Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka Nchi
Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kutumia majukwaa ya
kikanda, kitaifa na kimataifa kwa ajili ya kupaza sauti zao ili kusaidia
kuondolewa kwa vikwazo kandamizi vya kiuchumi kwa Jamhuri ya Zimbabwe.
Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Baraza
la Mawaziri wa SADC leo Jumatano (Machi 18, 2020) Jijini Dar es Salaam, Waziri
Mkuu Majaliwa alisema Tanzania kupitia nafasi yake ya Uenyekiti wa SADC
imeendelea kupaza sauti kwa ajili ya kuisaidia Serikali ya Zimbabwe.
Aliongeza kuwa mwezi Oktoba mwaka jana Tanzania
ilifanya kongamano kubwa la kihistoria lililowaleta pamoja wadau mbalimbali wa
kitaifa na kimataifa, ambapo katika kongamano hilo wadau hao walitoa, ambapo
Serikali ya Tanzania inaamini kuwa ujumbe wa mkutano huo uliwafikia walengwa.
Aidha Majaliwa alisema kuwa wakati Nchi Wanachama
wa SADC wakielekea kuitekeleza ya mwaka 2020 (SADC Post 2020 Agenda), mataifa
hayo hayana budi kuungana pamoja na kupaza sauti zao hadi hapo vikwazo hivyo
vitakavyoondolewa kwa Jamhuri ya Zimbabwe, vikwazo ambavyo athari zake zimekuwa
kubwa kwa uchumi wa wananchi na Nchi ya Zimbabwe.
‘’Vikwazo hivi vya kidhalimu, athari zake ni
kubwa kwa ustawi wa uchumi wa Zimbabwe na wananchi wake kwa ujumla, hivyo
hatuna budi kuungana pamoja katika kupaza sauti zetu ili kuisaidia Jamhuri ya
Zimbabwe kuondolewa vikwazo hivi’’ alisema Majaliwa.
Kuhusu mafanikio ya SADC, Majaliwa alisema tangu
Januari mwaka huu Tanzania kupitia nafasi yake ya Uenyekiti wa SADC, inaendelea
na jitihada mbalimbali za kuimarisha jumuiya hiyo ili kuweza kufikia malengo,
ambapo imefanikisha kufanyika kwa mikutano mitano ya kisekta ikiwemo Mkutano wa
Mawaziri wa Sekta ya Mawasiliano, Uchukuzi, TEHAMA na Hali ya Hewa.
Anaitaja Mikutano mingine ni pamoja na Mkutano wa
Mawaziri wa sekta za Maliasili na Utalii, Mkutano wa Mawaziri wa Sekta ya Afya,
Mkutano wa Mawaziri wa Sekta ya Kazi na Ajira, Mkutano wa Mawaziri wa
Menejimenti ya Maafa katika SADC.
Aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka 40 tangu
kuanzishwa kwa SADC, Jumuiya hiyo imeendela kupata mafanikio mbalimbali ikiwemo
miradi ya miundombinu, viwanda, elimu, mazingira na jinsia na kuzitaka Nchi
wanachama kuchukulia changamoto zinazojitokeza kwa sasa ikiwemo kisera, bajeti,
ushiriki hafifu wa sekta binafsi kuwa sehemu ya maandalizi ya Mpango Mkakati wa
miaka 10 ya Jumuiya hiyo wa 2020/2030.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi alisema Tanzania kwa
kushirikiana na Sekretarieti ya Jumuiya hiyo, imewezesha kwa kiasi kikubwa
kufanikisha mafanikio ya mkutano huo uliofanyika kupitia njia ya mtandao (Video
Conference) kutokana na tishio la uwepo wa homa kali ya mapafu inayosababishwa
na virusi vya COVID 19.
Prof. Kabudi alisema Tanzania kupitia nafasi yake
ya Uenyekiti imeendelea kuhakikisha kuwa ajenda ya utengamano wa Jumuiya
hiyo inafikiwa kama ilivyoanishwa katika Mkataba wa Uanzishwaji wa SADC
inayoongozwa na nyaraka mbili za kimkakati amazo ni Mkakati Elekezi wa Kanda
2015-2020 na Awamu ya Pili ya Mpango Mkakati wa Asasi za Siasa, Ulinzi na
Usalama.
Aliongeza kuwa kupitia maazimio na mikakati hiyo,
SADC imewezesha kuleta mchango na maendeleo makubwa ndani ya ukanda huo kwa
kuhakikisha kuwa nchi wanachama zinakuwa na mtazamo mpya wa kimkakati na kupata
matokeo chanya yatakayoakisi maendeleo jumuishi na endelevu kwa ajili ya ustawi
wa wananchi wa jumuiya hiyo.
Kwa mujibu wa Waziri Kabudi alisema katika
mkutano pia, Baraza hilo linatarajia kupokea na kujadili taarifa ya maandalizi
ya Dira ya Jumuiya ya 2050 pamoja na Mpango Mkakati wa utekelezaji wa malengo
ya dira hiyo na kutoa mtazamo mpya wa kimkakati unaotoa mwongozo kwa ajili ya
kuimarisha mtangamano.
Naye Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo, Dkt.
Stergomena Tax alisema Jumuiya hiyo imeendelea kupiga hatua za maendeleo katika
nyanja mbalimbali za kiuchumi ikiwemo viwanda, nishati, maji kupitia
utekelezaji wa maazimio na mipango mbalimbali ya utekelezaji iliyowekwa katika
mwaka 2019/2020 na 2020/2021.
No comments:
Post a Comment