Matokeo chanyA+ online




Thursday, October 31, 2019

RAIS MAGUFULI ANG'OA MIZIZI YA KUFANYA KAZI KWA MAZOEA



Imetimia miezi 48 sasa sawa na miaka minne tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alipochukua jukumu rasmi la kuiongoza nchi Novemba 5, 2015.


Kiongozi huyu amefanikiwa kuhakikisha watanzania wanatoka hatua moja kwenda nyingine kimaendeleo badala ya kubaki kama walivyo miaka nenda miaka rudi. Aina ya uongozi wa rais Magufuli umeonesha uwezo au karama ya kuondoa taratibu zilizooleka katika jamii na kisha kubuni, kuelekeza njia sahihi kwa vitendo ni ushindi wa mafanikio katika uongozi wake.


Katika kipindi kifupi rais Magufuli  amekuwa gumzo ndani na nje ya nchi kutokana  na uwezo alionao kushawishi watu kufikia maendeleo yaliyotarajiwa kwa kuondoa taratibu zisizofaa  kama vile uzembe kazini, ubadhirifu wa mali ya umma, na huduma mbovu za jamii kama vile maji safi na salama, elimu, afya.


 Akihojiwa na Idara ya Habari Maelezo mchambuzi  na mtafiti wa  wa masuala ya uchumi na siasa Dkt.  Bravious Kahyoza anamuelezea  Rais John Pombe Magufuli kama kiongozi  mwenye uthubutu wa kuamua mambo mazito na kuyatekeleza kwa wakati kwani   ameweza kuvunja taratibu zisizofaa ambazo zilikuwa  kizingiti cha maendeleo ya nchi jambo ambalo limemjengea imani kwa wananchi .


“hakuna jinsi nyingine kubwa ya kuhakikisha watu wanatoka hatua moja kwenda hatua nyingine kama taratibu za maisha yao zinabaki zilivyo na tafsiri za kiuchumi duniani zinaonesha kuwa maendeleo ya watu kiuchumi  yanahusiana na utaratibu wa maisha ya watu wenyewe, Rais wetu amevunja taratibu korofi ”. Anasema Dkt. Kahyoza.


Aidha, ameongeza kuwa kinachomtofautisha rais Magufuli na viongozi wengine kiasi cha kusababisha awe gumzo ndani na nje ya nchi ni muda mfupi aliotumia kuleta mageuzi makubwa nchini.  Pia namna alivyoonesha mfano wa kubana matumizi katika kutekeleza majukumu yake kama kiongozi wa nchi. 


Mwandishi David Lender katika kitabu chake cha ‘The Wealth and Poverty of Nations: why some are so rich and some are so poor (Utajiri na Umasikini wa Mataifa: kwanini mengine ni tajiri na mengine masikini.  Kitabu hicho kimeeleza kwamba mataifa ambayo yameweza kuwa na sehemu kubwa ya mabadiliko kati ya miaka 1961 na 2014 ni yale  yaliyobadilisha taratibu na tabia za watu zilizooeleka na kuzielekeza kwenda kwenye mtazamo wenye tija kwa taifa lao, miongoni mwa mataifa hayo ni ulaya na Asia katika nchi za Uingereza, Japan na Afrika ni nchi za Namibia, Botswana, Rwanda na Ethiopia.


Anasema, mfano hai ni kama vile uandaaji wa sherehe za kitaifa za gharama kubwa, sherehe  wakati wa uteuzi wa viongozi mbalimbali, kumbukumbu za kitaifa, sherehe za uhuru, muungano na uzinduzi wa miradi ambapo fedha nyingi hutumika kusherehesha wakubwa serikalini na baadhi ya jamii.


Rais Magufuli  alichukua hatua ya kubatilisha taratibu za ufanyaji wa sherehe hizo kwa kufanya kazi za kijamii kama vile usafi, kuhudumia wagonjwa na mara kadhaa kutumia fedha husika kwa ajili ya manufaa ya taifa ambapo sherehe za maadhimisho ya miaka 54 ya uhuru aliagiza fedha zitumike kwenye ujenzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco. 


Pia, Rais Magufuli alipounda Baraza  la Kwanza la Mawaziri 2015, Baraza lilikuwa mawaziri 19 tu huku baadhi ya wizara  zikibaki bila naibu mawaziri. Rais aligiza kiasi cha shilingi bilioni 2 zilizokuwa zitumike kwaajili ya semina elekezi kwa viongozi wapya zipelekwe Wizara ya Elimu kutunisha fungu la elimu bure ikiwa ni pamoja na kununua madawati ya wanafunzi.


Rais hakuishia hapo, alizuia safari za viongozi nje ya nchi  zisizokuwa za lazima na yeye mwenyewe kupunguza safari zake nyingi nje ya nchi na kuagiza balozi kumwakilisha katika masuala ya Kimataifa.


Aidha, uzoefu wake katika kulitumikia taifa kwa muda mrefu, aligundua ndani ya utumishi wa umma yapo makundi mawili ya wafanyakazi wanaolipwa mshahara kwa mazoea. Kundi la kwanza ni watumishi ambao kwenye kumbukumbu za utumishi wanaonekana waajiriwa  wa serikali wanaolipwa stahiki zote za utumishi lakini  si watumishi ambao kwa idadi walikuwa 20,000.


Kundi la pili ni watumishi ambao kwa mazoea wanafanya kazi lakini hawana sifa kwa nafasi walizonazo kwa idadi walikuwa 14,000. Watumishi hao baadhi  walitumia vyeti visivyo sahihi kuajiriwa na wengine walifanya kazi za taaluma ambazo hawakuwa na ujuzi nazo.


Kwa mamlaka aliyonayo, Rais Magufuli alitoa agizo kwa wakuu wa mikoa kuhakikisha  watumishi wa aina hiyo wanaondolewa sehemu zao za kazi. Zaidi ya watumishi 10,000 walipoteza ajira na serikali iliokoa zaidi ya shilingi Bilioni 15 za mishahara hewa huku Wakuu wa Mikoa walioshindwa kutekeleza agizo hilo kwa usahihi nyadhifa zao zilitenguliwa.


Pengine hali hii ndio iliyokuwa inasababisha hasira dhidi ya serikali kwakuwa wananchi hawakuona huduma zinatolewa kama zinavyostahili. Dkt. Kayhoza alisema kuwa nanukuu maneno ya rais Magufuli “Naagiza wakuu wote wa mikoa hakikisheni watumishi hewa yaani ambao hawapo wanaondolewa kwenye orodha ya utumishi na sehemu zao za kazi’. 


Pia, matokeo yake ndani ya kipindi kifupi serikali iliweza kutangaza nafasi za kwa wenye sifa katika sekta nyingi mathalani  Tamisemi ilitangaza ajira mpya kwa walimu wa shule za msingi na sekondari pamoja na sekta ya afya na nyingine nyingi.

 Hii leo watanzania tunaona mabadiliko makubwa ya kiutendaji katika utumishi wa umma.

Dkt. Kayhoza anasema, Rais Magufuli ameonyesha dhahiri kuwa kiongozi bora asiye mlalamishi bali ni kiongozi anayetafuta  ufumbuzi wa kila changamoto anayokutana nayo. Aidha, ni kiongozi mwenye uthubutu , maamuzi sahihi, mtekelezaji, mfuatiliaji wa maamuzi yake mpaka yanapokamilika.

“Hii inaonesha dhahiri uwezo alionao wa kuzisoma nyakati na kuhakikisha nyakati hizi zinaweza kutafsiriwa si tu kwa nchi anayoiongoza lakini pia kuangalia uchumi wa nchi unategemea masuala gani yanatokea na namna gani yanaweza kusaidia nchi kwenda mbele”. Amesema Dkt Kahyoza.

Maamuzi mengine aliyoyafanya ni serikali yake kuhamia Dodoma. Hadi sasa Mawaziri wote chini ya Waziri Mkuu, Naibu Mawaziri, Makatibu  na Kurugenzi zote muhimu zimehamia Dodoma.

Uamuzi wa serikali kuhamia Dodoma haukupewa kipaumbele kwa zaidi ya miaka 40 iliyopita tangu ulipoasisiwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwenye 1970. Kutokana na umuhimu wa kuhamia Dodoma watumishi wa serikali waliokuwa makao makuu walihamia Dodoma.  Hili ni funzo kwetu ambapo tukiamua tunaweza kwani ndani ya matumizi na mazingira yetu ya kawaida inawezekana tukapanga na tukatekeleza mambo yetu wenyewe kwa ufanisi.

Akitoa mfano juu ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa kufua umeme katika Mto Rufiji Dkt. Kahyoza amesema “Licha ya mradi huu utakaozalisha kilowati 2115 za umeme kupingwa na kukabiliwa na vizingiti ndani na nje ya nchi, Rais Magufuli ameweza kuvunja vizingiti hivyo ambapo Julai mwaka huu alizindua rasmi ujenzi wa bwawa la mto Rufiji  utakaogharimu  fedha za Tanzania za shilingi trilioni 6.5. 

Suala lingine ambalo rais Magufuli aliahidi kupambana nalo ni ukusanywaji wa kodi ambapo ukaguzi kwa kila sekta umekuwa mkubwa na matokeo yake ni kuongezeka kwa mapato ya taifa kutoka shilingi milioni mia nane kwa mwezi hadi kufikia shilingi trilioni 1.7 Septemba, 2019.



Rais alisema“unapouza toa risiti na unaponunua dai risiti”.  Alianza kwa kusisitiza kwa mtu mmoja mmoja kudai risiti kwa kila huduma anayopatiwa  na baadaye  akahimiza wafanyabiashara kulipa kodi ikiwa ni pamoja na taasisi za serikali kulipa kodi baada ya kupatiwa huduma  au bidhaa.

Hali hii imeleta mageuzi kwa kila mfanya biashara kuwa na mashine ya EFD (Eletronic Fiscal Divice) kitu ambacho hakijawahi kutokea miaka iliyopita. Amemalizia Dkt. Kayhoza



Naye Projestus Rwegarulila Mkurugenzi wa Mradi wa Utamaduni na Uzalendo anasema, Rais Magufuli amekuwa mstari wa mbele kutumia lugha ya Kiswahili kwenye mikutano mbalimbali ya Kimataifa anayoshiriki  jambo halijawahi kufanyika kwa viongozi wetu hivi karibuni.



 “Kitendo cha Rais kuongea Kiswahili kwenye mikutano ya kimataifa kimewalazimu wasiojua lugha hiyo kutafsiriwa na wengine kuamua kujifunza Kiswahili”. Anasema Rwegarulila.



Anasema, pamoja na watu kuvutiwa na kile anachozungumza Rais kwenye mikutano, kasi ya maendeleo ya Tanzania kwenye sekta mbalimbali ndiyo inawavuti wageni kuja kujifunza namna ambavyo nchi imepiga hatua  kama vile mradi kama vile mwendo kasi, kuanzishwa kwa sera sera mpya ya madini,  ujenzi wa bwawa kubwa la kuzalisha umeme ni baadhi ya baadhi ya mambo yanayoamsha kiu ya mataifa mengine kujifunza kutoka kwetu.

Na hakuna lugha nyingine isipokuwa kutafsiri Kiswahili katika lugha zao.



Naye mwanafunzi Hamida Khamis wa shule ya msingi Bunge jijini Dar es Salaam amesema kabla ya serikali ya awamu ya tano shule yao haikuwa na madawati ya kutosha, wanafunzi walikuwa wanasukumana kutafuta nafasi za kukaa kwenye dawati lakini mpango wa elimu bure umefanikisha shule kupata madawati ya kutosha.



Mkazi wa Mugumu Serengeti Herman Peter yeye anasema, kabla Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani huduma za afya zilipatikana katika Halmashauri ya Serengeti tu lakini sasa huduma zimesogezwa karibu baada Serikali kujenga Kituo cha Afya katika kata yao ya Nata kwa gharama ya shilingi milioni 400.



Nimalizie kwa kusema  vema tukafahamu Rais John Pombe Magufuli ameweza kuondoa taratibu  zilizokuwa zikichelewesha nchi kusonga mbele. Hakuleta sheria mpya au sera mpya, alichokifanya ni kuhakikisha yeyote anayepewa dhamana ya uongozi anatimize  wajibu wake, anaposhindwa kuleta mabadiliko  ndani ya muda mfupi anamwondoa katika madaraka  aliyokuwa nayo.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.



Na Lillian Shirima–Maelezo

SERIKALI YATATUA KERO ZA WALIMU MKOANI SIMIYU



Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, jana jioni alilazimika kumpigia simu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Bw. Hoseah Kashimba ili kutatua kero za walimu waliodai kuna wenzao wamestaafu hawajalipwa mafao yao.

Tukio hilo lilijitokeza wakati Dkt. Abbasi akijibu hoja za walimu mara baaya ya kuwasilisha mada wakati wa Mkutano ulioandaliwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) mkoani Simiyu na kuhudhuriwa na walimu kutoka mikoa ya Kigoma, Simiyu, Shinyanga, Mwanza, Geita, Mara, Tabora na Kagera 

Katika mkutano huo walimu walitaka kujua ni lini Serikali italipa pesheni kwa wastaafu ambao hawajalipwa kwa muda mrefu.

Dkt. Abbasi alionesha kushangazwa na hali hiyo kwani aliwaeleza wanasemina hao kuwa Serikali imeachana na utamaduni wa zamani wa kulimbikiza madeni yasiyo na sababu.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari -MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) jana mkoani Simiyu. Mkutano huo umewakutanisha walimu kutoka mikoa ya Kagera, Mwanza, Kigoma, Mara, Tabora, Shinyanga, Geita na wenyeji Simiyu.

Alitoa mfano kuwa licha ya TZS Bilioni zaidi ya 40 zilozotolewa mwaka 2017 kulipa madeni ya wastaafu, Serikali pia ilihakikisha kati ya hizo TZS Bilioni 16 zinahusu walimu.

Akaongeza kuwa hata mwaka huu kati ya Julai na Septemba Serikali imelipa madeni yanayofikia TZS Bilioni 85.62 ambapo kati ya hizo TZS Bilioni 50 ni madai ya pensheni, Bilioni 22 ni madai mbalimbali ya watumishi wa umma na nyingine ni wadai wa sekta binafsi.

Kutokana na madai ya kuwepo wastaafu wa kada ya elimu ambao hawajalipwa muda mrefu, baadhi wakidai kuwa ni mwaka mzima, Dkt. Abbasi alimpigia simu na kumuunganusha moja kwa moja kwenye kipaza sauti Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF.

Akijibu hoja hiyo, Bw. Kashimba alisema kuwa Serikali kupitia PSSSF imeendelea kuwalipa pensheni wastaafu wote kwa wakati na kutoa ofa kwa mwalimu yeyote ambaye hajalipwa kwa muda mrefu alete vielelezo suala lake litafanyiwakazi haraka.

“Mmesikia wenyewe, kama nilivyosema, Serikali ya Rais Magufuli ni ya kisayansi. Hili sasa limekwisha, sio kulalamika tena lete ushahidi wa majina na namba ya malipo ya mishahara ya mtumishi husika, suala lake litatatuliwa haraka,” alisema Dkt. Abbasi kuwaeleza walimu hao waliokuwa na furaha tele baada ya ofa ya Mkurugenzi wa PSSSF.

Baadhi ya walimu hawakuwa na vielelezo husika lakini wachache waliwasilisha nyaraka zao na zinafanyiwa kazi.

Dkt. Abbasi amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Mkoa wa Simiyu, ambapo awali aliudhuria hafla ya kufunga Kambi za Kitaaluma kwa Wanafunzi wa Kidato cha Nne katika mwaka 2019.
Na Immaculate Makilika- MAELEZO

SERIKALI KUENDELEA KULIWEZESHA KWA UJUZI KUNDI LA VIJANA NCHINI - NAIBU WAZIRI MAVUNDE

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi kiuchumi Beng'i Issa akizungumza wakati wa mafunzo hayo 


Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya kazi,Vijana na ajira Anthony Mavunde akizungumza wakati wa akifunga mafunzo ya ujasiriamali kwa Vijana yaliyofanyika mkoani Tanga

Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo

Serikali imesema itahakikisha inaendelea kuliwezesha kwa ujuzi kundi la Vijana ili waweze kushiriki kwa vitendo katika shughuli za kiuchumi na ujenzi wa Taifa

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya kazi,Vijana na ajira Anthony Mavunde Leo wakati wa kufunga mafunzo ya ujasiriamali kwa Vijana yaliyofanyika mkoani Tanga

Alisema kuwa kwa mujibu wa utafiti wa nguvu kazi wa mwaka 2014 inaonyesha kuwa ukosefu wa ajira kwa Vijana ni asilimia 11.7% duniani ambapo kitaifa ni asilimia 10.3%.

Hivyo kutokana na changamoto hiyo serikali imeweza kuja na mikakati endelevu ya kuliwezesha kundi Hilo kupata ujuzi wa kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa.

"Tunatambua kwamba kikwazo kikubwa kwa Vijana kushindwa kunufaika na fursa hasa za miradi ya kimkakati ni kutokuwa na ujuzi stahiki ,hivyo kwa mafunzo hayo Nina imani yatakwenda kumaliza changamoto ya ajira nchini"alisema Naibu Waziri Mavunde.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi kiuchumi Beng'i Issa alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa vijana kwani wanayahitaji kwa kutambua kuwa ujuzi ndio msingi mkubwa wa maendeleo.

Alisema kuwa mafunzo hayo yatawaongezea ubunifu na kutatua changamoto wanazokutana nazo katika shughuli mbalimbali za kiuchumi wanazozifanya.

Mpaka Sasa jumla ya vijana 1,222 wamenufaika na mafunzo hayo katika mikoa ya Dodoma,Ruvuma,Geita, Mwanza, Mbeya, Lindi na Tanga


SARATANI YA MATITI YAWEZA KUSHIKA NAMBA MOJA



Endapo hatua zisipochukuliwa za  saratani ya matiti inaweza kushika namba moja kwa kuwa na idadi  kubwa ya wagonjwa  nchini.

Hayo yanesemwa na Mkurugenzi wa huduma za Kinga ya Saratani  katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) Dkt. Crispian Kahesa  alipozungumza na waandishi wa habari  kuhusu mwezi wa uhamasishaji , uelimishaji na uchunguzi wa saratani ambao huadhimishwa kila mwezi oktoba kila mwaka.
Mkurugenzi wa huduma ya
kinga Dkt. kahesa

“Idadi ya saratani ya matiti  inaonekana kuongezeka nchini ambapo hivi sasa wanawake wenye umri  kuanzia miaka 20 na kuendelea nao wanagundulika  kuugua ugonjwa huu”. Alisema Dkt. Kahesa.

Alisema kuwa endapo hatua zisipochukuliwa  saratani hiyo itazidi kuwa tishio zaidi na kwamba  idadi kubwa ya wagonjwa wanaofika  hospitalini hapo wanatoka katika maeneo ya mjini ambapo mkoa wa Dar es salaam unaonekana kuongoza.

“Tathimini  ya miaka 10 iliyopita saratani hii ilikua inashika nafasi ya tano ,hivi sasa ni ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa,zamani tulikua tunawaona wagonjwa kuanzia miaka 55 ukashuka hadi miaka 50 na sasa tunaona hadi wenye umri wa miaka 20”.

Dkt. Kahesa alisema kuwa kwa mwaka huu pekee wameweza kuona wanawake 1443 ambapo kati ya 342 wamekutwa na uvimbe 170 walikuwa na dalili za awali za saratani.

Kwa upande wa saratani kwa wanaume Dkt. Kahesa alisema kuwa saratani hiyo huathiri asilimia moja kwa wanaume hata hivyo kwa upande wao ni hatari  zaidi na endapo isipogundulika huweza kuathiri mapafu yao kwa haraka.

“Saratani hii huathiri wanawake zaidi  kuliko wanaume kwa asilimia 99 na wanaume ni asilimia 1 tu,ambapo dalili kwa wanaume  ni tofauti  kidogo na wanawake,hivyo kwa mwanaume ni rahisi kugundua kuliko mwanamke kwa kuwa kifua chake kina mafuta mengi.

Aliongeza kuwa kati ya wanawake 170 waliofanyiwa vipimo  zaidi ya 68 waligundulika na vivimbe ambavyo ni ugonjwa wa saratani.

Hapa nchini saratani ya shingo ya kizazi inaongoza ikifuatiwa  na saratani ya matiti,saratani  ya njia ya chakula,saratani ya tezi dume na saratani  nyingine ni zile zinazoathiri  mfumo wa kinga. Na. Catherine Sungura, WAMJW-DSM


Wednesday, October 30, 2019

WAZIRI MKUU MAJALIWA AREJEA NCHINI

Waziri  Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza  na Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson Mwansasu kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam ,Oktoba 29, 2019 wakati  alipowasili nchini akitoka nchini  Azerbaijan ambako alimwakilisha Rais John Pombe Magufuli katika mkutano wa Nchi zisizofungamana na upande wowote ulifanyika jijini Baku. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Monday, October 28, 2019

KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA OFISI YA WAZIRI MKUU KWA MKAKATI WA AJIRA NA UWEZESHAJI VIKUNDI VYA VIJANA

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria imeipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa mikakati iliyoweka katika kuwajengea uwezo vijana kujiajiri na uwezeshwaji kiuchumi kwa vijana kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana “Youth Development Fund” na Mikopo kupitia mapato ya ndani ya halmashauri.

Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya vijana katika Mkoa wa Morogoro, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Najma Giga ameipongeza Serikali kwa mikakati iliyokuja nayo katika kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana kwa kuwajengea mazingira wezeshi na yanayowahamasisha kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi.
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria wakiangalia kitanda kilichotengenezwa na Kikundi cha Vijana cha Faraja Carpentry kilichopo Mkoani Morogoro. (Wa tano kutoka kulia) ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde. (Wa nne kutoka kushoto) ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Najma Giga.

“Matokeo ya utekelezaji wa mikakati hiyo tumeona kwa kiasi kikubwa imewawezesha vijana kutambua taratibu rasmi za kupata mikopo yenye riba nafuu na ambayo imewasaidia kuazisha miradi ya kiuchumi,” alisema Mheshimiwa Giga.

Aliongeza kuwa Serikali iendelee kutenga bajeti zaidi ya uwezeshwaji wa vikundi vya vijana kwa kuwa vina tija na vinapunguza tatizo la ajira kwa vijana kwa kiasi kikubwa.


Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Najma Giga akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo pamoja na watendaji wa halmashauri ya Morogoro walipotembelea Mkoa huo kwa lengo la kukagua miradi ya vijana walionufaika na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Mikopo kupitia mapato ya ndani ya halmashauri.

Sambamba na hayo Kamati hiyo iliitaka Ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kutoa maelekezo katika halmashauri zote kuelimisha vijana zaidi ili waweze kutambua taratibu za kupata mikopo kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana na asilimia 10 ya mikopo ambayo utolewa kwa Vijana 4%, Wanawake 4% na Wenye Ulemavu 2% kupitia mapato ya ndani ya halmashauri.

Akitoa maelezo ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde ameihakikishia Kamati ya Bunge kwamba Serikali itaendelea kuviwezesha kiuchumi vikundi vya vijana katika mkakati wa kuhamasisha vijana kujiajiri lakini pia kuwajengea uwezo wa kiuchumi vijana ili nao pia washiriki kikamilifu katika mnyororo mzima wa uchumi wa viwanda ambapo matarajio ni kwamba ifikapo mwaka 2025 zaidi ya asilimia 40 ya nguvukazi iwe imeajiriwa kwenye sekta ya viwanda.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde akielezea jambo kwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria walipofanya ziara ya kukagua miradi ya vijana Mkoani Morogoro. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Najma Giga

“Serikali iliazisha mfuko wa maendeleo ya vijana na programu mbalimbali ili kuwawezesha wananchi hususan vijana kuweza kupata mahitaji ya mitaji ya kuanzisha shughuli za kiuchumi zitakazo waingizia kipato,” alisema Mavunde

Akitolea mfano mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vijana kutumia teknolojia ya kitalu nyumba ni mkakati mzuri ambao Serikali imekuja nao katika kutatua tatizo la ajira kwa vijana kupitia sekta ya kilimo.

Kiongozi wa Kikundi cha Vijana cha Mazimbu Agro Enterprise Bw. Alexander Jokonia (wa nne kutoka kushoto) akifafanua jambo kwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria walipowatembelea katika eneo lao la kazi kujionea miradi ya kiuchumi inayofanywa na vijana katika Mkoa wa Morogoro. Kikundi hicho kimenufaika na mkopo kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Vijana unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Najma Giga wakipitia taarifa ya mradi wa vijana wa Mazimbu Agro Enterprise. (Katikati) ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde.

Aidha, Naibu Waziri Mavunde aliwahamasisha vijana kuandaa maandiko ambayo yataelezea shughuli zenye tija wanazotaka kuzifanya katika kujileta maendeleo ili waweze kupata mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya vijana na Mikopo kupitia mapato ya ndani ya halmashauri itakayowasaidia kuendesha shughuli zao.  

Kwa nyakati tofauti vijana wa Mkoa wa Morogoro wameishukuru Serikali kwa uwezeshaji kupitia Mfuko wa maendeleo ya vijana na kuomba kuwezeshwa zaidi ili kukidhi matarajio yao ya uanzishwaji wa viwanda katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tano katika uchumi wa viwanda.

Kiongozi wa Kikundi cha Vijana cha Faraja Carpentry Bw. James Luwanda akionyesha vitendea kazi wanavyotumia kutengeneza bidhaa zao. Kushoto ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde. (Wa pili kutoka kushoto) ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Najma Giga.
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria wakipata maelezo kutoka kwa Kiongozi wa Kikundi cha Vijana cha Faraja Carpentry Bw. James Luwanda namna wanavyobuni urembo (nakshi) katika meza ya chakula “Dinning Table”.


Sunday, October 27, 2019

MAKAMU WA RAIS MHE. SAMIA AFUNGUA SEMINA YA WABUNGE WANAWAKE AFRIKA




 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akifungua Semina ya Siku nne kwa Wabunge Wanawake wa Jumuiya ya Madola Kanda ya Afrika kuhusu  Juu ya kuhamasisha Wajumbe Wanawake katika masuala mbalimbali ya kuboresha Ushirikiano wa Wanawake katika Michakato ya kuongeza Idadi  yao kwenye Vyombo vya Maamuzi  hususan Bungeni, Jumla ya wajumbe kutoka Nchi 18 za Jumuiya ya Madola kanda ya Afrika wanashiriki kwenye Semina hiyo iliyofunguliwa  leo 27 Octoba 2019 katika Ukumbi wa  Gran Malia Jijini Arusha.  

 
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Wajumbe wa  Semina ya Siku nne kwa Wabunge Wanawake wa Jumuiya ya Madola Kanda ya Afrika kuhusu  Juu ya kuhamasisha Wajumbe Wanawake katika masuala mbalimbali ya kuboresha Ushirikiano wa Wanawake katika Michakato ya kuongeza Idadi  yao kwenye Vyombo vya Maamuzi  hususan Bungeni, baada ya kufungua Semina hiyo Jumla ya wajumbe kutoka Nchi 18 za Jumuiya ya Madola kanda ya Afrika wanashiriki kwenye Semina hiyo iliyofunguliwa  leo 27 Octoba 2019 katika Ukumbi wa  Grand Malya Jijini Arusha.  (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

RAIS DKT. MAGUFULI AONGOZA MAPOKEZI YA NDEGE MPYA YA BOEING 787-8 DREAMLINER JIJINI DAR ES SALAAM

RAIS Dkt. John Magufuli amesema Tanzania itaendelea kutekeleza kwa kasi kubwa miradi ya maendeleo nchini kwa kuwa Serikali imeimarisha nidhamu katika usimamizi na matumizi ya rasilimali zilizopo pamoja na ukusanyaji wa kodi.


Akizungumza katika hafla ya upokeaji wa ndege mpya ya Serikali ya Boeing 787-8 Dreamliner katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere leo Jumamosi (Oktoba 26, 2019) Jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli aliwataka Watanzania kujivunia na kuendelea kuiunga mkono Serikali yao kwa kuwa imedhamiria kuwaletea maendeleo ya kweli na ya haraka.




Rais Magufuli alisema Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla lina uwezo wa kufanya mambo makubwa  nay a haraka kutokana na kubarikiwa na rasilimali nyingi ikiwemo madini na hivyo Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kusimamia rasilimali hizo ili ziweze kuleta manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi walio wengi.




‘’Watanzania sisi ni matajiri tunaweza kufanya mambo makubwa na kununua vitu vizito kama ndege hizi, na tukiamua tunaweza kinachotakiwa sasa ni kuweza kuwa na matumizi mazuri ya fedha zinazopatikana kutokana na kodi tunazokusanya kutoka kwa wananchi wetu’’ alisema Rais Magufuli.




Aliongeza kuwa malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa sekta ya usafiri wa anga inapiga hatua kubwa ya maendeleo nchini na kwa kufanya hivyo Serikali imekusudia kuliwezesha Shirika la Ndege Nchini ATCL kuweza kutekeleza mipango na mikakati mbalimbali iliyojiwekea.




Akifafanua zaidi Rais Magufuli alisema ATCL kwa sasa ina jumla ya ndege 7 kati ya ndege 11 zilizopangwa kununuliwa na Serikali, hivyo aliitaka Menejimenti ya Shirika hilo kujipanga vizuri ili kuhakikisha kuwa linamudu ushindani wa kibiashara uliopo nchini ikiwemo kuimarisha mtandao wa usafirishaji abiria katika soko la ndani na nje ya nchi.




Kwa mujibu wa Rais Magufuli alisema ndege hiyo mpya ya Boeing 787-8 Dreamliner ni ndege kubwa ya kisasa yenye uwezo wa kubeba abiria 262 ikiwemo abiria 22 wa daraja la juu pamoja abiria 240 katika daraja la kawaida, hivyo kuitaka ATCL kuweka mipango na mikakati endelevu ya kuhakikisha itangaza vyema vivutio vya utalii vilivyopo nchini.




‘ATCL hamna budi kujiendesha kibiashara na mnapaswa kutambua ndege hii ni mali ya Serikali na si ya ATCL hivyo na hilo linajionesha katika mkataba tuliosaini baina ya Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu Mkuu (Uchukuzi), hivyo hakikisheni mnafikia malengo yote tuliyowekeana’’ alisema Rais Magufuli.




Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dkt. Leonard Chamuriho alisema Shirika la ATCL limeendelea kutekeleza kwa mafanikio makubwa Mpango Mkakati wa Shirika hilo, ambapo sasa limeweza kufikia mafanikio ya asilimia 73 la usafirishaji wa abiria katika soko la ndani.




Aidha Dkt. Chamuriho anaongeza kuwa kutokana na kuongezeka kwa idadi ya safari za abiria nje ya nchi, Shirika hilo pia limefanikiwa kuongeza idadi ya upokeaji wa shehena za mizigo kutoka nchini India na kufikia tani 178 na kuzisafirisha katika nchi mbalimbali ikiwemo Zambia.




Aliongeza kuwa Shirika hilo limepanga kushirikiana na Taaasisi ya Sekta Binafsi Nchini (TPSF) pamoja na Chemba ya Biashara,Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) kwa ajili ya kuweka nguvu na mkakati wa pamoja wa kuhakikisha kuwa inatanua mtandao wa usafirishaji wa shehena za mizigo nchini India.




Kuhusu soko la ndani, Dkt.Chamuriho aliongeza kuwa Shirika hilo limeweza kuongeza kituo cha usafirishaji wa abiria katika Kituo cha Mpanda Mkoani Rukwa pamoja na kupanga kuongeza idadi ya miruko ya ddege kutoka Dar es Salaam-Dodoma kufikia mara nne kwa siku ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.




Naye Kaimu Balozi wa Marekani Nchini , Dkt. Imni Patterson aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kutokana na juhudi na hatua mbalimbali za makusudi inazochukua katika kuimarisha sekta ya usafiri wa anga kwani kwa kufanya hivyo kutaweza kutangaza sekta ya utalii pamoja na kuimarisha uchumi.

MATUKIO KATIKA PICHA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na viongozi wengine na wadau akikata utepe kuashiria kupokewa kwa ndege mpya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam Jumamosi Oktoba 26, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mkuu wa Majeshi Jenerali Venance Mabeyo wakisiliza maelezo toka kwa Kepteni Dennis Mshami mmoja wa Marubani walioileta ndege mpya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner kutoka Seattle Marekani hadi katika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam Jumamosi Oktoba 26, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na viongozi wengine katika picha ya pamoja na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama alipoongoza wananchi katika mapokezi ya ndege mpya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam  Jumamosi Oktoba 26, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na viongozi wengine katika picha ya pamoja na marubani na wanaanga waliokuja na ndege wakati alipoongoza mamia ya wananchi katika mapokezi ya ndege hiyo mpya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam  Jumamosi Oktoba 26, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na viongozi wengine katika picha ya pamoja na Viongozi wa Dini alipoongoza mamia ya wananchi katika mapokezi ya ndege mpya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam Jumamosi Oktoba 26, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na viongozi wengine katika picha ya pamoja na Wakuu wa Wa Taasisi Mbalimbali za Umma na Binafsi alipoongoza wananchi katika mapokezi ya ndege mpya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Jumamosi Oktoba 26, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipongezwa na Mzee Omary Mkali, mmoja wa wazee waliofika katika mapokezi ya ndege mpya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam  Jumamosi Oktoba 26, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika kiti cha rubani Boeing 787-8 Dreamliner alipoipokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam Jumamosi Oktoba 26, 2019
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Kepteni saidi Hamadi mmoja wa Marubani walioleta ndege ya Boeing 787-8 Dreamliner kuoka Seattle Marekani alipoipokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam  Jumamosi Oktoba 26, 2019
Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli na Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa wakifurahia jambo baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuipokea ndege mpya ya Boeing 787-8 Dreamliner katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam  Jumamosi Oktoba 26, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mkuu wa Majeshi Jenerali Venance Mabeyo ndani ya Boeing 787-8 Dreamliner alipoipokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam  Jumamosi Oktoba 26, 2019
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mkuu wa Majeshi Jenerali Venance Mabeyo kwenye viti vya marubani wa Boeing 787-8 Dreamliner alipoipokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam  Jumamosi Oktoba 26, 2019.   



PICHA NA IKULU