Matokeo chanyA+ online




Saturday, March 28, 2020

WATANZANIA ENDELEENI KUKABILIANA NA CORONA - WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu  wakikagua jenereta lilitolewa na familia ya Karimjee  Jivanji ya jijini Dar es salam lenye thamani ya sh. milioni 75 wakati alipopokea michango kutoka kwa wadau mbalimbali  kwa ajili  ya mapambano dhidi ya  ugonjwa wa CORONA, Machi 28, 2020, Magogoni jijini Dar es salaam. Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mussa Azan Zungu.

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amewataka Watanzania kuendelea kukabiliana na ugonjwa wga  Corona ili Kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huu nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo na mheshimiwa Waziri Mkuu baada ya kukabidhiwa msaada wa vifaa kinga, fedha na dawa kutoka taasisi, kampuni na umoja wa mama ntilie nchini.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipima joto la mwili wakati alipowasili ofisini kwake  Magogoni jijini Dar es salaam kupokea michango kutoka kwa wadau mbalimbali  kwa ajili ya mapambano dhidi ya  ugonjwa wa Corona, Machi 28, 2020.
 Mheshimiwa Kassim Majaliwa amesema Kuwa Watanzania wanapaswa kuzingatia kuchukua tahadhari kama vile kunawa mikono Mara kwa Mara kwa maji yanayotiririka na kuepuka misongamano ili kudhibiti janga hili kubwa lililozikumba pia mataifa makubwa.

“Wakati tunaendelea kukabiliana na janga hili la Corona pia tunapaswa kujua kwamba ugonjwa huu utaleta athari za kiuchumi,” amesema Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa.

Waziri Mkuu amewashukuru Watanzania waliojitokeza kuchangia fedha, dawa na vifaa kinga kwa Kuwa msaada huo itasaidia watu WOTE waliokumbwa na COVID- 19 pamoja na kusaidia Watanzania kujikinga  ili Kuzuia kusambaa kwa homa kali ya mapafu.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hundi ya sh. milioni 230  ukiwa ni mchango wa Benki ya UBA wakati alipopokea michango kutoka kwa wadau mbalimbali  kwa ajili ya mapambano dhidi ya  ugonjwa wa CORONA, Machi 28, 2020, Magogoni jijini Dar es salaam. Kulia ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, kushoto ni  Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo, Usman Isaka na wa nne kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo, Farhiya Warsama. 

“Hivi vitu vyote tulivyopokea Leo ni gharama kubwa, tumeona Watanzania wenye moyo wamekuja hapa kuungana na Serikali kukabiliana na ugonjwa huu, hivyo hatuwezi kuacha hivi bila kutoa shukrani kwa wenzetu waliotoa msaada huu,” amesema Mhe. Waziri Mkuu.

Amesema Watanzania wanaopenda kuchangia jitihada za kukabiliana na ugonjwa huu, wachangie fedha Benki Kuu kupitia akaunti ya National Relief Fund Electronic, namba 9921159801 na kwamba wanaweza kuchangia kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitumika kitakasa mikono wakati alipowasili ofisini kwake  Magogoni jijini Dar es salaam kupokea michango kutoka kwa wadau mbalimbali  kwa ajili ya mapambano dhidi ya  ugonjwa wa Corona, Machi 28, 2020.

Baadhi ya Kampuni zilizochangia Serikali katika kukabiliana na Corona ni Benki ya NMB milioni 100, CRDB  Milioni 150, Benki ya UBA  milioni 230,  umoja wa mama ntilie  Milioni 2, Ashton Media  Milioni 104 na Kampuni mbalimbali zimechangia  fedha na vifaa kinga kwa lengo la kukabiliana ugonjwa wa Corona.

Wakati huohuo Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema kuwa kwa kipindi cha masaa 24 tangu jana Alhamisi Machi 27,2020 jumla ya sampuli 26 zimewasilishwa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii na zote zimethibitishwa hazina maambukizi'Negative', hivyo  mpaka sasa hapa nchini watu waliothibitika 'positive' kuwa na ugonjwa huo bado ni kumi na tatu(13).

No comments:

Post a Comment