Matokeo chanyA+ online




Friday, January 29, 2021

FEDHA ZACHELEWESHA NHC KUKAMILISHA MRADI HOSPITALI YA RUFAA MARA


Na Munir Shemweta, WANMM MUSOMA

 

Imebainika kuwa kuchelewa kupelekwa fedha katika mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara iliyopo eneo la Kwangwa kumesababisha Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kutokamilisha mradi huo kwa wakati.

 

Mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara ulianza kujengwa  na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Septemba 15, 2019 na kutarajiwa kukamilika Agosti 2020 ambapo hata hivyo Mkandarasi (NHC) aliomba kuongezewa muda wa miezi sita (6) kutokana na kazi zilizoongezeka nje ya mkataba pamoja na kuchelewa kupatikana Wakandarasi maalum wa mradi.

 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akisalimiana na akina mama waliopeleka watoto wao kupata huduma katika Bawa C la Huduma ya Mama na Mtoto katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mara wakati  akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa hospitali hiyo tarehe 28 Januari 2021 akiwa katika ziara ya siku moja katika mkoa wa Mara. (PICHA NA MUNIRI SHEMWETA WIZARA YA ARDHI)

Akiwa katika ziara ya siku moja katika mkoa wa Mara tarehe 28 Januari 2021 kukagua utendaji wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ukusanyaji kodi ya Pango la ardhi, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula  alielezwa na Katibu Tawala wa mkoa Mara Catherine Mthapura akiwa kwenye ofisi ya Mkuu wa mkoa kuwa, awali mradi huo ulikuwa ukiendelea vizuri lakini sasa kasi ya mradi huo imepungua kutokana na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kutopatiwa fedha za kutekeleza mradi huo kwa wakati na Wizara ya Afya.

 

"Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limefanya kazi kubwa ikiwemo kutumia fedha za Shirika kuharakisha ujenzi wa hospitali lakini sasa tangu Bawa C (Wing C) kuanza kutoa Huduma za Mama na Mtoto kazi imesimama tangu Juni 2020" alisema Katibu Tawala mkoa wa Mara.

 

Kwa upande wake Mhandisi wa Mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa mkoa wa Mara Renard Kazoba alimueleza Naibu Waziri Dkt Mabula wakati akikagua mradi huo kwamba, changamoto kubwa ya kutokamilika mradi huo kwa wakati ni kuchelewa kwa malipo ambapo pamoja na Mkandarasi kuidhinishiwa malipo ya Shilingi Bilioni 3,591,565,635.35 ili kuharakisha utekelezaji mradi na  Mshitiri kutakiwa kumlipa mkandarsi ndani ya siku 28 kwa kadiri ya mkataba lakini hadi sasa hakuna kiasi kilicholipwa.

 

 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa hospitali ya rufaa mkoa wa Mara tarehe 28 Januari 2021 akiwa katika ziara ya siku moja katika mkoa wa Mara, kushoto ni Msimamizi wa mradi huo Mhandisi Renard Kazoba.

 

Hata hivyo, alibainisha kuwa katika kukabiliana na changamoto aliyoainisha, Shirika la Nyumba la Taifa limefanya vikao na wahusika wakuu wa mradi na kutolea mfano wa kikao kilichofanyika tarehe 6 Novemba 2020 baina ya Shirika na wahusika hao na kukubaliana mambo ambayo Shirika la Nyumba la Taifa linasubiri utekelezaji wake.

 

Aidha, Kazoba alisema,  NHC imenunua Jenereta 250 KVA pamoja na vifaa vya kuliwezesha  kufanya kazi kwa kutumia fedha za ndani ili kufanikisha upatikanaji umeme wa uhakika katika jengo Bawa C.

 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula  alisema Shirika la Nyumba la Taifa ili liweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo linahitaji kupata fedha kwa wakati kupitia miradi inayotekeleza hasa ikizingatiwa halipokei ruzuku kutoka serikalini na kusisitiza kuwa lisipowezeshwa litashindwa kutekeleza miradi yake.

 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipata maelezo ya maendeleo ya ujenzi wa mradi wa hospitali ya rufaa mkoa wa Mara kutoka kwa Msimamizi wa mradi Mhandisi Renard Kazoba (kushoto) alipokwenda kukagua mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo akiwa katika ziara ya siku moja katika mkoa wa Mara tarehe 28 Januari 2021.

 

 Alisema, katika utekelezaji mradi wa ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara Shirika la Nyumba la Taifa linatakiwa kukamilisha mradi huo kwa gharama ya shilingi bilioni 15,082,481, 832.82  na hadi sasa zimelipwa bilioni 8,469,851,800.34 na kiasi kilichobaki ni bilioni 6,612,630,032.48 huku NHC ikiwa imetumia fedha zake za ndani  shilingi Bilioni 3,591,565,635.35 na kusisitiza kiasi hicho kisipolipwa shirika litashindwa kufanya kazi.

 

"Lengo la Shirika ni kufanya kazi bila kukwama na kukamilisha miradi yake kwa wakati naagiza Shirika kuhakikisha linawafuatilia Wadaiwa wote sugu wa kodi za nyumba za Shirika ili kuiwezesha NHC kupata fedha ya kutekeleza miradi yake" alisema Dkt Mabula.

 

Kaimu Mganga Mkuu katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Mara Dkt Lazoro Mwikabe alisema, tangu hospitali hiyo kuanza kutoa huduma katika sehemu ya Bawa C ( Wing C) zaidi ya watoto 1000 wamezaliwa na wananchi wa mkoa wa Mara wana imani kubwa na huduma za hospitali hiyo.

 

Aliongeza kwa kusema kuwa, hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara imejipanga na iko katika mazungumzo na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHF) ili kupatiwa mkopo wa kununua mashine ya CT Scan. 

 

Shirika la Nyumba la Taifa linadai takriban bilioni 27 kutoka kwa wapangaji wa nyumba mbalimbali nchini huku likitekeleza miradi mikubwa ya Serikali ya kimkakati ya  Hospitali za Rufaa za mkoa wa Mtwara na Mara sambamba na ujenzi wa miradi ya nyumba na ofisi za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

No comments:

Post a Comment