Matokeo chanyA+ online




Tuesday, October 5, 2021

NEEMA YA MAJI YAWASHUKIA WANANCHI LUDEWA/KULETEWA BILIONI MOJA


 Na Damian Kunambi, Njombe


Kufuatia kuwepo kwa changamoto nyingi za maji katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Ludewa mkoani Njombe imepelekea wizara ya maji hapa nchini kuahidi kutoa kiasi cha shilingi bilioni moja ndani ya mwezi huu ili kupunguza changamoto hizo.


Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa maji Merryprisca Mahundi baada ya kufanya ziara katika kata ya Masasi na Iwela na kusikiliza changamoto zao pamoja na kukagua mradi wa maji wa Iwela.


 Kabla ya Naibu Waziri huyo kutoa ahadi hiyo mbunge wa jimbo la ludewa Joseph Kamonga alielezea changamoto wanazozipata wananchi hao na kusema kuwa wananchi wake wamekuwa wakitembea umbali mrefu wa zaidi ya masaa mawili kwenda kuchota maji  kitu ambacho kinawaumiza  huku miradi mbalimbali ikikwama kwa kukosa maji.


 "Mheshimiwa Naibu Waziri mradi huu wa Iwela ni mkubwa sana! hivyo tunaweza kusambaza maji ya mradi huu hata katika vitongoji na vijiji vya jirani kama Kisaula , Lutala na kwingineko",amesema Kamonga.


Aidha kwa upande wa Naibu Waziri huyo amesema kiasi hicho cha fedha kitagawanywa katika baadhi ya maeneo yenye shida zaidi ili kuweza kuwapunguzia adha wanayoipata.


"Mbunge wenu alikuwa akinisumbua sana kwa kunitaka nifike katika jimbo lake na kuona changamoto hii ya maji inayowapata wananchi wake, na sasa nimefika nimejionea kwa macho yangu hivyo serikali haina budi kuleta fedha ili tumtue mama ndoo kichwani", amesema Mhandisi Mahundi


Hata hivyo Naibu Waziri huyo amemuagiza mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Iringa (IRUWASA) David Palangyo kuwasilisha andiko la kuongeza usanifu mpya wa vitongoji ambavyo vimekosa maji ya mradi wa Iwela.


Naibu Waziri huyo amesema mradi huo umejengwa kwa kutumia 'force account' na kuweza kuokoa milioni 500 mpaka kukamilika kwa mradi hivyo kuna uwezekano wa chenchi kubaki ambayo ndiyo itakayosaidia kuongeza mabomba ya maji.

 

Naibu Waziri wa maji mhandisi Merryprisca Mahundi sambamba viongozi mbalimbali wakiangalia maji yanayotiririka kutoka kwenye tenki la mradi
Naibu waziri wa maji Merryprisca Mahundi akiteta jambo na mbunge wa jimbo wa Ludewa wakati wa mkutano na wananchi wa kijiji cha Lihagule
Naibu waziri wa maji mhandisi Merryprisca Mahundi (kulia) akiwa na mbunge wa jimbo la Ludewa(kushoto) sambamba na viongozi mbalimbali wakikagua bomba la maji katika eneo la mradi wa maji wa Iwela.

Naibu waziri wa maji mhandisi Merryprisca Mahundi akicheza ngoma ya mganda baada ya kuwasili katika Kijiji cha Lihagule wilayani Ludewa mkoani Njombe
Baadhi ya viongozi wa chama na serikali waki wakiwa kwenye mkutano na wananchi wa kata ya Iwela kutoka kushoto ni diwani wa kata ya Iwela Joackim Lukuwi, mwenyekiti wa ccm wilaya ya Ludewa Stanley Kolimba, Naibu waziri wa maji mhandisi Merryprisca Mahundi, mkuu wa wilaya ya Ludewa Andrea Tsere, mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa Wise Mgina.
Mkuu wa wilaya Andrea Tsere (kushoto) akiongea na naibu waziri wa maji mhandisi Merryprisca Mahundi mara baada ya kuwasili wilayani Ludewa.
Naibu waziri wa maji mhandisi Merryprisca Mahundi (kushoto) akiteta jambo na mwananchi mkazi wa kijiji cha Lihagule wilani ludewa mkoani Njombe.

No comments:

Post a Comment