Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini
imeipongeza serikali kuunganisha gesi asilia katika viwanda mbalimbali nchini
jambo ambalo limesaidia kupunguza gharama za uendeshaji.
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Vedastus Mathayo,
alitoa pongezi hizo, Machi 17, 2020 baada ya Wajumbe wa Kamati kutembelea
Kiwanda cha kufua vyuma cha Lodhia, kilichopo Mkuranga mkoani Pwani kwa lengo
la kujionea manufaa yaliyopatikana kutokana na matumizi ya gesi asilia.
“Kama Kamati, tumefurahishwa sana na mafanikio
yaliyopatikana baada ya kiwanda hiki kuunganishiwa mtandao wa gesi asilia na
tunaipongeza sana Serikali kupitia Wizara ya Nishati,” amesema Mathayo.
Pamoja na pongezi hizo, Kamati imeishauri serikali
kuendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kuzalisha umeme ambayo
itasaidia upatikanaji wa nishati hiyo kwa wingi hivyo kuwezesha gharama yake
kupungua na hivyo kuwawezesha wawekezaji katika viwanda kuzalisha kwa tija
zaidi.
Akitoa maelezo ya serikali kutokana na maelekezo hayo
yaliyotolewa na Kamati, Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, ambaye
alimwakilisha Waziri mwenye dhamana, Dkt Medard Kalemani, alisema Serikali
itahakikisha inaendelea kusimamia kikamilifu miradi mbalimbali ya uzalishaji
umeme ili kuwezesha upatikanaji wa umeme mwingi na wa uhakika wenye gharama
nafuu.
“Tuna matumaini kwamba kukamilika kwa miradi mikubwa,
ukiwemo wa Julius Nyerere (MW 2,115) kutawezesha kushuka gharama za umeme kwa
kiasi kikubwa.”
Awali, akiwasilisha taarifa ya kiwanda hicho mbele ya
Wajumbe wa Kamati, Meneja Rasilimaliwatu, Martin Mkange alisema kupatikana kwa
gesi asilia kumewasaidia pamoja na mambo mengine kuondokana na matumizi ya
mafuta mazito ambayo yalikuwa na gharama kubwa katika uendeshaji.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa Kamati, Kiwanda cha Lodhia kinatumia
gesi asilia kiasi cha wastani wa futi za ujazo milioni 0.1 hadi 0.2 kwa siku,
sawa na makusanyo ya zaidi ya shilingi milioni 70 kwa mwezi.
Taarifa inaeleza zaidi kuwa kiwanda hicho kilianza
kutumia gesi asilia mwezi Juni, 2019.
Miradi ya usambazaji gesi asilia nchini inaendelea
kutekelezwa katika maeneo ambayo tayari kuna miundombinu wezeshi ikihusisha
mikoa ya awali ya Pwani na Dar es Salaam.
Veronica Simba – Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment