Veronica Simba – Pwani
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amekagua Mradi
wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) kwa mara ya 11 tangu kuanza utekelezaji wake
na kukiri kuridhishwa na maendeleo yake.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea
sehemu mbalimbali za Mradi huo ulioko Rufiji mkoani Pwani, Aprili 5 mwaka huu,
Dkt Kalemani amewataka Watanzania kuiamini Serikali na kuondoa hofu kuhusu
ukamilikaji wake kwa wakati.
“Napenda niwatoe hofu Watanzania kuwa, Mradi huu
haujawahi kusimama, hautasimama na utakamilika kwa wakati kama Serikali
ilivyoahidi.”
Waziri alikuwa akijibu swali la mmoja wa waandishi
aliyetaka kufahamu kuhusu tetesi kutoka kwa baadhi ya watu kuwa huenda Mradi
huo usikamilike kwa wakati.
Akieleza kwa kina kuhusu hatua iliyofikiwa katika
utekelezaji wa Mradi husika, Dkt Kalemani alibainisha kuwa kwa ujumla maendeleo
ni mazuri kwani tathmini inaonesha kuwa kwa kazi za msingi, ujenzi umefikia
asilimia 78.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani na Ujumbe wake, wakikagua maendeleo ya Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), Aprili 5 mwaka huu |
Alifafanua kazi hizo kuwa ni pamoja na ujenzi wa njia
ya kupokelea umeme (switch yard) ambayo hadi sasa Mkandarasi ametekeleza
kulingana na mpango-kazi.
Nyingine ni ujenzi wa eneo ambalo maji yataingia kwa
ajili ya kupelekwa kwenye mitambo (wáter in-take) ambalo nalo utekelezaji wake
hadi sasa unaendana na mpango-kazi wa mkandarasi.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani na Ujumbe wake, wakikagua maendeleo ya Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), Aprili 5 mwaka huu |
“Hata hivyo, katika eneo hili, kwenye kingo za maji
kuna shida kidogo kwa sababu maji ni mengi, hivyo nimemwagiza Mkandarasi
kuongeza kasi pindi maji yatakapopungua ili afidie muda na hivyo hali hiyo
isiathiri ukamilishaji kazi husika kwa wakati uliopangwa,” alieleza Waziri.
Alielezea kazi nyingine aliyokagua kuwa ni eneo
lililojengwa mitambo ya kusaga mawe kwa ajili ya kokoto za ujenzi ambapo
alibainisha kuwa kazi husika imekamilika kwa asilimia 100.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani na Ujumbe wake, wakikagua maendeleo ya Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), Aprili 5 mwaka huu |
Vilevile, Waziri alibainisha kuwa amekagua eneo ambako
zitafungwa mashine tisa kwa ajili ya kufua umeme na kubaini kuwa kazi ya ujenzi
katika eneo hilo hadi sasa imetekelezwa kwa kiasi kinachozidi kile
kilichoainishwa katika mpango-kazi kwa siku takribani 30.
Aidha, Dkt Kalemani alikagua pia kituo cha Reli ya
TAZARA cha Fuga ambacho ni maalumu kwa kushushia mitambo yenye uzito mkubwa
inayotumika katika ujenzi wa Mradi. Akiwa eneo hilo, Waziri alishuhudia mizigo
ikishushwa na kupelekwa eneo la Mradi.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani na Ujumbe wake, wakikagua maendeleo ya Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), Aprili 5 mwaka huu |
“Naipongeza Serikali kwa kujenga Reli hii na kuweka
Kituo rasmi kwa ajili ya kushusha mizigo ya Mradi huu. Hii inawezesha kazi za
Mradi huu kuendelea kama kawaida pamoja na changamoto ya mvua zinazoendelea
kunyesha nchini.
Hata hivyo, Waziri Kalemani alitoa wito kwa watendaji
wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kuijenga kwa kiwango cha lami,
barabara kutoka kituo cha Reli cha Fuga hadi eneo la Mradi, umbali wa kilomita
35.8 ili iwe katika viwango bora zaidi kuwezesha usafirishaji wa mizigo mizito
ya Mradi.
Waziri pia alikagua barabara zote zilizo ndani ya eneo
la Mradi na kuthibitisha kuwa zinapitika vizuri. Alitoa wito kwa Mkandarasi
kuendelea kukarabati maeneo korofi ya barabara hizo ikiwa ni pamoja na zile
zilizo nje ya Mradi, hususan zilizo ndani ya wajibu wake ili ziendelee kutumika
kusafirisha mizigo na wafanyakazi pasipo tatizo lolote.
Akizungumzia malipo kwa Mkandarasi, Dkt Kalemani
aliipongeza Serikali kwa kulipa jumla ya shilingi trilioni 1.19 kati ya
trilioni 6.5 za malipo yake yote, ambayo ni sawa na asilimia 18.8 huku
akibainisha kuwa kiwango hicho ndicho stahili iliyopaswa kulipwa kufikia wakati
huu, hivyo Mkandarasi hana kisingizio cha kutotekeleza majukumu yake.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani na Ujumbe wake, wakikagua maendeleo ya Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), Aprili 5 mwaka huu |
Katika hatua nyingine, Waziri aliushukuru Uongozi wa
Mikoa ya Morogoro na Pwani kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika usimamizi wa
Mradi.
Hata hivyo alitoa wito kwa Mikoa inayohusika na vyanzo
vya maji yatakayotumika katika Mradi huo, kuhakikisha kuwa pamoja na matumizi
ya maji katika shughuli zao za kiuchumi lakini wananchi wake wanapaswa
kuhakikisha matumizi hayo hayaathiri upatikanaji wa maji kwa ajili ya
utekelezaji wa Mradi.
Aliitaji mikoa hiyo kuwa ni pamoja na Morogoro,
Njombe, Iringa na Mbeya.
“Bwawa hili litakapokamilika litahitaji maji mengi
kiasi cha mita za ujazo bilioni 32.3 hivyo nawasihi sana wananchi wa Mikoa
husika kutoathiri upatikanaji wake,” alisisitiza Waziri.
Vilevile, Dkt Kalemani alitoa maelekezo kwa Uongozi wa
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuanza taratibu za kumpata Mkandarasi
atakayejenga njia ya kusafirisha umeme kutoka eneo la Mradi hadi Kinyerezi
jijini Dar es Salaam, umbali wa kilomita 167 ili kuuingiza kwenye gridi ya
Taifa.
“Nataka Mradi huu unapokamilika na njia ya kusafirisha
umeme huo iwe imekamilika tayari kwa kuanza kuusafirisha na kuuingiza kwenye
gridi ya Taifa.”
Katika ziara hiyo, Waziri alifuatana na viongozi
mbalimbali wa Serikali pamoja na wataalamu akiwemo Katibu Tawala wa Mkoa wa
Morogoro, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt
Tito Mwinuka, Meneja wa Shirika hilo mkoani humo, Mhandisi FedGrace Shuma,
Mwakilishi wa Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Ahmed Chinemba
pamoja na wataalamu wengine mbalimbali.
No comments:
Post a Comment