Matokeo chanyA+ online




Tuesday, December 29, 2020

MBUNGE SANGA ATIMIZA AHADI YAKE YA KUWEKA UMEME JUA ZAHANATI YA ILINDWE


Mbunge wa Makete Festo Sanga amekabidhi na kufunga umeme jua (Solar Panel) tatu katika zahanati ya Kijiji Cha Ilindiwe iliyopo Kata ya Mang'oto ikiwa ni ahadi yake aliyoitoa wakati akiomba kura kwenye kampeni za uchaguzi mkuu 2020.

Akikabidhi vifaa hivyo Sanga amewaomba wananchi kuvitunza Ili viwasaidie kwa muda mrefu wakati mchakato unaendelea wa kuunganishwa na umeme wa REA.

"Nilipokuja kuomba kura mliniambia hitaji lenu la kwanza ni Umeme wa Solar kwenye zahanati yenu hii, mlihitaji umeme kwa sababu huduma nyingi zinakwama nyakati za usiku na hasa zile zinazohitaji umeme,nami niliwaahidi kuwasaidia na leo nimetimiza ahadi yangu,"alisema.

Amesema ametimiza ahadi hiyo kwa haraka Ili kuendana na ahadi iliyotolewa katika ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2020-2025 ya kuimarisha huduma za afya Ili kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.



 "Natambua umuhimu wa Zahanati hii katika kuwahudumia wananchi,kama mbunge niliyepita kunadi Ilani hiyo nimeona ni vyema nikaitekeleza mapema ili mama zetu wanapohitaji huduma ya uzazi waipate masaa yote pakiwa na umeme, lakini wahudumu wetu wapumzike kutumia tochi kuhudumia wananchi nyakati za usiku na kwa kufanya hivyo tutafikia lengo na dhamira ya chama chetu,"alisisitiza.

Wakizungumza katika makabidhiano hayo baadhi ya wananchi wamemshukuru mbunge kwa kutimiza ahadi yake kwa haraka kwa kweli

"Changamoto ilikuwa kubwa hasa tulipohitaji huduma nyakati za usiku,tunamshukuru kwa kutimiza ahadi hii kwa kuwa wapo waliotangulia kuahidi lakini bado hawajatimiza, huyu Sanga ametupa matumaini makubwa sana sisi wananchi wa Ilindiwe tunamuombea kwa Mungu ambariki kwa pale alipotoa kwa ajili yetu,"alisema Sarah Singwa mkazi wa eneo hilo.

No comments:

Post a Comment