Matokeo chanyA+ online




Sunday, September 26, 2021

MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR ATOA MAAGIZO KWA TPA KUHUSU UPANUZI BANDARI TANGA,ATAKA IVUTIE KIMATAIFA


 Makamu wa Pili wa Rais Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,Hemed Suleiman Abdulla ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha kuwa wakati upanuzi wa Bandari ya Tanga ukielekea ukingoni wahakikishe kuwa wanaitangaza kimataifa ili kuvutia wateja.


Ametoa agizo hilo leo wakati akifanya ukaguzi wa Bandari ya Tanga ambapo yupo katika ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Tanga,hivyo upanuzi wa bandari hiyo unaotekelezwa na kampuni ya CHEC kutoka China ukielekea ukingoni ni vema mamlaka hiyo ikaanza mikakati ya kuitangaza bandari hiyo wakati ujenzi ukiendelea.


Amesema kuwa katika upanuzi huo, serikali imewekeza zaidi ya kiasi cha Sh.bilioni 400 hivyo lazima kuwe na tija kuona ni namna gani serikali itarudisha hiyo fedha."Serikali imetumia zaidi ya Sh.bilioni 400 katika upanuzi wa bandari hii ambayo ni nguzo muhimu kiuchumi sio kwa mkoa wa Tanga pekee bali hata mikoa ya kanda ya Kaskazini.


"Visiwani na nchi za Rwanda na Burundi,hivyo itangazeni hii bandari kimataifa ili wateja waanze kuja kabla hata ujenzi haujakamilika ikiwemo kuweka promosheni ili kuwavutia wateja na pia wekeni mazingira rafiki kwa wafanyabiashara ili walipe kodi kwa mujibu wa sheria," amesema.



Kwa upande wake,Mkurugenzi Mkuu wa Bandari,Eric Hamisi amekiri mamlaka hiyo kutoitangaza bandari hiyo na kuahidi kutelekeza agizo hilo mara moja ikiwemo kutumia ofisi za balozi za Tanzania zilizopo nje ya nchi kwa kutoa elimu kwa kutumia lugha za asili za nchi husika ili kuwa na uelewa pamoja na kuimarisha ofisi za TPA katika nchi hizo.


" Ni kweli bado bandari hii haijatangazwa sana kimataifa lakini mkakati uliopo ni kuhakikisha tunashirikiana na ofisi za balozi zetu nje ya nchi kwa kutoa elimu,kuanzaa vipeperushi,mawasilisho kwa kutumia lugha za nchi husika pamoja na kuimarisha ofisi zetu katika bandari hizo," alisema.


Wakati huo huo Ofisa Mradi kampuni ya CHEC, Lyu Wei amesema mradi huo umetekelezwa kwa awamu mbili,awamu ya kwanza ambayo imekamilika kwa asilimia 100 tangu Mei 2020,imetumia kiasi cha Sh.bilioni 172 na awamu ya pili imetumia Sh.bilioni 256 , ipo katika hatua ya mwisho ikiwemo kuleta mashine mbili za bandari.


Kwa upande wake,Meneja wa Bandari ya Tanga, Donald Ngaile amesema kuwa kukamilika kwa bandari hiyo kutaondoa msongamano katika Bandari ya Dar es salaam, kupunguza gharama ya kutoa mizigo mara mbili kati ya meli-tishali na kutoka kwenye tishali- nchi kavu kwa asilimia 40.


Pia kupunguza gharama za matumizi ya mafuta zinazotumika katika boti za kuvuta tishali ,kufupisha muda wa kuhudumia meli kutoka siku tano mpaka sita hadi kufikia saa 24 pamoja na kuongeza idadi ya kupokea meli nyingi na kuhudumia shehena kutoka tani 700,000 hadi tani milioni 3.



 

No comments:

Post a Comment