha taarifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira.
Mhe. Sima alisema kuwa ni kweli zipo changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya mazingira na Ofisi hiyo imeona ni jambo zuri kuanzisha Mfuko huo utakaosaidia kuimarisha mapato na hivyo kuweza kuzitatua.     
Akitolea majibu kuhusu maoni ya baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo waliopendekeza kuwa taasisi zingine za Serikali zenye uhusiano wa moja kwa moja na masuala ya mazingira zichangie sehemu ya mapato yake kwenye Mfuko wa Mazingira ili uweze kufanya kazi zake.
"Mheshimiwa Mwenyekiti tumeyapokea maoni ya wajumbe wa Kamati hii tutayafanyia kazi na sisi tutakaa na wataalamu wetu tutayaweka vizuri kuyaleta kwenye Kamati hii ili," alisema Naibu Waziri.
Awali katika taarifa hiyo iliyowasilishwa ilibainisha juhudi za Serikali katika kubabiliana na mabadiliko ya tabianchi kuwa ni pamoja na kutekeleza miradi na programu mbalimbali inayosaidia katika utunzaji wa mazingira.

SERIKALI YAZIGEUKIA KAMPUNI ZINAZOTANDAZA NYAYA ZA UMEME KWENYE MAJENGO

 
Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu (wa pili-kushoto), akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkandarasi wa Kampuni ya State Grid Electrical & Technical Works Ltd, WinGod Siyao (wa pili-kulia), anayetekeleza mradi wa umeme Morogoro Vijijini kuhusu hatua iliyofikiwa katika kazi hiyo. Naibu Waziri alikuwa katika ziara ya kazi eneo la Tununguo, wilayani humo, Agosti 28, 2019.
Serikali imetoa rai kwa kampuni zinazotandaza mfumo wa nyaya za umeme kwenye majengo maarufu kama ‘wiring’ kuangalia uwezekano wa kupunguza gharama zao hususan kwa wananchi walioko vijijini ili waweze kuzimudu.
Rai hiyo ilitolewa Agosti 28 mwaka huu na Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuhitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani Morogoro.
Alisema kampuni hizo zinatakiwa kutambua kuwa serikali imezitengenezea fursa kutokana na kupeleka miundombinu ya umeme maeneo ya vijijini, la sivyo wasingepata wateja hivyo nazo zinawajibika kuangalia hali za wananchi hao kwa kuiga mfano wa serikali ambayo imewapunguzia gharama za kuunganisha umeme kutoka shilingi 177,000 hadi kufikia 27,000 tu.
“Hizi bei za laki mbili hadi tatu, kwakweli siyo rafiki kwa wananchi wengi wa vijijini ambao serikali imewapunguzia gharama za kuunganishiwa umeme kutokana na uwezo wao. Sasa hawa wenzetu watafakari, itafika mahala umeme utafika, wananchi wanaounganishwa ni wachache na wao watakosa biashara.
Naibu Waziri aliiomba Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), kuangalia namna ya kusaidia jambo hilo. “Hatuna nia ya kuwadhibiti moja kwa moja, lakini waangalie ili bei ziendane na hali za watanzania vijijini pamoja na malengo ya kiserikali,” alifafanua.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri aliwataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini nchini kote kuongeza kasi na kusema kuwa serikali haitawaongezea muda bali itaendelea kusimamia makubaliano baina yao, kwamba ifikapo Desemba mwaka huu, wawe wamekamilisha ujenzi wa miundombinu husika na kubaki kazi za kuwaunganisha wateja.
Aidha, alitoa rai kwa wananchi vijijini ambao wameshafikiwa na miundombinu ya umeme wachangamkie fursa kwa kulipia shilingi 27,000 tu ili waunganishwe na kuutumia umeme kujiletea maendeleo.
“Wakati mwingine inatunyong’onyesha tunapokuta baadhi ya maeneo watu wana uhitaji mkubwa wa umeme lakini miundombinu haijawafikia na sehemu nyingine mradi umefika, watumiaji wachache.”
Vilevile, Naibu Waziri aliwasisitiza mameneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ngazi ya wilaya na mikoa, kuendelea kutekeleza agizo la serikali la kuwaunganishia umeme wananchi wa vijijini kwa bei ya shilingi 27,000 tu pasipo kuwalipisha nguzo na vifaa vingine.
Pia, alitoa onyo kwa mameneja kuacha kuwajibu wananchi wanaopeleka maombi ya kuunganishiwa umeme kwa gharama iliyoainishwa na serikali, kuwa bado hawajapata waraka husika. Alisema, Waraka wameshaupata na umeainisha gharama hiyo itumike kwa maeneo ya vijijini.
“Ni marufuku hiyo lugha ya kwamba waraka haujafika, au kwamba hiyo ni siasa, au kwamba hii ni ndani ya mita 30 au 40,” alisisitiza.
Alisema, suala la msingi wanalopaswa kufanya mameneja hao ni kuwaelewesha wananchi kwamba maombi yao yamepokelewa na wanapanga mikakati ya kuwafikishia huduma ya umeme maana ni wajibu wao kutumia ubunifu na kujipanga namna ya kuwafikia wateja, hususan wenye mahitaji ya nguzo nyingi.
Aliwahakikishia watanzania kuwa agizo la kulipia shilingi 27,000 tu kuunganishiwa umeme vijijini linatekelezeka na kwamba wale wanaohitaji nguzo nyingi wanapangiwa mpango wa kufikiwa, bali wote watahudumiwa kwa bei hiyo.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Lawrence Maro, alisema ofisi yake imepokea maelekezo yote ya Naibu Waziri na kuahidi kuwa watayatekeleza kikamilifu.
“Tangu agizo la kuwaunganisha wateja wa vijijini kwa shilingi 27,000 litolewe, tumeshaunganisha wananchi 3,195 katika kipindi cha mwezi Mei, Juni na Julai mwaka huu. Tunaendelea na zoezi hilo, hivyo wananchi wenye uhitaji njooni mtuone na tutawahudumia,” alisema.
Katika ziara hiyo ya siku mbili, Naibu Waziri aliwasha umeme katika vijiji kadhaa pamoja na kuzungumza na wananchi wa maeneo ambayo hayajafikiwa na miundombinu ya umeme ambapo aliwaeleza mikakati iliyopangwa na serikali kuwafikishia huduma hiyo. Na Veronica Simba – Morogoro

Wednesday, August 28, 2019

WADAU WAKABIDHI CHUMBA CHA UPASUAJI CHA WATOTO


Mkurugenzi Msaidizi wa huduma za Umma na binafsi wa Wizara ya Afya maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Wonanji Vivian leo amepokea chumba maalum cha upasuaji wa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi ambacho kimekarabatiwa na MOI pamoja na wadau kwa zaidi ya Tshs Milioni 500. 
Dkt. Wonanji amewashukuru wadau ,wafadhili pamoja na washirika wa MOI ambao wameshiriki katika ukarabatati na uanzishaji wa chumba hicho maalum. 
 “Leo tumekusanyika hapa kwa lengo moja kuu la kupokea rasmi chumba cha upasuaji kwaajili ya Watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi, hii ni hatua kubwa hapa nchini, nafahamu chumba hicho kilishaanza kutumika lakini leo kinakabidhiwa rasmi hongereni na ahsanteni wote mlioshiriki katika hili.” Alisema Dkt Wonanji. 
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface amesema chumba hicho kimejengwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali ambao ni chama cha Wazazi wenye watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi Tanzania ASBATH, Ndugu AKheri Kakoo kutoka Shia khoja athna asheri Muslim community, Cure International na Ubalozi wa Kuwait hapa nchini. 
“Chumba hiki kilianza kutumika mwezi Aprili na tayari watoto zaidi ya 352 wamefanyiwa upasuaji, ni matumaini yetu kwamba tutawahudumia watoto wengi zaidi ,awali tuliwafanyia upasuaji watoto 45-50 kwa mwezi sasa hivi tunawafanyia upsauji watoto 85-100 kwa mwezi hii imeondoa changamoto ya kusubiri upasuaji kwa muda mrefu.” Alisema Dkt. Boniface. 
Mwenyekiti wa Chama cha Wazazi wenye vichwa vikubwa na Mgongo wazi Tanzania Bw. Hakeem Bayakub amesema Takwimu zilizopo zinaonyesha kwamba zaidi ya watoto 4800 wanazaliwa na tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi kila mwaka hapa nchini, ambapo idadi ya watoto wanakwenda hospitali kupata huduma imeongezeka maradufu kutokana na uelewa kuongezeka. 
Imetolewa. Kitengo cha Uhusiano MOI

Tuesday, August 27, 2019

BARA LA AFRIKA LATAKA KUWEZESHWA KUJITEGEMEA




Nchi za Bara la Afrika Tanzania ikiwemo zimesema wakati umefika sasa kwa Nchi zilizoendelea kuisaidia Afrika kujitegemea na kuliwezesha kutumia rasilimali zake yenyewe kwa maendeleo ya watu wake badala ya kulifanya Bara hilo kama eneo la kupata malighafi ya kuhudumia viwanda za nchi zilizoendelea.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Prof. Palamagamba John Kabudi ameyasema hayo baada ya kushiriki Mkutano wa Mawaziri wa Maandalizi ya Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7) uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Pacifico jijini Yokohama, Japan.

Ameongeza kuwa mkutano huo pamoja na mambo mengine umesisitiza umuhimu ya uwepo wa miundombinu ambayo inaunganisha Nchi za Kiafrika ili kuliwezesha bara la Afrika kuwa na miundo mbinu ya usafirishaji imara na zenye kuleta tija kwa wote.

Aidha Prof. Kabudi ameongeza kuwa ni mkutano huo pia umeazimia kuzitaka nchi zilizoendelea kuongeza fedha zaidi kwa ajili ya kutoa huduma za kijamii hususani katika nyanja za afya hususani katika kupambana na malaria,kifua kikuu na ukimwi sambamba na Afrika kuwajibika kuchukiua hatua zote za kuhakikisha uwepo wa utawala bora,usalama na Amani.
Akifungungua mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Mhe. Kono Taro amezipongeza nchi za Afrika kwa kupiga hatua katika maendeleo kupitia ushirikiano na Japan na kwamba nchi yake itaendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na nchi hizo ili kuziwezesha kufikia malengo ikiwemo mapinduzi ya viwanda.

Mhe. Taro amesema kuwa, ushirikiano kati ya Afrika na Japan kupitia mpango wa TICAD umeendelea kuimarika tangu kuanzishwa kwa mpango huo mwaka 1993 na kwamba ni matarajio yake Mktano wa Saba utakuwa wa tija zaidi kwa pande hizo mbili.

“Nawakaribisha Mawaziri wenzangu Yokohama ambapo maandalizi ya mkutano wa saba wa kimataifa wa Tokyo kuhusu maendeleo ya Afrika yanaendelea. Jukumu letu ni kupitia na kupitisha rasimu ya Azimio la Yokohama na Mpango kazi wake ili hatimaye litunufaishe sote pale litakapopitishwa na Wakuu wa nchi” alisema Mhe. Taro.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano huo, Mhe. Sameh Shoukry ameipongeza Japan kwa kuendelea kuandaa mikutano hiyo ambayo ina nia ya kuifikisha Afrika katika mapinduzi ya viwanda na kuondokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana na nyingine nyingi.

Kwa upande wake, Naibu Mwenyekiti wa Kamishenii ya Umoja wa Afrika ambao ni miongoni mwa waandaaji wenza wa Mkutano wa Saba wa TICAD, Bw. Kwesi Quartey amesema kuwa, mkutano huo unafanyika wakati Umoja wa Afrika unaendelea kutekeleza agenda 2063. Agenda hiyo pamoja na mambo mengine inalenga kuziwezesha nchi za Afrika kufikia maendeleo ya hali ya juu kwenye sekta mbalimbali zikiwemo afya, elimu, teknolojia na miundombinu. 

Kadhalika Mkurugenzi wa Kituo cha Huduma za Kanda ya Afrika kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Afrika, Bw. Lamin Manneh alisema kuwa ushirikiano kati ya Afrika na Japan kupitia TICAD umekuwa na mchango mkubwa kwenye maendeleo ya Bara la Afrika.

Mkutano wa Saba pamoja na mambo mengine unatoa fursa ya kupanga mikakati ya ushirikiano na agenda za kimaendeleo zitakazotelezwa kati ya Japan na Afrika kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo kuanzia mwaka 2019 hadi 2021.

Agenda za mkutano wa mwaka huu zinalenga kujadili mageuzi ya kiuchumi na kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kukuza sekta na uvumbuzi. Pia kuimarisha usalama na ustahimilivu endelevu kwenye jamii pamoja na kuendeleza jitihada za kuimarisha amani na usalama barani Afrika. Agenda za Mkutano wa Saba zinaenda sambamba na agenda 2063 ya Umoja wa Afrika, Agenda 2030 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa na maazimio mengine ya kimataifa kama Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa.


Mkutano huu ambao umewashirikisha Mawaziri kutoka nchi za Afrika, na wadau mbalimbali wa maendeleo unafanyika ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali utakaofanyika kuanzia tarehe 28 hadi 30 Agosti 2019.

Monday, August 26, 2019

RAIS DKT.SHEIN AKUTANA NA UONGOZI WIZARA, KILIMO, MALIASILI, MIFUGO NA UVUVI


 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kushoto) akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi  katika mkutano wa utekelezaji wa malengo ya mpango kazi kwa kipindi cha Julai  2018-Juni 2019 na mpango kazi wa mwaka 2019-2020 katika ukumbi wa Ikulu Mjini Zanzibar leo.
 Waziri wa Kilimo,Maliasili,Mifugo na Uvuvi (kushoto) akichangia katika mkutano wa Wizara hiyo wa   utekelezaji wa malengo ya mpango kazi kwa kipindi cha Julai  2018-Juni 2019 na mpango kazi wa mwaka 2019-2020 uliofanyika leo katika ukumbi wa Ikulu Mjini Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (katikati)
Makamo wa Pili wa  Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi (kushoto) alipokuwa akichangia  wakati wa  mkutano wa utekelezaji wa malengo ya mpango kazi kwa kipindi cha Julai  2018-Juni 2019 na mpango kazi wa mwaka 2019-2020 wa Wizara ya  Kilimo,Maliasili,Mifugo na Uvuvi  uliofanyika leo katika ukumbi wa Ikulu Mjini Zanzibar,(katikati) Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi.Marium Juma Abdalla Saadalia chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (hayupo pichani).
 Baadhi ya Maofisa katika Wizara ya Kilimo,Maliasilio,Mifugo na Uvuvi wakiwa katika mkutano wa Wizara hiyo wa utekelezaji wa malengo ya mpango kazi kwa kipindi cha Julai  2018-Juni 2019 na mpango kazi wa mwaka 2019-2020 uliofanyika leo katika ukumbi wa Ikulu Mjini Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (katikati),[Picha na Ikulu.] 26/08/2019.

MGALU ATOA ONYO KALI KWA MKANDARASI WA UMEME VIJIJINI KILIMANJARO

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akiwasha rasmi umeme katika shule ya msingi Gararagua, iliyopo wilayani Siha, Mkoa wa Kilimanjaro akiwa katika ziara ya kazi, Agosti 25, 2019

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ametoa onyo kali kwa Mkandarasi Urban & Rural Engineering, ambaye anatekeleza mradi wa umeme vijijini awamu ya tatu mkoani Kilimanjaro, kwa kumwambia asiijaribu serikali kwa kutikisa kibiriti kwani njiti zimejaa na kitawaka.
Alitoa onyo hilo kwa nyakati tofauti Agosti 25, 2019 akiwa katika ziara ya kazi kwenye Wilaya za Hai na Siha, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi na viongozi wao kuwa kasi ya mkandarasi huyo hairidhishi.
Akizungumza katika mkutano na wananchi wa Hai, Naibu Waziri Mgalu alikiri mbele yao kuwa utendaji kazi wa mkandarasi husika unasuasua na zaidi ameonesha vitendo vya utovu wa nidhamu kwa serikali kwa kutoitikia wito alipoitwa kushiriki kwenye ziara hiyo pasipo kutoa sababu yoyote.
Akielezea zaidi, Naibu Waziri alisema yeye binafsi alijaribu kuwasiliana na mkandarasi huyo kwa njia ya simu pasipo mafanikio na hata ujumbe mfupi wa maandishi aliomtumia kumtaka apokee simu, haukujibiwa; kitendo ambacho alikiita ni dharau.
“Sasa mimi nataka nitoe salamu kwake. Mkandarasi Urban & Rural Engineering naona unatikisa kibiriti, unataka ujue kama kina njiti au hakina, na kama njiti zimejaa au zina baruti. Nataka nikwambie kibiriti kimejaa, njiti zina baruti na kitawaka.”
“Ulichokifanya ni dharau na unatupelekea tufanye maamuzi ya kuanza mapitio; na ni kweli nathibitisha ameshindwa kazi,” alisema Naibu Waziri.
Kufuatia hali hiyo, alimwagiza Msimamizi wa Mradi husika kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kumjulisha mkandarasi huyo kwenda Dodoma mara moja kushiriki katika kikao kitakachofanya mapitio ya suala hilo ili ikibidi hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.
“Kama ameshindwa kazi, tutawapatia wakandarasi wengine au hata TANESCO wanaweza kumalizia kazi husika.”
Awali, Meneja wa TANESCO wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Mahawa Mkaka, alimweleza Naibu Waziri kuwa, Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu mkoani Kilimanjaro unagharimu kiasi cha shilingi za kitanzania takribani bilioni 12.
Alisema, Mradi unahusisha ujenzi wa kilomita 150 za msongo wa umeme wa kilovoti 33, ujenzi wa kilomita 334 za msongo wa umeme wa kilovoti 400 na ufungaji wa mashine umba (transfoma) 132 na kwamba unatarajiwa kuunganishia umeme jumla ya wateja 3,572 katika vijiji 75 ndani ya mkoa.
Aliongeza kuwa, kwa ujumla utekelezaji wa mradi husika mkoani humo umefikia asilimia 43 hadi sasa.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri aliwasha umeme katika shule za msingi za Roo na Msamadi zilizopo wilayani Hai, pamoja na eneo la viwanda Mwangaza na shule ya msingi Gararagua wilayani Siha. Pia, alizungumza na wananchi wa Kata ya Ngarenairobi wilayani Siha. Na Veronica Simba – Kilimanjaro