Matokeo chanyA+ online




Wednesday, August 28, 2019

WADAU WAKABIDHI CHUMBA CHA UPASUAJI CHA WATOTO


Mkurugenzi Msaidizi wa huduma za Umma na binafsi wa Wizara ya Afya maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Wonanji Vivian leo amepokea chumba maalum cha upasuaji wa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi ambacho kimekarabatiwa na MOI pamoja na wadau kwa zaidi ya Tshs Milioni 500. 
Dkt. Wonanji amewashukuru wadau ,wafadhili pamoja na washirika wa MOI ambao wameshiriki katika ukarabatati na uanzishaji wa chumba hicho maalum. 
 “Leo tumekusanyika hapa kwa lengo moja kuu la kupokea rasmi chumba cha upasuaji kwaajili ya Watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi, hii ni hatua kubwa hapa nchini, nafahamu chumba hicho kilishaanza kutumika lakini leo kinakabidhiwa rasmi hongereni na ahsanteni wote mlioshiriki katika hili.” Alisema Dkt Wonanji. 
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface amesema chumba hicho kimejengwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali ambao ni chama cha Wazazi wenye watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi Tanzania ASBATH, Ndugu AKheri Kakoo kutoka Shia khoja athna asheri Muslim community, Cure International na Ubalozi wa Kuwait hapa nchini. 
“Chumba hiki kilianza kutumika mwezi Aprili na tayari watoto zaidi ya 352 wamefanyiwa upasuaji, ni matumaini yetu kwamba tutawahudumia watoto wengi zaidi ,awali tuliwafanyia upasuaji watoto 45-50 kwa mwezi sasa hivi tunawafanyia upsauji watoto 85-100 kwa mwezi hii imeondoa changamoto ya kusubiri upasuaji kwa muda mrefu.” Alisema Dkt. Boniface. 
Mwenyekiti wa Chama cha Wazazi wenye vichwa vikubwa na Mgongo wazi Tanzania Bw. Hakeem Bayakub amesema Takwimu zilizopo zinaonyesha kwamba zaidi ya watoto 4800 wanazaliwa na tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi kila mwaka hapa nchini, ambapo idadi ya watoto wanakwenda hospitali kupata huduma imeongezeka maradufu kutokana na uelewa kuongezeka. 
Imetolewa. Kitengo cha Uhusiano MOI

No comments:

Post a Comment