Matokeo chanyA+ online




Friday, January 29, 2021

WAZIRI KALEMANI ATOA MIEZI 6 KWA MKANDARASI WA KITUO CHA KUPOZA UMEME LUGURUNI KUKAMILISHA UJENZI

Na Dorina Makaya - Dar-es-salaam

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani ametoa miezi 6 kwa Mkandarasi anayejenga kituo kipya cha Kupoza umeme Luguruni kukamilisha ujenzi wa kituo hicho.

Waziri Kalemani ametoa agizo hilo tarehe 28 Januari, 2021 alipofanya ziara kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho jijini Dar-e-salaam.


 

Waziri Kalemani amebainisha kuwa, Mradi mzima wa kujenga kituo hiki cha kupoza umeme Luguruni utagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 15.2 na kuwa fedha hizo zimetolewa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100.

Waziri Kalemani amefafanua kuwa, ameamua kutembelea kituo hicho ili kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho kutokana na umuhimu wake hasa kitakapokamilika.

Waziri Kalemani amesema, hapa nchini tunajenga vituo vingi sana vya kufua umeme ama kupoza umeme. “tumeshajenga vituo zaidi ya 134 mpaka sasa na tumekamilisha vituo vipya 24 hivi karibuni vikiwemo vya Singida, Rusumo, Nyakanazi na vingine na tunaendelea kujenga vituo vingine vya kupoza umeme zaidi ya 24 vipya ambavyo navyo vitakamilika ndani ya miezi sita hadi minane inayokuja” amesema Dkt. Kalemani.

Waziri Kalemani amesema, lengo la kujenga hivi vituo vya kupoza umeme, ni kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa kutosha, wa uhakika na unaotabirika wakati wote.

Waziri Kalemani amesema, Kituo cha Luguruni ni muhimu sasa. Amesema, kwa Dar-es-salaam peke yake na Pwani, hadi sasa tuna vituo takriban 11 vya kufua na kupoza umeme. Dkt. Kalemani amefafanua kuwa, vituo vya kupoza na kufua umeme kazi yake ni kuwafikishia watumiaji umeme wa uhakika na unaotabirika baada ya kutoka kwenye uzalishaji wake.

Waziri Kalemani amebainisha kuwa, pamoja na kuwa na tuna vituo vya Ubungo I, Ubungo II, Tegeta, Kunduchi, Ilala, Kurasini, Ilala na tunajenga Dege, lakini kituo hiki kilikosekana kwa muda mrefu.

Amesema, Kituo cha Luguruni ndio kituo muhimu sana kwa maeneo ya Dar-es-salaam kwa kuwa kinakwenda kuhudumia maeneo mengi zaidi. Dkt. Kalemani amesema, kituo cha Luguruni kitachocha na kupoza umeme ambapo laini ya kwanza itapeleka umeme maeneo ya maili moja mpaka kuelekea Chalinze na Mlandizi na laini ya pili itapeleka umeme maeneo ya Tegeta, kwenye Hospitali ya Mloganzila hospitali ya rufaa, ambayo ni hospitali muhimu sana.

Waziri Kalemani amebainisha kuwa, Hospitali ya Mloganzila ilikuwa inapata umeme kutoka Ubungo ambapo ni mbali sana na hivyo umeme uliokuwa unafika kwenye hospitali ya Mloganzila ulikuwa unafika tayari ukiwa hafifu.

Amesema Kituo hiki ni muhimu sana kwani kitapeleka umeme katika maeneo ya Mikoa ya Pwani na Dar-es-salaam ikijumuisha Hospitali ya Taifa ya Mloganzila, Msigani, Kibamba, Kibwegere, Kisarawe, Mail moja na maeneo ya viwanda. Waziri Kalemani ameongeza kuwa kukamilika kwa kituo cha Luguruni, kutaimarisha upatikanaji wa umeme katika maeneo hayo na kupunguza mzigo wa mashine nyingine za Ubungo, Songas na maeneo mengine mpaka Kinyerezi. “Kwa hiyo wananchi wa maeneo tajwa yatakayopokea umeme kutoka katika kituo hiki wataanza kupata umeme wa kutosha na wa uhakika ndani ya miezi sita kuanzia sasa.” Amesisitiza Dkt. Kalemani.


WAMAASAI WANUFAIKA WA MKURABITA WAELEZEA WALIVYOKOPA BENKI KUTUMIA HAKIMILIKI ZA KIMILA MBARALI


Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mpango wa Urasimishaji wa Ardhi na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita), Balozi mstaafu, Daniel Ole Njoolay (kushoto), akizungumza na wafugaji wenye jamii ya kimasai Talas Taikoo (kulia) na Tirike Sandetwa wanufaika wa Mkurabika waliokopa fedha benki kwa kutumia Hati Hakimili za kimila wilayani Mbarali.
                                           Talas Taikoo

                                        Tirike Sandetwa

Na Richard Mwaikenda, Mbarali

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mpango wa Urasimishaji wa Ardhi na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita), Balozi mstaafu, Daniel Ole Njoolay (kushoto), akizungumza na wafugaji wenye jamii ya kimasai Talas Taikoo (kulia) na Tirike Sandetwa wanufaika wa Mkurabika waliokopa fedha benki kwa kutumia Hati Hakimili za kimila wilayani Mbarali.


Tukio hili lilitokea Januari 26,2021 katika Ofisi za Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya baada ya mkutano na viongozi wa halmashauri pamoja na wadau walionufaika kwa kutumia Hakimiliki za kimila kukopea mkopo benki.


Ndugu mdau nakuomba uendelee kuwasikiliza wanufaika hao wa Mkurabita wakielezea kupitia clip hii ya video jinsi walivyonufaika kimaisha na fedha walizokopa kupitia Hati za Hakimiliki za kimila.


FEDHA ZACHELEWESHA NHC KUKAMILISHA MRADI HOSPITALI YA RUFAA MARA


Na Munir Shemweta, WANMM MUSOMA

 

Imebainika kuwa kuchelewa kupelekwa fedha katika mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara iliyopo eneo la Kwangwa kumesababisha Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kutokamilisha mradi huo kwa wakati.

 

Mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara ulianza kujengwa  na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Septemba 15, 2019 na kutarajiwa kukamilika Agosti 2020 ambapo hata hivyo Mkandarasi (NHC) aliomba kuongezewa muda wa miezi sita (6) kutokana na kazi zilizoongezeka nje ya mkataba pamoja na kuchelewa kupatikana Wakandarasi maalum wa mradi.

 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akisalimiana na akina mama waliopeleka watoto wao kupata huduma katika Bawa C la Huduma ya Mama na Mtoto katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mara wakati  akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa hospitali hiyo tarehe 28 Januari 2021 akiwa katika ziara ya siku moja katika mkoa wa Mara. (PICHA NA MUNIRI SHEMWETA WIZARA YA ARDHI)

Akiwa katika ziara ya siku moja katika mkoa wa Mara tarehe 28 Januari 2021 kukagua utendaji wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ukusanyaji kodi ya Pango la ardhi, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula  alielezwa na Katibu Tawala wa mkoa Mara Catherine Mthapura akiwa kwenye ofisi ya Mkuu wa mkoa kuwa, awali mradi huo ulikuwa ukiendelea vizuri lakini sasa kasi ya mradi huo imepungua kutokana na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kutopatiwa fedha za kutekeleza mradi huo kwa wakati na Wizara ya Afya.

 

"Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limefanya kazi kubwa ikiwemo kutumia fedha za Shirika kuharakisha ujenzi wa hospitali lakini sasa tangu Bawa C (Wing C) kuanza kutoa Huduma za Mama na Mtoto kazi imesimama tangu Juni 2020" alisema Katibu Tawala mkoa wa Mara.

 

Kwa upande wake Mhandisi wa Mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa mkoa wa Mara Renard Kazoba alimueleza Naibu Waziri Dkt Mabula wakati akikagua mradi huo kwamba, changamoto kubwa ya kutokamilika mradi huo kwa wakati ni kuchelewa kwa malipo ambapo pamoja na Mkandarasi kuidhinishiwa malipo ya Shilingi Bilioni 3,591,565,635.35 ili kuharakisha utekelezaji mradi na  Mshitiri kutakiwa kumlipa mkandarsi ndani ya siku 28 kwa kadiri ya mkataba lakini hadi sasa hakuna kiasi kilicholipwa.

 

 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa hospitali ya rufaa mkoa wa Mara tarehe 28 Januari 2021 akiwa katika ziara ya siku moja katika mkoa wa Mara, kushoto ni Msimamizi wa mradi huo Mhandisi Renard Kazoba.

 

Hata hivyo, alibainisha kuwa katika kukabiliana na changamoto aliyoainisha, Shirika la Nyumba la Taifa limefanya vikao na wahusika wakuu wa mradi na kutolea mfano wa kikao kilichofanyika tarehe 6 Novemba 2020 baina ya Shirika na wahusika hao na kukubaliana mambo ambayo Shirika la Nyumba la Taifa linasubiri utekelezaji wake.

 

Aidha, Kazoba alisema,  NHC imenunua Jenereta 250 KVA pamoja na vifaa vya kuliwezesha  kufanya kazi kwa kutumia fedha za ndani ili kufanikisha upatikanaji umeme wa uhakika katika jengo Bawa C.

 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula  alisema Shirika la Nyumba la Taifa ili liweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo linahitaji kupata fedha kwa wakati kupitia miradi inayotekeleza hasa ikizingatiwa halipokei ruzuku kutoka serikalini na kusisitiza kuwa lisipowezeshwa litashindwa kutekeleza miradi yake.

 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipata maelezo ya maendeleo ya ujenzi wa mradi wa hospitali ya rufaa mkoa wa Mara kutoka kwa Msimamizi wa mradi Mhandisi Renard Kazoba (kushoto) alipokwenda kukagua mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo akiwa katika ziara ya siku moja katika mkoa wa Mara tarehe 28 Januari 2021.

 

 Alisema, katika utekelezaji mradi wa ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara Shirika la Nyumba la Taifa linatakiwa kukamilisha mradi huo kwa gharama ya shilingi bilioni 15,082,481, 832.82  na hadi sasa zimelipwa bilioni 8,469,851,800.34 na kiasi kilichobaki ni bilioni 6,612,630,032.48 huku NHC ikiwa imetumia fedha zake za ndani  shilingi Bilioni 3,591,565,635.35 na kusisitiza kiasi hicho kisipolipwa shirika litashindwa kufanya kazi.

 

"Lengo la Shirika ni kufanya kazi bila kukwama na kukamilisha miradi yake kwa wakati naagiza Shirika kuhakikisha linawafuatilia Wadaiwa wote sugu wa kodi za nyumba za Shirika ili kuiwezesha NHC kupata fedha ya kutekeleza miradi yake" alisema Dkt Mabula.

 

Kaimu Mganga Mkuu katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Mara Dkt Lazoro Mwikabe alisema, tangu hospitali hiyo kuanza kutoa huduma katika sehemu ya Bawa C ( Wing C) zaidi ya watoto 1000 wamezaliwa na wananchi wa mkoa wa Mara wana imani kubwa na huduma za hospitali hiyo.

 

Aliongeza kwa kusema kuwa, hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara imejipanga na iko katika mazungumzo na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHF) ili kupatiwa mkopo wa kununua mashine ya CT Scan. 

 

Shirika la Nyumba la Taifa linadai takriban bilioni 27 kutoka kwa wapangaji wa nyumba mbalimbali nchini huku likitekeleza miradi mikubwa ya Serikali ya kimkakati ya  Hospitali za Rufaa za mkoa wa Mtwara na Mara sambamba na ujenzi wa miradi ya nyumba na ofisi za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Thursday, January 28, 2021

MWAMBE AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA MKURUGENZI WA CTI LEODEGAR TENGA

 


 

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Geoffrey Idelphonce Mwambe (Mb), tar 27 Januari, 2020 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) Ndugu, Leodegar Tenga.

Mhe. Mwambe mefurahishwa na jinsi taasisi za sekta binafsi zinavyoshirikiana na serikali ili kufikia adhma ya kuifanya nchi yetu kuwa ya Viwanda.

Aidha Mhe. Mwambe amesema kuwa serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi hasa katika kuhakikisha mazingira bora kwa wawekezaji kwa kutatua changamoto zinazowakabili.

Katika mazungumzo hayo Leodegar Tenga amesema kuwa lengo la kukutana na Mhe. Waziri ni kueleza Majukumu ya Shirikisho ambayo ni kusukuma Maendeleo ya Viwanda nchini.

Leodegar Tenga ametoa ahadi kwa Serikali ya kuunga mkono mipango ya nchi kutumia Viwanda kama mhimili wa uchumi na kuhamasisha matumizi ya bidhaa zinazozalishwa ndani ya Nchi. Ameeleza kuwa, CTI inaishukuru Serikali ya awamu ya tano ambayo imetilia mkazo Maendeleo ya Viwanda nchini.

“Nimefarijika Sana kwa mawazo kutoka kwa Mhe. Waziri na nna imani Mhe. Mwambe atatufikisha katika malengo ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda kama ilivyo kauli mbiu ya Rais wetu Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli” Leodegar Tenga.

Katika kikao hicho kilichofanyika ofisi za Wizara Mtumba, ndugu Leodegar Tenga amekabidhi kwa waziri wa Viwanda na Biashara, 1. Mpango mkakati wa kuendeleza Viwanda nchini, 2. Kanuni za maadili ya wanachama wa Shirikisho la wenye Viwanda nchini (CTI) na
3. Jarida ambalo linatangaza mafanikio ya serikali na azma ya kujenga Tanzania ya Viwanda, mchango wa Serikali kuendeleza Viwanda na kutangaza bidhaa zinazozalishwa nchini.

KAMATI YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII YAKUTANA NA TAASISI ZILIZO CHINI YA WIZARA YA ELIMU


Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini HESLB Ndg. Abdul-Razaq Badru akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa bodi hiyo kwenye Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwenye Ukumbi wa Msekwa Bungeni Jijini Dodoma. (Picha na Ofisi ya Bunge)
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii wakifuatilia jambo wakati wakipokea taarifa ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwenye Ukumbi wa Msekwa Bungeni Jijini Dodoma. (Picha na Ofisi ya Bunge)
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania Dkt. Charles Msonde akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa baraza hilo kwenye Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwenye Ukumbi wa Msekwa Bungeni Jijini Dodoma. (Picha na Ofisi ya Bunge)

Wednesday, January 27, 2021

RC NCHIMBI AWATAFAKARISHA WATENDAJI WA MAHAKAMA YA MIAKA 100, AAGIZA TAKUKURU KUANZA KUWAMULIKA “BUSH LAWYERS”


Mkuu waMkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akihutubia kwenye sherehe zamaadhimisho ya uzinduzi wa wiki ya sheria, kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Kiomboi juzi.
Nchimbi akiwa na viongozi mbalimbali w amahakama na serikali kwenye maadhimisho hayo
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Luhaula akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Dkt Rehema Nchimbi akihutubia kwenye sherehe za maadhimisho ya uzinduzi wa wiki ya sheria mwaka huu, kwenye viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida.
Mkuu wa Mkoa akitembelea moja ya banda la wadau wa mahakama linalojishughulisha na kazi za usaidizi wa msaada wa kisheria wilaya ya Singida.
Akiwa kwenyebanda la Jeshi la Magereza.
Akiwa kwenye banda la Watumishi wa Mahakama.
Baadhi ya Watumishi na Mahakimu wa Wilaya ya Iramba wakifuatilia matukio mbalimbali kwenye uzinduzihuo
Wananchi kutoka Taasisi na Asasi mbalimbali wakishiriki maadhimisho hayo
Mada mbalimbali zikiwasilishwa.

Sherehe zauzinduzi zikiendelea.

Na Godwin Myovela, Singida

Mkuu waMkoawaSingida Dk. Rehema Nchimbi ameiagizaTaasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuanza mara moja msako wa kuwabaini na kuwachukulia hatua Mawakili na Mahakimu Umiza walioko mitaani maarufu‘Bush Lawyers’ ambao wamekuwa kikwazo kwa kushawishi, kuwatoza tozo kubwa na kuwavuruga raia ili wakatae, wakinzane au kutokukubaliana na mienendo halali ya kesi zinazoamriwa na mahakama kwa mujibu washeria.

Nchimbi alitoa agizo hilo kwa nyakati tofauti wakati akizindua maadhimisho ya wiki ya sheria kwa Wilaya za Iramba na Singida juzi, huku akisisitiza kwa kuwataka Takukuru kuanza kuwatafuta na kuwashughulikia watu hao kwa mujibu wa sheria kama walivyofanikiwa kudhibiti Wakopeshaji Haramu.

“Haiwezekani hata kidogo tukaendelea kufumbia macho jambo hili. Hawa mawakili umizana mahakimu uchwara huko mtaani wanaumiza sanawatu…wanawadanganya na wakati mwingine kusababisha mienendo ya kesi kubadilika mara kwa mara, hawa ni wavurugaji wakubwa wa mashauri!” alisema Mkuu wa Mkoa.

Akitoa tafakuri na tathmini juu ya maadhimisho hayo kuelekea kilele cha siku ya sheria mwaka huu, na mantiki ya umri wa miaka 100 ya mahakama katika muktadha wa uwiano wa haki nchini, Nchimbi alianza kwa kusema miaka hiyo ni faraja, ni sherehe na ni kitu cha kujivunia.

Alisema kwenye michezo ya  burudani siku zote mashabiki wananafasi kubwa ya kucheza wakiwa nje ya uwanja kuliko hata wachezaji wenyewe, na wakati mwingine mashabiki hao hao wanasahau kwamba jukumu la timu linawahusu na wao pia, wanafikiri wapo nje ya uwanja hapana!..na wao wapo ndani.

Nchimbi alisema asili ya sheria ni Mungu mwenyewe. Au kwa maana nyingine Mungu ni Sheria. Kama mwanadamu atamtii Mungu basi atazitii, atazifahamu, atazipenda, atazienzi, ataziheshimu na kuziishi sheria.

Alisema kila kilichoumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu hapa duniani kimeumbwa kwa kufuata sheria. 

Mkulima hawezi kustawisha mazao na kupata mavuno mengi kama atavunjasheria. 

Mfugaji hawezi kumudu kufuga ipasavyo bila kufuata sheria, mvuvi vile vile na kadhalika. 

Viungo vyote vya mwili macho, moyo, utumbo, masikio, miguu na kila kitu kimewekwa na kipo pale kwa mujibu washeria.

Aliwahamasisha Watendaji wa Mahakama kuongeza kasi ya kutoa elimu ili jamii ijue na kuzingatia sheria kwa ustawi wa haki na wajibu. 

“Pia watu wafahamishwe kuwa haya mambo ya kesi hayana shortcut (njiazamkato) nilazima jamii izingatie utii wa sheria bila shuruti kwa faida ya wewe, yule na mimi-kiusalama na kwa ustawi wa maendeleo.”

“Ikiwezekana hata Jeshi la Magereza nalo natamani siku moja livunje ule ukuta wa gereza kwa kuwachukua na kuwapeleka wafungwa hao wakiwa hivyo hivyo na sare zao kuchanganyikana na raia kwenye makanisa, misikiti na mashuleni ili watu na jamii ione kwa macho, iguswe na kujifunza madhara ya kubaka, kulawiti, kuiba, rushwa na aina nyingine ya makosa endapo mtu atavunja sheria,” alisema

 

Nchimbi alisema mahakama au kutimiza miaka 100 bado haitoshi kama watu hawatazipenda, hawata zingatia na kuziishi sheria. 

Ifike mahali tujiulize mathalani hata unapoajiriwa au kujiajiri ili kila jambo liende sawa sawa na kwa utaratibu mzuri ni lazima mahali hapo pawekwe sheria. Miaka hii100 itutafakarishe na kutuongoza kutathmini  kama taifa kwanini sheria? inamhusunani? na kwanini miaka 100 ya kutafsiri sheria? 

Na kwa muktadha huo, mchango wa mahakama katika Ustawi wa Tanzania ya amani, uhuru, udugu, demokrasia bora, utawala wa sheria, ustawi wa uchumi utaonekana kudhihirika…na mashabiki walio nje ya uwanja wataunga na nawachezaji, sote tutajiona tupo ndani ya uwanja, tutajiona ni sehemu ya mchezo husika, na tutazingatia.

Maadhimisho ya wiki ya sheria mpaka sasa yanaendelea kwenye maeneo mbalimbali katika wilaya mbalimbali za mkoa wa Singida kwa kwa watumishi na wadau mbalimbali wa mahakama kutoa elimu na huduma za msaada wa kisheria, sambamba na kutathmini kwa pamoja dhima kuu ya mwaka huu isemayo“Miaka 100 ya Mahakama Kuu: Mchango wa Mahakama katika kujenga nchi inayozingatia uhuru, udugu, amani na ustawi wa wananchi.”

UBUNIFU WENYE TIJA KWENYE TAASISI UMESAIDIA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WADAU - WAZIRI BASHUNGWA


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa akijibu  hoja za  Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii  kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu  Taasisi za Wizara yake baada ya  Kamati hiyo kupokea  Muundo na Majukumu ya Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo Januari 26, 2021  Jijini Dodoma. Kulia ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Abdallah Ulega na Kushoto ni Katibu Mkuu na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.Hassan Abbasi.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Abdallah Ulega akitoa maelezo kuhusu hoja mbalimbali zilizohojiwa na Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Taasisi za Wizara yake baada ya Kamati hiyo kupokea Muundo na Majukumu ya Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo Januari 26, 2021 Jijini Dodoma. Kulia ni Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Innocent Bashungwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe. Stanslaus Nyongo ambaye ni Mbunge wa Maswa Mashariki akizungumza baada ya kupokea taarifa ya Taasisi za  Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo zilizowasilishwa na Wakuu wa Taasisi hizo kwa kamati hiyo Januari 26, 2021  Jijini Dodoma .

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali  Dkt. Hassan Abbasi akifafanua masuala mbalimbali yaliyowalisilishwa na wajumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu   Muundo na Majukumu ya  Taasisi za Wizara hiyo Januari 26, 2021  Jijini Dodoma.

Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii wakiwa katika kikao cha kupokea   Muundo na Majukumu ya Taasisi za Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo hiyo Januari 26, 2021  Jijini Dodoma.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Wizara yake baada ya kumaliza kikao na Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii  kuhusu Muundo na Majukumu ya Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo Januari 26, 2021  Jijini Dodoma.


Na Shamimu Nyaki – WHUSM,Dodoma.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amesema ubuninifu wa kitendaji unaofanywa katika Taasisi za Wizara hiyo unaendelea kuleta mafanikio kwa wadau na Taifa.

Mhe.Bashungwa ameyasema hayo leo Jijini Dodoma wakati akijibu hoja za wajumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii wakati ilipopokea taarifa ya Muundo na Majukumu ya Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo.

Akiendelea kuzungumza, Mhe. Waziri Bashungwa amesema kuwa lugha ya Kiswahili inaendela kukua na imeendelea kutangaza nchi yetu.

“Ushirikiano kati ya COSOTA na TCRA ni jambo la msingi katika kusimamia kazi na maslahi ya wasanii ikiwemo kupatikana kwa mapato yanayotokana na kazi zao” alisema Mhe. Bashungwa.

Kwa upande Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Abdallah Ulega ameishukuru Kamati hiyo kwa mawazo na michango yao katika kusimamia Sekta zilizochini ya wizara hiyo pamoja na Taasisi zake, huku akiwashauri wajumbe hao kuwa mstari wa mbele katika kukuza michezo katika maeneo wanayotoka pamoja na kusimamia maadili mila pamoja na desturi za nchi.

 “Kesho Taifa Stars itakua uwanjani dhidi ya timu ya Guinea katika muendelezo wa mashindano ya CHAN,  nawasihi Watanzania tuiombee na kuitia moyo timu yetu na tusiwe watu wa kuishambulia kwakua ni vijana ambao tumewaamini katika kuiwakilisha nchi yetu” alisema Mhe.Ulega.

Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Stanslaus Nyongo ambaye ni Mbunge wa Jumbo la  Maswa Mashariki amelipongeza Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC)  kwa kutoa habari zenye ukweli na uhakika kwa wananchi, huku akilipongeza Baraza la Kiswahili la Taifa ( BAKITA) kwa kuendelea na kukuza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi.

Katika kikao hicho Wajumbe wa Kamati hiyo wametoa maoni ya kuendeleza Sekta na Taasisi  za Wizara hiyo ikiwemo kuongeza ubunifu, rasimali watu na miondombinu ya kufanyia kazi  pamoja na kusimamia vyema maslahi ya wadau inayowasimamia katika kuongeza vipato vyao pamoja na  kukusanya mapato ya Serikali.

TAKUKURU SINGIDA YAOKOA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 270


Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda (katikati) akitoa taarifa ya utekelezaji kwa kipindi cha miezi mitatu Oktoba hadi Disemba 2020 mkoani hapa juzi.

 Na Dotto Mwaibale, Singida

Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida imeokoa zaidi ya shilingi 270.7 kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo mikopo umiza.

Akitoa taarifa ya utekelezaji kwa kipindi cha miezi mitatu Oktoba hadi Disemba 2020 Mkuu wa Taasisi hiyo Mkoani hapa Adili Elinipenda alisema Takukuru imeokoa shilingi milioni 270,079,600 ndani ya kipindi hicho kutoka maeneo mbalimbali.

Elinipenda alisema shilingi milioni 154,416,000 pekee zimeokolewa kutoka mikopo umiza, shilingi milioni 28,000,000 ziliokolewa kutokana na fidia ya maeneo ya wananchi yaliyotwaliwa kufanya shughuli za uchimbaji madini Wilayani Mkalama,wakati kiasi kingine kikiokolewa kutoka maeneo mengine ikiwemo mahakama ya Manyoni.

"Fedha hizi tulizikabidhi kwa wahusika baada ya kuokolewa ambapo fedha tulizoziokoa kutoka mikopo umiza, Mkuu wa Mkoa Dk Nchimbi aliwakabidhi wananchi hao wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani Manispaa ya Singida." alisema Elinipenda.

Alisema katika kuhakikisha Vitendo vya Rushwa vinaisha Takukuru kwa kushirikiana na wadau wengine imeendelea kutoa Elimu kwa jamii kwa kushirikisha makundi mbalimbali ikiwemo Vijana wa shule za msingi, Sekondari na Vyuo.

Aidha Elinipenda alisema Taasisi hiyo imeanzisha utaratibu wa Takukuru inayotembea (MOBILE PCCB) ambapo itatenga siku moja ndani ya mwezi ili kuwatembelea wananchi kwenye maeneo yao lengo la kufanya hivyo ni kusikiliza na kutatua kero zao.

Hata hivyo Taasisi hiyo inazidi kutoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Singida kujiepusha na Vitendo vya Rushwa huku ikiwataka kushiriki kikamilifu katika kutoa taarifa za Vitendo hivyo pamoja na kutoa ushirikiano kwenye uchunguzi na kutoa ushahidi mahakamani

WADAU WA TIBA ASILI WATAKIWA KUCHANGAMKIA SOKO LA DAWA ZAO KIMATAIFA


  Mkurugenzi msaidizi wa tiba asili na tiba mbadala kutoka wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Dkt. Paul Mhame akitoa hotuba ya uzinduzi wa jukwaa hili.

Naibu Mkamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA upande wa utawala na fedha Prof. Amandus Mhairwa akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kuzindua rasmi jukwaa.

Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko akitia neno kwa wagana hao wa tiba asili na wadau wengine wakati wa uzinduzi wa jukwaa hilo.

Mkuu wa mradi huo wa GRILI Dkt. Faitha Mabiki akieleza kwa kifupia majukumua na malengo ya mradi huo wa GRILI na yale ambayo yamefanyika toka mradi uanzishwe.

  

Wadau wa tiba sili na tiba mbadala kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania wakifuatilia hotuba na maneno ya uzunduzi wa Jukwaa lao kutoka kwa viongozi.


Na Calvin Gwabara,   Morogoro.

Wataalamu wa chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA wametakiwa kushirikiana na wataalamu wa tiba asili na taasisi zingine katika kufanya tafiti za dawa ambazo zitasaidia dunia katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa COVID 19 na magonjwa mengine hatari kwa afya ya binadamu,Wanyama na hata mimea kwani  takwimu nchini Tanzania zinaonyesha tiba asili  inatoa mchango wa zaidi ya asilimia 45 katika unga wa matibabu.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi msaidizi wa tiba asili na tiba mbadala kutoka wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Dkt. Paul Mhame kwa niaba ya Katibu mkuu wa wizara hiyo wakati wa ufunguzi wa jukwaa la ubunifu la wadau wa tiba asili Tanzania uliofanyika SUA mkoani Morogoro.

Dkt.Mhame amesema kuwa Tiba asili inayo nafasi kubwa katika kukabiliana na magonjwa hayo ikiwa ni pamoja na kutafuta namna ya kuzuaia na kutibu na ndio maana kuna sheria ya tiba asili na tiba mbadala Na.23 2002.

“Upatikanaji a tiba asili na tiba mbadala inayotokana na mimea dawa itasaidia sana kufikia wananchi wengi hasa wanaoishi vijijini hivyo nimefurahishwa na malengo ya jukwaa hili kwani yanaendana na malengo ya serikali kupitia wizara yetu hii ya afya ya kuhakikisha tunaboresha afya za wananchi wetu kupitia za kisasa na tiba asili” Alisema Dkt. Mhame.

Amefafanua kuwa biashara ya tiba asili duniani inakuwa kwa kasi sana kwani kwa takwimu za shirika la fya duniani WHO zinasema mwaka 2000 mauzo yake yalikuwa dola za kimarekani bilioni 20,mwaka 2012 ilipanda na kufikia dola za kimarekani bilioni 60,Mwaka 2018 ikafikia dola bilioni 80 na sasa inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050 mauzo ya tiba asili yatafikia dola za kimarekani trilioni 3.

“Kwahiyo niwaombe sana ndugu zangu watafiti wa SUA na waganga wa tiba asili nchini kushirikiana ili kusaidia kujipanga vizuri ili Tanzania nayo inufaike kama China na nchi zingine duniani kwenye mauzo ya dawa za tiba asili wakati yakielekea kufikia Trilioni 3” Alisistiza Dkt. Mhame.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi huyo kuzindua jukwaa hilo Naibu Mkamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA upande wa utawala na fedha Prof. Amandus Mhairwa kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda amesema lengo la jukwaa hilo ni kuibua ubunifu nna kutatua changamoto zilizoko kwenye mnyaroro wa thamani wa biashara ya bidhaa za miti mimea dawa Tanzania ili iweze kuwa endelevu na kutoa mchango mkubwa kwenye kipato cha Wananchi na Tanzania kwa ujumla.

“Malengo ya Chuo chetu pia yanahusisha uendelezaji wa maarifa na ujuzi,bunifu,busaraza kitaalamu na uelewa kupitia mafunzo,matokeo ya tafiti,huduma za ugani  na ushauri wa kitaalamu na katika uzalishajiu  hivyo tunaamini kuwa uratibu wetu wa kuanzisha jukwaa hili uko kwenye mojawapo ya majukumu yetu na malengo ya uanzishwaji wa chuo chetu” Alifafanua Prof. Mhaurwa.

Aliongeza kuwa SUA kupitia watafiti wake kwenye mradi huu wamefanya tafiti nyingi ambazo zimeonesha kuwa kuna changamoto nyingi kwenye mnyororo mzima wa thamani wa biashara ya tiba asili na mimea dawa hasa ubunifu mchache unaoibuliwa kwenye biashara hii,SUA imeona ni vyema kutumia uzoefu wake wa ndani kwa kushirikiana na wadau wengine kuratibu uanzishwaji wa jukwaa hili.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko amewataka waganga hao wa tiba asili kuendelea kushirikiana na ofisi yake katika kupima viambata mbalimbali vinavyopatikana kwenye dawa zao ili kusaidia kuepusha madhara yoyote yanayoweza kutokea kwa wateja wao endapo dawa itakuwa na viambata ambavyo sio salama.

“Kazi ya ofisi yangu sio kuzuaia nyinyi kupata usajili wa dawa zenu bali tunataka kuona kila dawa mnayoitoa kwa wagonjwa iwe na viambata sahihi ili iweze kutibu vizuri na isilete madhara kwa wateja wenu lakini pia upimaji wetu ndio wa mwisho ili muweze kupata usajili wadawa tukiweka sahihi yetu kuwa dawa iko salama hakuna wa kupinga hivyo msiogope tushirikiane” Alisema Dkt. Mafumiko.

Mkemia mkuu huyo wa serikali alisema kuwa malengo ya waganga wa tiba asili na malengo ya ofisi yake ni moja tuu kuhakikisha usalama wa wananchi na watumiaji wa dawa hizo na ofisi yake inavyo vifaa na wataalamu wa kutosha kubaini kila kilicho kwenye dawa hivyo wale wachache wanaofanya udanganyifu waache maana watabainika.

Pia Dkt. Mafumiko ameipongeza SUA na watalaamu wake kwa jitihada kuwa wanazozichukua katika kuwasaidia waganga hao wa tiba asili kuweza kuboresha huduma ya tiba wanayoitoa kwa Jamii ili iweze kuwa bora na yenye viwango vinavyohitajika.

Mkemia mkuu huyo wa Serikali iliahidi kushirkiana na SUA kwenye mpango huo ili uweze kuleta tija inayokusudiwa kwa jamii na taifa kupitia wataalamu wa ofisi yake muda wowote watakapohitajika.

Kwa upande wake Mkuu wa mradi huo wa GRILI Dkt. Faitha Mabiki alisema kuwa toka mradi huo uanze mwaka 2018 umekuwa na mafanikio makubwa kwa wadau wa tiba asili Tanzania nab ado unaendelea kushirikiana nao kuhakikisha biashara ya tiba asili na mimea dawa inachangia uchumi wa wadau hao na taifa.

“ Wakati tunaanza mradi huu mwaka 2018 waganga wengi hapa wa tiba asili walikuwa wanauza dawa zao kwenye mkifuko ya Rambo,magunia na vifungashio vingine visovyo na ubora lakini tunafurahi leo wakati tunazindua jukwaa hili tunaona wote wameweka dawa kwenye vifungashio bora na vye viwango vinavyokubalika kitaalamu.”Alisema Alifafanua Dkt. Mabiki.

Aliongeza “Lengo letu ni kutaka kuona biashara ya mimea dawa na uuzaji wa dawa za asili haufanyiki tuu hapa nchini bali wataalamu hawa wa tiba asili waweze kufungasha vizuri na kuuza hadi nje ya nchi na kupata mapato wao wenyewe lakini pia na taifa kama ambavyo ilivyo kwa nchi nyingine duniani kama China na India”.

Dkt. Mabiki alisema ili hilo lifanikiwe pia lazima kuwe na uendelevu wa upatikanaji wa mimea dawa hiyo ili pale inapohitajika kwa wingi iweze kupatikana na ndio maana mradi unawafundisha namna ya kuanzisha mashamba ya mimea dawa ili waweze kulima na kuipata kwa wingi na kirahisi pale inapohitajika.

RAIS WA ZANZIBAR DK.HUSSEIN ALI MWINYI AKUTANA NA ASKOFU WA KANISA LA ANGLIKANA ZANZIBAR

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Baba Askofu wa Kanisa la Anglikana Mkunazini Jijini Zanzibar Askofu  Michael Hafidh, alipofika Ikulu kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi huo 26-1-2021.

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Baba Askofu wa Kanisa la Anglikana Mkunazini Jijini Zanzibar Askofu Michael Hafidh kulia kwa Rais akiwa na ujumbe wake Ndg.Edwin Mkwaya na Ndg.Luis Majaliwa, walipofika Ikulu kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu 26-1-2021

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi  akiagana na Baba Askofu wa Kanisa la Anglikana Jijini Zanzibar Askofu Michael Hafidh baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibaer na (kushoto kwa Rais) Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said.(Picha na Ikulu)