Matokeo chanyA+ online




Tuesday, July 30, 2019

MAKAMU WA RAIS AZINDUA MRADI WA KUTOKOMEZA UNYANYASAJI DHIDI YA WANAWAKE

Na Charles James, MICHUZI TV

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amezindua mradi wa kutokomeza vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji dhidi ya Wanawake na Watoto kwenye masoko na kushauri elimu iendelee kutolewa kupitia mikutano ndani ya Mitaa na Kata.

Hayo ameyasema leo jijini Dodoma wakati wa uzinduzi huo ambapo amesema katika kupambana na vitendo hivyo vya kikatili Serikali imeimarisha utendaji wa madawati 417 ya jinsia na watoto yaliyopo katika vituo vya Polisi nchini kwa lengo la kuwezesha huduma stahiki kwa watu wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia.

Mama Samia ameitaka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kushirikiana na Jumuiya ya Tawala za Mitaa ambao ndio waratibu wa mradi huo katika kuhakikisha afua zinazotekelezwa kupitia mradi huo zinakua endelevu hata pale utekelezaji wa mradi unapofikia mwisho.

" Ndugu zangu kila mmoja wetu ana haki ya kupinga na kutokomeza ukatili wa kijinsia, hivi vitendo havikubaliki na wala haviruhusiwi kisheria. Yeyote atakayethubutu kumdhalilisha mwanamke au mtoto tutamchukulia hatua kali.

" Ni jambo la aibu kuona tunatumia viungo vya wanawake kama matusi, huyu mwanamke unayemdhalilisha tukumbuke ni kama mama zetu majumbani mwetu, hatuwezi kuwa na Taifa lenye amani kama tutaruhusu vitendo hivi, tuungane katika kupiga vita na kutokomeza ukatili wa kijinsia, " amesema Mama Samia.

Akizungumzia ombwe la watoto wadogo kufanya biashara kwenye masoko, Mama Samia amezitaka kamati za masoko kuhakikisha zinashirikiana na mamlaka husika katika kuzuia watoto kufanya biashara sokoni na badala yake wawahimize kwenda shule na kuwaripoti wazazi wanaowatuma watoto wao kufanya biashara.

" Serikali yenu ya awamu ya tano iliwaahidi elimu bure kwa shule ya msingi hadi kidato cha nne. Tunapoona watoto wetu hawaendi shule na wanafanya biashara sokoni tunakua hatumtendei haki Rais wetu Dk John Magufuli kwa zawadi ya elimu bure aliyotuletea. Tuwazuie watoto kufanya biashara sokoni na tushirikiane kuwapeleka shule," amesema Mama Samia.

Aidha katika kutekeleza mradi huo, Mhe Makamu wa Rais amekabidhi Pikipiki 14 kwa ajili ya wataalam wa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Dodoma kwa Kata za Halmashauri ya Chamwino na kuielekeza Wizara kuendeleza utaratibu huo wa kupatia wataalamu hao usafiri ili iwe rahisi kwao kuwafikia wanawake wengi hususani wa vijijini na kuwaunganisha na fursa za kiuchumi.

Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe Ummy Mwalimu amemshukuru Makamu wa Rais kwa kuzindua mradi huo ambao utakua msaada mkubwa katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.

" Mhe Makamu wa Rais kama Wizara tumejipanga katika kuhakikisha tunaongeza elimu zaidi kwa wananchi iki tuzidi kupunguza wimbi la vitendo hivi, lengo letu ni kutokomeza kabisa vitendo hivi ili kuwa na Taifa imara ambalo litakua na mshikamano na amani baina yetu bila kujali huyu ni Mwanaume au Mwanamke," amesema Waziri Ummy.

Nae Mwenyekiti wa ALAT Mhe Gulamhafeez Mukadam amesema kuna changamoto kwenye dira ya pamoja juu ya utokomezaji wa vitendo vya ukatili wa kijinsia jambo ambalo linaleta athari ya maendeleo ya wanawake na hivyo kuzorotesha uchumi wa Nchi.

" Nimpongeze Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Mhe Godwin Kunambi kwa namna ambavyo amekua msaada kwa akina Mama wa Jiji hili kwa kuwapatia mikopo inayowawezesha kufanya biashara zao. Serikali za Mitaa jukumu lao ni kuwawezesha wananchi wao kuzipata fursa.

" Lakini pia kuna changamoto ya masoko, lugha chafu kwa wanawake sokoni hizi changamoto zinapaswa kushughulikiwa na kutokomezwa kabisa. Tukiwawezesha wanawake na kuwaepusha na vitendo vya unyanyasaji tutakua tunatengeneza Taifa imara na madhubuti na kuweza kufikia azma ya Mhe Rais ya uchumi wa kati kupitia viwanda," amesema Mhe Mukadam.
 Makamu wa Rais Mhe Mama Samia Suluhu Hassan akikata utepe kuashiria ufunguzi wa mradi wa kutokomeza vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika maeneo ya masoko. Uzinduzi huo umefnyika jijini Dodoma.
 Wananchi waliohudhuria uzinduzi wa mradi wa kutokomeza vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake wakimsikiliza mgeni rasmi ambaye ni Makamu wa Rais Mhe Mama Samia Suluhu Hassan (hayupo pichani) jijini Dodoma.
Maafisa Maendeleo ya jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino wakiwa na pikipiki walizokabidhiwa na Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan jijini Dodoma. Pikipiki hizo zimelenga kuwasaidia katika kuwafikia kundi kubwa la wanawake ambao wanafanyiwa unyanyasaji wa kijinsia.

No comments:

Post a Comment