Matokeo chanyA+ online




Tuesday, March 17, 2020

SERIKALI INA DHAMIRA YA DHATI KUONDOA UZEMBE NA UBADHILIFU MIONGONI MWA WATUMISHI - WAZIRI HASUNGA

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo katika ukumbi wa TPRI Jijini Arusha,  tarehe 16 Machi 2020. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Serikali inayo dhamira ya dhati ya kuondoa uzembe na ubadhirifu miongoni mwa watumishi wa umma hivyo ni vyema watumishi wajiepushe na matumizi ya lugha zisizo na staha muda wote wanapotekeleza majukumu yao.

Aidha, serikali imewataka wafanyakazi wote wa Wizara kuendelea kujengewa misingi ya uwajibikaji hasa katika kutambua wajibu wao kwa Umma na kuacha uzembe katika utekelezaji wa majukumu yao huku wakisisitizwa kutumia muda mwingi katika kufanya shughuli ambazo hazina tija zinazoathiri utendaji kazi.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ametoa rai hiyo wakati akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo katika ukumbi wa TPRI Jijini Arusha l tarehe 16 Machi 2020.

Katika mkutano huo ambao wajumbe watapata fursa ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2019/2020 na kujadili na kupitisha makisio ya bajeti ya mwaka 2020/2021 wametakiwa kota Mawazo muhimu katika hatua za utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2020/2021 na kujadili kwa kina na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha bajeti ya Wizara kwa Mwaka ujayo wa fedha.

Amesema kuwa Wizara ya Kilimo inalo jukumu kubwa katika Maendeleo ya nchi hasa kwa kuzingatia kuwa zaidi ya Watanzania asilimia 65.5 wameajiriwa katika kilimo, asilimia 28.7 ya pato la taifa, zaidi ya asilimia 30 ya fedha za kigeni, asilimia 65 ya malighafi za viwanda, asilimia 100 ya chakula chote nchini. 
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Ndg Gerald Kusaya akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kwa ajili ya ufunguzi wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo katika ukumbi wa TPRI Jijini Arusha,  tarehe 16 Machi 2020.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb), na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Ndg Gerald Kusaya wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo katika ukumbi wa TPRI Jijini Arusha,  tarehe 16 Machi 2020. 

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Arusha

Pamoja na mambo mengine Waziri Hasunga amewataka wajumbe hao kukumbuka kuwa wizara inawajibika na masuala yote yanayohusu Uendelezaji wa Sekta ya Kilimo hususani; Kuongeza Tija na Uzalishaji wa Mazao ya Kilimo; Kuwezesha Upatikanaji wa Masoko ya Bidhaa za Kilimo; Kuwezesha Uongezaji wa Thamani ya Mazao ya Kilimo; Kuimarisha Mfumo wa Ukusanyaji na Uhifadhi; Uchambuzi na Usambazaji wa Takwimu; Kusimamia Sera, Sheria, Kanuni na Mikakati katika Sekta ya Kilimo; Kuboresha Uratibu katika Sekta ya Kilimo; Kuboresha Uwezo wa Wizara wa kutoa huduma, kuwezesha na kuimarisha Ushirika na Asasi za Wananchi katika Kilimo na Sekta nyingine na Kuzingatia Masuala Mtambuka katika Kilimo.

Mhe Hasunga amesema kuwa katika  kutambua uzito na umuhimu wa majukumu hayo kila mmoja  katika sehemu yake ya kazi anatakiwa kuwajibika na kufanya kazi kwa bidii na kwa  uadilifu ili kuiwezesha Serikali kufikia malengo yake ya kukuza uchumi na kuondoa umaskini kwa wananchi.  

No comments:

Post a Comment