Matokeo chanyA+ online




Wednesday, May 5, 2021

RAIS SAMIA AHUTUBIA JUKWAA LA WAFANYABIASHARA WA TANZANIA NA KENYA JIJINI NAIROBI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama na mwenyeji wake Rais wa Kenya Mheshimiwa Uhuru Muigai Kenyatta wakati nyimbo za Mataifa Mawili ya Tanzania na Kenya wakati zikipigwa mara baada ya kuwasili Ukumbini kwa ajili ya kuhutubia Jukwaa la Wafanyabiashara wa Kenya na Tanzania lililofanyika Jijini Nairobi Kenya leo tarehe 05, Mei, 2021.





Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwahutubia Wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya katika Kongamano hilo la Wafanyabiashara lililofanyika Jijini Nairobi Kenya leo tarehe 05, Mei, 2021.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akipongezwa na Rais wa Kenya Mheshimiwa Uhuru Muigai Kenyatta mara baada ya kuhutubia katika Jukwaa hilo la Wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya lililofanyika jijini Nairobi nchini Kenya.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiagana na Rais wa Kenya Mheshimiwa Uhuru Muigai Kenyatta mara baada ya kuhutubia katika Jukwaa hilo la Wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya lililofanyika jijini Nairobi nchini Kenya.


Sehemu ya viongozi mbalimbali pamoja na Wafanyabiashara waliohudhuria Kongamano hilo jijini Nairobi. PICHA NA IKULU.
 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 05 Mei, 2021 amehutubia Bunge la Kenya lililojumuisha Bunge la Taifa na Bunge la Seneti ambapo ametoa wito kwa Wabunge hao kuchochea uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na Kenya.

Mhe. Rais Samia ambaye anakuwa Rais wa pili wa Tanzania kuhutubia Bunge la Kenya akitanguliwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amewashukuru Maspika na Wabunge wa Kenya kwa kukubali awahutubie na amebainisha kuwa huo ni uthibitisho wa udugu, urafiki, ujirani na nia njema ya Wabunge na Mhe. Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kukuza zaidi uhusiano uliopo na Tanzania.

Katika hotuba hiyo,  Rais Samia amesema haoni sababu ya Tanzania na Kenya kushindana bali anaona fursa ya kushirikiana zaidi katika uchumi kwa kuwa uhusiano wa nchi hizi ilioanza miaka 56 iliyopita sio wa hiari kutokana na kufungamanishwa uhusiano wa damu kwa jamii zilizopo pande zote, historia kutokana na kuwepo uhusiano hata kabla ya uhuru na jiografia kutokana na kuwa na mpaka mrefu na maeneo yenye rasilimali zilizoungana ikiwemo hifadhi na wanyama.

Ameahidi kuwa katika kipindi chake cha uongozi atahakikisha uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na Kenya unaimarika zaidi na ametoa wito kwa viongozi na watumishi wa Serikali kuendana na kasi ya ushirikiano waliyonayo wananchi kwani hivi sasa hali inaonesha wananchi wa Tanzania na wananchi wa Kenya wanashirikiana zaidi ikilinganishwa na namna viongozi na wafanyakazi wa Serikali wanavyoshirikiana.

Pia, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameahidi kuendeleza miradi ya ushirikiano ikiwemo ujenzi wa barabara, ujenzi wa bomba la gesi la Dar es Salaam – Mombasa, ujenzi wa njia ya umeme ya kilovoti 400 kutoka Singida Tanzania kwenda Kenya, kukamilisha vituo vya huduma za pamoja mpakani (One Stop Border Post) na amesisitiza kuwa yeyote anayefikiria kuichonganisha Tanzania na Kenya ajue kuwa uhusiano wa nchi hizi ulikuwepo, upo na utakuwepo sana.

Amewataka Wabunge hao kuwaongoza wananchi katika kuimarisha uhusiano huo badala ya kuudhohofisha na kwamba hata yeye amefanya ziara hiyo ili kurekebisha maeneo yote ambayo yalikuwa yanalegalega jambo ambalo limefanikiwa sana baada ya mazungumzo yake na Mhe. Rais Kenyatta.

“Kuongoza ni kuonesha njia sio kufunga njia” amesisitiza Mhe. Rais Samia na kubainisha kuwa pale kunapotokea tatizo kati ya pande hizi dawa iwe ni kulitatua badala ya kuliendeleza.

Kabla ya kuhutubia Bunge, Mhe. Rais Samia amekutana na wafanyabiashara wa Tanzania na Watanzania waishio Kenya (Diaspora) na amewaambia kuwa katika kipindi chake cha uongozi amedhamiria kukuza uchumi kwa haraka na hivyo ametoa changamoto kwa sekta binafsi kujipanga vizuri kutumia fursa mbalimbali ambazo Serikali ya Awamu ya Sita itazifungua na kuondoa vikwazo mbalimbali vya biashara.

Ametaja baadhi ya fursa hizo kuwa upanuzi wa huduma za bandari zitakazokidhi mahitaji na kwendana na kasi ya kukua kwa uchumi, kuanzishwa kwa maeneo maalum ya viwanda (industrial parks) yatakayozalisha bidhaa na kuajiri Watanzania wengi, kukuza na kuendeleza kilimo na amewaonya wale ambao wameshikilia maeneo makubwa ya mashamba lakini hawayaendelezi kuwa Serikali itayatwaa maeneo hayo na kuwapatia waliotayari kuzalisha mazao.

“Nataka kwenda faster, nataka kufuangua nchi, yeyote anayetaka kuwekeza aje awekeze yeye apate na sisi tupate, najua wawekezaji wengi watakuwa wa nje lakini nawaomba na nyie mchangamke na mtumie vizuri fursa za ndani zitakazojitokeza (local content)” amesisitiza Mhe. Rais Samia.

Mhe. Rais Samia ameitaka sekta binafsi ya Tanzania kumuunga mkono katika dhamira hiyo na amewaomba wafanyabiashara na wawekezaji waliowekeza nje ya Tanzania kurudi kuwekeza Tanzania kwani nyumbani kumenoga. Pia amewataka kuijulisha Serikali pale watakapoona jambo lolote halipo sawa zikiwemo sheria kandamizi ili zifanyiwe kazi.

Mhe. Rais Samia ameagwa na Mhe. Rais Kenyatta na amerejea Jijini Dodoma nchini Tanzania akitokea Jijini Nairobi nchini Kenya baada ya kumaliza Ziara Rasmi ya siku 2 nchini humo.


No comments:

Post a Comment