Matokeo chanyA+ online




Wednesday, July 29, 2020

RAIS JOHN MAGUFULI AONGOZA WATANZANIA KATIKA MAZISHI YA RAIS MSTAAFU BENJAMIN WILLIAM MKAPA LUPASO MASASI MKOANI MTWARA





Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiweka udongo kwenye kaburi la Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Marehemu Benjamin William Mkapa katika Mazishi yaliyofanyika katika Kijiji cha Lupaso Masasi Mkoani Mtwara.


Wanajeshi wa JWTZ wakiwa wamebeba Jeneza lenye Mwili wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Marehemu Benjamin William Mkapa kuelekea eneo la Makaburi kwa ajili ya Mazishi yaliyofanyika katika Kijiji cha Lupaso Masasi Mkoani Mtwara

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Viongozi mbalimbali pamoja Wananchi wa Lupaso waliohudhuria katika Mazishi hayo ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Marehemu Benjamin William Mkapa Lupaso Masasi mkoani Mtwara.


Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akishuhudia Mjane wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Marehemu Benjamin William Mkapa Mama Anna Mkapa akiweka udongo kwenye kaburi la Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Marehemu Benjamin William Mkapa katika Mazishi yaliyofanyika katika Kijiji cha Lupaso Masasi Mkoani Mtwara. 


Mabregedia Jenerali wa JWTZ wakishuhudia Jeneza lenye Mwili wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Marehemu Benjamin William Mkapa likishushwa kaburini Lupaso Masasi mkoani Mtwara.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na Mjane wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Marehemu Benjamin William Mkapa, Mama Anna Mkapa wakati wakielekea kuweka Udongo kwenye Kaburi la Marehemu Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Benjamin William Mkapa Kijijini Lupaso Masasi mkoani Mtwara

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Viongozi mbalimbali pamoja Wananchi wa Lupaso waliohudhuria katika Mazishi hayo ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Marehemu Benjamin William Mkapa Lupaso Masasi mkoani Mtwara. PICHA NA IKULU

Tuesday, July 28, 2020

RAIS MAGUFULI - TAIFA LIMEPOTEZA MTU ALIYETOA MCHANGO MKUBWA KATIKA KULETA MAGEUZI MAKUBWA YA KIUCHUMI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli akifuta machozi wakati akielezea namna alivyomjua Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Marehemu Benjamin William Mkapa wakati akihutubia katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Rais  Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 28 Julai, 2020 amewaongoza Watanzania kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamin William Mkapa aliyefariki dunia tarehe 23 Julai, 2020.

Mwili wa Hayati Benjamin William Mkapa ulianza kuagwa tarehe 26 Julai, 2020 katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam na kuhitimishwa leo ambapo pamoja na  Rais Magufuli na familia ya Hayati Mkapa, viongozi wengine wakiwepo Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dkt. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Jen. Alain Guillaume Bunyoni (kwa niaba ya Rais wa Burundi Mhe. Jen. Evariste Ndayishimiye) na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Idd wamepata fursa ya kutoa heshima za mwisho.


Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein, akitoa hashima ya mwisho kwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin William Mkapa, wakati wa hafla ya Kitaifa ya kuuaga mwili wa marehemu katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar leo


Wengine ni Waheshimiwa Maspika, Majaji Wakuu, Marais Wastaafu, Mawaziri Wakuu Wastaafu, Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Vyama vya Siasa na viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Katika salamu zake, Rais Magufuli amesema Taifa limepoteza mtu aliyetoa mchango mkubwa katika kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi, kuimarisha huduma za kijamii (elimu, maji, afya), kuanzisha na kuimarisha taasisi muhimu za Serikali, kuimarisha sekta binafsi, kujenga miundombinu hasa barabara na madaraja, kuinua ukusanyaji wa kodi, kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kimataifa, ukombozi na utatuzi wa migogoro ya Mataifa mbalimbali ya Afrika na aliyekuwa mahiri katika kuibua vipaji vya viongozi akiwemo yeye mwenyewe, Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dkt. Ali Mohamed Shein na Mgombea wa Kiti cha Urais wa Zanzibar  Dkt. Hussein Ali Mwinyi.


Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akitoa heshima ya mwisho kwa mwili wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Tanzania Benjamin William Mkapa, wakati wa hafla ya kuuaga mwili wa marehemu Kitaifa katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam Leo

Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa Hayati Benjamin William Mkapa ameacha mengi mazuri ya kujivunia na kuendelea kujifunza yakiwemo uongozi bora uliosimamia umoja, mshikamano, uchapakazi, uzalendo, uwajibikaji, uwazi na uhusiano mzuri wa kimataifa na ameahidi kuwa Serikali anayoiongoza itafanya kila liwezekanalo ili kudumisha na kuendeleza mambo yote mazuri yaliyoasisiwa nae.


Mjane wa Marehemu Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Tanzania Benjamin William Mkapa Mama Anna Mkapa akitoa heshima yake ya mwisho kwa mwili wa marehemu wakati wa hafla ya Kitaiga ya kuuaga mwili huo iliofanyika katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam Leo

Rais Magufuli amesema yeye binafsi amefanyiwa mengi mazuri na Hayati Benjamin William Mkapa ambaye hakutaka aanguke kwa kumlea kama mwanae na kwa upendo mkubwa.

“Mzee Mkapa ni shujaa wangu na ni mtu muhimu sana katika historia ya maisha yangu, hata nilipopatwa na shida ama kukumbwa na changamoto mbalimbali, Mzee Mkapa hakuniacha, hivyo kuondoka kwake ni pigo kubwa sana kwangu kwa vile nimempoteza mtu muhimu sana katika maisha yangu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.


Aidha, Rais Magufuli amewapa pole wanafamilia wakiongozwa na Mjane wa Hayati Benjamin William Mkapa, Mama Anna Mkapa na Watoto wake, amewaombea moyo subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi ya kuondokewa na mpendwa wao.

Amewashukuru Watanzania wote kwa utulivu na mshikamano katika kipindi hiki cha maombolezo ya tangu Benjamin William Mkapa afariki dunia, pia amewashukuru viongozi wa dini, vyombo vya ulinzi na usalama, vyombo vya habari, wageni mbalimbali na wote waliotuma salamu za rambirambi kufuatia msiba huu mkubwa uliolikumba Taifa.

Mwili wa Hayati Benjamin William Mkapa umesafirishwa kwa ndege ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwenda kijiji cha Lupaso, Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara ambapo hapo kesho utazikwa kwa taratibu kidini na kwa heshima zote za kijeshi.